Home KIMATAIFA Ni lini Mungu aliwarejeshea Wayahudi Palestina?

Ni lini Mungu aliwarejeshea Wayahudi Palestina?

1388
0
SHARE

Na Joseph Mihangwa

KWA miongo saba mfululizo tangu kuundwa kwa Serikali ya Israeli mwaka 1948, Wapalestina na Wayahudi wamekuwa vitani kugombea haki ya kukalia nchi inayoitwa Palestina na mji wake mkuu, Yerusalem.

Kila upande unadai kuwa na haki hiyo. Kwa mujibu wa historia na kimsahafu wa kidini – Kurani kwa upande wa Wapalestina, na Biblia kwa Wayahudi, wakiita “nchi hii ni ya Ahadi” waliyopewa na Mungu kama Taifa.

Kimsingi na kihistoria, Wapalestina na Wayahudi, au Wayuda na Waislamu ni watu wa asili moja na utamaduni mmoja, wakijulikana kama “Watu wa Kitabu” au wana wa Ibrahim au Abraham ambapo misahafu yao wote si kingine bali Torati ya nabii Mussa ya Agano la Kale katika Biblia.

Wakati wa Kampeni kuwania nafasi ya kuongoza Israeli mwaka 2015, Waziri Mkuu wa nchi hiyo, Benjamin Netanyahu wa Chama cha LIKUD, aliweka wazi kuwa hataruhusu kamwe dola la Kipalestina kuundwa katika nchi hiyo.

Lakini tunapopitia maandiko ya misahafu kwa mitazamo huru isiyo na kihafidhina, hatushindwi kubaini utata juu ya uhalali unaopiganiwa kama ni kwa kutumia kigezo cha kimisahafu pekee, kutufanya tuone kuwa njia sahihi ya kumaliza mgogoro ni kwa historia kuachiwa kuwa mwamuzi pekee. Sasa endelea…

Hakuna ubishi kwamba Agano la Kale ni kitabu pekee kinachotukuza utaifa (nationalism) Israeli. Ni hadithi juu ya jinsi Mungu alivyoingia ubia na kikundi maalumu cha watu na kuchochea adhabu ya umwagaji damu kwa taifa la kigeni lililowatawala; kisha wakaongoza njia kwenda nchi ya Kaanani na kufanya makao huko baada ya kuwafukuza wenyeji na wengine kuwaua kikatili kwa “kibali” cha Mungu huyo.

Inaelezwa, Mungu alimwahidi Ibrahimu kutoa nchi kwa vizazi vyake, lakini tatizo hapa linakuwa ni kwa vizazi vya Ibrahim kuwa waumini wa Kristo.  Mtakatifu Paulo anasema: “Na kama ninyi ni wa Kristo, basi mmekuwa uzao wa Ibrahim, na warithi sawa sawa wa AHADI” (Gal. 3:29).  Kwanini hili liwe tatizo?.

Ni kwa sababu Wayahudi (hadi sasa) hawamtambui Yesu kama Kristo; hivyo, wao pia hawawezi kutambulika kama wa uzao wa Ibrahimu (kwa mujibu wa Biblia), na kwa hiyo hawana haki ya kuirithi Palestina.  Hiyo ndiyo hoja ya kwanza.

Hoja ya pili ni kwamba, dhana ya NCHI YA AHADI ni ya asili ya kiroho, na sio ya Kijografia.Lakini potelea mbali, hebu tuchukulie ule mtazamo [potofu] wa Kiyahudi kwamba dhana hiyo ni ya kijografia.Hapa, lazima tutamke ule ukweli kwamba, zawadi ya nchi hiyo kwaWaisraeli ilikuwa kwa sharti kwamba watakuwa waaminifu kwa AGANO; lakini tunaambiwa hawakuwa hivyo, badala yake walimwasi Mungu wao, wakaanza kuabudu miungu na sanamu kiasi cha kuwatoa watoto wao sadaka ya binadamu (Wafalme 16:30-34).

