Home Makala Kimataifa Ni miaka 100 sasa tangu kumalizika Vita Kuu ya Kwanza ya Dunia

Ni miaka 100 sasa tangu kumalizika Vita Kuu ya Kwanza ya Dunia

2681
0
SHARE

NA HILAL K SUED

Jumapili iliyopita, Novemba 11 2018 ilitimia karne moja (miaka mia moja kamili) tangu Vita Kuu ya Kwanza (1914-18) kumalizika kule Ulaya ambapo majeshi ya Ujerumani ya Mfalme (Kaiser) Wilhelm II yaliposalimu amri kwa yale ya washirika (Allies) wa Marekani, Uingereza, Ufaransa, Ubelgiji na nchi nyingine za Ulaya.

Viongozi wakuu wa mataifa hayo wiki iliyopita walikusanyika katika maeneo mbali mbali yenye alama za kumbukumbu huko Ulaya katika maadhimisho hayo.

Tukio la kusalimu amri kwa Ujerumani ndilo liliipokonya Ujerumani makoloni yake katika Bara la Afrika ikiwemo nchi yetu kwa sasa inayoitwa Tanzania – (wakati huo ikiitwa Germna East Afrika au Deutsch Ostafrika).

Nchi nyingine ni Namibia (South West Africa), Cameroon na Togo iliyoko Afrika ya Magharibi. Baada ya kupokonywa eneo hili likapewa waingereza kuitawala chini ya udhamini wa Muungano wa Kimataifa (League of Nations) na walilipa jina Tanganyika.

Kwa nje ya Ulaya nchi yetu ndiyo ilihusika pakubwa katika Vita hiyo ya Kwanza ya Dunia kwani ilikuwa uwanja wa mapambano makali baina ya majeshi ya nchi tatu za kikoloni – Ujerumani na Uingereza na Ubeligiji, ingawa wazalendo ndiyo walikuwa sehemu kubwa sana ya askari na wafanyakazi wengine katika majeshi ya wakoloni hao. Huku kwetu vita hiyo ilimalizika rasmi Novemba 25 1918.

Baada tu ya vita hiyo kuzuka Ulaya Uingereza ilijiona haiko salama katika makoloni yake Afrika ya Mashariki, hususan Kenya, na pia Rhodesia (sasa Zimbabwe na Zambia na Nyasaland (sasa Malawi). Ilifanya matayarisho kulishambulia kivita koloni hili sambamba na mashambulizi dhidi ya Ujerumani kule Ulaya.

Kwa upande huu wa dunia vita hiyo ilijumuisha milolongo ya mapambano (battles), mengine yakiwa ya kuvizia (guerrilla) ambayo yalienea maeneo mengi ya nchi hii hadi Msumbiji (lililokouwa koloni la Wareno), Uganda na Congo (lilikowa koloni la Ubelgiji).

Inadaiwa lengo kuu la majeshi ya Ujerumani hapa yaliyoongozwa na kamanda machachari Luteni Kanali Paul von Lettow-Vorbeck ni kuhamisha nguvu ya majeshi ya muungano (allied forces) kutoka Ulaya kuja Afrika. Hata hivyo lengo hili lilipata matokeo tofauti kwani baada ya 1916, majeshi ya Vorbeck yalifurushwa kutoka nchi hii wakati ambao majeshi ya Muungano yalpata askari wengi wa asili ya Afrika ya Kusini, India na kutoka makoloni mengine.

Hata hivyo Wajerumani katika eneo hili walipigana kwa kipindi chote cha vita na walipata habari ya kusalimu amri kule Ulaya Novemba 14 1918, siku tatu baada ya Wajerumani kusalimu amri kule Ulaya.

