Home Makala Rai kwa viongozi wa dini katika mapambano dhidi ya corona

Rai kwa viongozi wa dini katika mapambano dhidi ya corona

1398
0
SHARE

NA FREDERICK FUSSI 

VIONGOZI wa dini wana dhamana kubwa katika mapambano mbalimbali ikiwemo milipuko ya magonjwa kama ilivyo kwa wa ugonjwa wa homa ya mapafu unaosababishwa na virusi vya corona. 

Hapa nchini viongozi wa dini wamepewa deni la kuaminiwa kwamba kupitia maombi na maombezi bila shaka Taifa litaondokana na janga la corona ambalo limeziathiri nchi zote duniani. 

Rais Dk. John Magufuli alitoa rai kwa viongozi wa dini kupambana na virusi vya corona kwa kufuata maelekezo ya watalaamu wa afya lakini pia kwa kufanya dua na maombi, akanukuu vitabu vitakatifu ikiwemo Quran Tukufu na Biblia Takatifu. 

Itakumbukwa kuwa katika nchi ya Korea ya Kusini, nyumba ya ibada ndio ilikuwa kitovu cha kusambaza virusi vya corona nchini humo. Kanisa la Shincheonji Church of Jesus katika mji wa Daegu, Korea Kusini ndio ilikuwa kitovu cha virusi vya corona kusambaa kwa katika nchi hiyo.  

Sababu ya virusi kusambaa kwa kasi kutokea katika kanisa hilo ni kwa sababu kanisa ni chombo cha kijamii kinachokusanya watu wengi kwa mara moja, wakati huo huo ugonjwa wa corona tabia yake ni kusambaa kwenye mikusanyiko mikubwa ya watu. 

Rais Dk. John Magufuli

Wakati maombi ni suala la Kitheolojia ugonjwa wa corona ni suala la kibaiolojia. Kwa hiyo mapambano yoyote ya Kitheolojia ili yawe na nguvu katika masuala ya kibailojia lazima, thiolojia iende kwenye uwanja wa kibailojia. 

Nitafafanua namaanisha nini. Jamii ya Wakristo wote ulimwenguni imesherehekea sikukuu ya Pasaka Aprili 12 mwaka huu, ikiwa ni kuadhimisha tukio la kihistoria la kuleta ukombozi kwa mwanadamu dhidi ya shetani kwa kufa na kufufuka kwa Yesu , ambaye katika jamii ya Wakristo anaaminika kuwa ni Mungu katika utatu mtakatifu wa Mungu Baba, Mungu Mwana na Mungu Roho Mtakatifu. 

Biblia inafundisha kuwa Yesu ni Mungu na yupo katika ulimwengu wa roho huko mbinguni kusikoonekana kwa macho ya damu na nyama. Lakini ili kuleta ukombozi ulimwenguni ambao ndio ulimwengu wa Kitheolojia ilimlazimu Yesu kutoka kwenye ulimwengu usioonekana kwa damu na nyama huko mbinguni na kuja kuleta ukombozi kwenye ulimwengu wa mwili unaoonekana ambao ni ulimwengu wa kibailojia ndio sababu akafa, akazikwa na siku ya tatu akafufuka kutoka katika wafu, akamnyang’anya shetani funguo za mauti na kuzimu ili kila anayemuamini Yesu apate uzima wa milele. Ndio maana ya sikukuu ya Pasaka. 

Kwa hiyo kama Yesu ambaye jamii ya Wakristo wanaamini kuwa ni Mungu aliuacha ulimwengu wa Theolojia huko mbinguni akaja katika ulimwengu wa Kibailojia huku duniani, hivyo hivyo viongozi wa dini wanapaswa kubaini kuwa adui coronavirus wanayeshindana naye Kitheolojia amehama kwenye ulimwengu wa Kitheolojia na sasa anafanya kazi katika ulimwengu wa kibailojia. Ili kumshinda ni lazima kupambana naye katika ulimwengu wa kibailojia huku ukitumia mbinu zinazofundishwa na wanatheolojia.

Mbinu zilizobainishwa na wataalamu wa kibailojia katika mapambno dhidi ya coronavirus, ni pamoja na kunawa mikono kwa maji safi na salama, kujitenga kijamii (social distancing) ikiwemo ile mbinu ya kukaa nyumbani (staying at home), kukaa mita moja kutoka mtu mmoja na mtu mwingine na kujikinga kwa kitambaa cha barakoa (mask) ni mbinu ambazo zinasaidia kuzuia hatari ya virusi kusambaa kwa kasi.  

