Home Makala Kimataifa NI NANI HUYU GRACE MARUFU MUGABE?

NI NANI HUYU GRACE MARUFU MUGABE?

796
0
SHARE

NA MWANDISHI WETU

Madai ya mwanamtindo raia wa Afrika ya Kusini, Gabriella Engels ya kushambuliwa na kuumizwa na mke wa rais wa Zimbabwe, Grace Mugabe yameibua maswali mazito kuhusu tabia na mwenendo wa mke huyo wa rais ambaye anatazamwa kama ni mrithi wa mme wake, Rais Robert Mugabe mwenye umri wa miaka 93.

Rais Mugabe na mkewe Grace walirejea nchini mwao Juimapili iliyopita baada ya kuhudhuria mkutano wa wakuu wa nchi za SADC nchini Afrika ya Kusini. Walirejea nchini mwao baada ya Grace kupewa kinga ya kidiplomasia  pamoja na kuwapo kundi moja la wanasheria na waandamanaji wengine wakitaka Grace Mugabe asipewe kinga ya kidemokrasia na hivyo afikishwe mahakamani kujibu tuhuma za kushambuloa na kuumiza.

KILICHOTOKEA

Gabriella Engels mwenye umri wa miaka 21 alidai kwamba Grace Mugabe (52) alimshambulia kwa kutumia kifaa cha kuunganishia umeme (extension cord) katika chumba kimoja cha hotel ya anasa mjini Johannesburg Agosti 13.

Gabriella anadai alikuwa kwenye chumba cha hoteli hiyo na marafiki zake wawili – watoto wawili wa kiume wa Mugabe na ghafla Grace alitinga chumbani humo na kuanza kumshambulia. Picha zilizosambazwa kwenye mitandao ya jamii zilimuonesha Gabriella akiwa na jeraha la damu mbele kichwani kwake, jeraha alilodai lilitokana na shambulio hilo.

Hata hivyo si Grace wala mumewe Rais Mugabe wamelizungumzia suala hilo ingawa kuna habari kwamba Grace alimtwanga mwanamtindo huyo huyo katika harakati za kujikinga (self defence). Inadaiwa kwamba hata watoto hao wawili wa Grace nao walikula kichapo kutoka kwa mama yao.

Kwa upande wake Gabriella aliliambia shirika la habari la AFP kwamba anataka Grace atupwe gerezani kutokana na kile alichomfanyia.

Tukio hili si la mara ya kwanza kwa Grace Mugabe kuhusika katika tuhuma za kushambulia hasa akiwa safarini nchi za nje. Mwaka 2009 akiwa Hong Kong, mpiga picha mmoja alimtuhumu kwa kumpa kichapo. Lakini tukio hili la sasa hivi limechukua mkondo wa kisiasa.

Nchini Afrika ya Kusini chama kikuu cha upinzani cha Democratic Alliance (DA) kilimuonya Rais Jacob Zuma na utawala wake kutomruhusu Grace Mugabe kuondoka nchini. Na wanasheria wa mwanamtindo huyo walisema watakwenda mahakamani kupinga hatua ya serikali ya kumpa kinga ya kidiplomasia Grace Mugabe kwani hastahili kupata kinga hiyo.

Hata hivyo kinga hiyo ilitolewa na kusainiwa na Waziri wa Mambo ya Nje wa Afrika ya Kusini Maite Nkoana-Mashabane, ambaye alisema amefanya hivyo “kuzingatia masilahi ya Afrika ya Kusini katika kutambua kinga na haki za Rais Mugabe.”

Lakini utolewaji wa kinga hiyo uliashiria kubadilisha hatua za awali za mamlaka za Polisi za Afrika ya Kusini. Wiki iliyopita polisi nchini humo walisema tayari walikuwa wameshatoa tahadhari katika vituo vya mpakani kwamba Grace Mugabe akamatwe iwapoa asingejisalimisha mwenyewe.

Peter Granitz, msemaji mkuu wa jeshi hilo alisema “kwa kuwa Grace siyo mkuu wa nchi, mwanadiplomasia au waziri wa serikali, hawezi kuwa na kinga ya kidiplomasia.”

Willie Spies mwakilishi wa masuala ya sheria wa kikundi cha AfriForum, taasisi inayowakilisha jamii ya Makaburu alisema ingawa Grace Mugabe ameondoka Afrika ya Kusini, lakini harakati za kisheria wanazochukua zitamuweka katika hali ngumu ya kuja tena Afrika ya Kusini siku za baadaye.

NANI HUYU GRACE MUGABE?

