Home Makala POMBE YAGEUZWA KITULIZO CHA WATOTO MBEYA

POMBE YAGEUZWA KITULIZO CHA WATOTO MBEYA

780
0
SHARE

NA FARAJA MASINDE – ALIYEKUWA MBEYA

KATIKA Kitongoji cha Isyesye, kaskazini mwa barabara kuu iendayo Tunduma katika Jiji la Mbeya, ndiko anakoishi Mariam Sungura, mama wa familia ya watoto watatu akiwamo mwenye umri wa miaka miwili na nusu.

Kwa maelezo ya Mariam, mumewe aliyemtaja kwa jina la Raymond hayupo nyumbani kwa takriban miezi sita sasa.

Ametimkia Arusha ambako amekwenda kutafuta maisha bora, hivyo kumwachia wajibu wa kuwatunza na kuwalea watoto wao watatu.

Jukumu la ulezi linamfanya Mariam (35) kila uchao kwenda kutafuta kipato kwa ajili ya matunzo ya watoto wake. Akiwa huko watoto wake huwaacha mikononi mwa mdogo wake wa kike akiamini wako salama.

Hata hivyo wakati mwingine aliyeachiwa watoto naye huondoka. Hivyo kuna nyakati ambazo ni dhahiri  kwamba watoto hawa wenye umri mdogo, hubaki peke yao katika nyumba pasipo uangalizi wa mtu yeyote.

Baadhi ya majirani wa Mariam wanasema katika mazingira hayo watoto hutoka na kuanza kuzunguka mitaani na katika nyumba za majirani wakicheza na wenzao na wakati mwingine kuambulia mlo katika nyumba hizi.

Pamoja na kutoshinda nyumbani, tabia hii ya watoto haimpendezi Mariam. Hivyo anaamua kuwadhibiti wanawe. Udhibiti huu si mwingine, bali anaamua kuanza kuwanywesha watoto hawa pombe ya kienyeji.

Hivyo watoto wanakunywa pombe aina ya kimbi. Ikiwakolea, wanalala usingizi kutwa. Wanaacha kuzurura!. Miongoni mwa watoto ambao wanafanyiwa vitendo vya aina hii yumo mtoto wake wa mwisho (jina tunalihifadhi) mwenye umri wa miaka miwili na miezi sita.

Mariam katika mazungumzo yake na gazeti hili anasema: “Ni kweli huwa nawapa pombe lakini siyo mimi peke yangu, ni utamaduni ambao upo kwa wanajamii wengi wa huku kuwapa pombe watoto wao na hata wengine kwenda nao kwenye vilabu hadi nyakati za usiku mkubwa”.

Anasema amekuwa akifanya hivyo kwa muda mrefu na kwamba lengo ni kuhakikisha wanakuwa watulivu huku akisisitiza kuwa watoto kupewa pombe ni utamaduni uliozoeleka kwa wakazi wengi wa eneo hilo la Isyesye.

“Kwangu mimi nimekuwa nikiwabebea pale ninapopata nafasi au inapotokea nimepewa ofa na mtu, na nimekuwa nikifanya hivi kwasababu walikuwa wakiniona nikija nyumbani na chupa ya pombe wanalilia hivyo inanibidi tu niwape,”anasema Mariam na kuongeza:

“Wakishakunywa tu wanalala kabisa usingizi kwa namna hiyo wanakuwa wananiepushia usumbufu wa kwenda kwa majirani nikiwa sipo”.

Anasema anaamini kwamba pombe hiyo haina madhara kwa watoto mbali na kuwalewesha tu na kisha kulala.

Muhudumu wa afya wa Kata ya Isyesye, Isaac Charles anasema changamoto ya wazazi kuwapa watoto pombe ni kama imeota mizizi licha ya hatua kadhaa ambazo zimekuwa zikichukuliwana serikali.

