Home Makala Nini muarobaini wa janga la ajira nchini?

Nini muarobaini wa janga la ajira nchini?

201
0
SHARE
Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Walemavu, Jenista Mhagama

NA KISIRI NYAGWISI 

TAKRIBANI ni miezi sita sasa dunia iko kwenye taharuki ya ugonjwa wa corona au Covid-19, hadi sasa kulingana na Shirika la Afya Duniani (WHO) zaidi ya watu 83,000  wamepoteza maisha wengi kutoka Italia, Hispania, China na Marekani.

Afrika pia kumetokea vifo kadhaa ambapo kulingana na ripoti hiyo ya WHO zaidi ya watu 608 wameishapoteza maisha, ugonjwa huu ni kama umebadilisha hali yetu ya maisha ya kila siku na hata kutufanya tusahau changamoto zetu za kila siku na pengine zenye madhara makubwa zaidi ya ugonjwa huu wa corona. 

Kwa Tanzania, ugonjwa huu unatokea katika kipindi muhimu, ikiwa ni mwaka wa uchaguzi mkuu, unaotarajiwa kufanyika Oktoba mwaka huu. Lakini pamoja na hayo wengi tuna hamu kusikia tathimini ya jumla ya utendaji wa serikali ya awamu ya tano kutoka kwenye kikao cha mwisho cha Bunge la Jamhuri ya Muungano ambacho tayari kinaendelea vikao vyake jijini Dodoma. Kwangu tathmini iko katika hotuba mbili kati ya hotuba zote zitakazowasilishwa katika bunge hili. 

Hotuba ya kwanza ni ile ya Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa ambayo tayari imewasilishwa na kujadiliwa na hatimaye kupitishwa na Bunge na hotuba ya pili ni ile ya Bajeti ya Serikali kutoka kwa Waziri wa Fedha na Mipango. Ambapo kimsingi tathimini yangu kwa serikali kupitia hotuba hizi, iko katika suala moja tu AJIRA kwani kwangu changamoto hii naiona pengine ina madhara makali zaidi na ya muda mrefu, kwa familia, jamii na taifa kwa ujumla zaidi ya kitu chochote kile, kama haitatafutiwa suluhu yake, nilikua na hamu sana kusikia namna ambavyo serikali imeshughulikia changamoto hii, matokeo yake na nini mikakati wake. 

Kwa leo nitaeleza machache juu ya hotuba ya Waziri Mkuu na baadaye kupendekeza njia mchanganyiko zitakazopelekea kupunguza tatizo hili kwenye jamii kama zikilidhibitiwa.

Baada ya kusikiliza hotuba yake wiki moja iliyopita, ni kweli nakubaliana na yeye kwamba serikali yetu chini ya Rais Dk. John Magufuli imefanya mambo mengi na mazuri katika maeneo mbalimbali yanayogusa maisha ya wananchi hususani katika suala la miundombinu ya barabara, sekta ya afya, nishati, madini, usafiri wa angana reli.

Bahati nzuri sehemu kubwa ya jamii ya kitanzania inajua ukweli huo, lakini binafsi kwa bahati mbaya sijaweza kusikia mkakati wa kina na mbadala juu ya suala la ajira, pamoja na ukweli kwamba waziri aligusia bayana kwamba vijana mamilioni kwa mamilioni wamepata ajira kwenye miradi ya serikali inayotekelezwa sehemu tofautitofauti nchini.

Lakini bado naona maelezo hayo hayatoshi kujibu changamoto hii mtambuka ya ukosefu wa ajira nchini kwa sababu kwanza miradi hiyo si ya kudumu lakini pia haiko nchi nzima mfano kama mradi uko Dar es Salaam na kuajiri vijana na wa sehemu hiyo  vipi vijana wa Mara, Shinyanga Kigoma, Lindi au Bukoba? 

