Home Makala Nini nafasi ya teknolojia ya mwanga katika sekta ya uvuvi

Nini nafasi ya teknolojia ya mwanga katika sekta ya uvuvi

258
0
SHARE
Wataalamu kutoka chuo cha Wofsburg cha nchini Ujerumani wakiendelea kutoa mafunzo jijini Mwanza jinsi ya kutumia, kutengeneza na kufanyia marekebisho taa za kisasa zilizobuniwa na Chuo hicho kwa kushirikiana na Tarea kwa ajili ya matumizi ya shughuli za uvuvi Ziwa Victoria. 

Na YOHANA PAUL-MWANZA

SEKTA ya uvuvi nchini ni miongoni mwa sekta zinazochangia kwa kiasi kikubwa katika pato la taifa sambamba na kutoa ajira nyingi kwa watu wanaojishughulisha na uvuvi, viwanda vya samaki pamoja na kina mama wajasiriamali wanaojishughulisha na uuzaji wa samaki kwenye masoko.

Miongoni mwa maeneo yenye mchango mkubwa kwenye sekta hii nchini ni maeneo ya kanda ya ziwa huku Mkoa wa Mwanza ambao ndio umechukua eneo kubwa la Ziwa Victoria ukiwa ndiyo mhimili wa sekta ya uvuvi katika eneo hili.

Ili kukuza sekta mbalimbali nchini ikiwemo uvuvi sina shaka kuwa maendeleo ya utumiaji wa vifaa vya kisasa vinavyoendana na maendeleo ya sayansi na teknolojia umekuwa na nafasi kubwa katika kuongeza uzalishaji wa mazao.

Kwa kulitambua hilo Jumuiya ya Wadau wa Nishati Jadidifu Tanzania (Tarea)   Kanda ya Ziwa mwezi uliopita ilitoa semina elekezi kwa wavuvi wanaofanya kazi zao ndani ya ziwa Victoria ili kutambulisha teknolojia ya taa mpya zilizobuniwa kwa kushirikiano na chuo kikuu cha Wolfzburg-Ujerumani kulenga kuboresha, kupunguzia gharama ya nishati hiyo pamoja na kudhibiti uchafuzi ziwani.

Utambulisho wa taa hizo ulienda sambamba na kutoa mafunzo kwa wavuvi ili kuwaongezea uelewa wa matumizi ya teknolojia hiyo pia na kuwafundisha ujuzi mafundi wa vifaa vya umeme ili waweze kuunda wenyewe taa hizo mbadala zilizobuniwa na wanafunzi wa chuo hicho na kuifanya sekta ya uvuvi ndani ya Ziwa Victoria kufanywa bila kuharibu mazalia ya samaki na kwa gharama nafuu.

Akizungumuzia mradi huo jijini Mwanza Katibu Mtendaji wa Tarea Kanda ya Ziwa, Jacob Ruhonyora anasema wameamua kuja na mradi huo ili kukabiliana na athari zinazotokana na matumizi ya taa za mafuta ya taa ambazo ni chanzo kikubwa cha hewa ya ukaa yenye madhara kwa viumbe wa majini na huchangia kwa kiasi kikubwa kuharibu mazalia ya samaki.

Ruhonyora anasema mbali na kukabiliana na uharibifu unaochangiwa na utumiaji wa taa za mafuta maarufu kama chemuli pia wanalenga kuwasaidia wavuvi kupata nishati mujarabu kwa gharama nafuu kiuendeshaji ambapo anaeleza kuwa taa hizo mpya walizoleta zitauzwa kwa gharama ya kawaida na zinaweza kutumika kwa takribani miaka mitatu.

Katibu huyo wa Tarea anasema kwa kutambua kuwa baadhi ya wavuvi wamekuwa wakitumia njia za asili kama sehemu ya kudumisha mila na tamaduni na kuamini kuwa zina msaada mkubwa katika kupata mazao mengi ya dagaa na samaki wao kwa kutumia nafasi waliyonayo wanaendelea kutoa elimu kwenye vyombo vya habari.

Kwa upande wao mwezeshaji wa mradi kutoka Chuo Kikuu cha Wolfzburg cha nchini Ujerumani, wanasema wameamua kulichagua jiji la Mwanza kama eneo la mradi kwa sababu majiji haya yamekuwa na mahusiano ya karibu kwa miaka mingi hivyo Tarea baada ya kubaini nyenzo duni za mwanga zinazotumiwa na wavuvi hasa wa ziwa victoria walifanya mawasiliano na chuo hicho ili kusaidia kubuni taa zitakazokuwa na msaada mkubwa kwa wavuvi wanaofanya kazi zao usiku ndani ya Ziwa Victoria.

Kiongozi wa mradi huo kutoka chuo cha Wolfzburg anasema wamelenga kuleta suluhu ya kudumu kwa wavuvi wa Ziwa Victoria na ndio maana sambamba na kutambulisha taa hizo za kisasa ambazo wamezibuni pia wanatoa mafunzo kwa mafundi wa vifaa vya umeme kutoka Mwanza ili waweze kuunganisha vifaa vya taa hizo ama kuzifanyia marekebisho bila kutegemea mafundi kutoka nje.

