Home Latest News NISHATI JADIDIFU MBADALA ENDELEVU WA MAKAA YA MAWE

NISHATI JADIDIFU MBADALA ENDELEVU WA MAKAA YA MAWE

4799
0
SHARE

NA GABRIEL MUSHI                      


MAKAA ya mawe ni aina ya mwamba mashapo, au mwamba metamofia na fueli kisukuu muhimu. Miamba hii ilitokea kutokana na mabaki ya mimea ya kale iliyogeuzwa kuwa aina ya mwamba katika mchakato unaochukua muda wa mamilioni ya miaka.

Tanzania ni mojawapo ya nchi duniani zilizosheheni makaa ya mawe ambayo ni chanzo kikuu cha nishati ya umeme. Kulingana na ugunduzi uliofanywa na watalaamu mbalimbali nchini, madini haya yanapatikana katika mikoa ya Ruvuma, Songwe na Njombe.

Mkoani Ruvuma, madini hayo yanachimbwa wilayani Mbinga na kampuni ya Tancoal katika mgodi wa Ngaka ambao ulianza shughuli za uchimbaji tangu mwaka 2011.

Kwa mujibu wa utafiti wa awali uliofanywa na wajerumani mwaka 1952, ulibaini kuwepo kwa madini ya makaa ya mawe tani milioni 79, na utafiti uliofanywa tena mwaka 2001 ulibaini kuwepo kwa madini ya makaa ya mawe kati ya tani milioni 200 hadi milioni 400 ambayo yanatarajiwa kuchimbwa kwa zaidi ya miaka 50 katika eneo hilo la Ngaka.

Mkoani Songwe, madini hayo yanachimbwa wilayani Ileje katika mgodi wa Kiwira tawi la Kabulo. Awali mgodi wa Kiwira ulianza shughuli za uchimbaji mwaka 1988 hadi mwaka 2008 kabla ya kuanza tena Aprili mwaka jana katika tawi la Kabulo.

Mgodi huo unakadiriwa kuwa na hazina ya makaa ya mawe tani milioni 35 ambazo zinatarajiwa kuchimbwa kwa zaidi ya miaka 50 vilevile.

Mkoani Njombe, madini ya makaa ya mawe yanatarajiwa kuchimbwa katika mgodi wa Mchuchuma ambao upo wilayani Ludewa. Eneo hilo linakadiriwa kuwa na tani za madini hayo zaidi ya milioni 536.

Athari za makaa ya mawe

Licha ya madini hayo kuwa na matumizi muhimu lukuki hususani katika uzalishani wa umeme unaotumika viwandani, shughuli za uchimbaji na matumizi yake bado zina athari mbalimbali kwa mwanadamu.

Kwa mujibu wa ripoti za Shirika la Mazingira la Umoja wa Mataifa zimebainisha kuwa moshi na chembechembe ndogo za makaa ya mawe husababisha vifo vya mapema zaidi ya 50,000 na kuathiri watu zaidi ya 400,000 ambao hupatwa na maambukizi  ya ugonjwa wa Mkamba (Bronchitis). Mkamba unatokana na maambukizo ya mifereji inayoingiza hewa mapafuni na kusababisha kikohozi chenye sauti mara kwa mara ikiambatana na makohozi.

Pia kwa mujibu wa ripoti ya taasisi ya Worldwatch iliyotolewa mwaka jana ilibainisha kuwa kila mwaka zaidi ya vifo milioni 1.5 duniani husababishwa na uchafuzi wa hewa unaotokana na makaa ya mawe.

Aidha, baadhi ya watalaam waliozungumza na RAI walibainisha kuwa uchimbaji uliofanyika katika migodi inayoendelea na shughuli zake kwa sasa pia umekuwa chanzo cha athari mbalimbali ikiwamo ugonjwa wa kifua kikuu (TB).

Mtaalamu wa masuala ya mazingira na uhifadhi endelevu, Dk. Michael Haule ambaye ni mwenyeji wa wilaya ya Mbinga mkoani Ruvuma penye mgodi wa Ngaka, anasema uchafuzi wa mazingira unaotokana na shughuli za uchimbaji katika mgodi huo zimesababisha malalamiko na athari nyingi kwa wananchi athari.

“ Mimi ni mzaliwa wa kijiji cha Litui, kipo kilimoita chache kutoka kwenye mgodi, ninapozungumzia athari za uchimbaji wa makaa yam awe ninaweza kuthibitisha kuwa nimeziona na wananchi wenzangu kweli wanaathirika.