Kuhusu Mariam, Charles anasema wanasikitishwa na vitendo vyake vya kuwapa pombe watoto wake ili tu walale na wasiweze kuleta usumbufu pale anapokuwa amekwenda kwenye mihangaiko yake jambo ambalo ni hatari kwa afya na ustawi wa mtoto hao

“Watoto hawa wamekuwa wakipewa pombe aina ya kimbi na kimpumu ili tu waweze kulala ndani na kutokwenda kwa majirani, utaratibu ambao umekuwa ukipewa nguvu sana na wanajamii wengi wa huku wa kuwapa pombe watoto wao ili wasiwasumbue bila kutambua athari zake kiafya,”anasema Charles.

Afya za watoto

Tabia na mwenendo wa Mariam unawafanya watoto wake wawili; mwenye umri na miaka mitano na yule mwenye umri wa miaka minne kuonekana kama wamedumaa, huku mtoto mwenye umri wa miaka miwili na nusu akithibitika kuwa na tatizo la utapiamlo mkali.

Hata hivyo utetezi wa Mariam ni kwamba inakuwa vigumu kwake kuwahudumia watoto wake ipasavyo kutokana na kutumia muda mwingi kwenye mihangaiko, hivyo kuwaacha wanawe chini ya uangalizi wa mdogo wake.

“Shida kubwa ni fedha pamoja na kwamba nina ‘fremu’ za maduka lakini bado sifaidiki na chochote kwani mume wangu alichukua fedha yote ya miezi sita na kuondoka nayo jambo ambalo inaniwia vigumu hata pale watoto wanapougua kuweza kuwatibia,”anasema Mariam.

Anasema kadri anavyoendelea kuishi maisha yanazidi kuwa magumu kwake na familia yake na kwamba amekuwa akijitahidi kufanya vibarua vya kulima na kufua nguo kwenye miji ya watu ambavyo vimekuwa vikimuingizia Sh 4,000 kwa siku.

“Hata hivyo pamoja na kupata kiasi hicho cha pesa bado hakitoshelezi mahitaji ya kuendesha familia kwani mahitaji ni mengi kuliko kipato ninachopata,” anasema.

Anasema katika mazingira hayo, amekuwa akijitahidi kuhakikisha watoto wake wanakuwa na lishe ya kutosha.

“Mimi ninavyofahamu lishe ni uji wa mahindi yaliyokobolewa, hivyo nimekuwa nikiwapa wanangu pale inapowezekana au wakati mwingine nawapa ugali na mchuzi wa mboga za majani, kwani ndio lishe ninayoifahamu,”anasema na kuongeza:

“Kwahiyo nalazimika kumpa uji asubuhi kisha naenda kibaruani kwani sina namna zaidi ya kuhakikisha kuwa nafanya hivyo ili mwisho wa siku niweze kupata chochote”.

Anaendelea: “Nikishamwandalia mtoto wangu uji pamoja na maziwa, namwachia mdogo wangu anamnywesha. Nilikuwa nikifanya hivyo hata kwa wengine waliotangulia,” anasema.

Takwimu za Wizara ya Afya zinaonyesha ni asilimia 9 tu ya watoto wa umri wa kati ya miezi 6 hadi 23 Tanzania Bara wanaopata viwango vinavyokubalika vya lishe bora kwa maana ya mlo katika muda unaoeleweka, uanuwai wa chakula na kiwango cha unyonyeshaji wa watoto kwa maziwa ya mama.

Katika Ripoti ya Utafiti wa Hali ya Lishe nchini ya 2014, Mbeya inatajwa kuwa miongoni mwa mikoa ambayo watoto wake wenye umri kati ya miezi sita na miaka miwili wanalishwa vyakula kutoka katika makundi (ya vyakula) chini ya manne.

Kwa mujibu wa ripoti hiyo iliyoratibiwa na Kituo cha Chakula na Lishe (Tanzania Food and Nutrition Centre – TFNC), ni watoto 10 tu kati ya 100 (asilimia 10) mkoani humo, ambao wanapata vyakula kutoka katika makundi manne tofauti.

