Home Makala ‘OPERESHENI UVUVI HARAMU’ INAATHARI KUBWA KWA MLEMAVU WA MACHO

‘OPERESHENI UVUVI HARAMU’ INAATHARI KUBWA KWA MLEMAVU WA MACHO

4687
0
SHARE

NA HARRIETH  MANDARI, GEITA


UPO msemo ambao wahenga walisema ‘ukistaajabu ya  Musa utayaona ya Firauni’. Msemo huu  unarandana na maisha halisi ya mkazi mmoja wa  kijiji cha Mbugani, Kata ya Butundwe wilayani Geita, Magessa Moshi, ambaye licha ya kuwa  ni mlemavu wa macho (kipofu),  lakini  shughuli yake kubwa ni uvuvi wa samaki aina ya  ‘furu’  kwa ufanisi mkubwa.

RAI  lilimtembelea  Magessa katika eneo lake la uvuvi  (mwaloni) katika Ziwa Victoria ambalo linakizunguka kijiji hicho na kumkuta akiwa anavua samaki bila kubabaika.

Historia yake ya maisha;

Magesa anasema alizaliwa miaka 30 iliyopita akiwa anaona vizuri hadi pale  alipofikisha umri wa miaka 13  ambapo alipatwa na ugonjwa wa Tetekuwanga kali iliyosababisha vipele kama vijipu katika macho yake na alipopona hakuweza kuona tena.

“Baada ya kupofuka nililelewa na mama yangu na nilipofika miaka 25, mama alifariki hivyo kuniacha nikiwa mkiwa kama kinda la ndege lililokosa malezi, ilinilazimu kutafuta shughuli ya kujitafutia kipato. Kwa haraka haraka niliona uvuvi utanitoa  kutoka kwenye ukali wa maisha na hapo ndipo safari ya  kuvua samaki ilipoanza hadi sasa,” anasema.

Anasema alipata pesa kiasi kutokana na mauzo ya samaki hao ambapo aliweza kupata mchumba na kumuoa Maria Paulo na kufanikiwa kuzaa watoto watano.

Anavua bila kukosea

Anasema kawaida huamka saa 10 usiku na kusindikizwa na mkewe –yeye humwita mkombozi na mpenzi wake wa ukweli hapa duniani—ambaye humsindikiza hadi sehemu ambapo kuna njia inayoongoza ziwani na akishamfikisha, hurudi nyumbani kwa ajili ya kuhudumia watoto.

“Ninapoingia kwenye mtumbwi wangu, ninatega ndoano zangu na nina kipaji kikubwa cha kugundua iwapo samaki wameshaingia kwenye mtego na pia hata kama kuna aina nyingine ya samaki, wengi wao nawafahamu kwa sauti za vilio vyao, kwa hiyo wakishanasa navuta ndoana zangu na kuendelea hadi hapo nitakapoona nimeanza kuchoka,” anasema Magesa ambaye  anajiamini na kuifurahia kazi yake.

Lakini anasema pamoja na kufanya shughuli hizo, amekuwa akikumbana na changamoto mbali mbali—hasa wakati wa kuingia kwenye mtumbwi, ambapo inapotokea siku hiyo anaenda peke yake inamuwia vigumu na kuchukua muda kupanda na kukaa sehemu sahihi ya mtumbwi.

“Ni lazima katika shughuli zetu hizi kuhakikisha una ‘balance’ mtumbwi wako kuweza kuelea vizuri kwa kuhakikisha unakaa katikati, au sehemu ya mtumbwi ambayo mtumbwi hautaweza kuzama hasa kunapotokea upepo mkali,” anasema huku akitabasamu.

Anasema hajutii kuwa kipofu, lakini anaomba jamii imsaidie baadhi ya mahitaji, ikiwemo kupata wasamaria wema kumchangia mkewe mtaji wa biashara.

Changamoto

Magessa anasema  changamoto nyingine ni kukosa ushirikiano kutoka kwa jamii inayomzunguka—hasa vijana wakati wa kuvua, kwani anatamani kuvua samaki wengi na kwenda  umbali mrefu ziwani, ili kupata samaki wakubwa, lakini wengi wao wanamkwepa.

“Tangu nianze kuvua samaki mwaka 2002, hadi leo nimekuwa nikisaidiwa na wavuvi wazee, vijana hawataki kabisa kuongozana na mimi kwenye kuvua kwa madai kuwa wanahofia iwapo itatokea ajali watashindwa kunisaidia,” anasema.

Anaongeza kuwa kwa kawaida kwa siku huambulia kiasi cha Sh 5,000 na wakati mwingine kiasi cha fedha zinazotokana na mauzo ya samaki huongezeka, lakini bado ana kiu ya kuboresha maisha yake.

“Mama wa watoto wangu anajitahidi sana kuhangaika kutafuta vibarua  vya kuchuma pamba, au kulima ambapo hulipwa kiasi cha Sh 5,000  kwa kila nusu ekari, lakini bado kiasi hicho hakikidhi mahitaji ya familia yangu yenye watoto watano,” anasistiza.

