Home Makala NI KIPINDI CHA KUJA NA MIKAKATI MIPYA KISIASA

NI KIPINDI CHA KUJA NA MIKAKATI MIPYA KISIASA

5040
0
SHARE

NA KIBONA DICKSON


MAPAMBANO ya kisiasa ni kama yale ya vita, muda wote wapambanaji ni lazima wawe na uwezo wa kubuni na kutekeleza mbinu na mikakati mipya.

Hali inapaswa kuwa hivi pia kwa vyama vya siasa nchini, hasa vile vya upinzani, vinapaswa kuwa na mbinu mpya.

Katika kufanikisha hilo nimewiwa nibainishe mbinu na mikakati kadhaa ambayo inaweza kusaidia katika mapambano ya kisiasa nchini.

Mkakati namba moja;

Ni lazima kubadili mbinu za kukabiliana na adui. Hali ya siasa nchini imebadilika sana. Dhamira ya watawala ni kuona upinzani unadhofika!

Kwa sasa malengo yanaelekezwa kwenye ngazi ya kitaifa, ili kusambaratisha kabisa upinzani. Wanaotenda udhalimu, wanafikiri viongozi wakuu wa upinzani wakikatishwa tamaa, basi hata wafuasi wao watakata tamaa na kutawanyika. Hii ndiyo maana ya kuwalenga viongozi wa upinzani. Ukweli ni kwamba ikitokea hawa wakavunjika moyo, basi kundi kubwa la watu watakata tamaa pia.

Ninafikri, upinzani ubadili mbinu ya mapambano na uendeshaji wa chama kuendana na hali iliyopo. Ni vema shughuli nyingi za chama zikahamishiwa kwenye ngazi ya chini, waliko wanachama.

Kwenye ngazi hii, wanachama wahamasishwe au wajipange kwenye ngazi ya kijiji au mtaa, au hata balozi. Shughuli za upinzani ziwe zinafanyika waliko wanachama wengi. Watu watakuwa jasiri sana kuendelea kukutana kuliko kuendelea kusubiri mikutano ya hadhara ambayo imepigwa maarufuku. Huu ni udhaifu kwetu.

Mkakati wa kuimarisha operasheni za chama kwenye ngazi ya chini uwe siasa za mbadala wa upinzani. Kwa maana tayari dola inawalenga viongozi wa kitaifa kutokana na ukweli kuwa nguvu za ushawishi na utendaji wa chama zipo kwenye ngazi ya kitaifa, kidogo na kanda. Hata wanachama wa kawaida wamejiweka pembeni wanaangalia viongozi wa kitaifa wanasema au wanafanya nini!

Sasa kupeleka operesheni za chama kwenye ngazi ya chini ni gharama. Rasilimali fedha na watu vinatakiwa kupelekwa huko pia. Ninapozungumzia fedha, ninazungumzia ruzuku ya chama, ipelekwe huko chini.

Ni gharama, lakini faida yake ni kubwa. Kwa mfano, wakubwa, wanaweza kuagiza vikao vya ndani vifanyike kwa wiki mara moja nchi nzima, ngazi ya tawi, halafu pawepo na usimamizi mzuri na yakinifu. Chama kitakuwa hai.

Mkakati namba mbili;

Ni kumweka mbele aliyekuwa mgombea Urais 2015, Edward Lowassa. Huyu  mzee, yale  mafuriko yake ya kwenye kampeni bado yako. Sasa asipokuwa mstari wa mbele, yale mafuriko yataishia mbali. Yatatengenezewa mifereji, ili yapungue au yafutike. Akae mbele maana ana mafuriko ya kutosha. Nguvu ya mwanasiasa kwa watawala ni kuwa na wafuasi wengi.

Mgombea urais aliyeshindwa kwa karibu, mara nyingi huwa anakuwa na agenda ya kuongoza na kuwanyima usingizi watawala. Kwanza, lazima atathimini sababu za kushindwa kwake, pili ni kuendeleza juhudi kuelekea kwenye uchaguzi mwingine. Katika mapambano yake anapambana kuondoa udhaifu iliomkosesha ushindi.

Hiki ndicho alichokifanya Raila Odinga baada ya kushindwa 2013. Alipogundua makamishena wa Tume ndio waliomwangusha, alianza mara moja harakati za  kupambana na hatimaye kuwango’a. Mwaka 2017 aliposhindwa, aliendeleza mapambano na baadaye kusalimu amri kwa kile alichodai ni masilahi ya Kenya.

Sasa hapa ujasiri unahitajika, sio ukimya kusubiri fadhila za watawala. Edward Lowassa afanye hata ziara ya kimataifa, ili yanayoendelea nchini yaangaziwe kimataifa.