Home Latest News NYERERE HAKUTUMIA VIBAYA IKULU, PALIKUWA MAHALI PATAKATIFU

NYERERE HAKUTUMIA VIBAYA IKULU, PALIKUWA MAHALI PATAKATIFU

4881
0
SHARE

NA BALINAGWE MWAMBUNGU


Kwa wale wanaorejea kusoma hotuba ya Mwalimu Julius Nyerere, aliyoitoa kwenye Mkutano Mkuu wa Chama cha Mapinduzi (CCM), mwaka 1995, hapana shaka wanatambua kuwa alikuwa mtu tofauti, linapokuja suala la uongozi.

Ni kwa sababu hiyo, nimeona niwaletee baadhi ya maandishi niliyoyasoma mtandaoni kutoka kwa wasomaji jinsi wanavyo mtafakari Mwalimu Nyerere.

Swali lilikuwa: Je, umewahi kusikia hotuba hii ya Mwalimu Nyerere?

Mmoja aliandika kwa Kiingereza: My president of all time yaani kwake hajakatokea rais mwingine kama Nyerere.
Mwingine akasema: Nyerere yuko vizuri. Maneno yake bado yanaishi. Na mwingine akajibu, ni kweli Mungu ashukuriwe kwa pumzi.

Akafuata mwingine akisema kwamba tangu Mwalimu ang’atuke tumekuwa na marais wanne lakini hawakuacha alama kama Nyerere, labda kwa sababu walidhani wangeweza kuzika fikra zake. Nyerere alituachia nchi ikiwa moja yenye mshikamano. Leo hii angalia wananchi wa sehemu fulani, kiongozi anatamka kwamba (hawapendi) walimnyima kura. Anawapenda watu wa ukanda fulani kwa sababu walimpa kura nyingi sana. Huu ni ubaguzi wa wazi wazi. Kiongozi anatakiwa awe kiungo awaunganishe wananchi.

Tulipokuwa kwenye mfumo wa chama kimoja, wakati wa uchaguzi mkuu, alisimamishwa Mwalimu Nyerere pekee na kulikuwa na watu waliompinga hawakumpa kura. Lakini mara zote, Mwalimu akichaguliwa alikuwa anawashukuru: “ Nawashukuru wote mlionipa kura, nawashukuru pia ambao hawakunipa kura, maana wametumia haki yao,” ndivyo alivyokuwa amasema Mwalimu.

Mwingine aliandika: “Mwalimu was ahead of his time (aliona mambo ya mbele), lakini mafisi walishinda.”

Huyu alimaanisha kwamba ‘unyang’au’ ni ulafi. Baada ya kifo cha Mwalimu, viongozi walitupilia mbali maadili, wakajinufaisha wao na familia zao juu ya rasilimali za nchi na kusahau wajibu wao kwa wananchi. Hawa Paulo Sozigwa (R.I.P), ambaye alikuwa mfuasi mwadilifu wa TANU (Tanganyika African National Union) na chama mrithi wake CCM, aliwaita watu wa namna hiyo kwa lugha ya Kizaramo ‘Mabukanya’ yaani watu ambao hasio kushiba kila chakula linachokuja mbele yao, halali yao. Watu kama hao, mwisho huvimbiwa, matumbo huwaka moto na wasiposaidiwa, wanaweza kudhurika Mabukanya hao.

Tumeona jinsi baadhi ya viongozi walivyoanza kujitajirisha baada ya Baba wa Taifa kuondoka. Pamoja na kwamba baadhi yao wanatahudumiwa na taifa hadi pumzi yao ya mwisho, hawakuacha ‘umabukanya.’ Walijitwalia mali na kuitumia nafasi yao ya uongozi kama ‘fursa’ ya kuchuma mali haramu na halali ili baada ya kustaafu waelee katika utajiri.

Wengine wamejenga mahekalu sawa na Ikulu walipoishi! Nyerere ndiye rais wa kwanza wa taifa letu ameondoka Ikulu baada ya miaka 23, akiwa hana kitu.

Akarudi kijijini alikozaliwa Butiama na kuishi kama mwanakijiji. Wakaamua ajengewe nyumba inayolingana na hadhi yake. Bahati mbaya Mwalimu hakuwahi kuishi kwenye jumba hilo. Na hata angekuwa hai, sidhani kama angeishi kwenye jumba hilo ambalo alilifananisha na ‘pango’

Mwingine aliandika: “Waliofata wamwige kama wanaona hawana mawazo na fikra za kiongozi na uzalendo kama yeye.” Hawawezi kumwiga Nyerere. Wengine wanasema wazi wazi, bila soni kwamba hawafurahii umaskini kwamba Nyerere alikuwa mfano mbaya kwamba aliutukuza umaskini.