Pande zote mbili ilibidi zisubiri uthibitisho wa habari hizo na hatimaye, tarehe 25 Novemba 1918 mkataba rasmi wa kuacha mapigano ulitiwa saini katika mji wa Chambeshi, karibu na mji wa Abercorn (sasa Mbala) Rhodesia ya Kaskazini (sasa Zambia) baina ya wawakilishi wa utawala wa ukoloni wa Waingereza wa Rhodesia na maafisa wa kijeshi wa Ujerumani akiwemo Lettow Vorbeck. Sehemu hiyo ya Zambia ndipo majeshi ya Ujerumani yalipofikia baada ya kukimbizwa na yale ya Uingereza.

Vita hii ilikuwa ya wazi zaidi, na matumizi ya mahandaki hayakuwa ya kiwango kikubwa kama ilivyokuwa kule Ulaya. Pande zote mbili zilivamia vijiji kwa ajili ya vifaa na vyakula na hapo hapo kuandikisha raia wenyeji kama askari. Sehemu kubwa ya wenyeji hawa walioandikishwa walipewa kazi ya upagazi – yaani wabebaji wa vifaa vya kijeshi na vyakula kwa ajili ya askari wapiganaji.

Wengi wao walikufa zaidi kutokana na kupata mlo kidogo, uchovu na maradhi kama vile malaria na malale kuliko kwa risasi. Sehemu nyingi za nchi zilipokonywa vijana wake na wanawake pia (wanawake ni kwa ajili ya ‘kuwahudumia’ askari na wapagazi hao).

Inadaiwa kwa kipindi chote cha miaka minne ya Vita takriban wapagazi milioni moja waliajiriwa kwa pande zote mbili kati yao zaidi ya 100,000 walikufa. Wanahistoria wanasema idadi hiyo ni ndogo sana – na kwa ujumla haijulikani ni wazalendo wangapi walikufa katika vita via hiyo.

Aidha ikumbukwe kwamba hapa nchini vita hii ilikuja miaka saba tu baada ya vita kuu nyingine, Vita ya Maji Maji – mapambano ya wazalendo dhidi ya ukoloni wa Kijerumani.

Kama ilivyotajwa hapo mbele majeshi ya Waingereza yaliundwa na askari kutoka makoloni yake mbali mbali wakati huo – kama vile Kenya, Ghana, Nigeria, West Indies, na Afrika ya Kusini na idadi yake ilifikia 150,000. Kwa upande Wajerumani idadi ya askari ilikuwa 25,000.

Aidha, tofauti na askari wageni, hakuna makaburi rasmi ya askari wazalendo pamoja na wapagazi yanayuoonekana. Vilivyoachwa nyuma baada ya kumalizika vita 1918 ni majengo makubwa makubwa ya wakoloni wa Kijerumani, hospitali moja Tanga, stesheni ya reli ya Kigoma, Mwanza na sehemu nyingine na miundo mbinu mingine kama vile Reli ya Kati walioijenga kuanzia 1908 hadi 1914 vita ilipoanza.

Kikubwa mtu atakigundua kwenye miundombinu hii pamoja na majengo ni kwamba yalijengwa ili yadumu muda mrefu. Na kweli imekuwa hivyo. Kama vile Waingereza baada yao, Wajerumani walidhamiria kujichimbia nchini kwa muda mrefu sana.

Vinginevyo ni alama chache sana zilizosalia zinazoonyesha kulipiganwa vita kubwa hapa nchini. Kwa mfano kuna makaburi ya askari wa kigeni waliokufa vitani Dar es Salaam, Tanga, Morogoro na sehemu nyingine.

Aidha kuna mnara maarufu jijini Dar es Salaam – Mnara wa Askari (Askari Monument) ambao ni kumbukumbu ya vikosi vya askari waliokuwa wabeba zana za kivita wa majeshi ya Uingereza (Carriers Corps).

Maeneo mengine kulikokuwa mapambano ni maeneo ya kusini mwa Tanzania pale askari wa Ujerumani walipokuwa wanayakimbia majeshi ya Uingereza hadi ndani ya nchi ya Msumbiji iliyokuwa ikitawaliwa na Wareno. Kwa mfano ni vigumu kupata kumbukumbu yoyote au alama kuonyesha kulikuwapo vita.