“Kwa sababu uchimbaji unaofanyika kwenye mgodi ule ni uchimbaji wa wazi, hawachorongi ndani kwa ndani kwa kutumia teknolojia ya kisasa kama nchi nyingine mfano Afrika kusini wanavyofanya, vilevile hata upakiaji na usafirishaji wa makaa hayo ni wa wazi.

“Kwamba yale malori yanayopakia makaa hayo hayafunikwi chochote, na hata yakipata ajali makaa yakimwagika njiani, hawayazoi, matokeo yake yanasambaa na kuleta athari kwa wananchi hasa ikizingatiwa barabara kule ni mbovu.

“Hapa ninamaanisha kuwa vumbi lile la makaa yam awe linawaathiri wananchi na hata kuingia kwenye maji ambayo yatatiririka kwenye mto Mungaka uliopo karibu na mgodi, mto huo hupeleka maji ziwa Nyasa, na kuna kipindi samaki walikufa katika ziwa hilo na tathmini ikaonesha ni sababu ya sumu ya makaa yam awe,” anasema .

Aidha, anasema madhara mengine ni pamoja na wananchi waliokuwa wakazi wa eneo la mgodi huo kutolipwa stahiki zao pindi walipotakiwa kuhama kupisha mgodi.

“Taaluma ya udaktari wangu unatokana na masuala ya mazingira hivyo nafahamu kabisa makaa yam awe ni sumu. Hivyo yanapaswa kuchimbwa kwa umakini na teknolojia ya kisasa.  Kunatakiwa kufanyike upembuzi yakifu ili kubani madhara yake zaidi,” anasisitiza.

Hoja hiyo inaungwa mkono pia na Mhandisi wa masuala ya madini kutoka taasisi ya ,Emmanuel Mbeya ambaye anasema kiujumla uchimbaji wa makaa ya mawe hapa nchini hutumia fedha nyingi lakini hayatumiki vizuri.

Anasema kwa upande wa uchimbaji unaoendelea katika mgodi wa Kabulo, bado haujaonesha athari kubwa kwa kuwa hakuna shughuli kubwa za uchimbaji zinazofanyika.

“Licha ya kwamba makaa ya mawe yana athari lakini kuna mbinu ya kisasa ya kuondoa uchafuzi huo, na teknolojia hiyo ni ghali sana sasa sijui kwa nchi yetu kama tunaweza kufikia huko.

Nini kifanyike

Kwa kuwa Tanzania inaongoza Afrika Mashariki kwa kuwa na hifadhi ya makaa ya mawe inayofikia tani bilioni 1.5, ipo haja ya kufanya tathmini ya kina kuhusu athari na faida za madini hayo kabla ya kueleke katika uchimbaji wa makaa ya mawe katika mgodi wa mchuchuma.

Kwa sababu taarifa za uchimbaji haramu wa makaa ya mawe zinasema tayari unaendelea na kwamba kiasi kikubwa cha maji yatakuja kutumiwa na tayari yanatumiwa kutoka kwenye mito. Miti mingi itachafuliwa na madini ya risasi na sumu nyingine, kama ilivyo kwa hewa ya sulphur na carbon dioxide.

Baadhi ya watalaam wanashauri umuhimu wa kuzingatia matumizi ya nishati jadidifu. Nishati jadidifu ni nishati ambayo vyanzo vyake ni endelevu na ni bora kutokana na kuzalisha kiasi kidogo cha hewa ya ukaa.

Hii inatokana na ukweli kuwa hewa ya ukaa ni chanzo kikubwa cha mabadiliko ya tabianchi ambayo athari zake ni hali mbaya ya hewa inayotokana na wingi wa hali ya hewa ambayo haihitajiki katika mfumo wa maisha ya binadamu na wakati mwingine kusababisha mvua za Elnino na mafuriko.

Kwa mujibu wa ripoti mbalimbali zinaonesha kwa zaidi ya tani bilioni tisa za hewa ukaa zinatolewa angani kila siku kutokana na shughuli za kibinadamu ikiwamo za viwandani.

Hivyo umefika wakati sasa wa kuhamia kwenye nishati jadidifu kama vile mionzi ya jua (Solar Energy), upepo, maporomoko ya maji, bayogesi na mvuke joto mkaa endelevu.

0715126577