Kwa sababu hii Mungu alitengua Agano hili la kwanza na Wayahudi na kutangaza Agano jipya kwa watu wote ambalo halikuwa na ahadi ya Nchi.  Kwa hiyo ahadi ya Mungu kwa Wayahudi ilikuwa kwa sharti ambalo hawakulitekeleza.

Ukweli, Musa aliwaambia Wayahudi kwamba kwa kushindwa kwao kumcha Bwana, aliwaongezea mapigo na magonjwa mazito ya kudumu na hali duni ya kijamii sawa na ile waliyokuwa nayo utumwani Misri. Wataendelea nahali hii hadi watakapoangamizwa; watapukutika na kusalia wachache kwa kuwa hawakusikia sauti ya Bwana Mungu wao, na watanyakuliwa (watatolewa) katika nchi hiyo (Kanaani) waingiayo kuimiliki (Torati 28: 58-63).

Mungu alikasirishwa na utovu huu kwa Agano na kutamka kwa mdomo wa Isaya: “Sikieni, enyi mbingu, tega sikio, Ee nchi, kwa maana Bwana amenena; Nimewalisha watoto (Wayahudi) na kuwalea, nao wameniasi. Ng’ombe amjua bwana wake, na punda ajua kibanda cha bwana wake; bali Israeli hajui, watu wangu hawafikiri. Ole wake, taifa lenye dhambi, watu wanachukua mzigo wa uovu, wazao wa watenda mabaya, wamemwacha Bwana, wamemdharau yeye aliye Mtakatifu wa Israeli, wamefarakana naye na kurudi nyuma” (Isaya 1:1-4).

Baada ya Mungu wa Israeli kuwaondolea Waisraeli hao haki na uhalali wa kuikalia Palestina, alihakikisha harudii tena kosa la kuwapa nchi “taifa” hili.  Alibatilisha Agano la kwanza na kutoa Agano jipya ambalo halikutoa haki ya kumiliki nchi: “Angalia, siku zinakuja, nitakapofanya Agano jipya na nyumba ya Israeli, (na safari hii pia) na nyumba ya Yuda. Si kwa mfano wa Agano lile nililolifanya na baba zao, ambalo walilivunja, ……bali nitatia Sheria yangu ndani yao, na katika mioyo yao nitaiandika; nami nitakuwa Mungu wao, nao watakuwa watu wangu (Yeremia 31: 31-33).

Katika Agano hili jipya, Mungu hakutoa nchi ya kijiografia kwa Wayahudi, badala yake alijitoa mwenyewe. Maana nyingine ni kwamba, kwa Agano hili jipya Mungu aliwanyang’anya Wayahudi nchi ya Palestina, wakapoteza haki ya kuikalia.

Kwa ukweli huu, Wayahudi wanapata wapi haki ya kuikalia Palestina kwa makeke na mabavu?  Uko wapi ushahidi wa Kibiblia kuhalalisha yote hayo?  Mnaotukuza Uzayuni na “Mungu” wa Israeli, tuambieni.

Kinachosumbua hapa si “uteule” wa Kimungu wa Wayahudi wa kuikalia Palestina, bali ni ubeberu wa Kiyahudi kwa jina la dini ya Uyuda katika kujaribu kuhalalisha ubeberu huo.  Ilikuwaje?.

Kwa karne nyingi, kabila la Wayahudi (sio taifa) limeshikilia ndoto ya kujitanua kiutamaduni na kiimani kwa kutumia Sheria zao za kale lionekane taifa “tukufu, imara na lisiloweza kuchanganyikana na mataifa mengine.  Wayahudi wanaunganishwa na imani ya dini yao asilia ya Uyuda (Judaism).

Kwa Wayahudi, kazi kuu ya Uyuda ni pamoja na kuimarisha na kuendeleza kwa vitendo maadili ya jamii ya Wayahudi wa kale kwa manufaa ya kabila lao wakiongozwa na Mungu mwenye wivu aitwaye – “Yahweh”.Mungu huyo, mkali na mpenda vita, hapendi kabila lake lichanganyike na makabila mengine, wala hapendi Wayahudi wapanue mipaka ya himaya yao na kuchanganyika na wengine, wasije wakapata “unajisi”.