Grace Mugabe ni mzaliwa wa Afrika ya Kusini na ni mke wa rais mwenye umri mkubwa zaidi duniani – Robert Mugabe. Wazazi wake waliishi Afrika ya Kusini hadi 1970.

Mme wake wa kwanza, Stanley Goreraza, ni rubani wa ndege za kivita, na sasa ni mwambata wa kijeshi katika ubalozi wa Zimbabwe nchini China. Alizaa naye mtoto mmoja wa kiume, Russel Goreraza mwaka 1984.

Akiwa kama katibu wa Rais Mugabe, Grace alikuwa na uhusiano wa kimapenzi na kiongozi huyo wa nchi wakati akiwa bado ndani ya ndoa yake ya awali. Alizaa naye watoto wawili Bona na Peter. Uhusiano wao wa kimapenzi ulianza hata kabla ya kufariki kwa mke wake wa kwanza Sally Hayfron mwaka 1992. Sally alikuwa mzaliwa wa Ghana.

Mwaka 1996 Grace na Mugabe walifunga ndoa katika hafla na misa kubwa iliyopachikwa jina ‘Ndoa ya Karne.” Mwaka 1997 Grace alimzalia Mugabe mtoto wa tatu, Chatunga.

Mwaka 2014 Grace alitunukiwa Udaktari katika fani ya jamii (doctorate in sociology) na Chuo Kikuu cha Zimbabwe. Shahada hiyo aliipata miezi miwili tu baada ya kujisajili chuoni hapo na bila hata ya kuandika andiko lake la mtihani (dissertation). Shahada hiyo ililalamikiwa sana kuwa ilikuwa feki.

MATANUZI NA KASHFA MBALI MBALI

Grace Mugabe amepigwa marufuku kusafiri nchi za umoja wa Ulaya na Marekani kutokana na mahusiano yake katika utawala wa Mugabe. Wakati anapigwa marufuku hiyo nchi za EU zilisema itasaidia kusitisha safari zake za matanuzi kutokana na umasikini wa wananchi wengi nchini mwake

Mwaka 2010 Mtandao wa Wikileaks uliibua tuhuma zilizikuwa zimetoka awali kwamba maafisa wa ngazi za juu wa serikali ya Zimbabwe na washiriki wao wa kibiashara akiwemo Grace Mugabe walikuwa wanatengeneza mamilioni ya Dola za Kimarekani kutokana na biashara ya almasi kutoka mgodi wa Chiadzwa mashariki mwa Zimbabwe.

Grace alifungua kesi dhidi ya gazeti moja nchini humo – The Standarad kwa kuripoti habari za Wikileaks zilizomhusisha katika kashfa hiyo na anadai fidia ya Dola 15 milioni.

Gazeti la Uingereza la The Telegraph liliandika kwamba katika moja ya safari zake za matanuzi Paris mwaka 2003, Ufaransa Grace alitumia Dola za Kimarekani 120,000 katika manunuzi ya muda mfupi mjini humo. Na mwaka 2004 alidaiwa kutoa Pauni za Uingereza muilioni 5 kutoka Benki Kuu ya Zimbabwe.

Ingawa Grace amekuwa akituhumiwa kwa safari zake za matanuzi na pia lile suala la shahada yake ya PhD aliyoipata kwa njia za mashaka mashaka, ameweza kujijengea umaarufu mkubwa wa kisiasa kutokana na shughuli zake nyingi za kijamii na kuhutubia mikutano katika sehemu nyingi nchini.

Mwezi uliopita kwa mfano, katika mkutano mmoja wa hadhara alitoa changamoto kwa mme wake ataje mrithi wake wa kiti cha urais, suala ambalo mara nyingi Mugabe amekuwa akilikwepa kulizungumzia hadharani.

Wakati wa uchaguzi wa 2008 Grace alisikika akisema kwamba mumewe ataendelea kuitawala Zimbabwe hata akiwa kaburini. Alisema: “Iwapo Mungu ataamua kumchukua, basi tutateua mwili wake kugombea urais.” Aliirudia kauli hiyo mapema mwaka huu kuhusu uchaguzi wa 2018.

Sasa hivi Rais Mugabe ameanza kampeni kutaka tena achaguliwe katika uchaguzi huo na mara kwa mara amekuwa akisisitiza kamwe hatachagua mrithi wake.

Grace huwa hakosi kuandikwa katika vyombo vya habari nchini humo na kwenye mitandao ya jamii – kwa mazuri au mabaya. Kama atakuwa hamkaripii waziri wa serikali basi ataandikwa kwa kumshambulia Makamu wa Rais au afisa mwingine mkuu wa serikali – akiwatuhumu kupanga njama za kutaka kumng’oa mme wake madarakani.