Mbinu zote hizo zinasaidia kupunguza kasi ya maambukizi na mbinu hizo pamoja na kuwa zinapunguza kasi pia ni mbinu zinazoweza kutumika Kitheolojia kuchochea kupungua na kuisha kabisa kwa ugonjwa huo. Nitafafanua namaanisha nini. 

Mbinu ya kujitenga na jamii au (social distancing) ambayo ni mbinu ya kibailojia inaweza pia kutumika kitheolojia na viongozi wa dini Tanzania wanaweza kuitumia na ikazaa matunda ya kupunguza kasi ya maambukizi na hatimaye kumshinda adui coronavirus, ambaye kwa asili yake haonekani kwa macho mpaka akuzwe kupitia vifaa vya kukuzia vijidudu vidogo yaani “microscope”.  Najua kuwa viongozi wa dini hapa nchini bado wanaendelea kukusanyika katika nyumba za ibada ili kutii agizo la Kitabu cha Biblia katika Waebrania 10:24 ambapo mtume Paulo, alikuwa anaelekeza watu Waebrania katika waraka wake kwao akisema “wala tusiache kukusanyika pamoja, kama ilivyo desturi ya wengine; bali tuonyane; na kuzidi kufanya hivyo, kwa kadiri mwonavyo siku ile kuwa inakaribia.” 

Sasa, desturi ya wengine leo duniani katika mapambano dhidi ya coronavirus ni kuacha kukusanyika na kubakia nyumbani. Yesu ambaye jamii ya Wakristo wanamwamini yeye alitoa maelekezo ya watu kubakia nyumbani (Staying at home) na kumwomba Mungu kwa dua na sala ukiwa katika chumba chako cha ndani. Chumba cha ndani katika mapambano haya ya coronavirus hakipatikani kwenye mikusanyiko ya watu. 

Katika kitabu cha Mathayo sura ya sita na mstari wa Sita (Mathayo 6:6), Yesu anapowaelekeza wanafunzi wake jinsi ya kusali aliwaambia hivi, “Bali wewe usalipo, ingia katika chumba chako cha ndani, na ukiisha kufunga mlango wako, usali mbele za Baba yako aliye sirini; na Baba yako aonaye sirini atakujazi” 

Kule Kanisa la Shincheonji Church of Jesus katika mji wa Daegu, Korea Kusini kama wangekumbuka kuwahimiza waumini wao kuzingatia maelekezo ya Yesu kuwa wasikusanyike ili kuzuia maambukizi kusambaa na wabakie nyumbani ili kumwomba Mungu baba katika vyumba vyao vya ndani, basi nchini Korea maambukizi ya virusi vya corona yasingekuwa mengi na yasingesambaa kutokea kanisani. Lakini kwa sababu ya viongozi wa dini wa Korea Kusini kukosa maarifa watu wengi katika kanisa lile walifariki kwa sababu ya kutokuwa tu na maarifa kuwa adui coronavirus amehama kutoka ulimwengu wa Kitheolojia na amehamia katika ulimwengu wa Kibailojia. 

Kwa hiyo viongozi wa kidini hapa nchini ambao bado wanakusanya maelfu ya watu katika nyumba zao za ibada wajifunze kwa mfano huu wa Kanisa la Shincheonji Church of Jesus. Pia wazingatie kuwa Kitabu cha Hosea 4:6 kinasema bayana kuwa “watu wangu wanaangamizwa kwa kukosa maarifa;…” 

Natoa Rai kwenu viongozi wa dini kuwa wapeni watu wa Mungu maarifa ili wasiangamie na virusi vya corona, kwani kubakia nyumbani na kusali na kuombea nyumbani katika vyumba vya ndani ni agizo la Yesu ambaye jamii ya wanaowafuata wanamuamini. 

Pale inaoonekana kubaki nyumbani inashindikana na ni lazima kukusanyika basi igeni mfano wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambalo limeorodhesha majina ya wabunge wachache tu wanaoruhusiwa kuingia kwenye Ukumbi wa Bunge ili kutimiza masharti ya kibailojia ya kukaa angalau mita moja kutoka mtu mmoja mpaka mwingine. Msikusanye watu, orodhesheni majina ili kudhibiti mikusanyiko ya watu wawe wachache ili kuzuia virusi visisambae kwa kasi. 

