Home Makala Nini tofauti ya kutekw, kukamatwa?

Nini tofauti ya kutekw, kukamatwa?

401
0
SHARE

Dk. Helen Kijo Bisimba 

Wiki iliyopita iliisha vibaya kwa sisi wanaharakati wa haki za binadamu hapa nchini na kwingine kote. Ilikuwa majira ya saa tano tulipopokea taarifa  za kutekwa kwa mwanaharakati mwezetu ambaye ni Ofisa Program wa Elimu kwa Umma Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu, Tito Magoti. 

Taarifa hii iliogofya na ilizua taharuki hasa kwa wafanyakazi wenzake. Tito kama ilivyokuwa kwa wafanyakazi wote wa kituo hicho alikuwa likizo na alikuwa anajipanga kusafiri siku hiyo.

Taarifa zilieleza kuwa alikuwa akishuka kwenye pikipiki [bodaboda] aliyoikodi, ndipo walipotokea watu watano wakamshika na kumwelekeza katika gari lao akiwa bado na kofia ngumu aliyoivaa  akiwa kwenye pikipiki, aliingizwa ndani ya gari hilo kwa nguvu baada ya kuonesha kutotaka kuingia.

Baada ya ndugu na rafiki na wanakituo kujaribu kumpigia simu ambayo haikupatikana ilionekana wazi kuwa ametekwa, hivyo walifika vituo mbalimbali vya polisi kuulizia iwapo amefikishwa mashuhuda waliokuwa katika eneo alilodaiwa kutekwa walisema kuwa walioegesha gari hapo walijitambulisha kuwa ni polisi na wako hapo kwa kazi ya kumkamata mhalifu hivyo wakiona purukushani wasishangae. 

Kila kituo cha polisi walipofika hakuwapo Tito hivyo wakaenda kutoa taarifa ya kupotea  au kutekwa kwa Tito katika Kituo cha Poilisi  Mabatini ambapo waliambiwa kwa mujibu wa sheria taarifa ya kupotea kwake itaandikwa baada ya masaa 24 tangu apotee.

Ilibidi LHRC kutoa tamko juu ya hali hiyo na watu mbalimbali wakainua na kupaza sauti mitandaoni wakidai Tito arejeshwe.  Wakati wote huo Jeshi la Polisi walikuwa wamesema hawamshikilii mtu huyo. 

Baada ya saa tano watu walifika nyumbani kwa Tito wakiwa na sare za polisi na silaha na wakajitambulisha kuwa ni polisi wamekwenda kufanya upekuzi. Baada ya saa moja Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Lazaro Mambosasa, alitangaza kupitia vyombo vya habari kuwa watu waache uzushi, Tito hajatekwa bali amekamatwa na jeshi la polisi pamoja na watu wengine watatu kwa makossa ya jinai. 

Watu hao watatu wengine hawakutajwa na hilo kosa lao nalo halikutajwa. Hapa ndipo tulipopata mkanganyiko wa kisheria kutaka kujua ni wakati gani mtu husemekana amekamatwa na wakati gani tunaweza kusema ametekwa. 

Bahati nzuri tuna sheria zinazosimamia masuala ya jinai hapa nchini zinazofafanua mtu anavyoweza kukamatwa akiwa amefanya kosa la jinai au akiwa anashukiwa kufanya kosa la jinai. 

Kwa mujibu wa Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai sura namba 20 kama ilivyorejewa mwaka 2002 utaratibu wa kumkamata mhalifu au mtuhumiwa wa uhalifu uko wazi. 

Askari anapokwenda kumkamata mtu ambaye si hatari kwa maana ya kuwa na silaha au asiyekubali kukamatwa, askari anatakiwa ajitambulishe na amweleze mshukiwa kuwa anataka kumweka chini ya ulinzi. Pia anapaswa kumtajia kosa linalofanya amkamate. 

Raia anayekamatwa ana haki ya kuwataarifu ndugu zake na hata wakili wake kuwa amekamatwa, mtu aliyekamatwa anapaswa kupelekwa kituo cha polisi na afikapo pia ana haki ya kuomba wakili wake awepo akiwa anatoa maelezo. 

Askari wakihitaji kufanya upekuzi kwenye gari, nyumba au ofisi ya wanayemtuhumu wanapaswa kuwa na hati ya upekuzi ambayo hutolewa na mahakama na wawepo mashahidi kushuhudia upekuzi huo.

