Home Makala Profesa Lipumba arejee alipoangukia  

Profesa Lipumba arejee alipoangukia  

1049
0
SHARE

 

Profesa  Ibrahim Lipumba 1AGHALABU siasa  za Tanzania zinanikumbusha Muasia raia wa Uingereza, Eric Blair maarufu kwa jina la George Orwell, na riwaya ya Shamba la Wanyama-Animal Farm.

Mtu huyu alizaliwa mwaka 1903 nchini India, mahali ambako babaye alifanya kazi katika utumishi wa umma huko Bengal.

Jamaa huyu alipelekwa Uingereza angali kinda, na kusoma katika shule nzuri  ya binafsi iitwayo Eton.

Kwa ujumla, jamaa huyu aliishi maisha ya kijungujiko, akajaribu kutafuta ajira hata ya upolisi, akaacha, akaosha vyombo hotelini huko London na Paris(Ufaransa)akaacha.

Aliwahi kuishi na ‘Machokoraa’  na ‘ma-Day Worker’ wa miji hii, hadi alipoamua kuandika vitabu kuhusu suluba za maisha yake huko mitaani London na  Paris.

Ameandika ‘Burmese Days’ akikumbuka zama alizopata upolisi huko Burma, siku hizi nchi hii inaitwa, Myanmar.

Kitabu kingine ni “Down and Out in Paris and London”, “Homage to Catalonia”, na vingine kama vine hivi.

Hata hivyo, kati ya vitabu hivyo vyote, kitabu kiitwacho, “Shamba la wanyama” kwa Kiingereza, The animal farm kinashabihiana sana na harakati za siasa za vyama vingi kutaka kuwakomboa Watanzania mikononi mwa Ukoloni Mamboleo na kujenga taifa lisilo na matabaka.

Orwell alifariki dunia Januari 1950 alikuwa mwandishi mashuhuri kutokana na kitabu hicho ambacho hakikuwa na lengo la kuzungumza kuhusu wanyama,bali binadamu.

Kitabu hicho kilibeba kejeli iliyohusu harakati za zama hizo za wanamapinduzi ili kutafuta haki na usawa.

Hadithi ilimhusu Joseph Stalin na harakati za mapinduzi Urusi ya zamani(USSR).

Mwisho wa hekaya yake tumegundua kwamba, kumbe harakati za kujenga jamii isiyo na matabaka, zitashindwa vibaya, ikiwa wanaoendesha harakati hizo ni watu maarufu sana (Public Figures) kama tulio nao siku hizi katika siasa za Tanzania.

Hawa ni wabinafsi,wanaotumia mabega ya wanyonge kujineemesha tu.

Nchini mwetu ni kama akina Profesa Ibrahim Lipumba, Freeman Mbowe, Tundu Lissu, Zito Kabwe, James Mbatia, Abdulrahman Kinana na wenzao wote ndani ya CCM, ACT- Wazalendo na Ukawa.

Katika siasa za Tanzania, pia kuna viongozi wa wanyama, “Akina Nguruwe” walioongoza Mapinduzi katika kisa hiki cha Shamba la wanyama wa Orwell, aliyeitwa mwanzoni mwa maisha yake, Eric Blair.

Viongozi wa wanyama yaani nguruwe, walijua kusoma na kuandika na walikuwa na uwezo wa kuwaunganisha ‘wanyama’ wenzao-hawa walikuwa wasomi(intellectuals) kama Profesa Lipumba,Tundu Lisu, Dk.Slaa, Mbowe, Zitto, orodha ni ndefu.

Kada ya mwisho ni sisi Watanzania wa kawaida, hasa wakulima vijijini na wafanyakazi wa kada ya chini wanaopinda mgongo kuiletea nchi maendeleo yasiyoonekana kwa urahisi-yanaliwa.

Hata JPM wa CCM naunga mkono ajenda yetu kusema, “Wanyonge tumekuwa tukiliwa”.

Mapinduzi ya wanyama yalifanikiwa kwa kuyasema mabaya ya binadamu beberu, aliyetaka kufanyiwa kila jambo na wanyama kazi hawa, yeye akafaidika na kula mema ya nchi kwa njia haramu ya rushwa na ufisadi.

Hili nalo JPM kathibitisha, wafanyakazi hewa, wanafunzi hewa, makandarasi hewa, kila kitu hewa-hewa tu!

Hatua iliyofuata ilikuwa kumfukuza ‘Binadamu’ asiendelee kumiliki Shamba la wanyama, kunywa maziwa, kula asali na mema yote ya Shamba la Wanyama(nchi) bila kuzalisha chochote!

‘Binadamu’ hawa waliotawala Shamba la wanyama walikuwa dhaifu, hawakuweza hata kukokota jembe, binadamu wasingeweza hata kukamuliwa maziwa, hawakuweza kuzalisha chochote, isipokuwa ng’ombe na punda, ngamia na farasi walipofanya kazi za harubu,binadamu walineemeka na kushiba!

Waliishi mithili ya peponi.JPM alisema wanaishi mithili ya malaika.

Badala ya wanyama kunufaika na kazi zao, binadamu fisadi alihakikisha wanyama kama ng’ombe hawamiliki kitu hochote, isipokuwa ngozi zao tu-tena walichinjwa siku walipozeeka na kudhoofu.

