Home Makala NUKUU YA KUMBUKUMBU YENYE MACHUNGU

NUKUU YA KUMBUKUMBU YENYE MACHUNGU

1326
0
SHARE

NA PROF. HANDLEY MAFWENGA


MEI 21, mwaka 1996, ndugu, jamaa, rafiki na jirani zetu walipoteza maisha katika ajali mbaya na ya kihistoria kutokea nchini.

Ni ajali ya Meli ya MV-Bukoba iliyozama ndani ya kina kirefu cha maji ya Ziwa Victoria, ikiwa ni miezi michache ya utawala wa Serikali ya awamu ya tatu. Ilikuwa ni simanzi.

Niwaambie Watanzania wenzangu, ukweli ni kwamba, hakuna mtu yeyote mwenye kutamani kufa kifo walichokumbana nacho wenzetu miaka 21 iliyopita.

Kifo kile cha ajali ya MV-Bukoba kilikuwa ni kifo kilichojaa tamaa ya wokovu, yaani kila aliyekufa kwa ajali ile alitamani kuokolewa ili aendelee kuishi.

Jambo ninaloliamini ni kuwa hata watu wanaotaka kufa na kwenda mbinguni moja kwa moja kwa Baba hawatamani kufa kwa kifo cha namna ile na upo uwezekano hawako tayari kufa kabisa!

Pamoja na ukweli huo wa wengi wetu kukiogopa kifo, bado agano hilo litasalia kuwa msalaba wetu kwa kila binadamu kuyaonja mauti.

Wote tutakipata kifo, tutake tusitake, itakuwa hivyo tu ingawa mara zote kifo kimekuwa kikituachia uchungu, majonzi na upweke usio koma hapa duniani.

Hakuna mtu aliyeweza kukwepa kifo hata Lazaro aliyefufuliwa na Yesu leo hii hayupo tena nasi, ameshakufa.

Hii inaamanisha kifo ni kitu pekee kilichogundulika katika maisha yetu, kifo ni wakala wa mabadiliko ya maisha, kutoka maisha ya hapa duniani kwenda maisha ya kuzimu.

Kifo kinaondoa uhai wa kilichopo, kinatunyima raha ya kupata utamu wa maisha ya dunia na kinatuondolea shida tunayoipata duniani.

Kifo huweka uhai kwa kinachozaliwa kupata ladha ya maisha ya dunia, huwa najiuliza mtoto anayezaliwa kwanini analia ili kupata uhai?

Kwanini mtoto yule asije duniani kimyakimya au kwanini asiingie duniani kwa kicheko? hii inadhihirisha dunia imetawaliwa na mateso zaidi ya furaha.

Hapa ni wazi tumefumbwa maono na ufahamu, binafsi ningependelea kuyaona maisha ya uzima baada ya kifo.

Kwamba kiumbe kinachokufa kipate tena pumzi ya kurejea uzimani ili kuja kuyaeleza yale aliyoyaona alipokumbwa na umauti.

Labda nafasi hiyo ingetoa muda kwa watu kujifunza kuhusu dunia na vitu vingine. Nayasema haya kwa sababu ya kutamani kuwaona ndugu zangu waliokufa kwa ajali ya MV-Bukoba wakiishji tena leo.

Wakipata nafasi ya kutusimulia hali waliyokutana nayo huko na pengine nini kiliwasababishia hasa kutowesha roho zao.

Warudi waje watuchambulie na kutuoanishia tofauti ya maisha ya ulimwenguni na ahera, ni fumbo kubwa.

Nani hatamani kujua kilichowasibu ndugu zetu wale, nani hayuko tayari kuridhia kulifuta tukio lile kwenye ulimwengu huu?

Bila shaka hakuna asiyetamani kuyajua niliyoyahoji hapo juu, lakini ukweli utabaki pale pale kuwa hakuna mwenye kutujibia maswali hayo, zaidi ya kumwomba Mungu atuepushe na madhila mengine yenye kulingana ama kufanana na yale ya MV-Bukoba.