Polisi huweza kutumia nguvu kumkamata mtu yule anayekataa kukamatwa na iwapo ataonesha wazi kuwa anataka kuwadhuru au kudhuru watu wengine katika eneo la kukamatwa. 

Iwapo sheria ipo wazi hivi tulipata shida pale askari walivyodai kuwa Tito hakutekwa bali amekamatwa. Iwapo Tito Alikamatwa tulitegemea awe amewasiliana na ndugu au mtu yeyote aliye karibu naye kueleza amekamatwa. 

Tulitegemea awe katika Kituo cha polisi kinachofahamika ili kama kawaida aweze kuonekana na kupatiwa mahitaji muhimu kwa vile atakuwa bado ni mtuhumiwa aliye rumande. Ikiwa Tito amekamatwa tulitegemea baada ya saa 24 awe amepelekwa mahakamani na shtaka lake lijulikane. 

Iwapo Tito alikamatwa tulitegemea  aweze kudhaminiwa akiwa polisi hasa iwapo kosa lake linajulikana kwa vile mtu hukamatwa kutokana na polisi kuwa na taarifa ya tuhuma  dhidi yake. Hata baada ya siku nne yote hayo yalikuwa hayajatokea hivyo kilichotokea lazima kionekane kuwa ni  utekaji. 

Jinsi alivyonyakuliwa hapo kwenye  eneo la tukio haikuwa ukamataji kwa kiwango chochote na iwapo jeshi la polisi linataka kutuaminisha kuwa wamebadili njia ya ukamataji na kuwa wanaweza kuwa katika gari lisilo la polisi na askari wasio na sare za polisi na kumnyakua tu  mtu  hii haiwezi kuwa sahihi.

Tunakuwa na hofu kwa vile hili si tukio la kwanza wapo watu kama Abdul Nondo waliochukuliwa kwa njia hiyo na baadaye ikasemekana amejiteka mwenyewe. Wapo watu ambao hawakuonekana tu yaani walipotea na haikujulikana walipoteaje.

Jeshi la polisi litusaidie raia kwani wakati mwingine watatokea watu wakajitambulisha kuwa ni polisi na raia wasiwaamini jambo ambalo linaweza kuleta maafa nchini hasa watakapoamua kuchukua sheria mkononi jambo ambalo hatuombei litokee.

Kwa hili la Tito  tumepata funzo kubwa kwamba mtu anaweza kutekwa kweli tukadhani amekamatwa au mtu anaweza kukamatwa kwa njia hii mpya tukadhani ametekwa. Katika nchi inayoheshimu haki za binadamu na utawala wa sheria ni vibaya kabisa kuacha mambo yaendelee hivi. 

Tunajua vipo vyombo mbalimbali vya ulinzi na usalama hapa nchini lakini vyombo vyote hivi vipo chini ya mamlaka ya sheria. Masuala yote ya jinai yanapaswa kushughulikiwa na Jeshi la Polisi kwa mujibu wa sheria.  Vyombo vingine vikikutana na masuala ya jinai dhidi ya raia vinapaswa kupeleka suala hilo polisi labda tu kama vina mamlaka mahsusi kama ilivyo kwa Takukuru na vinginevyo.
Uhuru wa mtu ni muhimu ikiwa ni moja ya haki za msingi, anaposhikiliwa mtu kwa njia kama hii kwanza uhuru wake umeingiliwa, usalama wake uko shakani na pia inazua taharuki kwa jamii kwa ujumla, jambo ambalo si haki wala sawa  katika nchi hii inayopaswa kuwa na amani kabisa. 

Iwapo mtu ni mhalifu taratibu zifuatwe na apelekwe sehemu husika kama sheria inavyohitaji. Haipaswi kabisa chombo kinachoheshimika kama polisi kuzua taharuki ndani ya jamii wakati kina weledi mkubwa wa jinsi kinavyopaswa kufanya kazi. 

Tunazidi kutahadharisha mamlaka zote nchini kuacha kufanya mambo nje ya utaratibu wa sheria maana madhara yake huenda yakaleta shida kubwa nchini kuliko tunavyofikiria. 

Mhalifu au anayeshukiwa kuwa mhalifu akamatwe na si kutekwa   au kufanya watu waone ametekwa. Heshima ya sheria na haki za binadamu  ni muhimu  katika jamii yetu  ili amani yetu iendelee kuwapo. 

Imeandikwa na Dk. Helen Kijo Bisimba