Naitafsiri hii kwamba ndio maana hawakuwa tayari kuipitisha Katiba ya Wananchi mwaka 2015. Wengi wa viongozi wa CCM, ambao ndio walikuwa wengi kwenye Bunge la Katiba,waliona kwamba Katiba ile ingewabana wakashindwa kujikusanyia mali. Wakaikalia kitako na kuunda katiba yao. Bila aibu wakaikabidhi kwa sherehe kubwa pale Dodoma, huku wakisifiwa kwamba wameandika historia. Mamilioni ya fedha za wananchi zilitumika na hazijaleta tija yeyote. Walifanya hivyo kwa kuwa walikuwa na ndoto ya kuingia Ikulu walikuwa wakijitengenezea maisha watakayoishi wakishika madaraka. Katiba ile iliyofinyangwa, inaota vumbi sio buku lile liko wapi Ikulu au Makumbusho ya Taifa!

Mwalimu alionya na kuasa kwamba watu wasikimbilie Ikulu kwa kuwa ni mahali ‘patakatifu’ kwa maana ya kiongozi anyekimbilia Ikulu anaina kuwa ni fursa. Mwalimu alisema Ikulu hakuna biashara. Ikulu sio pango la wanyang’anyi, lakini wengine wanaona kwamba Ikulu ndio yenye ufunguo wa Sesame ya Mashimo ya Mfalme Suleiman. Ukikamata Ikulu, umekamata Sesame! Ndio maana wanasiasa wako tayari kupoteza maisha ya watu wengine wanaowaona kuwa ni tishio. Wako kama Simba ambaye akishakamata windo lake, hataki kubughudhiwa. Ole wao manyang’au wamsogelee chamoto watakiona!

Mjibu hoja mwingine, analalamika kuwa maisha ni magumu sana (sasa hivi), lakini hakuna kitu kizuri kama kuvuta hii hewa ya Mungu. Kwa Watanzania waliowengi, inakuwa kama gurudumu limetereza na kurudi nyuma badala ya kwenda mbele. Hii inatokana na mazoea ya kwamba alipoishia aliyekutangulia, unaanzia hapo kwenda mbele. Baba wa Taifa alitujengea msingi mzuri nyumba yetu ilikuwa imara, tulivu na yenye matumaini—ya kuishi bila hofu, bila woga na kufanyakazi ya kujipatia riziki halali. Lakini waliubomoa msingi ule na kutaka kusimika mwignine.

Wakalizima Azimio la Arusha. Wakaufurahia utandawazi au utandawizi wakaja na Soko Huria, kumbe ni soko holela lazima maisha yawe magumu. Utawasikia wakisema eti mbuzi hula kutokana na urefu wa kamba yake.

“We miss you sana our Father of the Nation,” anachombeza mwingine. Ni viongozi wachache sana wanao ‘mmisi’ Mwalimu. Ila wakati wa kampeni waaitumia sana sauti yake kulinda Ikulu isichukuliwa na ‘maadui.’ Jina la Nyerere linakuwa midomoni mwao kila wakati. Radio na televisheni wanazitumia sana kuwakumbusha wananchi alichokisema Mwalimu. Baada ya kampeni na uchaguzi ni biashara kama kawaida Mwalimu anasahaulika.

“I admired him. He was a gifted speaker” Mwingine anamwuliza mwenye kuandika mstari huo:

“We …unamtukana nani? Hatukani mtu, lakini anamsifia Mwalimu kwamba alikuwa ana kipaji cha kupagilia hotuba zake. Mwalimu alikuwa harudii rudii hotuba zake, ndio maana watu wanazisoma na kuzisikilila hazichuji. Ni kipaji, watu hamuwezi kuwa na vipaji sawa.

Mwingine anamwona Mwalimu kama ‘Muona mbali’.

Kanikumbusha maneno ya mwalimu wangu Mzungu ambaye aliniambia: ‘Narere was born in the wrong place and wrong time’ yaani Nyerere alizaliwa mahali pasipostahili na wakati usiofaa.

Mwanzoni nilimfikiria Mzungu huyo kuwa mbaguzi. Lakini alininifafanulia—kwa kunipa mfano wa Yohana Mbatizaji. Alikuwa anawaletea Wayahudi habari jema, ya mambo yatakayojiri. Hawakumwelewa. Alikuwambele ya wakati.

“Unafiki na uchu wa madaraka….lakini mwisho wa yote ni kifo tu,” ana andika mwingine. Yaani yeye anaona viongozi wana uchu wa madaraka na ni wanafiki. Kivipi?

Nimetoa mfano wa Simba ambaye hataki mnyama mwingine amsogelee wakati anakula nyama. Mwenye uchu ni yupi kati ya hawa? Anayekula au anayenyemelea! Tafakari!

“OK fresh, be blessed Mwalimu Mkuu, kwa maneno ya busara,” ana andika msomaji. Kwake anaona maneno ya Mwalimu Nyerere kama ni ya leo halafu kila wakati alikuwa anasema maneo ya busara sio ya kuwatisha watu waliokuweka madarakani. ‘Mtakumbana na nguvu ya dola’ akisahau  kwamba dola ni ya wanachi. Mwingine amewahi kusema hajaribiwi. Laiti kama angelijua yaliyomfika  Rais Ferdinand Marcos wa Ufilipino.