Anasema mafunzo hayo yatapanua wigo wa teknolojia hiyo hata kwenda mikoa mingine na kuwafikia wavuvi wanaofanya kazi kwenye maeneo tofauti na Ziwa Victoria na pengine kupitia hao wachache waliopata fursa ya kufundishwa jinsi ya kutumia na kutengeneza taa hizo teknolojia hiyo inaweza kuenea Tanzania nzima.

Anasema kikubwa Watanzania wanachotakiwa kuelewa ni kuwa teknolojia ya taa hizo imefanyiwa majaribio na ufanisi wake umeonekana kuwa wa kiwango cha juu hivyo waunge mkono matumizi ya taa hizo za kisasa ambazo si tu zina uwezo mkubwa wa Mwanga lakini pia zimetengenezwa ili kukidhi gharama ya wananchi wa kawaida kabisa na matumaini yao ni kuwa zitasaidia kuinua kwa kiwango kikubwa sekta ya uvuvi ndani ya Ziwa Victoria.

Amini Abdullah ni Mratibu wa mradi huo kutoka Mwanza, anasema ujio wa mradi wa taa hizo za kisasa unaendana na sera za kupambana na mabadiliko ya tabia ya nchi na mazingira kwa ujumla wake hasa ndani ya Ziwa Victoria unaosababishwa na wavuvi kutumia nyenzo zinazochangia athari kubwa majini pasipo wao kujua.

Anaeleza baada ya kuongeza mwamko kwa wavuvi kutumia taa ndogo za sola walipokea malalamiko juu ya utendaji kazi wa taa hizo ukilinganishwa na gharama yake ndipo wao kama Tarea waliamua kushirikiana na chuo Kikuu cha Wolfzburg kufanya utafiti na kubuni aina bora ya taa zenye msaada kwa wavuvi kwa ufanisi na gharama yake.

Anasema taa zilizobuniwa zitauzwa kwa gharama nafuu na zitakuwa na ufanisi mkubwa ikilinganishwa na taa zile za sola za awali ambazo zimekuwa zikiuzwa hadi Sh 400,000 kiasi ambacho ni kikubwa na wavuvi wengi wameshindwa kukimudu.

Anaeleza ingawa mradi unasimamiwa na Tarea lakini mawazo ya kubuni taa za aina hiyo ulianza na wavuvi wenyewe kwa kutumia betri za magari na pikipiki baada ya kuelewa athari za mafuta ya taa.

Amin anasema mapokeo ya taa zilizobuniwa na chuo hicho yameonekana kuzaa matunda na kuwa na ufanisi mkubwa kwani baada ya kupokea taa hizo waliwashirikisha wavuvi na kuzifanyia majaribio yaliyoonyesha majibu chanya.

Mratibu huyo wa mradi anasema baada ya kujiridhisha ufanisi wa taa hizo ndipo wameamua kutoa semina ya awali kwa wavuvi juu ya matumizi ya taa hizo, semina ambayo inaenda sambamba na mafunzo kwa mafundi watakaoweza kufanya matengenezo ya taa hizo bila kutegemea wataalamu kutoka nje.

Anafafanua kuwa Tarea wamenuwia kupanua wigo wa matumizi ya teknolojia sahihi ya mwanga kutoka Ziwa Victoria na kwenye maeneo mengine ili mwisho wa siku wavuvi wote nchini waendeshe shughuli zao bila madhara, kwa gharama nafuu na bila kukumbana na kikwazo cha mwanga.

“Nakumbuka kutokana na dhana hiyo kuwa taa za sola zinaharibu mazalia ya samaki taa hizo zilizuiwa kuanzia Oktoba mwaka 2018 hadi Februari mwaka jana ndipo zikaruhusiwa na sote tulijionea gharama ya dagaa ilipanda mara dufu kwani wavuvi walirudi kutumia chemuli na vibatari zenye gharama kubwa kiuendeshaji kutokana na matumizi ya mafuta ya taa.

“Ni lazima sasa tutambue kuwa teknolojia ya mwanga inayo nafasi kubwa sana katika sekta ya uvuvi na ndio maana sisi kama Tarea tumeamua kulisimamia hili ili kuleta suluhu ya kudumu kwa wavuvi na kuboresha zaidi sekta ya uvuvi kwa kutumia nyenzo za kisasa zaidi,”anasema Amin.

Mtisi Hezroni ni mmoja wa mafundi waliobahatika kupatiwa mafunzo ya utengenezaji wa taa hizo za kisasa, anasema mafunzo hayo yamekuwa na maana kubwa kwao kwani yatapanua wigo wa ajira na yamewaongezea utaalamu wanaoweza kusambaza kwa watu wengine.

Wilbert Kamanzi, Katibu wa Kikundi cha Kuhamasisha Uboreshaji wa Mazingira Ziwa Victoria, anasema ujio wa taa hizo unakuja kuleta suluhu ya muda mrefu ambapo mwanga umekuwa kikwazo kikubwa kwa wavuvi wengi na kwa namna tofauti taa wanazotumia wavuvi zimekuwa zikiharibu mazalia ya samaki.

Sebastian Boniphace, Mwenyekiti wa Kikundi cha Wavuvi cha Bwiru Kijiweni anasema mbali na ujio wa teknolojia hiyo mpya ya mwanga lakini bado kuna haja ya serikali na taasisi zingine za kifedha kuangalia namna ya kurahisisha masharti kwa wavuvi kupata mikopo ili waweze kumudu gharama ya teknolojia mpya ya mwanga kwani una mchango mkubwa kwa sekta ya uvuvi.