Home Afrika Mashariki RAILA ‘ANATAKA’SERIKALI YA MSETO

RAILA ‘ANATAKA’SERIKALI YA MSETO

3101
0
SHARE

NA MWANDISHI WETU

MGOMBEA  wa urais wa Kenya kwa kupitia  muungano wa NASA, Raila Odinga anadaiwa kupanga karata zake za kisiasa ili kugomea marudio ya uchaguzi ili kutimiza lengo la kurejesha Serikali ya mseto.

Madai haya yanakuja kutokana na mashariti kadhaa yaliyotolewa na Raila katika kipindi ambacho nchi hiyo inaelekea kwenye uchaguzi wa marudio.

Mashariti hayo yanatajwa kuibua harufu ya mgogoro mkubwa wa kikatiba kutokana na kukosekana kwa dalili za maridhiano kati ya Raila na Rais wa nchi hiyo, Uhuru Kenyatta.

Mahakama ya Juu ya nchi hiyo iliagiza kurudiwa kwa uchaguzi baada ya kugundua dosari kubwa kutokana na ukiukwaji wa kanuni na sheria katika uendeshaji wa uchaguzi mwezi uliopita.

Mapema wiki hii Naibu Rais wa Kenya William Ruto alidai kwamba viongozi wa NASA walikuwa wanawachochea Wakenya kufanya vurugu na hata umwagaji damu kwa lengo la kutengeneza mazingira ya kufanya majadiliano ya kuwepo kwa kipindi cha mpito na hivyo kusimika serikali ya pamoja.

Katika mkutano wake wa kampeni katika County ya Nandi, Ruto alisema mgombea huyo wa NASA yuko huru kujiondoa kwenye kinyang’anyiro ili awaruhusu Wakenya wengine wamchague rais wao bila ya kutaka kulazimisha mambo.

Alisema Raila amekuwa anasimika kihunzi baada ya kihunzi kwa kuwa anafahamu hatashinda.

Pande zote mbili – NASA na Jubilee zimekuwa zikishikilia misimamo yao bila kuyumba. Kuanzia mapema wiki hii Raila Odinga aliitisha mandamano makubwa akitaka Tume ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) ifumuliwe kabla ya uchaguzi wa marudio uliopangwa kufanyika Oktoba 26 mwaka huu.

Raila anasema chama chake hakitakubali kushiriki uchaguzi endapo utasimamiwa na tume hii ambayo Mahakama ya Juu ilisema ilivurunda uchaguzi wa awali.

Kwa upande wake chama cha Jubilee kinapinga mabadiliko yoyote kwenye Tume hiyo kikisema upigaji kura lazima ufanyike chini ya watendaji hao hao wa Tume.

Wanasheria mashuhuri wa masuala ya katiba wanaonekana kutofautiana kuhusu kitu gani kitatokea iwapo uchaguzi wa marudio hautafanyika katika kipindi cha siku 60 hadi Novemba 1.

Kama ilivyoanishwa Kikatiba, ambapo wapo  baadhi yao wanasema Mahakama ya Juu haina mamlaka ya kuongeza muda huo.

Viongozi na wanasheria wa chama tawala cha Jubilee wanasema kama hakutafanyika uchaguzi wa marudio, Rais Uhuru Kenyatta ataendelea kukaa madarakani hadi 2022 na huenda hata ikawa ni halali kwake kugombea tena urais katika uchaguzi wa mwaka huo.

Lakini wenzao wa upinzani wameyajibu hayo kwa kusema ni ndoto tu za mchana na kuonya kwamba kutaibuka mgogoro mkubwa wa kikatiba iwapo uchaguzi wa marudio hautafanyika.

Mwenyekiti wa Chama cha Wanaseria Kenya (KLS), Isaac Okero ametoa wito wa utulivu kutoka pande zote mbili.

Alisema iwapo kutazuka hali ya kisiasa au matukio ambayo hayakuwa yanatarajiwa na Katiba, basi hali hiyo ndiyo kisheria huainishwa kuwa mgogoro wa kikatiba. Na ndivyo itakavyokuwa iwapo uchaguzi wa marudio hautafanyika katika kipindi cha siku 60.

Aliongeza kwa kusema kwamba vipengele vya Katiba lazima viongoze wakati wote na si wakati ambapo uongozi wa nchi au wananchi wanaweza tu kuchagua wakati gani wa kufikiria Katiba ndiyo muhimu kuliko vitu vingine.

Mwanasheria Faith Waigwa ambaye alikuwa mwenyekiti wa Kamati ya maamuzi wa chama cha Jubilee wakati wa mchakato wa uteuzi aliliambia gazeti la The Star wiki iliyopita kwamba Kenyatta anaweza kuendelea kukaa madarakani hadi 2022 iwapo uchaguzi wa marudio hautafanyika.

Alisema Kipengele Na 143 cha Katiba kinaruhusu hata hivyo haamini iwapo hili litajiri.

Alisema kama litatokea, hauwezi kuitwa muhula wake wa pili kwa sababu muhula wake wa kwanza haukumalizika kwa sababu hakukuwepo kwa uchaguzi.

Uchaguzi wa marudio unazidi kuweka wingu kwenye muonekano wa uchumi ambao hata hivyo ulikuwa unapungua na unahatarisha sifa ya nchi kuwa ya matarajio makubwa kwa wawekezaji katika Bara la Afrika.

Migogoro kadha iliyopita wakati wa uchaguzi ilikuwa inaibua ghasia hasa zile za baada ya uchaguzi wa mwaka 2007 ambao ulisababisha vifo vya watu zaidi ya 1000 na zaidi ya 350,000 wengine kuyakimbia makazi yao.