Home Latest News ‘Nikiwa rais nitawapa madaraka Al Shabab’

‘Nikiwa rais nitawapa madaraka Al Shabab’

2452
0
SHARE

0,,19086818_403,00MOGADISHU, SOMALIA

JUMANNE wiki hii yamefanyika maadhimisho ya Siku ya Mwanamke Duniani. Ni kumbukumbu inayojenga taswira chanya kuhusu mwanamke kokote duniani. Wakati dunia ikiwa kwenye sherehe hizo, nchini Somalia nyota ya mwanamke Fadumo Dayib imezidi kung’ara kutokana na kuikaribia Ikulu ya taifa hilo hadi sasa.

Swali moja linaloulizwa ni kama Somalia ipo tayari kuwa na Rais Mwanamke? Nyota ya Fadumo Dayib imepaa kwa kasi na kuwavutia watu mbalimbali nchini mwake na jumuiya ya kimataifa. Somalia ni nchi ambayo haijapata utulivu tangu miaka 1990 tangu kuangushwa kwa deikteta Siad Barre.

Aidha, inakabiliwa na wimbi la ugaidi kutoka kundi la Al Shabab huku wanajeshi 22,000 wakiwa nchini humo kufanya kazi za kulinda amani. Je, Fadumo Dayib yupo tayari kwa hilo na yeye ni nani?

SWALI:  Ni kitu gani kimevutia hadi kugombea urais?

Fadumo Dayib: Nimepata msukumo wa kugombea urais sababu naamini ni suala la maadili na utumishi wa umma, ambalo linaweza kabisa kutumika kuzuia umwagaji damu unaofanyika Somalia. Tumeshuhudia umwagaji damu kwa miaka 25 sasa ambayo hailingani na hatua ya mendeleo tuliyopiga kama taifa kutokana na wajibu wetu.

Viongozi waliopita na wa sasa wametuangusha, tunatakiwa kuchukua suala la mgogoro huo mikononi mwetu ili kutatua. Hiyo ndiyo sababu ya mimi kugombea urais. Nina dhamira ya dhati kutimiza malengo, uwezo na hamasa ya kiwango cha juu.

SWALI: Unaamini kwa kiasi gani kuwa unaungwa mkono na wananchi wa Somalia, nchi ambayo bila shaka haina uwezo wa kumuunga mkono mwanamke kugombea nafasi kubwa kama urais?

Fadumo Dayib: Hilo ni suala la jumuiya ya kimataifa pia. Si jambo linaloikabili Somalia peke yake. Wanamume wamekuwa viongozi wa jamii zetu duniani, lakini naamini kizazi kipya hakina muda wa kuichukulia jinsia fulani kuwa haiwezi kuongoza nchi.

Jinsia si jambo muhimu kizazi cha sasa. La muhimu ni kitu gani atakileta yule anayetaka madaraka hayo. Sawa, ipo changamoto hiyo, lakini tutahakikisha tunakabiliana nayo ili wanawake wasiwekewe kikwazo cha jinsia kuwa rais wa Somalia au madaraka yoyote.  Binafsi ninajiamini, naamini wananchi wa Somalia wataniunga mkono sababu wamechoshwa na mapigano, ….. wanataka amani nchini mwao… wanataka uongozi thabiti ambao utalinda watoto wao na kuwapa elimu bora.

SWALI: Kuna taarifa kuwa umepokea tishio la kuuawa, hivyo maisha yako yapo hatarini. Umechukua hatua gani dhidi ya vitisho hivyo?

Fadumo Dayib: Ninadhani hilo ni jambo la kushangaza sana, lakini pia ni ujumbe kuwa nawatumikia watu, … nafanya mambo sahihi kwa maslahi ya watu wa Somalia hivyo ni tishio kwa hao wanaonitishia kifo. Wanafahamu kuwa mimi ni tishio lao katika uongozi. Wanafahamu kuwa nina malengo ya kufanya kitu kizuri kwaajili ya Somalia. Wanauona uongozi mzuri ndani yangu, wanaona maono yangu ya utumishi thabiti wa umma kama kiongozi wa taifa hilo. Hilo ndilo linalowaumiza vichwa vyao sababu nikiingia madarakani wanajua nafasi zao hazitakuwepo. Natishia maslahi yao, hivyo wananiogopa.

SWALI: Jumuiya ya Ulaya inatarajia kurejesha misaada yake kwa serikali ya Somalia. Una maoni gani kwa uamuzi huo?

