Home KIMATAIFA Ni tajiri wa maadili, masikini wa mali

Ni tajiri wa maadili, masikini wa mali

1193
0
SHARE

Na; LEONARD CHAKUPEWA SOZA,

BUJUMBURA, BURUNDI.

Ni wazi kwa wengi inaonekana tumezaliwa ili kujishibisha tu na kujishibisha, na pindi tunapokosa nafasi ya kujishibisha zaidi tunajawa hasira na kuchanganyikiwa, na hujikuta tukiishi katika upweke na kutengwa…

Kihistoria, ulimwengu umewahi kushuhudia aina anuai za tawala, uongozi, viongozi na watawala tangu kuumbwa kwake. Naam, zama na enzi vimekuja na kupita, zikiwaibua watawala wengi na watu mashuhuri katika mifumo ya Kifalme, kidini au kiimani, kidemokrasia na mingine mingi katika vitabu na masimulizi ya vinywa kama Sulemani, Daudi, Muhammad (SAW), Alexander The Great, Kaisari Julius, Napoleon Bonaparte, Sundiata Keita, Mansa Kankan Mussa, Shaka ka Senzangankhona au Shaka Zulu, Adolf Hitler, Cetshwayo kaMpande, Malkia Nzinga Mbandi, Mirambo, Mkwawa nk. Kila mtawala ama kiongozi, anayo heshima, falsafa, wajihi au kaliba yake abebayo pindi awapo uongozini, na ambayo hata anapoyaacha madaraka husalia kama utambulisho wake. Duniani kote kwa miongo na karne imekuwa hivyo na inaendelea kubakia hivyo. 

Walikuwepo waliotawala na kujipambanua kama watekaji miliki za wenzao, wakatili, wapole na wacha Mungu nk. Hizo zote kwa hakika, ni sifa zinazompambanua kiongozi mmoja na mwingine, utawala mmoja na mwingine, ukuu mmoja na mwingine. Kule Amerika ya kusini, kuna historia ndefu sana katika mambo ya siasa, tawala, harakati za ukombozi na mapinduzi. Kwa wasiofahamu, ni huko ndiko alikozaliwa Ernesto Guevara de La Serna, alimaarufu “Che Guevara” kwa wengi, mwanamapinduzi kindakindaki wa Arjentina aliyekuwa muumini wa falsafa za Mjerumani Karl Marx, mwanamapinduzi aliyegeuka kivutio kikubwa duniani kote baada ya kuuawa kwake kule nchini Bolivia mwaka 1967, kinyume kabisa na mategemeo ya waliomuua wakiongozwa na Marekani waliojidanganya kuwa kifo chake kingelifuta jina lake, misimamo yake katika kuupinga ubepari pia umaarufu wake ndani ya mioyo na fikra za watu ulimwenguni. Huyu si kusudio letu leo kumzungumzia, tumwache kwanza na kuendelea na mtu mwingine kabisa….

Kuzaliwa Kwake na Makuzi

Kandoni mwa taifa la Arjentina, kuna nchi iitwayo Urugwai. Ukiitaja nchi hii, moja kwa moja unazungumzia taifa lenye historia ya pekee kisiasa. Siasa za nchi hiyo zina upekee hasa kufuatana na msingi uliojengwa na baadhi ya viongozi wake. Hapa ndipo jina la Jose Alberto ‘Pepe’ Mujica Cordano, rais wa arobaini wa taifa hilo, linapokuja. Huyu ndie mlengwa hasa wa makala hii, inayokwenda kwa upana kuangazia na kuyachambua maisha yake ili kuifanya jamii kutambua maana na umuhimu wa uadilifu katika kuwatumikia watu bila kujali nafasi ya uongozi. Kwa wengi inawezekana jina hilo likawa geni sana masikioni na fikrani, na haishangazi. Kutofahamika kwa jina la shujaa huyu kunatokana na haiba ya historia za viongozi wetu wengi ulimwenguni kujipambanua aghalabu kwa mambo yanayotisha au kushtua, anasa, ukatili usiosemeka au kutazamika nk. 

Kwa wengi, anafahamika kama ‘Rais masikini duniani kuliko wote waliopata kutokea’ Komredi Mujica ana historia ndefu na ya kusisimua sana kisiasa hadi kufikia kuwa rais wa taifa hilo la Amerika ya kusini. Alizaliwa mwaka 1935 kwa Bwana Demitrio Mujica, mkulima mdogo toka Hispania na Bibi Lucy Cordano, muhamiaji mwenye asili ya Italia. Iko wazi kwa hakika, Jose Mujica alizaliwa katika umasikini kweli kweli. Hakusimuliwa kuhusu umasikini, bali kuuishi tangu kuzaliwa kwake katika familia yao. 

Kwa bahati mbaya Jose hakupata kumfahamu baba yake mzazi kwa sura sana, kwa kuwa kipindi akiwa na miaka mitano tu ya uhai baada ya kuzaliwa, mwaka 1940, Bwana Cordano alifariki dunia akimwacha mtoto Jose kuishi na babu na bibi zake upande wa mama yake ambao nao walikuwa masikini sana, wenyeji wa Liguria. Baadhi ya duru kuhusu historia ya familia ya Jose Mujica hudai kwamba msongo wa mawazo ndio ilikuwa sababu ya Bwana Cordano Mujica kufariki, baada ya kufilisika na maisha kuwa magumu. 