Akizungumzia athari zilizowakumba baada kuanzishwa kwa oparesheni ya kudhibiti uvuvi haramu, Magessa analaani kitendo cha serikali kuanzisha ‘Oparesheni Tokomeza Uvuvi Haranu’ kwa madai kuwa imewasababishia washindwe kuendesha shughuli zao na kushindwa kumudu kununua nyavu zilizohalalishwa.

“Yaani kwa kweli huyo mtu anayeitwa sijui Mpina, ametufanya tuishi maisha magumu sana, kwani wavuvi wengi wamekamatwa na kupigwa vipigo baada ya kukutwa na nyavu hizo na wengine hata hawana hatia kabisa, hivyo kutufanya sisi kukaa kijiweni tu,” alisema.

RAI pia lilifanikiwa kwenda hadi nyumbani kwa Magessa na kushuhudia watoto watano wadogo, wa kwanza ana umri wa miaka sita. Familia hiyo, inaishi kwenye nyumba ya udongo iliyoezekwa nyasi.

Mkewe Maria, anasema jukumu la kulea familia hiyo ni moja ya changamoto kubwa kwake kwa sababu watoto bado ni wadogo.

“Watoto wetu bado ni wadogo na wamefuatana, ilitulazimu mimi na mume wangu kumpeleka mtoto mmoja kwa dada yangu, ili atusaidie kulea kutokana na hali ngumu ya maisha, hasa katika kipindi hiki ambapo nyavu zenye matundu madogo zimepigwa marufuku ma zilizoruhusiwa ni zile zenye matundu makubwa. Hatuwezi kumudu kununua kwa sababu zinauzwa kwa bei kubwa,” anasema.

Matukio akiwa ziwani

Magessa anasema akiwa anafanya shughuli za uvuvi ziwani, amewahi kukutwa  na matukio ya kutisha  ikiwemo la kukoswa koswa kuuawa na Kiboko.

“Nakumbuka siku hiyo nilitoka kwenda kuvua nikiwa na rafiki yangu Mzee Josephat Lazaro. Tukapanda mtumbwi kwenda kuvua kando kando ya Kisiwa cha Kasima saa 10 alfajiri. Kabla hatujafika alitokea kiboko akiwa na mtoto wake akaanza kutushambulia,” anasema.

Anasema walianza kupiga makasia kumkimbia kiboko huyo na kwa bahati nzuri ulitokea upepo mkali sana ukachukua mtumbwi wetu na kuutupa kwenye kisiwa kingine.

“Yaani ilikuwa ni baraka ya Mungu hata upepo ulipotokea ni Mungu tu  na tulipotupwa kwenye kisiwa hicho mtumbwi wetu ulipasuka na mimi na mwenzangu tukaangukia kwenye mawe na baadaye wavuvi wengine walipita karibu na kutuokoa,” anasema.

Anasema tukio lingine ambalo hatolisahau lilimkuta siku ambayo majira ya saa 10 alfajii alikutana na kivuko chenye abiria, na kwa kuwa hawakuwa na taa wala tochi ilikuwa ngumu kwa kivuko hicho kuwaona.

“Kilipotukaribia yaani ilikuwa tugongwe, kwa bahati nzuri kulikuwa na wavuvi wengine walimulika tochi kuelekea kwenye kivukom ilisaidia sana la sivyo nisingekuwepo leo,” anasema.

Akizungumzia kuhusu hali ya Magessa, Diwani wa Kata hiyo, Tindos Matuge anasema  kijana huyo amekuwa akikumbwa na changamoto nyingi zikiwemo wezi kumuibia nyavu mara kwa mara.

“Kwa kweli anahitaji msaada kwani pamoja na kuwa na watoto wengi wadogo, lakini kuoa ni haki yake ya msingi. Tunachofanya ni kumsaidia pale tupoweza na pia kumpa elimu ya uzazi wa mpango ambayo ni muhimu kwa maisha yake,” anasema.

Vijana wa kijiji hicho ambao Magessa aliwatupia lawama kuwa wanamkwepa, walikiri na kusema kuwa wanaogopa iwapo watapata ajali itawawia vigumu kumsaidia.

“Ni kweli huwa tunamkwepa kwa sababu sisi wenyewe tunatumia zana duni ambazo iwapo tutambeba kwenye mitumbwi yetu ziwani kuna mambo mengi, inaweza kutokea dhoruba kali ambayo nitashindwa kujiokoa mimi na yeye kwa wakati mmoja kwa kuwa haoni,” anasema mmoja wa kijana aliyekataa kujimbulisha jina.

Wito wake kwa Serikali

Pamoja na mambo mengine Magesa analaani kitendo cha Serikali kukamata nyavu zinazodaiwa kuwa ni haramu kabla ya kuandaa mazingira mazuri ambayo hata mvuvi wa kipato cha chini kama yeye, ataweza kumudu kununua nyavu zinazotakiwa.

Vilevile anawaasa vijana wenye viungo kamili, wavitumie vizuri kwa kufanya kazi kwa bidii.

“Na kwa wale wasioona kama mimi, au aina nyingine ya ulemavu, waache tabia ya kuchukulia ulemavu kama chambo cha kujipatia pesa, badala yake wabuni njia au mradi wowote ambao utawaingizia kipato kwani Mungu alituumba kwa mfano wake, awe mlemavu awe mzima,”anasema.