Home Habari Profesa Mabula: Tumejipanga kutoa elimu SADC

Profesa Mabula: Tumejipanga kutoa elimu SADC

791
0
SHARE

LEONARD MANG’OHA NA FERDNAMBA MBAMILA

PROFESA Audax Mabula ni Mkurugenzi Mkuu wa Makumbusho ya Taifa na mbobezi wa masuala ya sanaa akiwa na Shahada ya Uzamivu katika eneo hilo.

Novemba mwaka 2013 aliteuliwa na Rais Mstaafu, Jakaya Kikwete kushika nafasi hiyo akitokea Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM).

Mapema wiki hii, gazeti hili limefanya mahoajiano na mbobezi huyo wa masuala ya sanaa.

RAI: Taarifa zinaonesha kuwa sekta ya utalii kwa ujumla ndiyo inayoongoza kwa kuingiza fedha nyingi za kigeni, nafasi ya utalii kihistoria au urithi ikoje?

PROFESA MABULA: Utalii wetu wa Tanzania kiasi kikubwa unategemea rasilimali za asili kama wanyamapori, mbuga, milima na hasa Kilimanjaro, tunaongezea fukwe ili kuwe na fukwe nyingi na nzuri, tunazungumzia mambo ya Kreta kwa mfano ile ya Ngorongoro ni Kreta kubwa Afrika nzima.

Lakini pia sasa hivi kuna vivutio vingine vya kiijiolojia ambavyo pia vinawavutia watalii wengi, kwa hiyo utalii wetu mwingi ambao kwa sasa unaingiza pato kubwa la Taifa ni utalii wa maliasili. Lakini nchi hii pia ina utajiri mwingi wa urithi wa utamaduni ambapo umegawanyika katika aina mbili.

Kuna utamaduni wa urithi ambao ni pamoja na masalia ya zamadamu, masalia ya akiolojia kama zama za mawe na zama za chuma za zamani, mambo ya ‘arecheolgy sites’, michoro ya miambani. Huu utalii tuli una miaka milioni 3.6 mpaka takribani miaka 2000 iliyopita.

Lakini tunayo pia aina nyingine ya utamaduni hai, mfano Tanzania ina makabila zaidi ya 120 na makabila hayo kila mmoja lina lugha yake, mila na desturi zake, ngoma na hadithi zake na huu ni utamaduni mwingi.

Tanzania ukiondoa haya makabila lugha kuu za Afrika ni kama nne, sisi tuna bahati kwamba lugha hizi zote nne zipo Tanzania. Kwa mfano kuna hawa Nairotiki, inaongelewa na Wamasai na Watatoga, kuna Bantu wanaongea makabila mengi Tanzania, kuna Kushitick inaongelewa kwa hapa Tanzania na wa Irakwi, lakini kuna lugha ya San au Wahadzabe na Wasandawe.

Hakuna nchi nyingine Afrika yenye makabila makuu manne isipokuwa Tanzania kwa hiyo unaweza kuona kwamba huu urithi wa utamaduni tuli na hai ni utajiri mkubwa, ndio maana Wizara ya Maliasili na Utalii imeona hili na inataka ifanye mageuzi ya kuuzalisha uwe zao la utalii. Huu urithi wetu tunaweza tukauboresha ukawa mazao yanayovutia watalii kuingia nchini.

Wizara inafanya mabadiliko katika huu urithi wa utamaduni tuli au malikale sasa hivi unaboreshwa na taasisi mbalimbali kama Tanapa, Ngorongoro, NCA, Tawa, Makumbusho ya Taifa, TFS ili vivutio hivi viwe zao la utalii.

Lakini wizara pia imeanzisha tamasha la urithi festival celebrate our heritage, lengo ni kubadilisha utamaduni hai kuwa vivutio vya utalii.

Lile tamasha linakua kwa mwezi mzima, linasheherekewa na Watanzania wote na wana-promote vyakula vya kitanzania, mavazi ya kitanzania lakini pia ku-promote biashara za wajasiriamali ambao wanatengeneza vitu na zana kwa ajili ya kuuza.

