Home Habari OLE SABAYA: Nimejifunza kuwa mnyenyekevu

OLE SABAYA: Nimejifunza kuwa mnyenyekevu

264
0
SHARE

GABRIEL MUSHI

MKUU wa Wilaya ya Hai, Lengai Ole Sabaya amesema mojawapo ya vitu alivyojifunza tangu ateuliwe na Rais Dk. John Magufuli kuitumikia nafasi hiyo ni kuwa mnyenyekevu mbele ya wale anaowatumikia.

Ole Sabaya ambaye aliteuliwa Julai 2018, pia amesema amejifunza kuwa kipimo cha utu na heshima kitapimwa na yale kiongozi husika anayoyafanya na sio kuyasema.

‘Sasa nimejifunza zaidi kuwa mnyenyekevu, mtu yeyote hapaswi kudharauliwa kwa rangi yake, udini wake au itikadi yake,” alisema Ole Sabaya.

Katika mazungumzo yake na RAI wiki hii, Ole Sabaya ambaye pia alikuwa Mwenyekiti wa UVCCM Mkoa wa Arusha, alisema amejifunza kuwa Mungu hupanga madaraka yaende kwa nani, na sasa ametumia Rais Magufuli kama njia ya kumwelekeza watu wanaopaswa kumsaidia kutenda kazi. Endelea kusoma mahojiano hayo kwa kina zaidi.

 RAI: Unazungumzia vipi miaka 42 ya chama

OLE SABAYA: CCM ya miaka hii sio CCM tuliyoizoea, tulikuwa na CCM ambayo ni kama kichaka cha wahalifu kujificha… walikuwa wanafanya mambo yao na kuja kujificha ndani ya chama, na wengine bado wapo, ila CCM ya Rais Magufuli, imejibadilisha yenyewe kuanzia kwenye mfumo wake kiuendeshaji, usimamizi na uadilifu wake. Hata kama kuna mashaka ni mambo madogo ya kibinadamu yaliyobaki.

Mambo makubwa yameanza kufanyika na wananchi wanaamini kwamba kweli CCM ni chama cha wananchi, chama cha wakulima na wafanyakazi na watumishi. CCM imeondoka  kwenye ile CCM ya genge la watu na makabaila waliokuwa na uwezo wa kufanya lolote na kujificha humo bila kufanywa chochote, sasa ni chama cha kuwatetea watu wa kawaida, walioko mashambani, viwandani na wafanyakazi.

CCM bado inafanya mabadiliko hayo ila kuna changamoto yake, na sehemu kubwa  wanaojaribu kureform ni Mwenyekiti na Katibu Mkuu ila bado tunaendelea kujifunza kusema ukweli. Lazima CCM ijifunze kuwakemea sio kusubiri rais au katibu mkuu, lazima kukemea adui pale anapojitokeza.

Nasema hivyo kwa sababu CCM ina kanuni za kwamba nitasema kweli daima, fitina kwangu mwiko. Lazima wajifunze na waakisi kwenye misingi za ahadi za mwana TANU.

RAI: Mwenyekiti wa CCM, Rais John Magufuli amekuwa na mwamko wa kuwateua vijana katika nafasi mbalimbali za kuitumikia serikali, je unatoa wito gani kwa vijana wenzako kuzitumia nafasi wanazopatiwa kwa uweledi na uadilifu?

OLE SABAYA: Kwanza ni heshima kubwa kupewa nafasi na Rais, heshima yangu zaidi si kuteuliwa na Rais, heshima yangu ni kuteuliwa na aina ya Rais Magufuli, hilo kwangu ndio kubwa zaidi, kwa hiyo vijana lazima wajue kwamba wameaminiwa na Rais, kwamba wana uwezo wa kuungana na wengine kujenga Taifa letu.

Ukweli, uwazi, uadilifu na nidhamu ni vitu muhimu. Pia lazima kukumbuka kwamba hii njia ambayo tumetoka tusihangaike sana kupanda miiba kwani unaweza kurudi miguu peku. Tunapaswa kujua kwamba wenye mamlaka siku zote ni wananchi, tunapaswa kujinyenyekeza kwao, tuwaheshimu lakini kuwatendea haki na kutekeleza yale ambayo yeye anakuteua anategemea matakwa yake uyafanye.

