Home kitaifa PROF. MRUMA: MPANGO WA UPOKEAJI MAFUTA KWENYE GHALA MOJA UTAKOMESHA WIZI...

PROF. MRUMA: MPANGO WA UPOKEAJI MAFUTA KWENYE GHALA MOJA UTAKOMESHA WIZI BANDARINI

4531
0
SHARE
Mwenyeki wa Bodi ya kampuni ya Kuhifadhi Mafuta ya Tanzania (TIPER) Prof Abdulkarim Mruma

NA MWANDISHI WETU


MOJAWAPO ya changamoto iliyokuwa inaikabilia bandari ya Dar es Salaam, ni upotevu na wizi wa baadhi ya vifaa na mizigo inayopitishwa katika bandari hiyo.

Hali hiyo ilichangia kwa kiasi kikubwa kudorora kwa shughuli za forodhani katika bandari ya Dar es Salaam na kutoa mwanya kwa bandari shindani kujitanua.

Hata hivyo, kutokana na uongozi dhabiti na mikakati iliyoboreshwa ndani ya bandari hiyo, hali imekuwa tofauti huku wateja wakianza kumiminika.

Mipango hiyo pia imeenda mbali zaidi ikiwamo katika sekta ya mafuta ambayo nayo iliingiliwa na wimbi la changamoto lukuki.

Katika kumaliza changamoto hizo Kampuni ya Kuhifadhi mafuta Tanzania (Tipper) inatarajia kuwa kituo pekee cha  upokeaji  wa  mafuta yote yanayoingia nchini kupitia bandari ya Dar Es Salaam.

Hayo yamebainishwa hivi karibuni wakati Bodi ya Wakurugenzi ya kampuni hiyo  (TIPER) ikikabidhi kwa Rais John Magufuli  gawio la Sh bilioni tatu ikiwa ni sehemu ya gawio la Sh bilioni 6 kwa mwaka 2017 ambalo Tipper imetoa kwa wanahisa wake ambao ni serikali pamoja na Kampuni ya Addax-oryx group ya nchini Uswiss.

 

Akizungumza kwenye hafla hiyo, Mwenyekiti wa Bodi wa Kampuni hiyo Prof.  Abdulkarim Mruma anasema kiasi hicho ni ongezeko kutoka kiwango cha Sh bilioni moja kwenye miaka ya 2000 na wastani wa karibu Sh  bilioni mbili katika kipindi cha kati ya 2010-2013.

“Uongozi wa kampuni unaona fahari kubwa kuweza kusimamia uendeshaji  na  kuweza  kukuza gawio kwa wanahisa wake.’’ anasema.

Akizungumzia mpango wa upokeaji wa mafuta kwenye ghala moja ambao kampuni hiyo inatarajia kuwa kituo pekee cha  upokeaji  wa  mafuta yote yanayoingia nchini kupitia bandari ya Dar Es Salaam, Prof. Mruma anasema manufaa  yanayoyotarajiwa           kupatikana   kutokana   na  mpango huo yameshajadiliwa na kupokelewa vyema na wadau wote.

“Faida za mpango huu zipo wazi ambazo ni pamoja na udhibiti bora wa kiwango cha mafuta kinachoingia nchini, kupunguza upotevu na wizi wa mafuta, kuzifanya gharama za ucheleweshaji wa meli zinazolipwa sasa kwa wamiliki wa nje wa meli kuwa mapato ya serikali.’’ anasema

Anasema ili kufanikisha mradi huu, Bodi ya Wakurugenzi  ya TIPER  imepitisha  mpango  mahususi  wa uwekezaji wa zaidi ya Dola za Marekani milioni 22  ndani  ya kipindi  cha 2018 mpaka 2019.

“Tumeazimia kuongeza uwezo wa kuhifadhi mafuta  kwa asilimia  50  kutoka  mita  za ujazo  213,000 mpaka mita za ujazo 319,000 kwa kujenga matanki mawili mapya yenye ujazo wa mita za ujazo 30,000 kila moja na  kukarabati  tanki  moja  lililokuwa  la  mafuta  ghafi  lenye  ujazo  wa mita za ujazo 46,000.’’ anasema.

Anataja  azimio lingine kuwa ni kutandika bomba la pili la mafuta ya  Petroli  kati  ya  Kurasini  na  Kigamboni Kuongeza uwezo wa kusukuma mafuta kwa zaidi ya asilimia 50 kwa

kujenga kituo kipya cha kusukumia mafuta ambacho kitakua na mashine sita mpya pamoja na  kukarabati mfumo wa kuzima moto ili kuongeza kiwango na kufikia viwango vinavyokuballiwa kimataifa iii kuhakikisha mafuta yako salama ndani ya ghala la TIPER.

“Mpango huu wa upanuzi wa ghala unafanikishwa kwa fedha inayotokana na mapato ya  ndani pamoja na mkopo wa Dola za Marekani milioni 15 kutoka benki.’’

Anasema mafanikio ya mradi huo yatakuwa ni chanzo cha kushughulikia miradi mingine kama ghala maalumu  la Forodha ambalo litavutia mafuta mengi kuingia nchini ili koboresha  nguvu  ya  ushindani  na kuifanya Bandari ya Dar Es Salaam kuwa Bandari mkakati itakayovutia uingizaji wa kiwango kikubwa cha mafuta kwa ajili ya Biashara ya nchi jirani katika ukanda huu.

“Niwashukuru wadau wote upande wa Serikali na Sekta binafsi  ambao  walituwezesha  kufikia matokeo mazuri ya pato halisi la Sh bilioni 9.9 kwa  mwaka  2017  kutoka pato la Sh bilioni 6.5  mwaka  2016,  na kufanikiwa  kuongeza  gawio kwa kiwango hicho.’’ anasema