Lengo kubwa ni kwamba ukifanya hivi watalii watakuja kuangalia maliasili, lakini pia watakuwa na nafasi ya kuangalia huu utalii wa utamaduni.

Kwa hiyo tutawafanya watalii wakae kwa muda mrefu ndani ya nchi na kadiri wanavyokaa ndivyo wanavyotumia fedha. Kutakuwa na ongezeko kubwa la pato la Taifa kutokana na utalii lakini pia utalii huu wa utamaduni utawafanya watalii kupata hamu ya kwenda na kurudi.

Kwa mfano nikikwambia urithi wa maliasili za wanyama ukimuona simba Serengeti ni simba yule yule utamwona Mikumi, Kenya, Botswana na sehemu zingine.

Lakini ukiona utamaduni wa kuchezea nyoka wa Wasukuma wanaojua kumchezea nyoka ni kwamba ni hao hao, kwa hiyo utakuwa na hamu ya kurudi kwa sababu utakuwa na hamu ya kuona ngoma ya watu wa Songea kwa sababu haichezwi mahali pengine popote, utakuwa na hamu ya kuona ngoma ya Wagogo na nyimbo zao kwa hiyo mtalii atakwenda na kurudi mara kadhaa.

Serikali ya awamu ya tano imeona fursa iliyopo katika utalii wa utamaduni, mfano nchi ya Misri haina wanyama, haina milima lakini vivutio vyake vikubwa ni vitu vilivyotengenezwa kama pyramid na ina uchumi mzuri inaingiza fedha nyingi. Sisi tukiunganisha hivyo viwili tutakuwa na fursa kubwa ya kukuza utalii.

RAI: Mmejipanga vipi kuweza kujipenyeza katika mkutano wa SADC ili kuwezesha wageni na wazawa kufahamu mambo muhimu yaliyopo katika eneo hili la utalii wa urithi?

PROFESA MABULA: Tutakuwa na onesho litakalohusu mchango wa Watanzania katika kupigania uhuru katika nchi za Kusini mwa Afrika na lengo letu ni kutoa elimu na kuonesha members (wajumbe) wa SADC jinsi Tanzania ilivyoweza kujitoa muhanga, siyo tu kiitelijensia. Tulijitoa kijeshi, ujuzi wa kijeshi, vifaa vya kijeshi lakini wapo askari wetu walikufa.

Kwa hiyo watu wa SADC wajue mchango wa Tanzania sio kujitoa tu kupigana, kupiganisha na kuongoza lakini pia Tanzania ilikuwa makazi ya wapigania uhuru, walikuja wakakaa hapa shughuli zote zilianzia hapa. Kwa hiyo tunawakumbusha kwawapa elimu waone umuhimu na mchango wa Watanzania.

Hata hapa Makumbusho tumejipanga tutakuwa na ugeni siweze kuutaja sasa ila tutakuwa na ugeni mkubwa wa viongozi kutoka nchi za SADC, siwezi kusema ni kina nani lakini sisi tumejipanga kupokea ugeni wa kitaifa na Taifa linajua makumbusho inahifadhi urithi wa kitamaduni na urithi kwa ajili ya kizazi hiki na kijacho.

Lakini pia urithi wa Bara la Afrika na ni urithi wa dunia nzima. Kwa hiyo wakija tutawaambia na tutawaonesha kuwa Tanzania ndiyo chimbuko la binadamu.

RAI: Ni ujumbe gani ambao mmepanga kuufikisha kwa washiriki wa mkutano huu ambao kwa kiasi kikubwa umelenga kukuza maendeleo ya viwanda katika jumuiya?

PROFESA MABULA: Dhima nzima ya SADC ni mambo ya viwanda. Sisi tunaona viwanda vimeanza miaka milioni 2.6, wakati watu walipoanza kutengeneza hizi zana za mawe, hicho ni kiwanda tumekuja nazo watu walikuwa wanatengeneza chuma miaka 2000 iliyopita.

Tulikuwa na chuma kizuri sana hata wakoloni walipokuja walikuta watu wanatengeneza bunduki, chuma, mishale na mikuki vyote hivyo vilikuwa ni viwanda.