Fadumo Dayib: Nafikiri uamuzi huo umefikiwa sababu ya kuongezeka kwa vitendo vya kigaidi Somalia. Jumuiya ya Ulaya inaangalia kile inachotoa na matunda yake. Naamini kuna sababu za msingi zilizowafanya waache kutoa misaada Somalia, na pia ningependa kutoa ushauri kwa Umoja wa Afrika (AU) ufanye mapitio ya sera zake nchini Somalia. Ni lazima Umoja wa Afrika uongeze nguvu ya ulinzi na usalama wa wananchi wa Somalia, waongeze majeshi ya kulinda amani katika sekta ya ulinzi ili kuangamiza vikundi vinavyoharibu amani.

SWALI: Labda tuseme ndoto yako kuwa rais wa Somali itatimia mwaka huu; ni kitu gani cha kwanza utakachofanya kuhusu hali ya ulinzi na usalama wa Somalia?

Fadumo Dayib: Endapo nitachaguliwa, uongozi wangu utaondoa kabisa mfumo wa jadi wa 4.5 wa mgawanyo wa madaraka kwa makabila yaliyopo (kwamba uongozi wa juu wa jadi ndiyo unachagua rais). Kwasababu mfumo uliopo umewatenga wananchi wengi wa Somalia. Mfumo uliopo umechangia sana kuzorotesha hali ya amani na ulinzi, nchi inanuka ugaidi kila kona. Mtu yeyote anayechaguliwa kuwa rais aondoe kabisa matumizi ya mfumo 4.5 wa jadi (4.5 Clan System). Mtu anaweza kutumia mfumo huo kwa kutoa rushwa, ni lazima awe mla rushwa sugu sababu alishinda kwa mlungula.

Ili kukabiliana na tatizo la usalama wa Somalia, kama nitachaguliwa kitu cha kwanza kukifanya ni kuwaita viongozi wa Al Shabab katika meza ya mazungumzo. Sababu mikakati ya kupambana na kukitokomeza kikundi cha Al Shabab haijafanikiwa kabisa Somalia. Ukiwahoji Al Shabab utaona wanakueleza matatizo ya kijamii na kiuchumi, hayo ni makubwa Somalia.  Al Shabab wanazungumzia uhaba wa elimu bora, wanahoji ulaji rushwa, halafu wanafanya vitu ambavyo wananchi wanavitaka kutoka kwa viongozi wao, ikiwemo kuwapa matumaini na kuondoa kero za kijamii pamoja na kuwainua waliokata tamaa.

SWALI: Unaonekana kuwa mwanamke shupavu na mhamasishaji, ni nani anakufanya uwe hivyo ulivyo?

Fadumo Dayib: Aghalabu nimekuwa nikivutiwa na mama yangu. Nimefika hapa sababu yake ingawaje alifariki dunia mwaka 1995. Wakati wa uhai wake alikuwa akinihamasisha mambo mengi, hivyo bado najisikia hisia zake zinanitawala na kunipa msukumo zaidi.

FADUMO DAYIB NI NANI?

Fadumo mwenye umri wa miaka 42 kwa sasa alizaliwa nchini Kenya, wazazi wake ni raia wa Somalia. Akiwa mdogo wazazi wake walirejea Somalia, baada ya vita kupamba moto waliikimbia nchi hiyo na kwenda kuishi nchini Finland. Alijua kusoma na kuandika akiwa na umri wa miaka 14, na amekulia kambi za wakimbizi. Sasa ana shahada ya kwanza ya afya ya umma. Nia yake ya kuwa rais ilianza baada ya kuwa mfanyakazi wa Umoja wa Mataifa kwa miaka 12.

Naam, Fadumo Dayib anatarajiwa kuwa miongoni mwa wagombea urais wa Somalia ifikapo Agosti mwaka huu. Ufaransa limekuwa taifa la kwanza kubainisha kuwa litamuunga mkono. Aidha, kumeanzishwa ‘Kamati ya Marafiki wa Fadumo’ yenye makao yake jijini Paris, Ufaransa. Kamati hiyo inasisitiza upatikanaji wa amani Somalia pamoja na kumchagua Fadumo kuwa Rais wa kwanza mwanamke ambaye amepania kumaliza vita vya wenyewe kwa wenyewe nchini humo. Ana kauli moja ya kusisimua, “Kwetu Somalia tunayo jamii ambayo haifahamu aina nyingine ya maisha zaidi ya vita. Hii ni ishara mbaya”

Makala haya yametafsiriwa kutoka tovuti ya Deutch Welle.