Home Makala RAIS ANAIKANA ILANI YA CCM KUHUSU KATIBA?

RAIS ANAIKANA ILANI YA CCM KUHUSU KATIBA?

835
0
SHARE

NA MARKUS MPANGALA,

NOVEMBA mwaka jana, Rais John Magufuli, alifanya mahojiano na wahariri wa vyombo vya habari mbalimbali pale Ikulu, jijini Dar es salaam  na kusema ana mkakati wa kuinyoosha nchi kwanza, badala ya kushughulikia suala la Katiba mpya.

Yalikuwa mahojiano ya kwanza akiwa mkuu wa nchi, ambapo pamoja na mambo mengine, alisistiza juu ya kuhakikisha anashughulikia matatizo makubwa ya msingi ya nchi, lakini siyo suala la kukamilisha mchakato wa Katiba mpya.

Uamuzi wa Rais unatokana na kile alichosema kuwa nchi yetu inakabiliwa na matatizo mengi mazito, hivyo suala la Katiba halikuwa kipaumbele chake.

Wakati wa kampeni za uchaguzi mwaka 2015, miongoni mwa mambo yaliyozungumzwa zaidi au tuseme sera iliyokuwa imevutia wapigakura, ilikuwa suala la kuandikwa kwa Katiba mpya.

Ilifahamika kuwa Katiba mpya ilifikia kiwango cha kukamilishwa na Bunge la Katiba, hivyo kilichobaki ilikuwa ni kuipigia kura za maoni Katiba Pendekezwa.

Wataalamu wa masuala ya Katiba, wameeleza bayana juu ya upungufu yaliyomo kwenye Katiba iliyopendekezwa. Wamebainisha masuala mbali mbali ambayo yanatakiwa kufanyiwa marekebisho kabla au wakati wa mchakato wa kura za maoni.

Licha ya kauli ya Rais Magufuli kubainisha kuwa Katiba sio kipaumbele chake, bado upo umuhimu wa kiongozi wetu kukumbushwa juu ya ulazima na umuhimu wa Katiba kwa manufaa ya nchi yetu.

Tunaweza kumkumbusha kwa kupitia Ilani ya Chama cha Mapinduzi (CCM), kwa miaka mitano (2015-2016) ambayo inataka kuendelezwa mchakato wa Katiba mpya.

Ilani hii ilitungwa na CCM wenyewe kwa madhumuni ya kuomba kura kwa wananchi. Baadaye ikamkbidhi mgombea wake John Magufuli, ambaye alishinda kiti cha urais.

Mosi, hiyo ilikuwa na maana kuwa Magufuli anaagizwa na chama chake cha CCM kusisimamia mchakato wa Katiba mpya bila kujali marekebisho.

Jambo la pili, Katiba iliyopendekezwa inalalamikiwa na makundi mbali mbali kwa madai kuwa ina upungufu unaotakiwa kufanyiwa kazi.

Yapo maeneo kama ya uteuzi unaofanywa na mkuu wa nchi ambayo yangelibaki mikononi mwa mwaziri. Mathalani, hadi leo Katiba inayopendekezwa, imeliacha suala la wakurugenzi wa mikoa mikononi mwa Rais. Suala la makatibu wa wilaya na mikoa, limo mikononi mwa Rais.

Ni matumaini yangu kuwa itafika mahali tutaliona suala hili muhimu mno la kumwachia Rais majukumu mazito ya nchi. Ingelifaa zaidi wakurugenzi wa wilaya wangekuwa wanaomba kazi kama nafasi zingine.

Kwamba nafasi ya ukurugenzi wa wilaya, manispaa au jiji, ingelifaa kuwa ya wataalamu wa maendeleo, mipango miji, utawala na kadhalika. Nafasi hizi zingelikuwa zinatangazwa kama ajira, ili kuongeza ufanisi na uhuru wa mamlaka.

Uhuru wa mamlaka kwa maana ya kuhakikisha waombaji hao, wanafanya kazi kulingana na weledi. Hatutarajii kuwa na wakurugenzi ambao wanaomba kazi lakini wakivurunda wanahamishiwa vituo vingine vya kazi.

