Home Makala NIDHAMU MWALIMU SASA DONDOSHA KIBOKO

NIDHAMU MWALIMU SASA DONDOSHA KIBOKO

2418
0
SHARE

NA BALINAGWE MWAMBUNGU


UMEKUWAPO mjadala wa muda mrefu kuhusu nidhamu katika shule, sio tu hapa kwetu Tanzania, bali katika nchi zote duniani. Inadaiwa kwamba wanafunzi shuleni siku hizi hawana nidhamu kama walivyokuwa wazazi, au watangulizi wao. Na inaeelezwa kwamba hii imetokana na kuondolewa aina za adhabu wanazopewa na hasa viboko.

Adhabu ya viboko imekuwa inatumika nyumbani na shuleni kama njia ya kudumisha utii na nidhamu. Wazazi na walimu wengi wanaamini kuwa bila kiboko, mwanafunzi hawezi kuwa mtiifu, kutofanya bidii katika masomo na kazi nyingine anazopangiwa.

Walimu wanapendelea adhabu ya viboko kwa sababu ni rahisi kutekeleza, ni ya papo kwa hapo kuliko adhabu nyingine ambazo inamlalizimu mwalimu au kiranja aisimamie na hivo kuonekana kuwa mwalimu au kiranja, anakuwa sehemu ya adhabu hiyo na huwa inachukua muda mrefu.

Kuna dhana kwamba kukataza adhabu ya viboko kumechangia sana kushuka kwa nidhamu shuleni. Wanafunzi wanakuwa jeuri kwa walimu, hawana heshima. Wanafunzi wakubwa wanawaonea wadogo, huwadharau walimu wa kike, na hawatii mamlaka ya walimu. Matokeo yake, wanafunzi wakiisha maliza masomo, wanakuwa sehemu  ya jamii—na kwa kuwa vijana ni wengi kuliko watu wazima, jamii nzima inaonekana haina nidhamu.

Wanafunzi wengi siku hizi hawajui utii. Wanafanya fujo darasani na kupiga kelele na kuzomea. Wanaweza kumgomea mwalimu, hawatii maelekezo. Wanakataa hata kufanya kazi za nyumbani (home work), ambayo ni kwa faida yao wenyewe. Mfano halisi ni tukio lililotokea mjini Mbeya hivi karibuni, wanafunzi wa Kidato cha Tatu, waligoma kufanya kazi ya nyumbani—na mmoja wao akakataa kutii amri halali ya mwalimu wa somo.

Katika somo la malezi vyuoni, walimu wanafundishwa kwamba wakiwa shuleni, wao ni wazazi mbadala. Lakini dhana hii inakolea vizuri zaidi katika shule za bweni. Sheria za shule ni pamoja na msisitizo wa utii—ili maisha ya wanafunzi yawe ‘orderly’—waishi kwa mpangilio mzuri kama ilivyo jeshini—kila kitu kinakwenda kwa mpangilio. Moja ya kanuni ya adhabu shuleni inamtaka mwanafuni afanye adhabu kwanza, ahoji baada ya kuitimiza. Lakini siku hizi wanafunzi wengi hawajui kuwa utii ni jambo la lazima katika maisha—kuanzia nyumbani, shuleni hadi kazini. Jeshi la Polisi wameibua kauli mbiu ya—tii amri bila shuruti ili maisha yako yaende kwa mpangilio.

Lakini kwa nini wanafunzi wanakosa nidhamu? Kuna mambo mengi yanayochangia—wazazi kutofuatilia maendeleo na mwenendo wa watoto wao. Mazingira ya kusomea kutokuwa rafiki, ukosefu wa vifaa ya kufundishia, msongamano mkubwa wa wanafunzi. Ikama ya wanafunzi katika darasa moja ni watoto 45. Lakini siku hizi darasa moja linakuwa na watoto zaidi ya 100. Ni wazi kwamba mwalimu hawezi kumudu darasa kama hilo.

Darasa la watoto 45 wakikaa kwa mpangilio, kila mwanafunzi na dawati lake, nirahisi kwa mwalimu kumfahamu mtoto mmoja mmoja—kwa jina, tabia,uwezo na mapungufu yake. Lakini kwa wanafunzi 100, tena waliokaa chini, sio rahisi. Ukaaji kama huu unachangia utoro, uzembe na ukosefu wa nidhamu. Katika shule za bweni, ni rahisi kujua idadi ya wanafunzi, mahudhurio yao na uwezo wa kila mmoja wao. Nidhamu ni muhimu sana hata kwenye michezo. Nidhamu ni sehemu muhimu sana hata katika jamii. Nidihamu ndio inayojenga madili katika jamii.

Lakini ukosefu wa nidhamu shuleni, mara nyingine huchangiwa na walimu ambao walisomea uwalimu kwa sababu walikosa kazi—hawa  ni walimu wa kipato. Uwalimu ni kazi ya wito kama ilivyoku kwa upadre na utabibu.

