Home Michezo Kimataifa Pogba anasubiri nini Man United?

Pogba anasubiri nini Man United?

1153
0
SHARE

HASSAN DAUDI NA MITANDAO

KWA sasa ni wazi mashabiki wa Manchester United hawana raha kwa kile kinachoendelea kati ya mabosi wa klabu hiyo na kiungo wake, Paul Pogba.

Pogba ameonesha nia ya kuondoka, ushahidi ni kauli yake ya wiki chache zilizopita, kwamba ni ndoto ya kila mchezaji kutua Real Madrid, moja kati ya klabu zinazomtaka.

Wakati ikiwa hivyo kwa upande wake, mabosi wa Man United hawataki kuona akiondoka. Wanapambana kila wanavyoweza kumbakiza.

Mfano mzuri ni kile walichosema mwanzoni mwa wiki hii, kuwa wako tayari kumpa mshahara wa Pauni milioni 500,000 kwa wiki.

Lakini je, kwanini Man United waendelee kumshinikiza mchezaji ambaye si tu hataki kubaki, pia ni mtukutu, akipewa jeuri na rekodi ya usajili ya Pauni milioni 89?

Ubaya ni kwamba historia inaonesha kuwa Pogba ni mchezaji wa aina hiyo tangu akiwa na umri wa miaka 19, licha ya ukweli kwamba hiyo haitoshi kusema ni mchezaji mbovu.

Akiwa Man United kipindi hicho, alikorofishana mara kadhaa na kocha Alex Ferguson na hiyo ilikuwa moja kati ya sababu za kutimkia Juventus, ingawa tamaa ya fedha aliyokuwa nayo wakala wake, Mino Raiola, nayo ilichangia.

Juu ya hilo la kutokuwa na maelewano na Ferguson, itakumbukwa kuwa Pogba aliwahi kushangilia bao la mchezaji wa timu pinzani dhidi ya Man United.

Ulikuwa ni mtanange dhidi ya West Ham na mfungaji siku hiyo alikuwa nyota mwenzake katika kikosi cha timu ya taifa ya Ufaransa, Dimitri Payet.

Ikiwa ni miaka saba imepita tangu alipooneshwa mlango wa kupitia kujiunga na Juve, ambako ndiko alikoweza kujitangaza upya kama mchezaji wa kiwango cha dunia, haionekani kuwa Pogba amebadilika.

Ingawa Mashetani Wekundu waliamua kuvunja kibubu na kumnunua kwa ada iliyovunja rekodi ya usajili duniani, bado Pogba hajaonekana kutambua thamani yake.

Msimu uliopita ulimalizika kwa tabu, matukio yake ya nje ya uwanja yakichangia kiwango kibovu alichokuwa nacho, hivyo kukorofishana na kocha wake, Jose Mourinho.

Akiwa amepewa heshima kubwa kwa kutangazwa kuwa nahodha msaidizi, alijikuta akipoteza heshima hiyo kutokana, kabla ya kuanza kusugulishwa benchi mara kwa mara.

Kama hiyo haitoshi, iliwashangaza wengi kwa kitendo chake cha utovu wa nidhamu baada ya kocha huyo wa kimataifa wa Ureno kutimuliwa Old Trafford.

Haikuchukua muda mrefu baada ya Man United kutangaza kuwa Mourinho si kocha wao tena, Pogba aliingia katika mitandao ya kijamii kuonesha kukoshwa na hatua hiyo ya mabosi wake.

Mbaya zaidi, huku akiwa kwenye kiwango kibovu, safari hii nyota huyo anashindwa kuiheshimu Man United kwa kauli yake kuonesha wazi nia yake ya kwenda Madrid.

Ni kwa mazingira hayo ya utovu wa nidhamu, unaweza kuona ilivyo ngumu kwa kocha yeyote kufanya kazi na Pogba, ikitilia shaka pia kuwa huenda akashindwana na Zinedine Zidane anayemtaka kule Hispania.

Tukirejea kwa Mourinho, hata alipofukuzwa na kibarua chake kutua kwa Ole Gunnar Solskjaer, haikuchukua muda mrefu kabla ya mambo kurejea kule kule. Hiyo ilithibitisha kuwa huenda Mourinho hakuwa tatizo, bali aina ya wachezaji waliopo, hasa wale wa aina ya Pogba.

Ukitazama mambo yanavyokwenda pale Old Trafford, unaweza kuona hata uhusiano wake na Solskjaer si wa kuuamini.

Miezi michache iliyopita, mkongwe huyo wa Man United aliweka wazi kuwa mchezaji yeyote anayetaka kuondoka klabuni hapo afanye hivyo, kauli ambayo kwa wafuatiliaji wa filamu ya Pogba, wanaweza kuona ililenga kumpa ‘makavu’ nyota huyo.

Mwishowe, kumuuza kutaipa Man United si chini ya kitita cha Pauni milioni 85, ambazo Adrien Rabiot, Youri Tielemans, Tanguy Ndombele au Ivan Rakitic.