Wayahudi wanahimizwa kutambua kwa macho na masikio wazi, mafanikio na nguvu ya maadili yao ya kale, kama yalivyoandikwa katika Biblia yao ya Kiebrania kama msahafu wao mkuu. Wanatakiwa kuzingatia pia kwamba mafanikio hayo yanawapa Wayahudi wote haki na nafasi muhimu katika historia ya ustaarabu wa ulimwengu dhidi ya wengine.

Ni kwa mtazamo huu mkali kwamba, licha ya uchache wao, wameweza kuiunganisha falsafa ya Uyuda na utawala wa Serikali ya Israeli vikawa kitu kimoja, chini ya itikadi ya Uzayuni (Zionism).  Itikadi hii ni sawa na iliyokuwa ya Makaburu wa Afrika Kusini, iliyoshamirisha ubaguzi wa rangi kabla ya uhuru wa nchi hiyo.

Hakuna kipindi chochote Wayahudi wamewahi kuitwa taifa.  Kwa karne zote mbili za mwisho, Wayahudi wamechukuliwa kuwa kama kabila tu, lenye kuzungumza lugha moja; wala hawajawahi kuwa sehemu ya ustaarabu wa Kimagharibi.Ustaarabu wao (Uyuda) ni wa kipekee na wa aina yake, unaozingatia “maono” ya kidini ukikua na kuendelea kupitia Sheria zisizoandikwa (Oral Law). Lugha ya Uyuda ni Kiebrania.

Uyuda umejengeka katika misingi ya Kibaguzi wa Kijamii ambao ni ubaguzi wa kikabila.  Haya tunayosoma katika msahafu wao, kwamba wakati wakiingia katika nchi ya Palestina, waliagizwa (na Mungu wao wa Kiyahudi) kuwafukuza mataifa yote saba yaliyokuwa wakazi asili wa nchi hiyo, na Mungu wao akaagiza wana wao na mabinti zao wasioeau kuolewa na watoto wa mataifa hayo eti wasije wakaharibu mbegu na utamaduni wao (Kutoka 34: 16).

Ni kutokana na ubaguzi huu kwamba, tofauti na Ukristo au Ubudha, dini ya Uyuda (udaism) haiwanii kupata au kuingiza waumini zaidi mbali na Wayahudi wenyewe.  Ni kutokana na ubaguzi wa aina hii kwamba Wayahudi hawataki kukaa pamoja na Wapalestina.  Na hiki ndicho chanzo cha vita isiyokwisha kwa nchi hizo mbili.

Wayahudi hawalitambui Agano jipya lililowanyang’anya Palestina linalohubiri juu ya Mungu mmoja kwa wanadamu na kwa mataifa yote.  Wala hawamtambui Yesu kama mkombozi (Masiya) aliyetumwa na Mungu; na kwamba tofauti na imani ya Kikristo, wao bado wanasubiri kuja kwa Masiya (Mkombozi) wao.

Ndiyo maana walipobaini kwamba Yesu anaitwa au kujiita “Masiya”  hawakuchelewa kumuua kwa kosa la kujifanya mwana wa Yahweh, Mungu wao.

Kwa hiyo, katika historia nzima ya Wayahudi hofu yao sio juu ya vita ya ana kwa ana na makabila mengine, bali hofu ni juu ya kuchanganyika na makabila mengine na kuharibu utamaduni wao wa asili na hiyo “dini” ya Uyuda.

Ndiyo maana katika miaka ya 1970, Israeli ilianzisha mpango wa “Operesheni Musa” ya kuwatafuta Wayahudi mahali pote walikokuwa  duniani ili warejee makwao.  Waliorejeshwa ni pamoja na Mafalasha (weusi) wa Ethiopia wenye asili ya Kiyahudi. 