Huwezi tu ukasali kumwomba Mungu kitheolojia kuwa aondoe virusi vya corona ambavyo vipo kibailojia kisha ukaendelea kupuuza masharti ya kanuni za kibailojia na kuacha watu wagusane katika mikusanyiko mikubwa. 

Kwa sababu si kusudi la Mungu watu wa Kanisa la Shincheonji Church of Jesus waangamie kwa virusi. Na pia sio kusudio la Mungu kuwa watu wanaoenda makanisani hapa Tanzania waangamie. 

Nitamalizia na nukuu ya Stanley McChristal, ambaye ni Kamanda mstaafu wa Jeshi la Marekani katika Vikosi vya Usalama vya Kimataifa vilivyokuwa nchini Afghanistan, alipokuwa akihojiwa na Kituo cha Habari cha CNN nchini Marekani katika vita dhidi ya ugonjwa wa corona, alisema kuwa “Endapo unataka kushinda vita, unatakiwa kumchambua adui yako na kumshinda kwa undani zaidi” (if you want to win a war you need to break your enemy and defeat him in detail”. Nitoe Rai kwa viongozi wa dini, wanapokuwa wanatoa maelekezo kwa waumini wao jinsi ya kusali katika vyumba vyao vya ndani, hawana budi kumchambua adui coronavirus ili wanaposali kwa Mungu iwe rahisi kumshinda kwa undani zaidi. 

Katika uchambuzi wa kibiblia nilioufanya nimebaini kuwa adui coronavirus ni mnyama anayezuka kutoka baharini kama ambayo Mtume Yohana alimwona katika maono yake alipokuwa katika kisiwa cha Patmos, ambacho leo kipo katika mwambao wa magharibi wa nchi ya Uturuki katika bara la Asia. 

Mtume Paulo katika maono yake aliyoandika katika Kitabu cha Ufunuo kuanzia sura ya Kumi na tatu na mstari wa kwanza na kuendelea, (Ufunuo 13:1-18), Mstari wa kwanza unapoanza ndipo anapomtaja mnyama anayezuka kutoka baharini. “Kisha nikaona mnyama akitoka katika bahari, mwenye pembe kumi na vichwa saba na juu ya pembe zake ana vilemba kumi na juu ya vichwa vyake majina ya makufuru.” 

Ukisoma tafasiri ya lugha ya Kingereza unabaini kuwa kile anachokiita Mtume Paulo kuwa ni vilemba kumi, tafsiri yake ni Taji za Kifalme yaani “royal crowns”. Tafsiri ya kingereza ya International Standard Version (ISV) inasema kuwa “I saw a beast coming out of the sea. It had ten horns, seven heads, and ten royal crowns on its horns. On its heads were blasphemous names.” Wakati tafsiri ya King James Version (KJV) inasema: “And I stood upon the sand of the sea and saw a beast rise up out of the sea, having seven heads and ten horns, and upon his horns ten crowns, and upon his heads the name of blasphemy.” 

Sasa virusi vya corona au COVID-19, vimepewa jina la corona, kwa sababu neno corona ni la Kigiriki linalomaanisha “Crown” au kwa Kiswahili Taji ya Kifalme. Virusi vya corona vikitazamwa kwenye vifaa vya kukuzuia vijidudu vidogo yaani “microscope” vinaonekana vimevalishwa taji za kifamle yaani “crowns” hii ndio sababu vinaitwa kwa kigiriki coronavirus yaani virusi vilivyovikwa taji ya Kifalme. Niliposoma Mtandao wa Shirika la Afya la John Hopkins unaotoa takwimu za hali ya corona duniani, nimemnukuu mtaalamu wa Shirika hilo la Afya Bibi Lisa Maragakis,( M.D., M.P.H, ), ambaye ni Mkurugenzi wa Kuzuia Magonjwa ya Maambukizi wa shirika hilo, alisema kuwa: “familia nzima ya virusi vya Corona, imepewa jina Corona kwa sababu neno Corona maana yake ni taji ya Kifalme, hii inamaanisha kuwa virusi hivi vinamwonekano wa kuvikwa taji ya kifalme vinapochunguzwa kupitia vifaa vya kukuzia vijidudu vidogo yaani microscope.” Ukipenda kujua undani wa uchambuzi wangu, niandikie barua pepe au nitumie ujumbe mfupi wa maandishi.