Home Habari kuu NYALANDU SASA AITESA CHADEMA

NYALANDU SASA AITESA CHADEMA

1291
0
SHARE

NA MWANDISHI WETU

MAOMBI ya aliyekuwa Mbunge wa Singida Kaskazini, Lazaro Nyalandu ya kuomba wanachama wa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), yanatajwa kukitesa chama hicho ingawa tayari baadhi ya viongozi wamesharidhia kumpokea. RAI linaripoti.

Nyalandu amechukua uamuzi wa kujivua uanachama wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) sanjari na nyadhifa zake zote ikiwa ni pamoja na ubunge mapema wiki hii.

Alisema amechukua uamuzi huo kutokana na kutoridhishwa na mwenendo wa kisiasa wa chama hicho.

Duru za habari kutoka ndani ya Chadema zinabainisha kuwa uamuzi wa Nyalandu wa kutaka kuhamia Chadema unabeba sura mbili, moja ikiwa ni kukiimarisha chama hicho na au kukidhoofisha zaidi chama hicho.

Hoja ya kukiimarisha chama hicho inaeleza kuwa Nyalandu si mwanasiasa wa kubeza kutokana na mizizi aliyonayo mkoani Singida hasa hasa jimboni kwake Singida Kaskazini.

Wanaobeba hoja hiyo wanakwenda mbali zaidi kwa kudai kuwa Nyalandu mbali ya kuwa na nguvu za kisiasa Singida, lakini pia anaonekana kuwa na ushawishi mkubwa kwa matajiri mbalimbali wa Ulaya na Marekani, hali inayoweza kuimarisha mfuko wa chama.

Aidha utaratibu wake wa kusaidia watu mbalimbali hasa kwenye huduma za afya nayo inaonekana kama mtaji kwa hoja kuwa upo uwezekano ujio wake ndani ya Chadema unaweza kubeba idadi kubwa ya watu wa kada mbalimbali.

Ukiachana na hoja hizo, lakini pia wanaamini endapo ataingia Chadema na kutaka kuwania ubunge wa jimbo lake aliloliacha ni wazi mwanasiasa huyo atashinda hali itakayosaidia kulihamishia jimbo hilo kwa upinzani.

Kitendo cha Nyalandu kuwa karibu na Mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu tangu apigwe risasi Septemba 7, mwaka huu nacho kinachukuliwa kama mtaji wa kisiasa kwa mwanasiasa huyo ambaye kabla ya kuhama CCM alikuwa akitazamwa kama mbunge pekee wa chama hicho tawala asiyeangalia itikadi za vyama.

Hatua ya Nyalandu kumtembelea Lissu, Hospitali alikolazwa kiliibua mjadala mzito uliosababisha kuwapo kwa madai kuwa ameonywa na chama chake cha zamani, hata hivyo yeye mwenyewe alikanusha madai hayo.

Wakati hoja ya kukiimarisha chama ikipambwa na sababu hizo, wale wanaoamini ujio wake unaweza kukidhoofisha chama hicho, wamebeba sababu kadhaa kubwa ikiwa ni uwezekano wa kuja na watu wake hatua inayoweza kukigawa chama hicho hasa kwa kuzingatia historia ya mwaka 2015.

Mwaka 2015 Waziri Mkuu wa zamani Edward Lowassa alijiunga na Chadema akitokea CCM na kukabidhiwa dhamana ya kuwania Urais.

Uamuzi huo ulitazamwa vibaya na baadhi ya makada akiwemo aliyekuwa Katibu Mkuu wa Chadema, Dk. Willbroad Slaa ambaye baadae aliamua kujiondoa kundini.

Habari za ndani zinabainisha kuwa hatua hiyo hadi sasa bado inakitesa chama kwani wapo baadhi ya makada wanaojiita wazawa hawakubaliani na baadhi ya maamuzi hasa yale yanayoonekana kubeba sura ya kuwapa nafasi makada waliohamia kwenye chama hicho mwaka 2015.

Kwa kufuata historia hiyo, wapo baadhi ya makada wanaoamini kuwa upo uwezekano wa Nyalandu kupata upendeleo maalum katika baadhi ya mambo na kuwaacha baadhi ya  makada wa muda mrefu wa chama hicho.

