Home Habari Profesa Lipumba atia nyavu Chadema

Profesa Lipumba atia nyavu Chadema

1666
0
SHARE

*Ateta na mbunge wake, Kasulumbayi ajiunga CUF

Na MWANDISHI WETU-DAR ES SAALAM

MWENYEKITI wa Chama cha Wananchi (CUF), Profesa Ibrahim Lipumba, ametega nyavu ndani ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), huku akichukua baadhi ya wanachama wake.

Hatua hiyo inatokana na uamuzi wake wa kuamua kuanza ushawishi kwa baadhi ya wabunge wa Chadema, kutaka wamuunge mkono huku mkakati wake huo ukielezwa kuwa huenda ukafanikiwa kuelekea uchaguzi wa Serikali za Mitaa, Vijiji na Vitongoji unaotarajiwa kufanyika Oktoba pamoja na Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2020.

Uamuzi huo unalenga kuimarisha CUF ambayo kwa sasa inaonekana kupukutika, hasa kwa upande wa Zanzibar, baada ya aliyekuwa Katibu Mkuu, Maalim Seif Sharif Hamad kuhamia Chama cha ACT-Wazalendo huku akiungwa mkono na wafuasi wake.

Mapema wiki iliyopita, Profesa Lipumba alikutana na Mbunge wa Bukoba Mjini, Wilfred Lwakatare (Chadema), ambaye aliwahi pia kuwa Naibu Katibu Mkuu wa CUF Bara kabla ya kukihama chama hicho na kujiunga na Chadema Juni 25, 2009.

Lwakatare ambaye alishika nafasi ya Naibu Katibu Mkuu Bara kwa zaidi ya miaka 10, alitangaza kuondoka CUF baada ya kupata ushauri kutoka kwa ndugu jamaa na marafiki zake.

Katika moja ya kauli zake wakati akijiunga na Chadema, alisema: “Mimi ni Chadema kuanzia saa 1:30 usiku (Juni 23, 2009).”

Akiwa katika ofisi hizo za CUF, Lwakatare alikutana na Profesa Lipumba kwa dakika kadhaa huku kile walichokizungumza kikibaki ndani ya mioyo yao.

Lwakatare pia alikutana na Naibu Katibu Mkuu wa CUF Bara, Magdalena Sakaya pamoja na wanachama waliokuwapo katika ofisi za chama hicho – Buguruni, Dar es Salaam.

Inaelezwa kuwa kwa sasa CUF ipo katika mikakati ya kutafakari namna gani inaweza kujiimarisha, hasa baada ya kundi kubwa la wanachama wake kujiondoa na kumfuata Maalim Seif ndani ya ACT-Wazalendo.

Pamoja na hali hiyo, kwa sasa CUF na Chadema vipo kwenye vita kali ya maneno, huku kila upande ukimtuhumu mwenzake kwamba anavuruga mapambano ya upinzani bila kupatikana ushahidi wa moja kwa moja.

Akizungumza na gazeti dada la MTANZANIA mapema wiki hii, Lwakatare alikiri kuingia kwenye ofisi za CUF huku akidai kwamba alialikwa na aliyekuwa Mbunge wa Micheweni, Zanzibar Shoka Khamis Juma ambaye nyumba yake iko karibu na ofisi hizo.

“Wakati nikiwa CUF, Shoka alikuwa rafiki yangu na hata sasa ni rafiki yangu sana, sasa alinialika kwenye dua nyumbani kwake, akaniomba niende kuitembea familia yake ambapo nyumba yake iko karibu kabisa na ofisi za CUF.

“Kama ulishatembelea CUF, pale kuna mazingira ya wafanyabiashara, kila kitu ni vurugu kwenye ile barabara, kwa hiyo sehemu pekee ya kupaki gari ni sambamba na ofisi za CUF kwa mbele.

“Hivyo rafiki yangu Shoka, alinipokelea pale nje mbele ya ofisi ya CUF, nikaenda kwake tukala biriani na pilau, tulipomaliza sasa wakati ananisindikiza kumbe CUF walikuwa na kongamano pale tangu asubuhi, na nasikia walimpokea na Silvester Kasulumbayi (aliyekuwa Mbunge wa Maswa Mashariki-Chadema ).

“Sasa kumbe wakati sisi tunatoka na wao CUF walikuwa wamemaliza kongamano lao, na watu walikuwa wanatoka kwa wingi kwenye geti lile la CUF, kwa hiyo baadhi yao waliponiona wakasema ‘ooh naibu katibu mkuu wetu wa zamani’.

“Hivyo watu wakapata shauku ya kuja, kwa kweli wakaja kwa hamasa kubwa na ‘spirit’ kubwa ya kutaka kuniona, na miongoni mwa waliokuja ni aliyekuwa katibu wangu msaidizi ambaye sasa ni katibu msaidizi wa Profesa Lipumba.

“Akaja akanikumbatia pale nje ya geti, akaniomba kwamba Profesa Lipumba yuko ndani ofisini, hivyo niende nimsalimie, na wanachama wote waliokuwa wamenizunguka wakasisitiza niende.

“Sasa mimi kwa kawaida yangu sina fitna, majungu wala visasi na sina tatizo lolote, ndiyo nikaridhia, tukaingia ndani ya geti wakawa wanaimba nyimbo za CUF, wao wakabaki chini nikapanda juu ofisini kwa Profesa (Lipumba) na aliponiona akafurahi sana akainuka, akanisalimia na bahati nzuri alikuwa anaendelea na kikao, na wabunge na baadhi ya viongozi wengine wa CUF wote wakapata hamasa ya kunisalimia ‘karibu bwana ofisi yako ya zamani’.

“Na mimi nikawaambia mwenda kwao sio mtumwa, nikawaambia nashukuruni kwa upendo wenu, na ilikuwa saa 12 jioni, nilitumia kama dakika 10 pale,” alisema Lwakatare.

Alisema hana mpango wowote wa kujiunga na chama hicho na kwamba yeye ni mwanachama wa Chadema na mbunge.

“Mimi nina chama change, ni mbunge. Hivi kweli inalipa mimi muda kama huu niwe na ndoto au njozi ya namna hiyo, niweke tu wazi kwamba mimi ni muumini wa siasa za kistaarabu, sipendi siasa za kutekana, kutukanana, kuumizana, ndivyo nilivyo na ndivyo ninavyoasalimiana na watu wa CCM na ACT-Wazalendo,” alisema.

Alisema kuna wakati alizushiwa kuwa anajiunga na CCM, lakini jibu alilolitoa kwa watu waliomuhoji ni kuwa siku zote matendo ndiyo yanazungumza kuliko maneno.

“Taarifa ile kuwa ningeunga mkono juhudi ikajifia, hata hii najua itajifia yenyewe, nataka tu kuwaambia mimi siasa zangu ni za ‘principle’, niko vizuri ndani ya chama changu ambacho ndicho kilichonipeleka bungeni,” alisema.

Naibu Katibu Mkuu wa CUF Bara, Magdalena Sakaya alisema kuwa Lwakatare alipita na kusalimia na wala hajajiunga na chama chao.

“Hata tulipojaribu kumshawishi ili arudi CUF, alisema aachwe kwa sasa ana chama chake ambacho ni Chadema,” alisema Sakaya.