Kwa hiyo ujumbe wangu tunapoingia kwenye hii dhana ya viwanda sisi Makumbusho ya Taifa ya Tanzania tunayo nafasi kubwa, tutawaonyesha wageni na wajumbe wengine kwamba Tanzania imekuwa na mchango mkubwa katika dhana na falsafa ya viwanda, wakija wataona viwanda ambavyo vilikuwapo na wataona dhana  za viwanda hivyo.

Lakini pia wakija makumbusho ya Taifa watajifunza juu ya chimbuko lao na wote wataamini Tanzania imekuwa na mchango mkubwa na sio ajabu wote tumetoka Tanzania.

RAI: Ni kundi gani la watu hupendelea aina hii ya utalii na hutembelea vivutio hivi kwa sababu zipi kulingana na taarifa mnazozikusanya?

PROFESA MABULA: Makumbusho duniani kote ni taasisi na kwa sisi ni taasisi ya kiserikali, hatutengenezi faida lakini ni tasisi ya kisayansi na kiutamaduni na kazi zetu kuu  ni kutafiti na kuelimisha watu, kuonesha na kuhifadhi huu urithi, taifa lina utamaduni wake sasa unahifadhiwa hapa Makumbusho ya Taifa. 

Wewe unaweza ukawa hujaona kuna hayo mafuvu lakini hata tunaposema muungano, chimbuko la muungano lipo hapa ule mchanga na udongo ambao mwalimu aliuchanganya, vile vibuyu. kile chungu vipo hapa vimehifadhiwa na vinatunzwa.

Sasa ni mahali pa kupata elimu kutokana na maonyesho lakini pia ni mahali pa kupata elimu kwa wanafunzi wanaokuja kujifunza kufanya ‘project’, ni mahali pa kupata taarifa kwa watafiti wanaokuja kufanya utafiti.

Pamoja na hiyo elimu ni mahali pa kuburudika, unapokuja kuna maonesho lakini pia unapata burudani, kuna magari ya kihstoria, ni burudani ya kutosha, unaona magari ya Mwalimu (Julius Nyerere) aliyokuwa anayatumia wakati wa kampeni za uhuru, gari ambalo wakati mwalimu anakuwa Rais wa Tanganyika na baadaye Tanzania alilokuwa anatembelea, hiyo ni burudani.

Kwa hiyo tuna wageni wa aina nyingi wapo kutoka Ulaya, Amerika na wapo kutoka Asia, lakini pia wapo watalii kutoka Bara la Afrika nchi jirani na nchi kama hizo za SADC. Watalii wa ndani wamegawanyika kuna wanafunzi wanaokuja ambao ni wengi wanafunzi wengi wanapenda kuja makumbusho kujifunza na kuburudika .

Watalii wa ndani watu wazima wanakuja lakini si wengi ukilinganisha na wanafunzi lakini hili ni mtazamo watu waelewe kwamba makumbusho ukienda unakwenda na watoto, familia, unakwenda kuelimika na kuburidika ni tofauti na kwenda bar.

Ukienda bar unakwenda baba peke yako ni mara chache, wanakwenda na mama au mama naye anakwenda peke yake. Lakini bar si mahali pa kwenda kujifunza na ukapata ile burudani na familia.

Hata beach sikatai kwamba watu wasiende beach lakini nako siyo mahali pazuri sana pa kujifunza, utapata burudani lakini kujifunza hakupo lakini sio mazingira mazuri ya kulea watoto na mabinti wadogo katika mila na desturi za kitanzania. Lakini makumbusho zote wewe ukija upo free.

RAI: Ni aina gani vivutio vya urithi wa utamaduni huwavutia watu wengi?

PROFESA MABULA: Binadamu tuna tabia ya kudadisi, katika kila kabila au jamii wanadadisi chimbuko lao ni wapi, hiyo ipo kila mahali. Kwa hiyo chimbuko au asili yetu tumetoka wapi na tumefikaje hapa tulipo kuna hizo simulizi na historia za kimila, vitabu vya neno la Mungu, lakini pia kuna sayansi.