Masikini punda na mbwa, walipoonekana wamechoka, walifungwa kamba na kupelekwa porini ili wakafe kwa njaa!

Kwa kifupi, mapinduzi yalikuwa kumfukuza binadamu asiendelee kuwanyonya wanyama walioota kujenga jamii yenye usawa na upendo, ambayo ingekuja kufaidi matunda ya uhuru wao.

Jamii hii ya wanyama ilitunga ‘Katiba Mpya’ ambayo msingi wake ulikuwa kwamba ‘wanyama wote ni sawa’ hakuna mnyama bora kuliko wenzake.

Wanyama hawa ndugu waliitana, “comrades” wakatunga Amri Kuu saba zilizosema hivi:

  1. Yeyote anayetembea kwa miguu miwili(hasa binadamu)ni adui.
  2. Kila anayetembea kwa miguu minne au mbawa ni rafiki.
  3. Itakuwa haramu mnyama kuvaa nguo
  4. Itakuwa marufuku mnyama kulala kitandani
  5. Itakuwa marufuku mnyama yeyote kunywa pombe
  6. Itakuwa kosa la uhaini mnyama kumuua na kumla mwenzake
  7. Wanyama woote watakuwa sawa sawia.

Katiba hii ilitungwa baada ya utawala wa kiimla wa binadamu kupinduliwa,binadamu wakafukuzwa,ili kupisha utawala wa wanyama na wanyama kwa manufaa ya wanyama (demokrasia).

Binadamu alikuwa ameshindwa kutawala. Ni dhaifu, hazalishi hata lita moja ya maziwa, hatagi hata yai moja, lakini ng’ombe na kuku wanapozalisha mayai na maziwa, hawapewi japo kiduchu; binadamu anafakamia peke yake!

Wanyama, walijikuta hawamiliki chochote walichozalisha kutwa -kucha, isipokuwa walijikuta na ngozi zao tu! Walichinjwa siku binadamu akijisikia.

Hili ndilo chimbuko la Katiba Mpya ya wanyama kusema, binadamu wote ni adui na wanyama wote ni rafiki (tazama Animal Farm ukurasa wa 5, 6 na 14).

Hata hivyo, baada ya binadamu kukimbia Shamba la wanyama (nchi), yaani baada ya mapinduzi ya kumtimua binadamu mamlakani, akina nguruwe (Intellectuals) wakaanza kushika sukani, walisahau amri saba tukufu!

Katiba ikabadilishwa. Mahali Katiba hii iliposema, “Hakuna ruhusa mnyama kumuua mnyama mwenzake,” pakaongezewa maneno na kusomeka hivi, “Hakuna mnyama atakayeruhusiwa kumuua mnyama mwenzake bila sababu”.

Neno hilo, ‘Bila sababu’ liliwekwa ili kuwapa nafasi wanyama watawala kuwafyeka wasaliti walioanza kupinga Katiba ya Kijamaa kubadilishwa ili kutoa upenyo kwa wakubwa kuwaua wapinzani wao.

Wapinzani(wanaopinga ubeberu uwe wa binadamu au wanyama wenzao)waliitwa wasaliti, wakapigwa, wakafukuzwa shambani na kuuawa!

Ilisemwa kwamba, kulikuwa na sababu nzuri za kuwaua wasaliti wa mapinduzi.

Hivyo, wasaliti wenye kidomo-domo,waliuliwa-alifukuzwa Shambani mwa wanyama, waliobaki walikaa kimya.

Viongozi wa wanyama ndiyo akina Nguruwe, wakasigina Katiba, wakafanya kama binadamu alivyofanya na kuzidi, walilewa pombe, walivaa suti safi, walikunywa maziwa na asali, walitembea kwa miguu miwili (kama binadamu).

Walisema hivi:

“Four legs good, but Two legs better”.(Ukurasa wa 80.)

Kwa kifupi, Katiba ilipokanyagwa, uovu ukarejea katika nchi kuzidi kwanza,wanyama wakajutia mapinduzi na kusema, “Kheri utawala wa binadamu katili, kuliko huo wa wanyama wazandiki na waovu sana!”

Mauaji yalikuwa kila mahali kwa kisingizio cha usaliti na uhaini, usawa uliondoka Katiba iliyosema, ‘All animals are equal’ ilibadilishwa kusema, “All animals are equal, but some animals are more equal than others”.

Kufuatia tabia hii, wanyama viongozi waliruhusiwa kulala vitandani, walilewa kama kawaida, walitembea na kuvaa suti, walijigawia ruzuku kwa visingizio vingi walivyojiwekea, walipiga marufuku mwanachama wa kawaida wa shamba kuhoji chochote, asije akaitwa msaliti na kutimuliwa au kuuawa.

Viongozi wa shamba hili walihodhi madaraka yote, hawakuaka tena demokrasia waliyojidai kudai zama za utawala wa binadamu.

Nchi ilijaa machafuko na vita(Ukurasa wa 85 wa kitabu hiki, Animal Farm kilichoandikwa kati ya Novemba 1943 na Februari, 1944.

Ilikuwa kabla ya Tanzania kuwa huru, kabla ya TANU na AFRO Shiraz Party kuwepo, kabla ya CCM na CUF au Chadema kufikiriwa kuzaliwa.