Na pia miradi hii sio mingi sana ya kuweza kuajiri vijana wote walio mitaani tangu mwaka 2015, nadhani bado serikali iko na wajibu mkubwa wa kuandaa mpango kambambe wa kukabiliana na janga hili.   

Pamoja na ukweli kwamba Tanzania si nchi pekee barani Afrika na duniani kwa ujumla inayokabiliwa na tatizo la ukosefu wa ajira kwani taarifa ya mwenendo wa ajira ulimwenguni ya mwaka 2019 iliyotolewa na Shirika la Kazi la Duniani (ILO), inatueleza bayana ya kwamba zaidi ya watu milioni 170 duniani hawana kazi ikiwa ni sawa na asilimia 5.1 na wafanyakazi bilioni mbili wapo katika ajira isiyokuwa rasmi ikiwa ni sawa na asilimia 61.2. 

Pia kulingana na Shirika la Maendeleo ya Viwanda la Umoja wa Mataifa (UNIDO) kwa kila mwaka wahitimu zaidi ya 700,000 huingia sokoni lakini ni takribani wahitimu 40,000 wanaopata ajira serikalini pamoja na kwenye mashirika binafsi.

Ni kutokana na na hali hiyo hata Rais wa awamu ya tatu, Benjamini William Mkapa katika kitabu chake cha “Maisha Yangu Wajibu Wangu”(My life My purpose), alionyesha hofu yake juu ya tatizo hili hasa kwa vijana ambao wengi wao wanazagaa mtaani pasipo kuwa na shughuli za kufanya, anasema “Ninatishika kwa kweli ninavyoona vijana wengi wakiwa mtaani bila ya kuwa na shughuli za kufanya na kibaya zaidi hakuna mipango ya haraka ya kukabiliana na tatizo hili la ajira,” Mkapa anasema nchi lazima iwe na mipango endelevu ya kukabili tatizo la ajira kwa vijana na hasa wale wanaohitimu vyuo na shule mbalimbali.

Wadau mbalimbali wa elimu kutoka kada tofauti tofauti akiwemo Waziri Mkuu mstaafu, Mizengo Pinda wamekuwa wakishauri mfumo wetu wa elimu ubadilishwe ili kuruhusu wanafunzi kujikita zaidi kwenye stadi za ufundi na ujasiriamali kuliko hali ya mfumo ilivyo sasa ambapo elimu imejikita zaidi kwenye nadharia kuliko uhalisia kitu ambacho hata mimi binafsi naunga mkono. 

Lakini pia ningependa kuongeza ya kwamba tatizo la ajira lipewe kipaumbele inavyopaswa, sambamba na mikakati mathubuti yenye matokeo halisi katika kukuza uchumi na kuleta hali ya ustawi kwa jamii yetu. 

Pili katika zama hizi za matumizi makubwa ya teknolojia na uchumi jumuishi imethibitika kuwa ni sekta ya biashara ndogo na za kati (Small and Medium Enterprises), kwa bidhaa na huduma ndiyo pekee muarobaini wa kutatua tatizo la ajira. Hii ni kutokana na utafiti wa Dk. Samwel Muriith wa Chuo Kikuu cha Daystar University nchini Kenya, hivyo wajibu wa serikali katika kutatua tatizo la ajira ni kutambua na kuchagua sekta zinazoweza kuleta matokeo yanayotarajiwa na kuweka  mazingira wezeshi kushughulikia uwezeshaji.

Mambo haya yataruhusu kuanzishwa biashara nyingi maeneo mbalimbali ya nchi yetu, yataruhusu biashara hizo kukua na hatimaye kusaidia kupunguza tatizo la ajira kwa kiwango kikubwa. Itaendelea.

Mwandishi ni mchambuzi wa masuala ya kisiasa na kijamii. Anapatikana kupitia; 

0766354819,  HYPERLINK “mailto:ernestfrank606@gmail.com” ernestfrank606@gmail.com