Home Habari Ni kweli ukitaka mambo yakunyookee kumbatia CCM?

Ni kweli ukitaka mambo yakunyookee kumbatia CCM?

1799
0
SHARE

NA HILAL K SUED 

Ukitaka mambo yako yaende vyema ingia CCM. Kauli hii iliwahi kutolewa na si mwingine, bali aliyekuwa Waziri Mkuu wa Awamu ya Tatu kwenye mkutano mmoja wa hadhara katika Mkoa wa Singida.

Ni kauli iliyokuwa na ujumbe mahsusi, mzito na wenye dhamira makini, hasa hasa kwa wafanyabiashara na wengine wanaotafuta manufaa au ahueni fulani inayotokana na matatizo yao mbali mbali. Lakini pamoja na kauli yake hiyo, sasa hivi Sumaye hayuko tena CCM kwa miaka kadha sasa na haijulikani iwapo mambo yake yanamnyookea.

Nimetaja wafanyabiashara kwa sababu wakishafanikiwa katika biashara zao, hawa huwa wachangiaji wakubwa wa mapesa kwa chama hicho kikongwe – hasa wakati wa chaguzi.

Na baadhi yao walikuwa wanajua namna ya kuzirejesha fedha zao na hata kulimbikiza zaidi kutokana dili/zabuni wanazopewa serikalini ama kukwepa kodi bila kuulizwa sana.

Ilikuwa ukienda popote hapa nchini, katika miji mikubwa ya mikoa, au hata ile ya wilaya ilikuwa nadra sana kumkuta mfanyabiashara mkubwa katika wilaya fulani ambaye haikumbatii CCM. Nakiri kwamba walikuwapo wafanyabiashara wakubwa ambao siyo wafuasi wa CCM, lakini hawa ni wachache mno, na mara nyingi walikuwa hawajionyeshi.

Kwa wafanyabiashara kuwa wafuasi wa chama tawala siyo dhambi au jinai, kwani ni haki yao ya kikatiba – na bila shaka ni mambo ya kupita tu. Nasema hivi kwa sababu endapo chama hicho kitapoteza dola kwa kupokonywa na chama kingine, yumkini wafanyabiashara hao, baada ya muda, wangehamia chama hicho kingine bila taabu yoyote.

Huko Zambia kwa mfano, wafanyabiashara wengi wakubwa wakubwa waliokuwa wakikikumbatia chama cha UNIP wakati wa utawala wa Mzee Kenneth Kaunda, baadaye walikikumbatia kilichokuwa chama tawala cha MMD cha rais Frederick Chiluba na baadaye Rais Levy Mwanawasa.

Lakini hapa kwetu katika awamu hii ya utawala wa John Magufuli mambo hayo sasa yanabadilika kwani wafanyabiashara wengi wamejikuta wakigonga mwamba katika harakati zao hizo.

Kwa mfano wafanyabiashara wengi katika maeneo mbali mbali walijikuta wanakadiriwa upya kodi ya mapato na kutakiwa kulipa. Wengine hata kutiwa mbaroni na kufunguliwa mashitaka yakiwemo uhujumu uchumi, utakatishaji fedha, ukwepaji kodi n.k nk. Wakati katika Awamu iliyotangulia walikuwa hawaguswi. Kwa ufupi tu tulishuhudia baadhi ya wafanYIbiashara wakubwa wakifunga biashara zao pamoja na wao kuwa wafuasi wakubwa wa chama tawala.

Zabuni za serikali sasa hazipatikani kiurahisi kama ilivyokuwa na zile zilizotolewa katika awamu zilizopita zimekuwa zikipitiwa upya – mfano mikataba ya madini.

Aidha mbali na wafanyabiashara pia kuna wanasiasa vigogo ambao baadhi yao wanamiliki biashara na ambao baada ya uchaguzi uliopita walifukuzwa kutaka chama tawala kwa sababu walikuwa wanamshabikia na kumfanyia kampeni kigogo mmoja aliyehamia upinzani na kugombea urais kule.

Hatimaye wengi wa vigogo hawa waliohama na baadaye kufukuzwa waliomba msamaha na kurejea CCM – wengi wao bila shaka walijikuta wanaathirika kibiashara.

Lakini kama nilivyosema ingawa si jinai au dhambi kwa wafanyabiashara kukikumbatia chama tawala, maovu hutokea iwapo mahusiano yao yatakwenda kinyume cha taratibu halali zinazokubalika. Na matokeo yake ni kuzuka kwa ufisadi katika ngazi za juu, hali inayosababishwa na uhusiano wa karibu mno baina ya wakuu wa serikali na wafanyabiashara hao.

Kama nilivyotaja hapo juu kinachotokea ni ukwepaji wa kodi, zabuni zilizozidishwa bei, mikataba mibovu isiyo na masilahi kwa taifa na mengineyo mengi. Thibitisho ni ripoti za kila mwaka za CAG – za ukaguzi wa mahesabu ya serikali.

Lakini haya yote ingawa yalikuwapo tangu Awamu ya Kwanza, yaliongezeka kuanzia mfumo wa utawala wa vyama vingi ulioanza mwanzoni mwa miaka ya 90. Wakati wa enzi ya utawala wa chama kimoja wafanyabiashara wakubwa hawakuwa wanakitetemekea sana chama tawala, ingawa walitakiwa kuwa wanachama kwanza ili kupata liseni za biashara zao. Baadhi yao walikuwa wanakataa kutoa michango kwa chama wanapochangishwa, na chama au serikali havikuwa vinawafanya kitu chochote.