Mikoa mingine katika kundi hilo ambalo liko chini ya wastani wa kitaifa ambao ni asilimia 25 kwa sasa ni Iringa, Singida, Tabora, Manyara na Katavi hali ambayo inatajwa na ripoti hiyo kuwa ni mbaya.

Ripoti hiyo inaonyesha kuwa hali ilikuwa tofauti katika mikoa miwili;  Kilimanjaro na Tanga ambayo watoto wake katika umri huo wanapata vyakula katika makundi manne muhimu kwa asilimia 66.3 na 79.5% sawia.

Maisha ya Mariam

Mariam kwa upande wake anakiri kuwa hawezi kupata usingizi iwapo hatapata lita moja ya pombe kila siku iendayo kwa Mungu, ambayo inauzwa Sh 500 kwa lita.

Anasema ni mazoea hayo ya kupenda pombe ndiyo yamesababisha hadi awe anaileta nyumbani na kuwanywesha watoto wake kwa lengo la kuwatuliza na kuwasaidia kupata usingizi.

“Msema kweli siku zote ni mpenzi wa Mungu ni kweli pombe nimekuwa nikinywa na hata hapa ninavozungumza na wewe koromeo linakwangua kweli (saa 10 jioni) ingekuwa ni uwezo wangu sasa hivi nimeshaenda kilabuni kupata lita moja.

“Pombe yenyewe siyo pesa nyingi ni Sh 500 tu kwa lita unapata kimbi yako hivyo siwezi kuacha kuchangamsha akili kwasababu ya kubana matumizi kwani hata nikiacha hiyo Sh 500 bado haitoshi kuendesha maisha,”anasema Mariam na kuendelea:

“Mara ninapokuwa nimerudi nyumbani kutoka kibaruani jioni au mchana nafika na kubadili nguo kisha baada ya hapo naoga na kula chakula kwakuwa mdogo wangu tayari anakuwa amepika ugali na mboga za majani kama ilivyo kawaida yetu na watoto wanakuwa tayari wamekula basi naenda kupata lita moja ya kimbi hadi saa nne au saa saba usiku narudi nyumbani.

“Kwa kuwa mahala ninapokunywa pombe siyo mbali sana na nyumbani lakini pia watoto wanakuwa na mama yao mdogo hivyo nakuwa sina wasiwasi labda tu kwa huyu wanayesema kwamba anaumwa utapiamlo”.

Kwa upande wake Charles anasema Oktoba mwaka jana, ofisi yake ilipokea malalamiko kutoka kwa majirani wa karibu na Mariam juu ya tabia zake zisizofaa za kuwapa watoto pombe kali badala ya lishe bora jambo ambalo limesababisha utapiamlo kwa mtoto mdogo.

“Mtoto (anamtaja jina) tulimbaini hali yake baada ya kuambiwa na majirani ambao walikuwa wakimsaidia kumpa chakula pale inapowezekana kutokana na mama yake kujisahau kwenye ulevi, baada ya kumuona tulichukua jukumu la kumpima na kubaini kuwa alikuwa na utapiamlo mkali sana.

“Hivyo tulimtaka mama yake ampeleke kwenye zahanati haraka iwezekanavyo, lakini alitujibu kuwa tayari alikuwa amempeleka mtoto huyo kwa mganga wa kienyeji na kupewa dawa za kupaka na kuchanja mwilini kwa kile alichoamini kuwa alikuwa amelogwa,” anasema Charles na kuongeza:

“Baada ya kumlazimisha sana alimpelaka mtoto kwenye zahanati ya Isyesye na kubaini kuwa alikuwa na utapiamlo mkali ambao ulihitaji kupatiwa ufumbuzi haraka iwezekanavyo ikiwamo kupata lishe bora”.

Mtaalamu huyo wa afya anasema kutokana na mama huyo kudai kwamba hana uwezo kifedha kwa ajili ya kumhudumia mwanaye, ofisi yake ilimpatia Sh 50,000.

“Baada ya hatua hiyo ofisi iliamini kwamba mtoto alikuwa akipatiwa huduma, lakini mama yake alifanya kinyume kwa kuanza kumfungia ndani ili kuepusha majirani wasimuone kwa kuamini kuwa ndio waliofichua uovu huo.

