Home Habari Pan-Africanism: Ni Wamarekani weusi waliobuni uhuru wa Afrika

Pan-Africanism: Ni Wamarekani weusi waliobuni uhuru wa Afrika

405
0
SHARE

NA JOSEPH MIHANGWA

ZAMANI kidogo enzi za kabla na baada ya uhuru tulipokuwa skuli ngazi ya shule ya msingi, walimu wetu walizoea kutuimbisha wimbo ambao haukuingia akilini na ambao pia ulikuwa wimbo wa beni [band] usemao: 

“Afrika nakutamani sana, nikikumbuka sifa zako; 

Utumwa ni kitu kibaya sana, tuliuzwa kama samaki; 

Samaki wa kwetu wanono, nakukumbuka Afrika”.

Wengi hatukujua kwamba maneno ya wimbo huo yaliwakilisha kilio na maombolezo ya mtu mweusi aliyeuzwa utumwani huko Marekani, Visiwa vya Ki-Karibian [Caribbean Islands] na vya Uhindi Magharibi [West Indies] na Uingereza kabla ya karne ya 19, pale biashara ya watumwa na utumwa ilipopigwa marufuku ulimwenguni kote.

Inakadiriwa kuwa, biashara hiyo ya kudhalilisha utu na ubinadamu, ililipokonya bara la Afrika nguvu kazi ya zaidi ya watu milioni 20 hadi kupigwa marufuku kabisa mwaka 1865. Na pale ilipofikia kikomo, “watumwa” hao huru walibakia walikokuwa kama raia wa nchi hizo, lakini wenye kubaguliwa kwa sababu tu ya rangi yao na hadhi ya kijamii kama “watu wa kuja” au walowezi wasio na pa kwenda.

Pengine ni kubaguliwa huko kulikowafanya kutunga wimbo huo “Afrika Nakutamani”, na haifahamiki vipi uliwafikia walimu wetu vijijini, katika kipindi hicho cha teknolojia duni ya mawasiliano. 

Lakini pamoja na hayo, jambo moja lilikuwa dhahiri; kwamba Waafrika hao waliouzwa na kutumikishwa ughaibuni walikuwa wakiipasha dunia kwamba bado walikumbuka asili yao [Afrika] na kutamani kurejea lakini wasiweze.

Ukatili ulitawala maisha ya watumwa; jaribio pekee la kutaka kutoroka adhabu yake ilikuwa kifo. Sababu za vifo kutokana na ukatili vilivyorekodiwa sambamba na vya ng’ombe,  nguruwe na farasi, zilikuwa ni pamoja na “vidonda vya tumbo”, “kifo cha ghafla”, “kupigwa risasi kwa bahati mbaya”, “homa”, “ugonjwa wa tauni” na “ukoma”.

Wakati utumwa ukikomeshwa Marekani mwaka 1865 kwa mfano, watumwa waliosalia hai nchini humo walikuwa si zaidi ya 4,000,000; Visiwa vya Karibbean na West Indies 1,370,000;  Uingereza na makoloni yake watumwa 700,000 na wengine walipelekwa  kuanzishiwa makazi mapya Freetown, Liberia, kama watu huru.

Kukomeshwa kwa biashara ya watumwa na utumwa karne ya 19 kulitokana na maendeleo/mapinduzi ya kiviwanda kwa nchi za Ulaya ambapo uzalishaji mali ulianza kutegemea nyenzo za mashine badala ya nguvu kazi ya watumwa.  

Jambo la kutia moyo ni hili tulilosema kwamba licha ya kizazi cha watumwa hao kukaa zaidi ya karne mbili ugenini, hawakusahau asili yao kwani ndio hao walioanzisha wazo la “ukereketwa wa Afrika” [Pan-Africanism] uliozaa harakati za ukombozi/uhuru wa Afrika karne ya 20 kabla Waafrika wenyewe hawajawazia jambo hilo.

Ukereketwa huu, ambao kwa kukosa neno sahihi nitauita tu “Pan Africanism”, ulibuniwa, kuenezwa na kusanifiwa na mtumwa huru mweusi wa Marekani aliyeitwa Dk. William Du Bois na kuingizwa kwenye mkondo wa harakati za ukombozi wa Afrika.

