Home Makala NORWAY NI NCHI YENYE FURAHA KULIKO ZOTE DUNIANI

NORWAY NI NCHI YENYE FURAHA KULIKO ZOTE DUNIANI

2805
0
SHARE
Watu wa Norway wakifurahia maisha yao.

Hali ya baridi kali haizuii Norway kujivunia hali ya kuwa nchi yenye furaha kuliko nchi nyingine zote duniani, kufuatana na ripoti ya Umoja wa Mataifa iitwayo “Ripoti ya Furaha Duniani” iliyotolewa Jumatatu wiki hii.

Norway ilipanda kutoka nafasi ya nne mwaka jana hadi juu kabisa ingawa bei ya mafuta yasiyosafishwa yanayozalishwa na nchi hiyo imeshuka sana. Miongoni mwa nchi nne za juu ni zile za jirani yake za Scandinavia – Denmark, na Icelend. Pia Uswisi imo.

“Nchi zote hizo nne za juu ziko nafasi ya juu katika vigezo vyote vinavyozifanya kuwa na furaha kama vile, uhuru, serikali kuwajali raia wake, ukarimu, uaminifu, afya, kipato na utawala bora,” ripoti hiyo ilisema katika muhtasari wake.

Nchi zingine katika kumi za juu ni Filand (ya 5), Uholanzi (6), Canada (7), New Zealand (8), Australia na Sweden zikifungana katika nafasi ya 9.

Nchi zote kumi ni nchi tajiri zilizoendelea. Hata hivyo fedha si kigezo pekee katika kuleta furaha katika nchi, ripoti iliendelea kusema.

Ripoti inaendelea kusema kwamba miongoni mwa nchi tajiri, tofauti katika viwango vya kuwa na ‘furaha’ inatokana na tofauti katika afya ya kiakili (mental health), afya ya kimwili (physical health) na mahusiano binafsi na watu wengine – na kwamba chanzo kikubwa cha tabu na huzuni ni magonjwa ya kiakili.

Inasema tofauti za kipato ni sababu kubwa ya kukosa furaha katika nchi za masikini, ingawa magonjwa wa kiakili pia ni chanzo kingine cha huzuni.

Nchi nyingine kubwa – China – imepiga hatua kubwa kiuchumi katika miaka ya karibuni, lakini watu wake hawana furaha zaidi ya walivyokuwa miaka 25 iliyopita, ripoti inasema.

Na kwa upande wake, Marekani imeporomoka hadi kufikia nafasi ya 14 kati ya nchi 155 kutokana na mchango mdogo wa serikali kwa jamii, pamoja na ufisadi mkubwa – sababu ambazo kwa kutokuwa navyo ndivyo zimezifanya nchi za Scandinavia kufanya vyema.

Na inadaiwa kwamba chini ya sera za Donald Trump nchi hiyo itashuka zaidi katika viwango vya furaha kwa wananchi wake.

Inadaiwa kwamba Marekani ni nchi ambayo inatafuta ‘furaha’ kutoko sehemu zisizo sahihi, anasema Jeffrey Sachs mhadhiri wa uchumi wa Chuo Kikuu cha Columbia, New York ambaye alihusika katika utayarishaji wa ripoti hii. Anasema Marekani inazama katika mgogoro ndani ya jamii, mgogoro ambao unazidi kuwa mkubwa siku hadi siku.

Nchi hiyo yenye uchumi mkubwa zaidi duniani iko nyuma sana kwa Norway, ingawa iko juu ya Ujerumani (iliyo nafasi ya 17), Uingereza (19) na Ufaransa (32).

Nchi zenye na tabu na huzuni kubwa duniani ziko Mashariki ya Kati na Bara la Afrika, huku nchi zenye vita – Yemen na Syria ziko miongoni mwa nchi kumi za chini, kufuatana na ripoti ya Umoja wa Mataifa. Tanzania, Burundi na Jamhuri ya Afrika ya Kati zimo katika nchi tatu za mwisho kabisa zenye huzuni na tabu.

Ripoti hii ya Umoja wa Mataifa inatokana na kura za maoni za taasisi ya Gallup International iliyochunguza maisha ya watu katika nchi husika, viwango vya ufisadi, ukarimu, na uhuru na mwaka huu ilikuwa na taarifa maalum kuhusu kupungua kwa furaha nchini Marekani.