Hata sehemu iitwayo Mahiwa kulipotokea mapambano makubwa na ambako vifo vilifikia maelefu kwa kipindi cha siku tatu tu hakuna alama yoyote kuonyesha hili lilitokea miaka 100 iliyopita.

Kuna kanisa moja ambalo lilikuwa ni Misheni ya Kikiristo. Makanisa yalikuwa yakitunza kumbukumbu ya maisha ya watu kila siku na kabla ya kuanza vita – yaliandika wanavijiji kuuza mifugo yao ili wapate fedha za kutosha kuwawezesha kuikimbia vita, na pia zilionyesha idadi ya wanafunzi mashuleni ikiteremka.

Na katika sehemu ya Mto Rufiji unapoingia Bahari ya Hindi bado yako mabaki ya meli ya kivita SMS Konigsberg ambayo ilikuwa meli kubwa ya kivita katika eneo hili la dunia wakati wa vita ile ambayo nayo yanaweza kuwa kivutio cha watalii kutoka nje katika kipindi cha maadhimisho ya miaka 100 tangu kumalizika kwa Vita Kuu ya Kwanza.

Meli hilyo ilifichwa na Wajerumani kuogopa kushambuliwa na Waingereza, ingawa baadaye meli za kivita za Uingereza ziliigundua ikiwa mafichoni na kuizamisha kwa makombora mwaka 1915.

Mbali na meli hiyo kuna meli nyingine ya kivita ya Wajerumani iliyokuwa ikiitwa SMS Graf von Gotzen katika Ziwa Tanganyika ambayo pia Wajerumani waliizamisha kwa hofu ya kutekwa na Waingereza.

Lakini baada ya Wajerumani kuondoka, Waingereza waliinua na kuifanya kuwa meli ya kubeba abiria na wakaipa jina la MV Liemba.

Bila ya kuwepo kwa mabaki haya machache ingekuwa vigumu kumaminisha mtu yoyote sasa hivi kwamba kulikuwapo vita kubwa hapa nchini karne moja iliyopita. Mabaki haya ni nadra sana huzungumzwa au kuchochea shauku ya kutaka kujua kwa watu wa kizazi hiki humu Tanzania, na mara nyingi hutumiwa na watu wa Ulaya wanaokuja kama watalii na kadhalika. Kwa Watanzania wengi mabaki haya si minara ya kumbukumbu, bali ni alama ya ukoloni wa zamani.

Nchi jirani yetu ya Kenya wana maono tofauti kidogo. Ni kweli mapambano makubwa baina ya Uingereza na Ujerumani yalifanyika katika ardhi yetu na siyo Kenya, lakini Kenya wametupiku katika kutumia vita hiyo ya kihistoria kwa kujinufaisha kiutalii.

Ukilinganisha na Tanzania, Kenya wana eneo moja tu la vita – pale ambapo pambano kubwa na la kwanza la vita hiyo lilifanyika – maeneo ya Taita-Taveta karibu na Mbuga ya Wanyama ya Tsavo ambako kwa miezxi kadha nyuma wenzetu wamekuwa katika matayarisho ya kuweka vivutio vya kitalii kwa ajili ya kukaribisha maadhimisho ya kumalizika kwa Vita ya Kwanza ya Dunia katika eneo hili la Afrika.

Vivutio hivyo ni pamoja na Mwashoti Hill – sehemu iliyokuwa ngome ya vikosi vya Waingereza na pia makaburi ya pamoja ya askari wa Ujerumani na Waingereza. Aidha kampuni moja ya hoteli – Saravo Hotels Ltd imejenga mnara mpya katika eneo hilo kama kumbukumbu ya askari wa Kiafrika waliokufa wakiwapigania Waingereza.

Sehemu nyingine ambayo wenzetu Kenya wanaifanya kuwa kivutio cha utalii ni reli ya kutoka Voi hadi Taveta mpakani mwa Tanzania ambayo Waingereza waliijenga kwa madhumuni ya ya kupamnana na Wajerumani waliokuwa wamejichimbia katika Vilima vya Salaita (Salaita Hills).