“Anaye mlaani Nyerere anaishangaza dunia. Huyu alikuwa zawadi (yetu)  kutoka kwa Mungu. Tunahitaji watu wenye roho kama yake. Tunajua hakukamilika kwa kuwa yeye sio malaika, lakini kwa 75% alikuwa mtu mzuri. Amefanya kazi yake vizuri na amemaliza vizuri. Viongozi wengine wajitathmini.”

Mwingine kaandika: “Nimemkumbuka baba yetu JKN, ungekuwepo wengi wangekuwa jela!”.

Na mwingine anasema: “Nyerere was far ahead of his time. Yaani huyu mzee was a genius and a good orator and intellectual. Basi tu kifo ni lazima, ila alitakiwa aishi angalau kufikia  miaka 100, ili tuchote busara zake.”

Huyu kanikumbusha habari za Waziri Mkuu (mstaafu) wa Malaysia, Dk. Mahadhir bin Mohamed (93), ambaye aliingoza nchi hiyo kwa miaka 22 mfululizo. Alistaafu mwaka 2003, lakini akarejea kwenye siasa.

Hakufarishwa jinsi  mrithi wake, Abdullah Badawi alivyokuwa anaendesha nchi. Akashiriki kumng’oa mwaka 2009.

Lakini serikali ya BN (Bosian National Coalition), ambayo  chama chake UMNO United Malays National Organiztion, kililuwa mshirika mkuu, iliendelea kuendeleza rushwa na ufujaji wa rasilimali za nchi.

Mahadhir pamoja na baadhi ya vigogo kutoka UMNO, wakaunda Malaysian United Indigenous Party na kujiunga na muungano wa upinzani wa Pakatan Harapan.

UMNO na muungano wake, kilikuwa madarakani kwa miaka 60. Ngome yake kuu ilikiwa vijijini. Mahathir aliweza kukipenyeza Pakatan vijijini. Katika uchaguzi mkuu uliofanyika Mei, mwaka huu, kimenyakua madaraka. Mahadhir amekuwa Waziri Mkuu tena na ameaahidi kurejesha utawala wa sheria na kupambana na ufisadi.

Mwalimu Nyerere aliwahi kutishia kukihama CCM. Hakupendezwa na mwenendo wake. Akakisifia Chama cha Demokrasia na Maendeleo kwamba angalao kilikuwa kinafananafana kisera, na chama chake cha zaamani. Nani kama Mwalimu hivi sasa!

Mwingine aliandika: “Kuungana ni jambo mhimu sana, Ndiyo ushindi. Umoja ni nguvu.”

Kweli kabisa. Kwa mfano huo wa Malaysia, vyama vinaweza kuungana na kujijipenyeza vijijini ambako chama tawala kinamizizi. Imewezekana Makaysia, inawezekana hapa pia.

Mwingine kaandika: “Pengo lako (Mwalimu), kamwe halitazibika.” Na mwingine kaongeza: “Anastahili kuitwa Baba.”

Mambo mengi ambayo yanatokea sasa, alikwisha yatabiri. Alizungumzia Katiba. Akasema Katiba ya sasa inampa Rais madaraka makubwa sana. Akasema angetaka kuwa dikteta, angeweza kuwa kwa muujibu wa Katiba ya sasa.

“Mzee wewe ulikuwa kichwa.”  Ndio. Aliweza kupambana na makaburu na wakoloni. Aliwashinda kwa hoja waliokuwa wakimpinga. Hakuwa mtu wa kutumia nguvu. Lakini hakupenda kuonewa. Makumbuka ya Jenerali Iddi Amin wa Uganda!

“Mhmm baba Mungu akulaze mahali pema peponi. Kama kuna ulilomkakosea,  wewe ulikuwa binadamu, ila mengi uliyafanya vizuri.  Siishi kukukumbuka daima,” ana andika msomaji.

“Nimekuwa nikimfuata na kumsikiliza Mwalimu tangu mwaka 1973, ambao ndio mara yangu ya kwanza kukanyaga nchi ya Tanganyika (Tanzania). Hadi leo (2017), ningali natekwa na busara yake, lugha yake, lafudhi yake, tamathali zake za usemi, na vicheko vyake. Hakuwa na kifani!

Wala sisemi Mwalimu alikamilika katika hali zake, lakini hata hivyo akarehemiwa akili na ujuzi wa hali ya juu.” Ni maoni ya msomaji.

“Bora Nyerere angekuwepo, nchi isingekuwa hivi. Amepotea kabisa. Ndio hatutamwona tena, lakini Mwalimu anaishi kwa kuwa ametuachia maandiko” na hotuba kumbukumbu ambazo hazitatoweka milele.

“Mzee huyu alikuwa na maono makubwa sana, na pili, hakuwa na ubaguzi katika maendeleo ya mikoa. Mara sasa haina kiwanda chochote.  Nimtazamo tu.” Ana andika mjibu hoja.

Viwanda alivyovijenga Mwalimu, kama watawala wangekuwa makini na uzalendo kama alivyokuwa yeye, tusingekuwa tunaongelea kujenga viwanda. Tanzania ingekuwa tayari ni nchi ya viwanda.