Home Habari Ni wiki ya kusimama au kuanguka kwa Lipumba?

Ni wiki ya kusimama au kuanguka kwa Lipumba?

1862
0
SHARE

MWANDISHI WETU

MWANZONI mwa wiki hii Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam, ilitengua uteuzi wa wajumbe wa bodi ya chama cha Wananchi –CUF iliyoteuliwa na Mwenyekiti wake, Ibrahim Lipumba.

Wajumbe hao wa bodi walipendekezwa na Prof. Lipumba ambaye hana uhusiano mzuri wa kikazi na Katibu Mkuu wake, Maalim Seif Sharif Hamad tangu Agosti 6, 2015 mara baada ya msomi huyo wa uchumi kutangaza kujiuzulu nafasi yake ya uenyekiti.

Hata hivyo Prof. Lipumba alijirejesha kwenye nafasi yake hiyo mwaka mmoja baadae na kuteua bodi ya wadhamini waliosajiliwa na Wakala wa Usajili, Udhamini na Ufilisi (Rita) kama ilivyoelekezwa katika sheria namba 5 ya vyama vya siasa ya mwaka 1992.

Uamuzi huo umetazamwa kama ushindi kwa kambi ya Maalim Seif na huku ukibeba dhana ya kushindwa kwa kambi ya Prof. Lipumba.

Kwa miaka minne sasa CUF imekuwa ndani ya mgogoro mzito wa kiuongozi, hali inayochagiza kuwapo kwa kesi za mara kwa mara kati ya pande hizo mbili.

Mara baada ya kutolewa kwa hukumu ya kesi hiyo ya kuwapinga wajumbe wa bodi ya chama hicho, iliyofunguliwa na Mbunge wa Malindi, Ally Salehe, kesho itatolewa hukumu nyingine dhidi ya uhalali wa Prof. Lipumba kuwa mwenyekiti baada ya kutangaza kujiuzulu.

Prof. Lipumba alitangaza uamuzi huo kwa kile alichodai kuwa ni kutoridhishwa na uamuzi wa vyama vilivyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) kumpitisha Edward Lowassa kuwania tiketi ya urais.

Endapo hukumu inayotarajiwa kutolewa kesho na Mahakama hiyo hiyo iliyotoa uamuzi wa kutengua uteuzi wa wajumbe wa bodi, itaharamisha uhalali wa Prof. Lipumba kwenye nafasi ya uenyekiti ni wazi wiki hii itakuwa mbaya kwa mwanasiasa huyo.

Uamuzi wowote ambao hautakuwa na maslahi kwa Lipumba, utaibua mjadala mzito na kuhalalisha malalamiko ya muda mrefu ya baadhi ya makada wa CUF upande wa Maalim Seif, wanaodai kuwa mwenzao huyo wa zamani anabebbwa na serikali.

Tayari kambi ya Maalim Seif imeshaonesha furaha yake na kuwataka wafuasi wao kuendelea kuwa watulivu ili kile wanachodai kuwa ni haki yao kipatikane.

“Nawaomba wanachama wa CUF wawe watulivu, wakati tukisubiri uamuzi mwingine utakaotolewa Ijumaa.”

Ukweli ni kwamba endapo mahakama itatoa uamuzi wa kuharamisha uenyekiti wa Prof. Lipumba huenda ukawa mwanzo wa uimara zaidi wa mwanasiasa huyo au akajikuta nje ya ulingo wa siasa za upinzani.

Upo uwezekano mkubwa wa Prof Lipumba kupepesuka na pengine kujiondoa kabisa kwenye uga huo kama alivyofanya kwa hiyari yake mwaka 2015.

Tayari Maalim Seif ameshamtaka Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), kufanya ukaguzi wa fedha za ruzuku za chama hicho zilizokuwa zikimilikiwa na kambi ya Prof. Lipumba.

Maalim Seif ametaka kufanyika kwa ukaguzi huo kwa hoja kuwa bodi ya aliyekuwa mshirika wake kisiasa haikuwa halali.

“Tumeupokea kwa furaha uamuzi wa Mahakama Kuu umekata mzizi wa fitina wa madai yetu dhidi ya Rita, nilishasema tangu awali tuko tayari kupokea uamuzi wowote wa Mahakama,” alisema Maalim Seif.

CUF KUREJEA ZANZIBAR

Kabla na hata baada ya uchaguzi wa mwaka 2015 CUF ilizatamwa kuwa na nguvu kubwa ya kisiasa Zanzbibar, hadi pale chama hicho kilipoingia kwenye mgogoro wa wenyewe kwa wenyewe mwaka 2016.

UUamuzi wa wiki hii unaweza kurejesha uimara wa chama hicho Zanzibar, hatua inayoonekana kuwa na matokeo mabaya kwa Prof. Lipumba na washirika wake.

Nguvu ya chama hicho Zanzibar inatambulika wazi kwani kilishawahi kuingia kwenye Serikali ya Umoja wa Kitaifa (SUK) iliyoundwa kutokana na mwafaka wa pili kati ya chama hicho na Chama cha Mapinduzi (CCM) baada ya mgogoro wa kisiasa ulioibuka kutokana na uchaguzi wa mwaka 2010.

Ujio wa SUK huku Maalim Seif akiwa Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, ulichagiza kuingia serikalini kwa baadhi ya makada wake.

Kwa vipindi kadhaa huko nyuma CUF ndiyo kilikuwa kama chama tawala kisiwani Pemba kikiwa na masheha, wawakilishi na wabunge katika Bunge la Muungano.

Kukosekana katika vyombo hivyo vya maamuzi na uwakilishi Zanzibar pamoja na mgogoro wa wenyewe kwa wenyewe vinatajwa kupunguza nguvu na ushawishi wa chama.

Uamuzi wa Mahakama Kuu wa wiki hii unaweza kukiimarisha chama hicho na kudhoofisha nguvu za kiongozi mmoja mmoja kati ya Maalim Seif na Prof. Lipumba.