Kifo kimechukua roho za ndugu zetu waliokuwa wakisafiri kwa upendo, wakitegemea kwenda kujumuika na wazazi wao, bibi zao, babu zao, watoto wao, dada zao, kaka zao, kuwajibika katika kazi zao, kuwahudumia wasiojiweza na pengine hata kutangaza injili, wote hao hawakufanikiwa kutimiza malengo yao, walikufa vifo vya uchungu ndani ya maji, miili yao ilielea kama maboya, wapo ambao miili yao iligeuka chakula cha samaki.

Kupoteza mamia ya watu si jambo dogo, linaumiza na kutesa moyo, kadhia hii itaendelea kuliumiza Taifa miaka na miaka.

Takribani watu 800 kufa kwa pamoja ni jambo linaloacha imani kuwa kifo hakina hofu wala woga, kinaweza kupambana hata na mamilioni ya watu ndani ya dakika moja.

Kwa hisabati za Kushirikisha (Assimilation Modeling), watu 800 waliweza kujenga familia pweke na yatima ipatayo 1600 kwa wastani wa wategemezi wawili na watu zaidi ya milioni 1.6 kwa muongo mmoja.

Tunapowakumbuka sasa ni ishara kuwa Taifa limepoteza zaidi ya watu milioni 3.2 kwenye ajali ya MV-Bukoba, ikijumuisha yatima. Hakika maisha ya waliokufa yamo katika kumbukumbu ya sisi tulio hai, tunapaswa kuwakumbuka daima kwani maisha ya uzima na kifo ni kitu kimoja kama ambavyo mto na bahari vinavyokutana.

Wenzetu walikufa sisi tuko hai, imani niliyonayo ni kwamba bado tuwamoja na tuna usawa ndani ya Yehova- Allah.

Pamoja na kifo kuchukua roho za wapendwa wetu, ukweli utasalia kuwa kifo kinapaswa kuendelea kuheshimika.

Hatua ya kutoa maua, fedha, majeneza ya thamani, sanda, nyimbo za utukufu na sala nzito zenye kujenga faraja ni hatua ya kutambua uwapo wa kifo.

Maana yake sote tunakiri na kukubali kuwa kifo si pepo, bali ni moja kati ya sherehe muhimu kwa binadamu.

Ni kweli kifo kinatuachia majonzi na uchungu mwingi, lakini faraja yake ni kwa kuwa karibu na mfariji mkuu Yehova-Allah tukiamini ni sherehe, tukiamini kifo hupangwa na Mungu.

Pamoja na yote hebu tujiuliuze, nani alikutana na Mungu na akaambiwa yeye ndiye aliyepanga kifo?

Jibu la swali hili ni jepesi tu. Mungu ndiye  mpangaji wa yote yaliyo kwenye mpango wake. Hata hivyo, yapo matukio yanayofanywa na binadamu hayampendezi Mungu.

Yapo tunayoyapanga kwa kumshirikisha shetani bila ya uwapo wa mipango ya Mungu. Tukumbuke kamwe hatuishi hapa duniani kwa dhamira ya kukizoea kifo.

Ukweli ni kwamba, uzima wa milele upo ndani ya walio hai. Ndugu zetu waliokufa na MV-Bukoba baada ya kufa kwao bila shaka wamekuwa kama walivyokuwa kabla ya kuzaliwa kwao kwa maana kabla ya kuzaliwa huwakuwepo na baada ya kifo hawapo.

Watanzania wenzangu kama tunapoteza upendo na heshima miongoni mwetu ndipo kifo hutokea.

Wengi tulio hai tunapenda kuitwa waheshimiwa, kuliko kuhofia kifo, basi yatupasa kutambua kuwa uheshimiwa wetu uende sambamba na kuheshimu kifo, Mungu uwape pumziko la milele wenzetu waliokufa kwa ajali ya meli ya MV-Bukoba.

Mwandishi wa makala haya ni Prof. Handley Mpoki Mafwenga Simba –TAX GURU with 24 Valves.