Pamoja na ubaguzi wanaouendeleza nchini Palestina, Wayahudi hawatulii, wametawanyika duniani kote.  Kwao, hao ndio wanaoitwa “kondoo wa nyumba ya Israeli waliopotea”; ndio wanaohofiwa kupoteza utamaduni wa taifa lao;  wako Marekani, Urusi, Ujerumani, na ni rasilimali kubwa kwa mambo mengi katika nchi hizo, kwa kuwa ni wabunifu.

Lakini pamoja na hayo jeuri ya Israeli haipimwi kwa idadi yao nyumbani, na ni watu wa ajabu sana.  Kwa kupitia dini yao ya Uyuda hawaamini kushindwa kitu, na kwamba kutawanyika kwao hakuathiri nguvu ya wachache wanaosalia nyumbani katika kulinda hadhi yao, tangu kale hadi sasa.  Hawa wenye msimamo mkali wa Uyuda ndio wanaoitwa “mabaki ya Israeli” (Isaya 10: 20–21). Hapa ndipo kiburi cha Wayahudi kilipojikita kwa kupewa nguvu na Uyuda ambao wao huuita ni “Sayansi ya uhai”; uhai kwa sababu ndiyo inayowapa ari na nguvu ya kupambana na tamaduni zingine za dunia, licha ya uchache wao.

Kwa mfano, mwishoni mwa karne ya 17, Wayahudi walifikia idadi ya milioni moja tu, lakini dhana ya kidini ya Uyuda ilijidhihirisha wazi duniani kote.  Na miaka ya 1940, ustaarabu wa Magharibi ulianza kuwakumba na kuwageuza baadhi ya Wayahudi, lakini wao, kama alivyo Kanga, ambaye hatagi ugenini, hawazoei mahali wakasahau utamaduni na dini yao.

Kwa mfano, karibu vyama vyote vya kimapinduzi nchini Urusi viliwahi kuingiliwana kuongozwa na wanaharakati wenye asili ya Kiyahudi kwa mshangao wa wengi kwa jinsi ilivyotokea; na ndivyo ilivyokuwa kwa nchi za Ulaya ya Kati na Marekani, kiasi kwamba dhana ya “Uyuda wa Kisasa” (Reformed Judaism) ilianza kuzitikisa nchi hizo.

Huko Ujerumani, itikadi ya Uyuda wa Kijerumani uliokarabatiwa (Germany Reformed Judaism) ya karne ya 19, ilitikisa nchi hiyo kwa kuhubiri kwamba taifa la Ujerumani lilipashwa kuongozwa na imani kuu tatu zenye hadhi na uhalali ulio sawa: imani ya Kiprotestanti, Ukatoliki na Uyuda wa Kiyahudi (The Mosaic Persuasion). Huo ndio ulikuwa mwanzo wa ngamia kuingiza kichwa katika hema.

Kwa hili, Wayahudi waliamini wangeweza kuendeleza utamaduni na utaifa wao ugenini. Ni kutokana na “utukutu” huu wao katika nchi za kigeni kwamba, dikteta Adolf Hitler,aliwastukia Wayahudi na kustuka; aliamua kuwachoma katika matanuru ya moto kama hatua ya kuliangamiza kabila hilo.Wayahudi milioni sita waliangamizwa nchini Ujerumani pekee.

Chuki dhidi ya Wayahudi miongoni mwa jamii ya kimataifa ingali ikiendelea hadi leo.  Wakati wa ziara yake nchini Italia mapema mwezi Novemba 2003; Waziri Mkuu wa Israeli Ariel Sharon, aliwataka Wayahudi wote waishio Italia warejee nchini mwao kwa kile alichodai “kuepuka mashambulizi yanayolenga kuwamaliza sehemu mbali mbali duniani”.

Huku akinukuu vifungu kutoka katika Biblia ya Kiyahudi inayozingatia Agano la kale kuonyesha uteule wa Mungu kwa Wayahudi, Sharon alisema, “Sote ni mashahidi wa jinsi tunavyosakwa; na sasa hivi kuna mpango wa kueneza chuki dhidi ya Wayahudi ambao ni mabaki ya Israeli” (Soma pia Isaya 10: 20-21 na Torati 28: 58 – 63) kumwelewa Sharon.