RAI: Kumekuwapo na dhana kuwa vijana wa upinzani wanaohamia CCM kuunga mkono juhudu za Rais Magufuli wanapewa kipaumbele kuliko vijana waliopo CCM, Je, kwa upande wako unaweza kuwaeleza nini vijana hao wa CCM wenye malalamiko ya chini kwa chini?

OLE SABAYA: Kijana anayeanzisha huu mjadala maana yake lolote analofanya ni kwa ajili ya kutaka madaraka, wakati madaraka siku zote hutoka kwa Mungu. Mwenyezi Mungu amemtumia Rais Magufuli  kwa kumwambia huyu na huyu anaweza kukusaidia kutenda kazi.

Wanaotajwa kama vile Patrobas Katambi, David Kafulila na wengine, wale watanzania wenzetu, kinachotazamwa zaidi sio itikadi… ni moyo na dhamira ya dhati ya kuwasaidia watanzania ukweli kilichomo ndani yao kwamba kina thamani zaidi ya kile wanachokishikilia.

Kwa hiyo wale wameonesha na kuthibitisha kwamba wanaweza na ndio maana bado wapo. Na hawa wengine waangalie mijadala mikubwa mambo ya korosho, ujenzi wa reli ya kisasa, ununuzi wa ndege… waseme kwa dhati kabisa wananchi wajue kwa sababu Rais amefanya kwa vitendo. Wakianzisha mjadala kuwa hawa wa upinzani wanakuja kuchukua nafasi zetu pia basi waseme nani alikuwa na garantii kuwa anateuliwa na Rais?  Binadamu hawaishi maneno, maana rais ametumia vyombo vyake na kuwapima dhamira zao.

RAI: Kwa kuwa ni mara ya kwanza umeteuliwa kuwa Mkuu wa wilaya, kuna kitu gani umejifunza tangu ulipokabidhiwa jukumu hilo la uwatumia wananchi wa HAI?

OLE SABAYA: Kubwa nililojifunza ni kuwa mnyenyekevu, rais amekuteua ila wanaokupa nguvu ni wale unaowatumikia, kipimo chako cha utu na heshima kitapimwa na yale unayofanya na sio kuyasema, sasa nimejifunza zaidi kuwa mnyenyekievu, mtu yeyote hapaswi kudharauliwa kwa rangi yake, udini wake au itikadi yake.

Nimejifunza kuwa Mungu amepanga yote anatufundisha na kutuita zaidi kwamba yale ambayo tunataka sisi tuwatendee wananchi wetu. Ndio maana rais anasisitiza kwamba tuwasikiliza na kutatua kero za wananchi  wa chini, kwa hiyo tunaheshimu kukaa kwenye viti hivi kuhakikisha tunaondolea watu wetu kero.

RAI: Pamoja na malalamiko kuwa una hulka ya kuchukua hatua kali kwa baadhi ya watendaji, wawekezaji wanaokwenda kinyume na matakwa yako, ni zipi changamoto nyingine ulizokumbana nazo?

OLE SABAYA: Haohao wanaosema hatua ni kali sana, ndio haohao walikuwa wanasema hatua hazichukuliwa, kwa sababu zamani Rais aliyepita alikuwa mpole sana, sasa amekuja huyu wameanza kumwita ‘dikteta’, unapofanya maamuzi utegemee kwamba watu wote hawakusifu. Kwanza usifanye ili usifiwe ila ufanye maamuzi ya haki kwa manufaa ya wengi.  Hilo ndio nalitazama zaidi.

Hata ibada kanisani kuna wakati maaskofu wanazungumza watu wanapinga, Yesu mwenyewe alipingwa, aliwezesha vipofu kuona na viziwi kusikia lakini wakamuua.  Sembuse mimi ambaye ni mwanadamu, kwa hiyo changamoto hizo zipo lakini kama kuna jambo ambalo linatusaidia linanifanya kuwa imara zaidi.

RAI: Viongozi wakuu na Rais Magufuli mwenyewe amekemea utaratibu wa kuwaweka mahabusu watu saa 48, kuwa utumike kwa uweledi na busara, ukiwa mmoja wa wateule wake umepokeaje maagizo hayo?

OLE SABAYA: Kwa kuwa hayo ni maelekezo ya Rais amesema tumieni vizuri, hayo ni malekezo ya rais na yatatekelezwa ipasavyo kwa uweledi na busara. Kubwa ninalopenda kuwaambia wana HAI wenzangu kuwa nina heshima kufanya kazi hapa bila shaka sitawangusha.