Home Habari RAHA NA KARAHA SIKU SITA ZA MAGUFULI ARUSHA

RAHA NA KARAHA SIKU SITA ZA MAGUFULI ARUSHA

981
0
SHARE

Na ABRAHAM GWANDU, ARUSHA

RAIS John Magufuli wiki iliyopita  alifanya ziara ya kikazi ya siku sita mkoani Arusha kuanzia Septemba 20 hadi 25 mwaka huu ambapo pamoja na mambo mengine alifungua rasmi barabara iliyojengwa kwa kiwango cha lami kuanzia Kia hadi Mji mdogo wa Mirerani.

Wakati wa hafla ya ufunguzi wa barabara hii ya Kia Mirerani, Rais Magufuli alitumia fursa hiyo kuzungumzia madini ya Tanzanite, suala la ukosefu wa maji safi na ya uhakika katika eneo hilo lenye  utajiri mkubwa lakini hata hivyo wakazi wake wakiishi kwa dhiki isiyoelezeka.

Habari njema kwa wakazi wa eneo hilo na Wilaya nzima ya Simanjiro, kiongozi huyo aliwaahidi kutatatua kero hiyo ya maji kwa kuyavuta kutoka eneo la Boma Ng’ombe wilayani Hai bila shaka kutoka chanzo kinachotoka Mlima Mrefu kuliko yote Afrika, Mlima Kilimanjaro.

Jambo lingine lililopokewa kwa hisia mchanganyiko na wachimbaji, wanunuzi, madalali na wananchi wa kawaida ni uamuzi aliotoa Rais Magufuli wa kujenga ukuta kuzunguka eneo la migodi ya Tanzanite kuanzia kitalu A mpaka D.

Wengi wanajiuliza baada ya ukuta kujengwa nini kitafuata? Ni kweli lengo ni kuzuia wizi wa madini hayo? Je sio kwamba ukuta ukikamilika wachimbaji wadogo wataswagwa nje kwa nguvu? Wapo wanaoeneza uvumi kuwa eneo hilo watakabidhiwa jeshi ili kwa kushirikiana na Shirika la madini la taifa (STAMICO) pamoja na baadhi ya wachimbaji wakubwa waliendeleze kwa kile kinachosemwa sasa kwamba wachimbaji wadogo hawalipi kodi.

Baadhi yao wanadai leseni za uchimbaji zitapitiwa upya ili kurekebisha kasoro zilizopo ili kila mchimbaji, wanunuzi na madalali wabanwe ipasavyo kwa kulipa kodi zinazostahili.

Katikati ya mtanziko huo, tayari  Jeshi la Wananchi wa Tanzania kama ilivyo kawaida yao ya kuongozwa na utii na nidhamu limeshafanya ukaguzi na upembuzi bila shaka yakinifu ili kujua ukubwa na uzito wa jukumu walilopewa na Amiri Jeshi Mkuu kujenga ukuta (Tanzanite great wall).

Pia alitunuku kamisheni ya cheo cha luteni usu  maafisa wanafunzi 422 wa Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ ) kundi la 61 wa Chuo cha Kijeshi cha Monduli, Shule ya Mabaharia na Shule ya Anga.

Kinyume na mazoea ya shughuli hizi za kijeshi kufanyika kambini eneo la Chuo cha Kijeshi Monduli, mara hii ilifanyika katika Uwanja wa Michezo wa kumbukumbu ya Sheikh Amri Abeid Kaluta katikati ya Jiji la Arusha.

Mimi sio mtaalamu wa maswala ya Kijeshi, sifahamu chochote kuhusu ulinzi na usalama lakini uelewa wangu tu wa kawaida wa kutambua mambo mtambuka naweza kusema pasipo shaka kuwa siasa iliharibu kazi nzuri aliyofanya Rais kwa siku zote sita za kuwa hapa Arusha.

Mbali na siasa, ujio wa Rais hapa Arusha uliambatana na kero, usumbufu, amri na hata adhabu kwa baadhi ya wananchi wa Jiji la Arusha na viunga vyake. Wananchi wasiojua lolote kuhusu itifaki na ulinzi wa Rais.

Siku moja kabla ya Jumamosi hiyo ya tarehe 23 Septemba, Mitaa na  barabara kadhaa zinazoelekea au zilizo mkabala na Uwanja wa Michezo wa Sheikh Amri Abeid zilifungwa, watu walikatazwa kupanda juu ya majengo marefu kuelekea uwanja huo, waliovuka mstari ‘uliochorwa’ walikumbana na adhabu za kijeshi na hata kipigo .

Jiji hili lenye barabara chache likakumbwa na msongamano na misururu ya watu na magari. Wagonjwa ilibidi wasubiri kupisha shughuli hiyo, wafanyakazi ilibidi kuchelewa kazini na haijulikani walipokewa vipi na waajiri wao. Wafanyabiashara ambao maeneo yao yalifungwa hawajaeleza bado hasara waliyopata na nani wa kufidia.

Na kama inavyofahamika Arusha ni kijiwe cha maneno, wapo wanaosema uwanja ulijazwa na watu ambao haikuwa hiari yao. Eti wafanyakazi wa viwanda karibu vyote waliamriwa kupitia wamiliki wao kwenda kumsikiliza Rais. Watumishi wa serikali nao halikadhalika uwanja ukajaa pomoni, ndio lazima wafike kumsikiliza mwajiri wao mkuu, wanakosaje kwa mfano!

Tukiacha hayo ya uwanjani, pia kila alipopita Rais, wananchi walijitokeza barabarani na ‘kuzuia’ msafara wake. Naye bila ajizi kwa upendo mkubwa alionao alijitokeza kuwasabahi wananchi wake na kuwaeleza namna anavyojitahidi kuwatumikia.

Ratiba yake awali tulitangaziwa kuwa angezuru pia Wilayani Longido kwenda kuweka jiwe la msingi katika mradi mkubwa wa maji wenye gharama ya bilioni 16 mradi ambao utawezesha makao makuu ya Wilaya hiyo kuwa na maji ya uhakika kutoka chanzo kilichopo Mlima Kilimanjaro ukianzia Siha.

Huko Dk. Magufuli hakwenda, badala yake aliwakilishwa na Waziri Mkuu wa Tanzania Majaliwa Kasimu. Kama ilivyo ada ziara ya kiongozi wa ngazi ya kitaifa anapozuru mahali basi msafara wake huambatana na viongozi wengine wengi.

Walikuwepo Mawaziri, Makatibu Wakuu wa Wizara, Mkuu wa Mkoa, Mkuu wa Wilaya na baadhi ya Wabunge hususan wa CCM. Panapokuwa na mchanyato wa namna hiyo ni aghalabu sana siasa kutofanyika hata kama jambo lenyewe halihusiani na siasa za moja kwa moja.

Longido kwa muda sasa haina mwakilishi wa wananchi katika chombo chao cha kutunga sheria yaani Bunge. Sina haja kueleza kwanini, kila moja anafahamu kilichotokea. Kinachosubiriwa ni Tume ya Taifa ya Uchaguzi kutangaza tarehe ya uchaguzi wa mdogo kujaza ombwe lililopo.

Lakini hata kabla NEC kutangaza tarehe ya uchaguzi, wana CCM tayari walishaanza kupiga jaramba. Ukiwauliza mbona mmeanza kampeni kabla hamwoni kuwa mnajiandalia pingamizi? Jibu lao rahisi na fupi! Nalo ni “serikali yao”! Mungu ibariki Tanzania.