Lakini baadaye, katika hali ya ushindani – ushindani mkubwa wa kisiasa na wa kibiashara pia — hali ikawa tofauti sana kwani wafanyabiashara wakubwa wenyewe walikuwa wanaiendea CCM kuipa michango kwa matarajio ya kupata upendeleo fulani wa kibiashara kutoka serikalini ili waweze kuwapiku wafanyabiashara wenzao.

Na kwa upande wake, serikali ili ivipiku vyama vingine vya siasa katika kuwania uongozi wa dola, ilikuwa inaonyesha “makucha” yake kwa wafanyabiashara wakubwa ili wakichangie chama na kukiweka madarakani kwa manufaa ya pande zote mbili.   

Katika enzi za mfumo wa chama kimoja, ulazima wa kuwa mwanachama ulikuwapo hasa kwa baadhi ya watu wa kawaida tu – hususan wanafunzi wanaofukuzia masomo nchi za nje, na pengine kupandishwa vyeo kwa baadhi ya wafanyakazi wa serikalini na mashirika yake.

Lakini, kama nilivyosema hapo mbele, baadhi ya watu, mbali na wafanyabiashara, waliokuwa wakikikumbatia chama tawala hufanya hivyo kwa lengo maalum, kama vile kusaka manufaa au ahueni fulani inayotokana na matatizo yao mbali mbali.

Nitatoa mifano kwa matukio ya kweli yaliyotokea: Miaka kadha iliyopita, kuna kiongozi mmoja kutoka kimojawapo ya vyama vya michezo hapa nchini alifikishwa mahakamani akituhumiwa kutafuna fedha za chama hicho.

Baada ya kesi kusikilizwa ikaja siku ya hukumu, siku ambayo mshitakiwa alikuja mahakamani akivalia T-Shirt iliyoandikwa “CCM No 1.” Hakimu alimpata na hatia na akamhukumu kwenda jela. Tukio hilo liliwekwa vyema kwa njia ya katuni katika gazeti moja siku iliyofuata. Bila shaka alikuwa na sababu maalum ya kuvaa T-Shirt yenye maandishi yale – kujaribu kumyumbisha hakimu.

Mfano mwingine: Miaka kadha iliyopita kulikuwapo mpango wa kubomoa nyumba zilizokuwa za Shirika la Reli na zilizouzwa kwa baadhi ya wafanyakazi wake katika maeneo ya Kamata jijini Dar es Salaam ili kupisha ujenzi wa kituo cha mabasi ya Mradi wa Mwendokasi.

Baadhi ya wamiliki wa nyumba hizo walipinga hatua hiyo ya kubomolewa nyumba hizo ambazo walikuwa wameuziwa karibuni tu ingawa mamlaka husika ilitangaza kulipa fidia. Wananchi hao walijihamasisha katika umoja na kuandaa mkutano wa pamoja na viongozi wa halmashauri ya Jiji.

Katika mkutano huo baadhi ya wenye nyumba hizo waliosimama kuzungumza walikuwa wamevalia sare na kofia za kapelo zilizoandikwa “Chagua CCM.” Lengo lao ni kujaribu kuuyumbisha uamuzi wa serikali ambao tayari ulikuwa umeshatolewa.

Mifano hii miwili inaonyesha kwamba hakuna garantii katika ule ujumbe wa “Ukitaka mambo yako yaende vyema kumbatia CCM.” Zile nyumba hatimaye zilikua kubomolewa.

Na tukizungumzia sare katika vyama vya siasa, hakika chama tawala kinaongoza katika kuzihamasisha. Kwa mfano, hata katika shughuli ambazo moja kwa moja ni za kiserikali, utaona watu na makada wa CCM wakizivalia sare hizo. Rais anaporejea nchini kutoka safari za nje ya nchi baadhi ya wanaompokea huvaa sare za chama.

Kwa wenye kumbukumbu za historia, katika miaka ya 1930 baada ya chama cha Nazi cha Adolf Hitler kutwaa madaraka (kwa njia ya kidemokrasia) nchini Ujerumani, wafuasi wa chama hicho walikuwa wanavalia sare za chama hicho, sio katika shughuli za kichama tu, bali hata wakiwa katika shughuli zao. Na wakati huo, sare hizo ndizo zilikuja kuwa kinga kubwa ya kutobughudhiwa na vyombo vya usalama na vya kijasusi vya Hitler hasa katika kuwabaini wapinzani wake.

Siamini iwapo hali imefikia hivyo hapa kwetu, na inawezekana hata inaanza kuwa hasi kwa chama hicho, hasa katika kipindi hiki cha tuhuma mbali mbali za ufisadi zinazoelekezwa kwa baadhi ya viongozi wakuu wa serikali na wa chama tawala.

Wakati wa kampeni za uchaguzi mkuu uliopita wa 2015 iliripotiwa katika baadhi ya magazeti kwamba huko Mbeya, kuna baadhi ya makada wa CCM waliokuwa wamevalia sare za chama chao walizomewa na wananchi kwa kuwaita “Mafisadi hao!”