Wengi wa wasomi wa Kiafrika waliokwenda masomoni Marekani miaka ya 1930 na 1940 na baadaye kuwa viongozi wa harakati za uhuru wa nchi zao, walijasirishwa na fikra za watumwa hao huru wenye uzoefu wa mapambano ya kupigania haki za mtu mweusi aliyebaguliwa kama wao.

Mashuhuri kati ya viongozi hao na ambao walitokea pia kuongoza harakati za uhuru wa nchi zao ni pamoja na Dk. Namdi Azikiwe [Nigeria] ambaye ushawishi wake haukuwa kwa Nigeria tu, bali Afrika nzima; Dk. Kwame Nkrumah [Ghana] ambaye aliiletea Afrika dhana ya “vyama vya umma” [Mass Parties] katika suala zima la ukombozi na wengine.  Nkrumah ndiye aliyewasha moto wa “Pan Africanism” kwa Afrika nzima na harakati za kudai uhuru kutoka kwa Wakoloni.

Filosofia ya “Pan-Africanism” kama ilivyobuniwa na Du Bois, ilikuwa juu ya “nguvu ya kisiasa na heshima ya mtu mweusi ulimwenguni kote”. Kwa Du Bois na wenzake, heshima ya mtu mweusi ilimaanisha “heshima ya watu wote wenye asili ya Kiafrika”. Na kwa masaibu aliyoonja chini ya mfumo wa utumwa nchini Marekani, yenye kudhalilisha mtumwa na mmiliki wa mtumwa kwa pamoja, ambapo mtumwa alikuwa mtu mweusi na mwenye kumiliki mtumwa, mweupe; alifikia uamuzi kwamba dharau hii ingekoma kama  Afrika ingekuwa huru.

Lakini mawazo yake juu ya uhuru yalitofautiana na yale ya viongozi wa baadaye wa Kiafrika, wakimwona kama mtu mwenye siasa kali kwa sababu tu ya kudai kwamba “uhuru wa kitaifa ilikuwa ni hatua tu ya kwanza na muhimu kuelekea Umoja wa Afrika kama sharti muhimu kwa Waafrika kuwa huru kikweli kweli na kwa ustawi wa bara zima.

Pengine ni kutokana na ushawishi wa fikra za Du Bois, kwamba, Rais wa kwanza wa Ghana, Kwame Nkrumah, akiwa kama msemaji na mtetezi mkuu wa Pan-Africanism barani Afrika, alibuni kile kibwagizo maarufu kwamba, “utafuteni kwanza uhuru wa kisiasa na mengine yote mtazidishiwa”.

Hofu ya Du Bois na Nkrumah ilikuwa kwamba, wakati dunia [nchi za Ulaya] ilikuwa ikiungana kuunda umoja wenye nguvu, kusalimika kwa Afrika katika dunia hiyo ya uhasama kulitegemea tu Afrika kuungana kuunda Taifa moja kubwa.  Bila hivyo, Afrika ingegeuzwa uwanja wa mashindano kwa nchi za Ulaya kugombea kudhibiti vyanzo vya malighafi. Kwa maneno mengine, Afrika dhaifu, isiyo na umoja ingekuwa mhanga wa uporaji wa kigeni wa rasilimali kufanya ukoloni mkongwe uonekane “cha mtoto”.

Mkutano maarufu wa tano wa “Pan-African”, ulifanyika Manchester, Uingereza mwaka 1945 baada ya kumalizika kwa vita ya pili ya Dunia.  Ni katika mkutano huo mawazo juu ya “Pan-Africanism” yalichambuliwa kwa kina kwa misingi ya matukio na matokeo ya vita ya pili ya Dunia.  Kwame Nkrumah, wakati huo akiwa mwanasiasa tu wa kuibukia lakini mwenye kuguswa na dhana ya harakati za ukombozi wa Afrika, aliteuliwa kuwa Katibu Mkuu wa mkutano huo na kumfanya kuwa karibu zaidi na Du Bois kikazi na wakereketwa wengine weusi waliohudhuria, akiwamo Jomo Kenyatta wa Kenya.