Harakati za Ukombozi Kijeshi 

Akiwa kinda wa miaka 13-17, alilazimika kuikabili dunia na dhahma zake kujaribu bahati yake, pia kusaidia mahitaji ya nyumbani kwa babu na bibi yake waliokuwa taabani na uzee pia hali mbaya kiuchumi. Maisha ya wahamiaji wakati huo nchini Urugwai yalikuwa magumu, kutokana na sera kandamizi dhidi yao zilizokuwepo chini ya serikali iliyokuwa madarakani. Katika kipindi hiki, Jose alitafuta kujiunga na makundi mbalimbali ya kijamii na kisiasa, ndipo wakati mmoja akafanikiwa kuwa mwanachama wa chama cha Kitaifa (National Party), hatua iliyomsogeza karibu na wanaharakati mbalimbali waliokuwa na heshima na majina makubwa nchini humo wakati huo, akiwemo Enrique Erro.  

Katikati mwa miaka ya 60, kama sehemu ya jitihada zake kujaribu bahati ya maisha, alijiunga na kundi la waasi la MLN-Tuparamos, lililoendesha harakati za mapinduzi kijeshi kutokana na hamasa kubwa waliyopata kutoka nchini Cuba, ambako Commandante Fidel Castro na nduguye Raul halikadhalika Che Guevara wakati ule walifanikisha kuikomboa nchi toka mikononi mwa ya kiongozi dikteta na ‘mbwa wa Marekani’, Fulgencio Baptista. 

Jose akiwa tayari kijana machachari kabisa aliyepata mafunzo chini ya kundi hilo la kijeshi, alianza rasmi kushiriki harakati hizo. Mwaka 1969, kundi hilo lilifanya shambulizi maarufu kama ‘Pando’ ambapo vikosi sita vya kundi hilo vilishambulia maeneo muhimu ya serikali iliyokuwa madarakani, kama njia ya kuishinikiza kuridhia mazungumzo ya kuunda serikali yenye uwakilishi toka pande zote. Kitendo hiki kilisababisha uhasama mkubwa baina ya MLN-Tuparamos na serikali nchini humo wakati huo, hivyo kuweka mikakati kamambe ya kulikabili na kulithibiti vilivyo kundi hilo, hasa kwa kuwatia mbaroni viongozi wake, halikadhalika wapiganaji wake mahiri. Mwaka 1970 Jose alishambuliwa vibaya na vyombo vya usalama katika jaribio la kumkamata. Kwa hasira, aliwashambulia na kuwaua askari wawili wa serikali, tendo lillilosababisha achakazwe risasi mara sita katika maeneo kadhaa ya mwili wake, zilizotishia uhai wake kutokana na majeraha makubwa aliyopata na kupoteza damu nyingi. Hata hivyo, kwa juhudi za madaktari, aliweza kupona majeraha yote aliyokuwa amepata, na akafanikiwa kukwepa mtego wa kutiwa nguvuni uliokuwa umewekwa na polisi. 

Mara tano polisi walimuwinda na kumkosa, lakini mara ya sita haikuwa bahati kwake. Mwaka 1972, polisi walifanikiwa kumnasa kutokana na mtego mkali aliowekewa. Kabla ya kutiwa nguvuni katika tukio hilo, alijaribu bila mafanikio kujiepusha na kukamatwa. Waswahili husema, ‘Siku ya kufa kwa nyani, miti yote huteleza’ Hatimae, serikali ya kidikteta iliyomuwinda kwa muda mrefu bila mafanikio ya kumnasa, ikamsweka gerezani miaka 13, yeye na makomredi wenzake kadhaa toka kundi la MLN-Tuparamos. Kufungwa kwake na wenzake pakubwa sana kulikuwa kama mwiba mkali kwa harakati za kundi hilo la ukombozi, kutokana na wapiganaji wake kukata tamaa na wengine kujitoa katika harakati moja kwa moja. Ulikuwa myumbo na hasara kubwa katika tasnia ya mapambano kwa ajili ya kuikomboa nchi.

Kuachiwa Huru, Harakati za Kisiasa, Ndoa na Uongozi

Baada ya kusota jela miaka 13, toka mwaka 1972 hadi 1985, nchini kwake kulitokea mabadiliko kisiasa. Mageuzi ya kisheria yaliyofanyika hasa zile zinazohusu Haki za Binadamu kimataifa, yalipelekea mbinyo wa Jumuiya ya Kimataifa kuongezeka, kuitaka serikali iliyokuwa madarakani kuwaachilia huru wafungwa wa kisiasa akiwemo Jose Mujica na wenzake. Ni kwa mbinyo huo mwaka 1985 hatiame, Jose na makomredi wenzake kadhaa waliachiliwa huru na kurejea uraiani kuendelea na maisha ya kawaida. 

Miaka kadhaa badae, Jose na wanachama wenzake wa zamani katika kundi la kijeshi la MLN walianzisha chama cha siasa chenye kuamini katika sera za mrengo wa kushoto, kilichoitwa Movement Of Popular Participation, ambacho kiliridhiwa katika Muungano mama wa vyama vya upinzani kitaifa wakati huo, BROAD FRONT. Rasmi harakati za uongozi kisiasa kwa Jose Mujica zikaanza.