Aidha, nafasi kama makatibu wa wilaya na mikoa, ingelifaa wawe waombaji wa nafasi hizo badala ya kuteuliwa. Dhumuni kubwa  la kutaka nafasi hizo ziwe za kutangazwa, ili kuongeza ushindani na ufanisi miongoni mwa watendaji wa Kitanzania.

Tumeshuhudia idadi kubwa ya wateule,  ambao wamekuwa na nasaba na Chama cha Mapinduzi (CCM). Ninafahamu kuwa wanakuwa na vigezo vinavyotakiwa. Nafahamu kuwa wana CCM siyo tatizo ikiwa wanatimiza majukumu yao kwa ufasaha. Lakini manung’uniko ni namna ya utendaji wao wa kazi. Kumeibuka dhana kuwa wao wanatakiwa kukitumikia Chama cha Mapinduzi kwanza, kisha Watanzania na mambo mengine ya utumishi baadaye.

Tumeona wateule wengi ni makada wa CCM. Jambo hilo pekee limechangia kuibuka kwa lawama na kuwa kikwazo cha ajira kwa baadhi ya Watanzania.

Ninaamini Katiba iliyopendekezwa, ingelifaa kuweka msingi wa ajira kama hizo—kwamba  watumishi wawe wanaomba kazi badala ya kuteuliwa.

Tunafahamu kuwa taratibu zingine zinasema ni muhimu sana kuwapandisha vyeo watumishi wa umma kujaza nafasi hizo kwa kuangalia   uzoefu wao. Hatua hii ingekuwa kichocheo katika kufanya kazi kwa uwadilifu na bidii. Kila mwajiriwa anapenda kufanya vizuri ili mwajiri ampandishe cheo (promotion). Hii  ingesaidia sana kuibua changamoto ya ufanisi.

Aidha, jambo jingine ambalo linaweza kupunguza mzigo wa madaraka kwa Rais, ni kuhakikisha watumishi wote, wanakuwa chini ya Wizara ya Serikali za Mitaa, kuliko kuwekwa mikononi mwa Rais.

Ndiyo kusema utekelezaji wa Ilani ya CCM, ni pamoja na kuhakikisha marekebisho ya Katiba iliyopendekezwa yanafanyika kwa ufasaha. Pia ni muhimu kwa Serikali ya awamu ya tano, kutumia fursa ya mabadiliko ya Katiba kama moja ya faida kwao mbele ya wananchi.

Aghalabu tumekuwa tukisema kuwa mabadiliko ya kikatiba hayakusudii kupoka madaraka ya yeyote, badala yake yanajenga msingi wa kuimarisha madaraka pamoja na kuhakikisha mwenye madaraka hayo, anasimamia kwa ufanisi, pamoja na kuchukua hatua stahiki kwayo.

Nchi yetu imejipatia tuzo ya kuharakisha mambo muhimu, likiwemo suala la Katiba. Tumeahirisha mara nyingi. Tumemezea mara nyingi mapungufu yaliyopo kwenye utawala wan chi yetu. Lakini bado tumejikuta ni watu wa kulalamikia mambo mbali mbali.

Kama sheria inasema mtu aliyehujumu nchi kwa kiasi cha shilingi bilioni 3, alipe faini ya milioni 10, kisha tukajiona tumefanikiwa, bila shaka tutakuwa mabingwa wa ujuha.

Mabadiliko ya kisheria yanatakiwa kufanywa maeneo mengi. Kwa hiyo, tuna pakuanzia—Katiba mpya (marekebisho ya katiba iliyopendekezwa yanahitajika).

Kwahiyo Ilani ya CCM inaweza kuwa mwongozo mzuri wa kumkumbusha Rais kuwa atimize ahadi yake kama alivyowaahidi wapigakura—kwamba atahakikisha kuwa Katiba mpya inapatikana.

Baruapepe; mawazoni15@gmail.com