“Hivyo mtoto akawa ni wakufungiwa ndani kwa maana kwamba mama akitoka mtoto anakuwa wa ndani na akiwepo pia bado mtoto hatoki kwa kile alichoeleza kuwa hakuwa na uwezo wa kumhudumia,” anasema Charles. Mtoto huyo hadi sasa hawezi kusimama wala kuzungumza kinyume kabisa cha umri wake.

Hali ya utapiamlo

Charles anasema familia kadhaa katika Kata ya Isyesye zina watoto wenye tatizo la utapiamlo na kwamba unywaji pombe unachangia kwa kiasi kikubwa.

Anasema sababu nyingine ni wazazi kutumia muda mwingi kutafuta fedha na kuwaacha watoto wao bila uangalizi madhubuti.

“Ukiachilia mbali wazazi kutokuwa na uelewa wa kutosha juu ya lishe bora lakini pia shida kubwa imekuwa kwenye mila potofu kwani mzazi anaamini kuwa hakuna ugonjwa unaosababishwa na ukosefu wa lishe unaoweza kuathiri afya ya mtoto zaidi ya kulogwa,”anasema.

Anasema kwa sasa wamepiga marufuku vilabu vyote vinavyouza pombe hizo za kienyeji ili kuwafanya wazazi kuwajibika zaidi kwenye familia zao.

Afisa Maendeleo Kata ya Isyesye, Elly Mwakaswaga naye anakiri kwamba kumekuwa na kazi kubwa katika kuwaelimisha wananchi juu ya kuwapa watoto lishe bora.

“Changamoto kubwa inayosababisha tuendelee kuwa na idadi kubwa ya jamii yenye watoto wenye udumavu na utapiamlo ni kwamba watu wanaotumika kutoa elimu kwa wananchi wanafahamika hivyo ni vigumu kusikilizwa na jamii.

“…kwahiyo hakuna mzazi anayetilia maanani mafunzo na  matokeo yake hali ya udumavu na utapiamlo vinaendelea kuwapo. Wazazi wapo tayari kushinda kwenye kilabu cha pombe kuliko kuandaa lishe bora kwa ajili ya familia, kibaya zaidi wanabeba hizo pombe na kuwapa watoto wao nyumbani,” anasema Mwakaswaga.

Ripoti ya Utafiti wa Hali ya Lishe nchini ya 2014 iliyozinduliwa Aprili 2015 zinaonyesha kuwa Mbeya ni miongoni mwa mikoa ambayo kiwango cha udumavu kwa watoto wake kiko juu wa wastani wa kitaifa ambao ni asilimia 34.7, kiwango ambacho hata hivyo bado ni kikubwa kwa mujibu wa Shirika la Afya Duniani (WHO) .

Ripoti hiyo iliyoratibiwa na TFNC inaonyesha kuwa kiwango cha udumavu mkoani Mbeya ni asilimia 37.7 sawa na mkoa wa Mtwara.

Mikoa hiyo imetanguliwa na mikoa na viwango vyake kwenye mabano ambayo ni Rukwa (56.4), Njombe (49.4), Ruvuma (44.4), Kagera (41.7), Iringa (41.6), Geita (40.5), Tanga (39.4), Katavi (38.8), Mwanza (38.6) na Kigoma (37.9).

Ripoti hiyo pia inaonyesha kuwa takribani watoto milioni 2.7 wenye umri chini ya miaka mitano walikuwa na udumavu, 600,000 walikuwa na utapia mlo wa kadri huku 100,000 wakiwa na utapiamlo mkali.

Ripoti hiyo ilipendekeza kuchukuliwa kwa hatua za haraka katika mikoa yenye viwango vya juu vya udumavu kwa watoto pamoja utapiamlo mkali, Mbeya ukiwa mmojawapo. Mikoa mingine katika orodha hiyo ni Kagera, Kigoma, Dodoma na Mwanza.