Home Makala PROF. RUTATORA: Nimejipanga kuisafisha KCU (1990) Ltd

PROF. RUTATORA: Nimejipanga kuisafisha KCU (1990) Ltd

1133
0
SHARE

NA MWANDISHI WETU

BAADA ya wajanja wachache kukitumia Chama Kikuu cha Ushirika mkoani Kagera KCU (1990) Ltd kujinufaisha, hatimae serikali ya awamu ya tano iliona haja ya kuufumua ushirika huo.

Dhamira kuu ya kufanya hivyo ni kuhakikisha ushirika huo unakuwa na tija iliyokusudiwa kwa wakulima wa kahawa mkoani Kagera.

Ili kufanikisha tija hiyo, baadhi ya viongozi walitumbuliwa na wengine kuhamishwa. Kutumbiliwa kwao kuliwakwaza wengi hasa wapambe na vibaraka wao, ambao wameapa na kujiapiza kuwa watatumia kila mbinu kuhakikisha waliotumbuliwa wanarejea madarakani.

Mikakati haramu na halali imekuwa ikifanyika kuhakikisha hilo linafanikiwa, haielezwi wazi wazi sababu ya baadhi ya viongozi hao waliotumbuliwa  kuung’ang’ania ushirika huo.

Jambo la kushukuru na lililotazamiwa na wengi ni hatua ya serikali kumtafuta mtaalamu na msomi wa masuala ya kilimo ambaye ni Mhadhiri katika Idara ya Ugani Chuo Kikuu cha Kilimo cha Sokoine (SUA) Profesa Deogratias Rutatora.

Prof. Rutatora ambaye sasa ndiye Mwenyekiti mpya wa Bodi ya ushirika huo wa Kagera ni mchapakazi mwenye kuyajua vema mabaya na mazuri ndani ya sekta ya kilimo, lakini pia ni mbobezi katika uongozi hasa wa eneo hili la kilimo.

Amefanikiwa kuandaa maandiko lukuki yenye tija, yanayotoa mwanga wa kuendeleza na kuboresha kilimo nchini, anaujua umuhimu wa sekta ya kilimo.

Alipata kusema kuwa sekta ya kilimo ndiyo pekee inayoweza kulivusha taifa kutoka katika umasikini, amekuwa akiwataka wakulima kujitambua na kutambua thamani yao kwa kulimo kwa bidii ili kujikomboa.

Kutokana na sifa hizo, RAI liliiona haja ya kufanya mahojiano na msomi huyu wa kilimo ili kuzungumzia masuala mbalimbali ikiwa ni pamoja na madai ya kuiogopa ofisi yake mpya ya KCU (1990) Ltd.

RAI: Zipo taarifa umegoma kuripoti ofisi yako mpya kwa hofu ya kuhujumiwa?

PROF: Si kweli, taarifa hizo zinapaswa kupuuzwa, sina sababu ya kuogopa kutekeleza majukumu yangu mapya, ikumbukwe mimi sikuiomba nafasi hiyo, nilipigiwa simu mara kadhaa na wahusika, wakitaka nikaifanye kazi hiyo.

Sikuona sababu ya kukataa maana najua uwezo wa kuifanya kazi hiyo ninao na hata uzoefu wa kutosha upo, hivyo sikuona haja ya kukataa.

Wanaosema naogopa kuanza jukumu langu jipya hawana uelewa wa kutosha, mimi nimeshaanza majukumu yangu na nimeshafanya vikao  kadhaa na wenzangu, bahati mbaya nimeshindwa kutekeleza majukumu yangu kwa kasi ninayoitaka kwa sababu, baadhi ya watu watendaji ambao nilishaanza kufanya nao kazi wamehamishwa.

Siwezi kuendelea na mipango yangu kabla ya kuwa na wajumbe wa bodi, nasubiri wateuliwe wengine na nadhani tayari baadhi yao wameshaanza kuteuliwa, zoezi hilo likikamilika tutaendelea na kile tulichokianza.

Nimejipanga kuusafisha ushirika wa Kagera, sitataka uzembe, sitaki kuwepo na madudu, kila mtumishi wa ushirika nitataka ajipime mwenyewe, nataka nifanikisha dhamira njema ya serikali yangu ya kuniona naweza kuwa msaada kwa wakulima wa Kahawa mkoani Kagera.

Ni lazima tuwe na mikakati imara, hatuwezi kukurupuka maana nataka ushirika uwe kimbilio la wakulima, sitaki niondoke pale nikiacha kilio, hapana hilo sitalipa nafasi.

Kiu yangu ni kuhakikisha kila mtumishi wa ushirika ule anafanya kazi kwa maslahi ya wakulima, sitakuwa na utayari wa kulea uzembe na kama mtu ataona hawezi kwenda na kasi yangu nitamruhusu anipishe.

Halitakuwa jambo rahisi kuendelea kuwa na mtumishi ambaye hanafaida kwa ushirika.

Hivyo niseme kwa kifupi tu, sina ninachoogopa, ninachofanya ni kusubiri kuundwa kwa bodi ili kile nilichokianza kiendelee, tayari nimeshaanza kupita vijijini na maeneo mengine mengi ili kuangalia nitafanikishaje malengo yangu.

Nataka niache kitu kizuri ndani ya ushirika katika kipindi changu chote cha utumishi. Hamu yangu ni kuuendesha kibiashara maana ile ni biashara si kijiwe.

RAI: Zipo taarifa uongozi wa awali utarejea madarakani ndani ya wiki hii, kuna ukweli juu ya hili?

PROF: Nashindwa kulisemea hili kwa sababu ni suala gumu, lisilowezekana hata kama ingekuwa ni ofisi binafsi sidhani kama lingewezekana.

Tukumbuke waliokuwapo wamewekwa pemeni kwa sababu fulani fulani hivi, sasa inawezekanaje kurejea madarakani kwa sababu gani na kwa uamuzi wa nani. Hata hivyo sitaki kulisemea hili sana kwa sababu silijui, muhimu kwangu ni kuona natekeleza majukumu yangu na tayari nimeshaanza kuyatekeleza kwa ufanisi.

RAI: Matarajio yako hasa ni kufanya nini ambacho unaona kimewashinda watangulizi wako?

PROF: Siko tayari kujifananisha au kushindana na yeyote, ile nadhani yapo mapungufu na ndio maana nimeteuliwa kuongoza pale. Sasa hitaji langu ni kuhakikisha nasawazisha mapungufu hayo ili ushirika uwe na tija.

Natambua hali hii si kama imeukuta ushirika wa Kagera pekee, ni matatizo yapo kwenye vyama vyote vya ushirika nchini, sasa mimi dhamira yangu ni kutaka kuonesha njia sahihi ya kupita ili hata atakayekuja acute njia sahihi, nadhani unajua kuwa mimi ni kama mwenyekiti wa mpito tu na kazi yangu ni kusawazisha mambo ili watakaokuja wapate pa kuanzia.

Ombi langu kwa wanaushirika wote wa Kagera ni vema wakatupatia muda ili mimi na bodi kwa ujumla tufanye kile kinachopaswa kufanywa, kwa sasa tunakwama kwa sababu ndogo ndogo ikiwa ni pamoja na mabadiliko ya Mrajisi.