Ni dhahiri kwamba dhana ya “Nchi ya ahadi” ni batili, na kwamba msamiati huo una lengo pekee la kuficha na kuendeleza ubeberu wa Kiyahudi nchini Palestina kwa jina la dini.

Kufikia hapo tujiulize: Je, mgogoro wa Palestina unaweza kutatuliwa kwa njia za kidini?  Je, inawezekana kuwageuza Wayahudi waamini kwamba hakuna “Nchi ya Ahadi” kwao, na Palestina ni ya Wapalestina wenyewe?.

Kama mgogoro huu hauwezi kutatuliwa kidini je, tunaweza kupata ufumbuzi kwa kuitumia jumuiya ya kimataifa?  Nini kitakachofuata au kutokea?.

Hatudhani kwamba mgogoro wa Palestina utaweza kutatuliwa kwa njia za kidini pekee.  Nani ataifanya kazi hiyo?  Kwa Wayahudi kutolitambua “Agano Jipya” na mwakilishi wa Agano hilo, Yesu, ina maana kwamba dhana ya Nchi ya Ahadi haijafutika wala haiwezi kufutika katika imani zao.  Kwa hiyo ni kazi bure kuwahubiri kinyume cha hilo.

Yesu mwenyewe alijaribu, akashindwa, wakamuua; sembuse binadamu hohe hahe kama sisi?  Ilikuwaje?  Yesu alihubiri kwa kuwataka Wayahudi waachane na ubaguzi wao na wamwone Mungu kama baba mwema anayejali kwa usawa watu wa mataifa yote.  Watu wengine walimwelewa lakini sio Wayahudi, waliomkashifu na kumbeza.

Kwa Wayahudi hawa wenye mioyo migumu na wasiosikia la mtu nje ya Uyuda wao, alisema: “Nawaambieni, wengi watakuja kutoka Mashariki na Magharibi kuja kushereheka na Ibrahimu, Isaka na Yakobo katika ufalme wa mbingu.  Lakini waliozaliwa katika ufalme (Wayahudi) watatupwa nje katika giza, ambapo ni mahali pa kulia na kusaga meno”. Ni dhahiri kwamba hapawezi kuwa na mwafaka kwa njia ya Kidini kuhusu suala la Wapalestina na Wayahudi.

Mipaka ya mataifa ya leo haikuwekwa na Wazalendo wa Mataifa hayo, bali ni matokeo ya Ukoloni mkongwe wa mataifa makubwa  yaliyokuwa yakipanua himaya zao, ikiwamo mipaka ya Taifa jipya la Israeli iliyowekwa na Waingereza, kisha kuthibitishwa na kuridhiwa na Umoja wa Mataifa kwa maazimio na Mikataba mbali mbali.

Mipaka hii inatambuliwa na kuheshimiwa popote duniani kuliko mipaka mingine yoyote. Mfano, hapo kale Mpaka wa Tanganyika ulijumuisha nchi za Rwanda na Burundi kama Koloni la Wajerumani kwa jina Deuscht Ostafrika, ya Afrika Mashariki ya Wadachi.

Lakini baada ya Vita ya Kwanza ya Dunia ya mwaka 1914-18 ambapo Wajerumani walishindwa na Tanganyika kutawaliwa na Waingereza chini ya udhamini wa Mataifa, Rwanda na Burundi walipewa Wabelgiji kwa maelewano ya Mataifa makubwa chini ya Mkataba wa Heligoland Treaty na mambo yako shwari.

Inavyotokea huko Palestina, kama na sisi tungeamka leo, kwa kuongozwa na mizimu ya mababu zetu na kwa jina la Mungu Mkuu, Mlungu, Seba au Katonda kwa majina yake mengi, tukadai kurejeshewa Rwanda na Burundi amani ingetoka wapi dunia hii ya leo bila kuheshimu mipaka ya Wakoloni?.

Yafaa Wayahudi na Wapalestina nao washauriwe kuheshimu mipaka hiyo, wapendane kama binadamu badala ya kupigia kelele dunia kwa mihemko ya Kitheolojia isiyokita kwa wote.