Sasa sisi makumbusho tuko kwenye ile sayansi, tunaongelea sayansi na chimbuko la binadamu limemgusa kila mtu, kwa hiyo litamvutia kila mmoja. Ndiyo maeneo kama ya Bonde la Olduvai ambako masalia ya Zamadamu yamepatikana miaka milioni mili0NI 1.8, 1.5 na kuendelea.

Lakini na zana za mawe zingine tunazo hapa tunazionesha na mafuvu tunayo hapa. Zana za mawe ambazo walianza kutengeneza watu miaka milioni mbili iliyopita, sasa hivi teknolojia unarekodi kwa simu lakini chimbuko lake ni pale walipoanza hawa kugonga mawe na kutengeneza zana. Sasa nani hapendi kujua hilo.

Mwandishi unapenda kula nyama ya ng’ombe, mbuzi, kuku chimbuko la sisi kula nyama lilianza lini na wapi, kumbe walipoanza kutengeneza zana ndipo hapo wakaanza kuchuna wale wanayama.

Lakini wapo wanaopenda kujua historia, uhusiano wetu na nchi za nje ulianza lini, biashara karne ya 12, 13,  nane na tisa, masalia ya Kilwa Kisiwani karne hizo za nane na tisa ulikuwa mji mkubwa Afrika. Wazungu wanakuja wanaona ni mji mkubwa, hadi ulianza kutengeneza sarafu, nenda hata Kaole uone yale masalia na kuna visima pale visivyo kauka maji na iko imani kwamba ukiyatumia yale maji sijui unakuwa namna gani.

Nenda Kondoa Irangi uone ile michoro ya miambani ni mizuri na huwa tunafikiri ‘is the begining of human imagination’ watu wakaanza kufikiria miaka 40,000. Hiyo michoro picha zile ukiziona utastaajabu ni kama umbile la mtu, tena mzuri. Ni nani hapendi kuona vitu hivyo?

Watanzania watapenda kutembelea majengo ya kihistiria mengine yapo hapa dare s salaam kila mtu anapenda kuyaona.

RAI: Kutokana na umuhimu wa aina hii ya utalii unatoa wito gani kwa jamii hususan vijana katika kuuendeleza urithi huu?

PROFESA MABULA: Mwalimu Nyerere alishasema taifa lisilo na utamaduni ni taifa ambalo limekufa, ni mkusanyiko tu wa watu lakini hawana ile roho inayowafanya wawe taifa. Urithi wa utamaduni ndiyo unaotupa ile identity (alama) ya kuwa sisi ndiyo Watanzania.

Urithi wa utamaduni unaleta umoja kwa kuonesha kwamba tuna historia na urithi huo wa utamaduni ni kwa ajili ya kizazi hiki na kijacho unatakiwa uhifadhiwe, uenziwe, utunzwe lakini urithishwe.

Kwa hiyo kizazi cha vijana ni lazima kithamini urithi wao, ndiyo unayofanya  wawe taifa, ndiyo unaokufanya uwe  mtu.

Ukiulizwa mahali unasema mimi ni Mtanzania, utanzania una historia, Watanzania wana maadili ya Tanzania, wanao utamaduni wao wa kitanzania, wana lugha yao. Kwa hiyo ombi na rai yangu kwa vijana ni kuuthamini kuutambua, kuuhifadhi na kuurithisha kwa kizazi kijacho.

RAI: NI maeneo gani ya urithi wa utamaduni mnayoyaona yanapotea katika jamii aidha kwa kujua ama kwa kutofahamu lakini yanaweza kutumika kama njia ya kukuza utalii huu nchini?

PROFESA MABULA: Maeneo ya urithi wa kiutamaduni na kihistoria yapo nchi nzima. Urithi huu mwingine upo ardhini, watu wa kale wapo maeneo tofauti tofauti na kila wakati unagunduliwa.

Kwa hiyo yapo maeneo mengine ambayo hayajawa promoted vizuri , hayajagunduliwa vizuri, hayajawekewa maelezo vizuri, lakini tunajua juu ya Olduvai lakini yapo maeneo kule Ziwa Eyasi.