Wanaharakati wengine waliohudhuria kutoka visiwa vya West Indies, ni George Padmore na Marcus Garvey na hivyo kupanua ukereketwa huo kuwa si wa Wamarekani weusi pekee, bali wa weusi wote ughaibuni [Diaspora] ng’ambo ya Bahari ya Atlantiki kuweza kuitwa “Trans-Atlantic Pan-Africanism”.  

Du Bois na Padmore walipewa uraia wa Ghana ilipopata uhuru mwaka 1958 kama washauri wa Nkrumah juu ya harakati za ukombozi hivi kwamba, Nkrumah, Padmore na Garvey walijipa jukumu la kuinjilisha dhana hiyo barani Afrika.

Msisitizo wa mkutano huo juu ya “Pan Africanism” ulikuja kipindi kigumu katika historia ya dunia wakati Marekani na Urusi zilikuwa zimeibuka na kujitangaza rasmi kwenye Mkutano wa Yalta, Februari mwaka 1945 kuwa mataifa mawili yenye nguvu duniani [Superpowers] baada ya kuigawa Ulaya kabla hata mbabe Adolf Hitler wa Ujerumani hajasalimu amri katika vita, Mei mwaka 1945.

Madhumuni ya waanzilishi hao wa “Pan Africanism” yalikuwa ni kutumia kipindi hicho cha mpito kwa mambo makuu ya nchi za Ulaya, Urusi na Marekani kubadili mwelekeo wa dunia kwa vizazi vijavyo; kuipa Afrika miongozo sahihi kujiimarisha katika dunia iliyokuwa ikibadilika kwa mataifa makubwa kuhodhi maamuzi.

Nkrumah alikuwa kiongozi pekee wa Kiafrika aliyetambua umuhimu wa maono ya Pan-Africanism na alitumia nguvu zake zote na rasilimali za Ghana kusaidia Ukombozi wa Afrika na baadaye katika kuanzisha OAU mwaka 1963, kama hatua ya kwanza kuelekea Serikali moja ya Shirikisho la Afrika. 

Mawazo yake yalionesha utofauti wa kiharakati, kati ya viongozi wa Kiafrika waliopata elimu yao Ulaya, hasa Uingereza na Ufaransa walioonekana kutawaliwa na siasa “poa” kwa kukosa uzoefu, ujasiri, ari na mtizamo wa kimapambano wa mtu mweusi; na viongozi waliosoma Marekani [kama Nkrumah, Azikiwe] waliojihusisha na harakati za ukombozi wa mtu mweusi hata kama ni kwa njia ya mapambano ya silaha.

Waliosoma Marekani walikuwa na maono mapana juu ya nafasi ya Afrika katika dunia ijayo; walikuwa wajasiri kwa fikra na kwa vitendo; walilenga mambo makuu kwa matarajio makubwa na walifikiri kwa misingi ya bara zima. Hawa, kwa mtizamo wa kiharakati, waliongozwa na fikra za siasa za mrengo wa Ki-Karl Marx, fikra za kimapinduzi.

Waliosoma Uingereza na Ufaransa walikosa ujasiri na uthubutu, watanashati waoga na wenye kutishika; walifikiria juu ya hatima ya Afrika kwa mtizamo wa “uhuru” wao pekee, uhuru wenye ukomo ambapo “mjasiri” sana miongoni mwao hakufikiri zaidi ya ushirikiano wa kikanda.

Hawa hawakufikiria kuona siku moja Afrika huru yenye kujitegemea kutoka kwenye makucha ya Ulaya kiuchumi na kiutamaduni licha ya wao kuongoza “nchi huru”;  walifikiri kikanda chini ya utegemezi wa Wakoloni walioondoka kwa matarajio ya kujitegemea hatua kwa hatua baadae.

Mitizamo hii miwili kinzani, ilizua kasheshe kwa siasa za Umoja wa Afrika [OAU] na kuzaa mgongano wenye kutema cheche kati ya watetezi wake wakuu wawili – Rais Nkrumah wa Ghana na Rais Julius Nyerere wa Tanganyika kufikia wawili hao kutoleana maneno machafu. 

