Home Maoni Ongezeko ufaulu Darasa la saba  uwe chachu ya kuboresha elimu

Ongezeko ufaulu Darasa la saba  uwe chachu ya kuboresha elimu

1681
0
SHARE

Matokeo ya mitihani ya kitaifa ya Darasa la Saba ya mwaka huu yaliyotangazwa mapema wiki hii yameonyesha ongezeko la ufaulu kwa asilimia 4.9 kwa mwaka huu 2018, habari ambazo zina kila sababu ya kupongezwa.

Aidha kwa mujibu ya matokeo hayo yaliyotangazwa na Baraza la Taifa la Mitihani (NECTA), ufaulu wa masomo ya Kiingereza, Hisabati, Sayansi na Maarifa ya jamii umepanda maradufu – kitu ambacho kinatia moyo kwani masomo hayo ni msingi mzuri wa maendeleo ya baadaye kwa ajili ya kupata wataalamu katika fani mbali mbali kama vile madaktari, mainjinia na wahasibu waliobobea.

Pengine kilichotia dosari kidogo katika matokeo ya mwaka huu ni kushuka kwa ufaulu wa lugha ya Kiswahili, kitu ambacho sababu zake bado hazijajulikana, ikitiliwa maanani kwamba Kiswahili ni lugha ya taifa.

Hata hivyo pamoja na habari za ufaulu kupanda kwa ujumla, mitihani ya mwaka huu iligubikwa na uvujaji wa mitihani katika baadhi shule, suala ambalo mara moja serikali, kwa maana ya wizara husika ilichukua hatua za kuifuta.

Kutokuwa na elimu – yaani ujinga ni mojawapo ya vitu vitatu ambavyo baada ya kupata uhuru wetu miaka 57 iliyopata, Baba wa Taifa Mwalimu Julius Nyerere alitangaza kuvipiga vita. Vingine ni umasikini na maradhi.

Na siku zote tunaambiwa kwamba taifa lisilo na elimu haliwezi kupiga hatua za maana kimaendeleo, achilia mbali maendeleo binafsi ya mtu mmoja mmoja. Daima hukumbushwa kwamba neema mbele yetu itatokana na elimu tu, si kingine.

Tena elimu iliyo bora, wanaongezea. Lakini kwa Watanzania walio wengi pengine huu ni wimbo kutoka serikalini unaonekana si kitu ambacho mtu anaweza kukitia maanani, hasa wanapoona hali inavyozorota katika sekta hiyo.

Hakuna anyepinga kwamba elimu ina gharama kubwa, kifedha, lakini mbadala wake — yaani ‘ujinga’ pia una gharama kubwa kwa taifa na hasa kwa serikali yake ambayo ndiyo yenye kubeba jukumu la kuona wananchi wake wanapata elimu.

Sasa hivi mtu anaweza kuandika kurasa elfu kadha kuhusu kuporomoka kwa viwango vya elimu na kwa nini ilitokea hivyo na bila serikali kuonekana kuguswa. Aidha mijadala  mikubwa mikubwa imekuwa ikifanyika kuzungumzia changamoto za elimu na mengi yamependekezwa katika juhudi za “kuirudisha elimu katika njia yake.”

Hivyo tunashauri kwamba ufaulu huu mzuri wa watoto wetu mwaka huu serikali iuchukulie kama chachu katika jitihada zake za kuiboresha sekta hiyo muhimu.

Vinginevyo itakuwa haingii akilini iwapo nchi hii yenye utajiri mkubwa wa maliasili yakiwemo madini ya kila aina tuliojaliwa na Mwenyezi Mungu itashindwa kuboresha sekta yake ya elimu kufikia viwango vya kuridhisha.