Baadhi ya nafasi zinazotazamwa kuelekezwa  kwa Nyalandu moja kwa moja ni kuwania ubunge wa jimbo aliloliachia mwenyewe au kuja kupewa au kuwania nafasi kubwa zaidi ndani ya  chama siku zijazo.

Tayari baadhi ya makada ndani na nje ya CCM wanaamini kuwa huenda Nyalandu ameamua kutimkia Chadema ili kwenda kufanikisha nia ya kuwania urais baada ya kukosa nafasi hiyo ndani ya CCM kwenye uchaguzi Mkuu uliopita.

Kabla ya kujiondoa CCM Nyalandu alipata kuliambia RAI kuwa kwa sasa jukumu lililombele yake ni kuwahudumia wapiga kura wake na si urais.

“Unajua wanasiasa wana mipango mingi, kwa sasa nitakosea sana nikisema nina mpango wa kugombea tena nafasi ya urais wakati mwaka 2015 katika uchaguzi mkuu nilimpigia kura Magufuli, nilimuunga mkono kwa hali na mali hadi chama chetu kikashika madaraka.

“Kusema ukweli sasa nina kazi ya ubunge ambayo wana Singida Kaskazini wamenipa na hata sasa ninapozungumza na wewe nipo jimboni kwangu natekeleza majukumu ya kuhakikisha miradi ya Singida inatekelezwa kwa usimamizi wa hali ya juu kwa faida ya wanaSingida na Watanzania wote kwa ujumla.

“Kwa maana hiyo nitaifanya hii kazi ya ubunge kwa moyo wangu wote bila kujali itikadi yoyote ya kisiasa ili kuleta maendeleo kwa Watanzania kama vile Rais wetu John Magufuli alivyodhamiria.”

Hata hivyo hisia hizo zinatajwa kuwa ni mateso na mzigo mzito kwa baadhi ya makada ndani ya chama na kwamba suala la Nyalandu lisipoangaliwa kwa umakini linaweza kukigawa chama hicho, ingawa idadi kubwa ya makada wa Chadema hasa wale wasioamini katika kupewa nafasi wamefurahishwa na uamuzi wake wa kujiondoa CCM.

Mkurugenzi wa Itifaki, Mawasiliano, Uenezi na Mambo ya  Nje wa Chadema, John Mrema aliliambia RAI juzi kwa njia ya simu kuwa kamwe ujio wa Nyalandu hauwezi kukitesa chama hicho kwa sababu tayari viongozi wanakutana ili kuangalia namna sahihi ya kumpokea mwanasiasa huyo.

Alisema wanajua nguvu ya Nyalandu kisiasa na kwamba si mwanasiasa mdogo na tayari wameshamkaribisha, lakini bado hawajampokea kwa sababu mapokezi yake yanahitaji kuandaliwa kikamilifu.

“Tunajua uzuri na ubaya wa kupokea wanasiasa wakubwa, tahadhari zote hizo zinachukuliwa, lakini kamwe hatuwezi kuacha kumpokea, Nyalandu ni mwanasiasa mkubwa na ametupa heshima kubwa hivyo viongozi wa juu wanahitaji kukaa ili kuangalia ni namna gani bora tutampokea,”alisema.

Kuhusu mahali patakapotumika kumpokea Nyalandu, Mrema alisema bado hawajaamua kama watampokea jijini Arusha au jijini Dar es Salaam na ndio maana viongozi wameiona haja ya kukutana ili kujadiliana namna ya kumpokea.

Alipoulizwa nafasi atakayoandaliwa Nyalandu ndani ya chama na kama ataachiwa kuwania ubunge wa jimbo la Singida Kaskazini.

Mrema alisema chama chao kina taratibu zake, uongozi utakaa na kujadili juu ya suala hilo na kama atakuwa na nia ya kutaka kuwania ubunge ndani ya jimbo hilo anaweza kupewa nafasi hiyo.

“Hili la kuwania ubunge ndani ya jimbo aliloliachia, litaamuliwa na viongozi na kama yeye mwenyewe ataonesha nia hiyo basi akipitishwa ni wazi atawania tu,”alisema.

Duru za habari zimeliambia RAI kuwa upo uwezekano mkubwa wa Nyalandu kupokelea jijini Arusha kwenye uzinduzi wa kampeni za udiwani.