Inapofikia suala la chimbuko letu sisi binadamu yapo maeneo yalipotolewa masalia ya binadamu kama sisi miaka 130,000 iliyopita lakini hata Iringa yapo miaka 190,000 iliyopita. Yapo maeneo mengine yana michoro ya miamba, maeneo ya kihistoria. Hata hapa Dar es Salaam yapo mengi.

Kwa mfano Mbwa Maji kule Kigamboni, Kunduchi, watu wengi hawajui, kabla mji haujawa mkubwa kilikuwa ni kijiji cha wavuvi, hapo ilipo Ocean Road ilikuwa ndio Mzizima. Kwa hiyo yapo masalia pale na hata masalia ya watu wa kale walizikwa, historia hii ipo kila mahali ndiyo maana nafikiri siyo kwa vijana tu  hata sisi watu wazima vijijini kule  tuyaenzi haya maeneo .

Yako maeneo ya machifu mbalimbali wayaenzi kwa sababu ni kivutio cha utalii, tumekuwa tukishirikiana na chifu mmoja Semike atakuwa na onesho lake hivi karibuni kule Mwanza ni eneo lililokuwa limetelekezwa lakini amekuja tumeshauriana ameliboresha kuwa kivutio cha utalii.

Ujumbe kwa Watanzania ni kuthamini, kujali na kutunza huu urithi wao wa kiutamaduni na kuhakikisha tunarithisha kwa kizazi kijacho. Pia lazima kuthamini na kujali hizi taasisi zinazohifadhi huu utamaduni, ni taasisi nyeti.

Makumbusho katika mataifa mengine ni taasisi muhimu, lakini hata hapa Tanzania sasa Serikali inaona umuhimu wa taasisi hizi ndiyo maana viongozi wakija lazima waletwe Makumbusho ya Taifa. Sasa kama wanakuja hao viongozi wa nje kwanini sisi tusithamini hata viongozi wa kwetu wakienda huko nje wanakwenda kuona makumbusho za nchi hizo.

Makumbusho ni sehemu pekee ambayo unaweza ukaijua nchi husika, historia yao, utamaduni wao, uchumi wao na siasa yao kwa muda mfupi na kwa pesa kidogo. Akija hapa kwa saa moja au mbili kwa kiingilio cha Sh 1500 kwa mwenyeji na mgeni 6,500 utajua mambo ya Tanzania na uchumi wake na jiografia ya nchi, madini yake, watu na makabila mbalimbali kiasi kwamba angetaka atembelee maeneo haya  ingemchukua muda mrefu na gharama kubwa.

Kwa mfano pale kijiji cha makumbusho tunaonyesha nyumba za kiutamaduni za makabila mbalimbali, kwa kushirikiana na Wakala wa Majengo (TBA) tumefanya land use , tumelipima lile eneo, tuna ekari kama 11, tumelikata vipande viwili, eneo moja tumeamua nyumba zetu tuzijenge kwa ramani ya Tanzania na mwaka jana tumeanza kujenga nyumba za watu wa Lindi.

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa alizindua na wakati wa tamasha la watu wa Lindi nyumba zao mbili nyumba za watu wa pwani na watu wasio wa pwani. Nyumba zao zipo tofauti lakini hata vitu wanavyotumia mle ndani ni tofauti, tutaweka Ziwa Viktoria, huku Ziwa Nyasa, Ziwa Tanganyika na bahari.

Mle tutafuga samaki alafu tutaweka barabara kwa sababu ni eneo kubwa tutaweka bajaji watu wanapokuja wanatembea.

Watu wa kabila fulani wanaruhusiwa kuja kujenga nyumba yao, tutawapa eneo watajenga nyumba, kutokana na ujuzi wao wanaojuwa nyumba hizo zinajengwaje. Kwa mfano ya wasukuma inakuwa ya aina gani ili watu watunze utamaduni wao.

Lakini kuna eneo jingine tumeweka kwa ajili ya kituo cha biashara, wale wasanii wachonga vinyago na wachoraji wa Mwenge na wengine ambao hawana mahali rasmi pa kufanyia kazi zao waje pale. Kwa mbele tutajenga mahali pa kuuzia na kwa nyuma tutajenga workshop (karakana) ili mtalii aone process mpaka mwisho anaona fainal product anaamua kununua.