Lakini wanapokuwa vyuoni, walimu hawafundishwi uongozi wa shule. Wanafundishwa jinsi, ya kufundisha na saikolojia ya watoto. Ulikuwapo utaratibu pia wa kuwarudisha vyuoni walimu kupigwa msasa ili waendane na mambo ya kisasa na teknolojia. Vinginevyo wanafunzi wakiwa wajuzi kuliko walimu wao, ni vigumu kuwaheshimu.

Aidha, walimu wanaweza kudumisha nidhamu shuleni ikiwa wanawajibika ipasavyo. Walimu wawe na ari ya kufundisha. Wazazi wasiingilie masuala ya shule. Lakini mara nyingine, wazazi wanagombana na walimu wakihoji kwa nini wanawaadhibu watoto wao.

Katika shule za kutwa, hasa za mijini, utoro huwa ni jambo la kawaida. Wanafunzi kutoka familia nzuri kiuchumi, mara nyingine zinawakwaza walimu. Mwanafunzi anampa mwalimu fedha ili wazazi wasijue kwamba hawahudhurii masomo. Au anamhonga mwalimu ili amendee kwenye matokeo ya mtihani. Mwanafunzi anaaga kwamba anakwenda shuleni, kumbe anachepuka na kweenda kwenye vijiwe—huko ndiko wanafundishana mambo ya ovyo.

Mwanafunzi analetwa shuleni kwa gari, badala ya kuingia darasani, anaenda anakotaka. Saa ya kurudi nyumbani ikikaribia, anarudi langoni, begi mgongoni anachukuliwa! Baadhi ya wanafunzi wanamaliza miaka ya masomo wakiwa na uelewa mdogo wa masomo—vilaza.

Walimu ambao hawakupitia mfumo rasmi wa uwalimu, hawawezi kuwa mfano mzuri na kuhimiza na kuendeleza nidhamu shuleni. Hawafuati miiko ya uwalimu—wanashirikiana na wanafunzi katika maovu—bangi na dawa za kulevya na uhusiano wa kimapenzi—hasa katika shule mchanganyiko za kutwa.

Wazazi wengine hawaendi kuonana na walimu hata wakialikwa Siku ya Wazazi—ambayo ni maalumu kwa walimu kufahamiana na walimu na kuelezwa maendeleo na matatizo ya mtoto wao. Siku hizi baadhi ya wanafunzi, hasa wa shule za kutwa, Siku ya Wazazi huenda na ‘wazazi bandia’ ili kuficha udhaifu wao.

Je, viboko ni dawa ya tabia mbaya shuleni? Hili ni swali ambalo linaulizwa na linajadiliwa katika nchi nyingi. Ziko aina nyingi za adhabu kama vile kufanya kazi za mikono, kuruka kichura, kusimama juani, kushika vidole gumba vya miguuni, kupiga magoti nje au mbele ya darasa.

Adhabu nyingine ni pamoja na kushika masikio kwa kupitisha mikono  nyuma ya magoti, kusimama kwa mguu mmoja, pushapu. Kwa shule zilizo nje ya miji, mwanafunzi hupewa adhabu ya kukata kuni, kung’oa visiki, kupigwa makofi, ngumi na mateke. Adhabu nyingine ni kuvutwa nywele, kukimbia kuzunguka uwanja wa mpira na kufukuzwa shule kwa muda.

Lakini adhabu zote hizi hata walimu wanasema haziwezi kurejesha adhabu shuleni—kiboko kinawafanya wanafunzi kuwa na adabu. Lakini katika nchi nyingi, suala hili limekuwa la kisheria. Kenya kwa mfano, viboko vilikatazwa rasmi wakati wa utawala wa Rais Mwai Kibaki. Serikali ilitoa Notisi ya Kisheria Machi 30, 2001, inayopiga marufuku viboko shuleni, lakini inasemekana kuwa licha ya katazo hilo, kiboko bado kinatumika katika baadhi ya shule.

Hapa Tanzania bara kiboko bado kinatumika shuleni kama ilivyoainishwa katika Sheria ya Elimu Namba 25 ya mwaka 1978, lakini kwa makosa maalumu na kwa kibali cha mwalimu mkuu na viboko visizidi vine. Wanaharakati wanataka sheria ya viboko ifutwe kwa kuwa ni ya kikatili. Mrembo wa  Tanzania 2016, Diana Edward anaendesha kampeni ya ‘Maasai dondosha wembe’ na wanaopinga viboko shuleni wanasema; ‘Mwalimu sasa dondosha kiboko’ na kulitaka Bunge liifute sheria hiyo.

Katika nchi zilizoendelea kama Marekani, kiboko kiliondolewa rasmi katika shule za serikali za majimbo mwaka 1987 na shule binafsi mwaka 2009.

Lakini hata katika nchi zilizofuta adhabu ya kiboko, baadhi ya wazazi wanataka kirejeshwe kwa madai kwamba ni njia pekee ya kuweka nidhamu shuleni. Wengine wanasema kiboko ilikuwa njia ya zamani ya kudumisha nidhamu nyumbani na shuleni na imepitwa na wakati.