Wakati Nkrumah alitaka nchi ziungane mara moja [Africa Now] kuunda Taifa moja la Afrika [United States of Africa – USA] kama ilivyo Marekani [USA], Nyerere alitaka Muungano kama huo ufikiwe kwa kuanza na miungano ya kikanda [regionalism] kama vile Shirikisho la Afrika Mashariki [EAF] alilokuwa akifukuzia wakati huo, kati ya Kenya, Zanzibar, Uganda na Tanganyika.

Nkrumah alimwonya Nyerere kwamba, mawazo yake hayo yenye kutoa ridhaa kwa ukoloni mamboleo kuzikaba koo nchi za Afrika zisiweze kuungana kamwe, yalikuwa ya hatari kwa umoja, na akashangaa kwa nini Makao Makuu ya Harakati za Ukombozi wa Bara la Afrika yalipelekwa Dar es Salaam kwa mtu [Nyerere] anayelipwa na mabeberu.

Ugomvi wa Nyerere na Nkrumah ulijidhihirisha kwa upevu kwenye Mkutano wa OAU mjini Cairo mwaka 1964 mitizamo hii miwili kinzani ilipojadiliwa ili OAU iridhie mmoja kati ya hiyo, pale Nkrumah alipomshambulia Nyerere kwa kumwita “kibaraka na wakala wa Mabeberu”; naye Nyerere akajibu mapigo kwa kumwita Nkrumah “hayawani kiwango zaidi ya mwendawazimu”.

Kwenye mpambano wa majabali hayo mawili, uliopewa jina “The Great Cairo Encounter”, kambi ya Nyerere, ya mtizamo wa kikanda ilishinda na kuwa ndiyo sera ya OAU kuhusu njia sahihi kuelekea Umoja wa Afrika imara.

Nkrumah, kwa kuongozwa na fikra za Du Bois, alisikika akilalama pembeni akisema, kwa Afrika kukubali msimamo wa Nyerere itajutia hatua hiyo na kuendelea kuwa dhaifu, kwamba haitaungana kamwe; na pia kwamba wale walioiburuza kufikia uamuzi huo, historia itawahukumu.

Ni ukweli ulio dhahiri, kwamba zaidi ya nusu karne ya uhuru hadi leo, Afrika haijaungana; Miungano ya kikanda kama vile EAF na ECOWAS [Afrika Magharibi] imejaribiwa na kuvunjika hima.  Nyerere, baada ya kushindwa kwa juhudi za kuunda Shirikisho la Afrika Mashariki kwa msaada wa Uingereza na Marekani, aligeukia muungano duni zaidi [hapa tena kwa msaada wa Marekani na Uingereza], kati ya Tanganyika na Zanzibar ambao hata hivyo hautoi matumaini wala ishara njema kuelekea Muungano wa Bara zima.  Afrika ni dhaifu zaidi leo kuliko ilivyokuwa enzi za uhuru.

Kufikia hapo tunaweza kuhitimisha makala yetu kama ifuatavyo:  Pan-Africanism ni wazo turufu na chimbuko la harakati za ukombozi wa mtu mweusi lililowasha moto wa ukombozi kwa nchi za Kiafrika, kwa kuanza na Ghana ya Nkrumah iliyopata uhuru mwaka 1958 na kuenea nchi zingine Barani. Madhumuni ya Pan-Africanism yalikuwa pia ni kulinda na kuinua heshima ya mtu Mweusi asiendelee kubaguliwa na kunyanyaswa na kabila la Weupe kisiasa, kiuchumi na kiutamaduni kwa kujitangazia ukuu kwa njia ya Muungano [USA] imara wenye kuogopwa na kuheshimiwa.

Mkakati huu wa mwisho uliingia nyongo baada ya Viongozi wa nchi huru kutofautiana, kwa baadhi yao kutaka kuendeleza uhusiano na wakoloni walioondoka na uhuru ukageuka “uhuru wa bendera” kwa kukabwa koo na ukoloni mamboleo.

Ingetokea kwamba Afrika imeheshimu fikra za Du Bois na Kwame Nkrumah, je, ingekuwa imara na salama zaidi kuliko ilivyo sasa?.  Mungu ibariki Afrika.