Home Makala Rais asaidiwe, akosolewe kwa hoja zenye mashiko

Rais asaidiwe, akosolewe kwa hoja zenye mashiko

1297
0
SHARE

dk.magufuliNa Dk. Vera F Mugittu, Scotland

KIMSINGI tukubaliane kuwa Rais John Magufuli ndiye kiongozi anayestahili kwa nchi yetu ilipofika. Hakuna haja ya kupoteze muda kwa kumpunguzia nguvu ili ashindwe ama kumpa mapenzi ya ‘mama kuchelea mwana kulia’… vinginevyo tutalia wenyewe..

Huyu ndiye Rais tuliyekuwa tunamtafuta na kumsubiri kwa muda mrefu, tusikengeuke tena kwani muda hautusubiri. Ifahamike kwamba Rais huyu akifeli, wote tumefeli, nieleze wazi kwamba Watanzania tujue tulichonacho kabla hatujakikosa.

Ili tufanikiwe yapo mambo muhimu tunapaswa kuyapa kipaumbele kama taifa; Mosi; Tufahamu kuwa Rais Magufuli ndiye aina ya kiongozi tunayemhitaji kwa sasa kwasababu ana dhamira ya dhati ya kuleta maendeleo, uthubutu wake, chuki yake dhahiri dhidi ya ubadhirifu wa fedha za umma, na uadui wa dhati dhidi ya ufisadi si rahisi kuvipata ndani ya kiongozi mmoja katika Bara la Afrika kwa sasa. Nasihi tusilichukulie hili kwa wepesi, na pengine kuruhusu unafiki na maslahi binafsi kuughubika ukweli huu.Tuamue kuumba mtazamo huu chanya kwani kufanya hivi ni faida zaidi kuliko vinginevyo.

Pili: Rais Magufuli si malaika na si Mungu. Hivyo hawezi kutenda, kutimiza wala kuenenda kwa kadiri inavyotakiwa kwa asilimia 100. Lazima atapelea na kupungukiwa. Hivyo apewe fursa ya kutenda anayoweza, huku akiungwa mkono na kukosolewa kwa hoja za msingi na si kebehi.

Avumiliwe na kusaidiwa bila kuchoka. Kikubwa asaidiwe kutambua kuwa yeye hajui kila kitu, na washauri wake wasimpotoshe wala kumsusia. Pia asihukumiwe kwa kushindwa wala asiachwe kujiamini kupita kiasi.

Yeye ni rais wetu, ambaye akifeli sote tumefeli pia. Kamwe chuki isiruhusiwe kukaa katika mioyo yetu dhidi yake…. Na isitumike wakati wa kurekebisha na kushauri. Chuki ina madhara makubwa kuliko tunavyofikiri. Ni kansa kwa taifa.

Naomba tusimchukie Rais wetu hata kwa siri… Kwani chuki ya kimya kimya dhidi ya kiongozi mkuu wa nchi inadhuru ‘mwili na nafsi ya taifa”…na taifa likiumwa ndani kwa ndani, hakuna atakayesalimika.

Tatu: Tukubali bila unafiki kuwa, Rais Magufuli anakidhi mahitaji yetu ya kiungozi ya sasa kwa zaidi ya asilimia 70. Hivyo tumshukuru Mungu kwa hili na tuhakikishe hazungukwi na hisia za chuki, husda, wala utashi wa kumsubiri ashindwe! Kwa wale wasiompenda…. naomba niwakumbushe kuwa hakuna faida yoyote kumpunguzia nguvu na utashi wa kumsubiri na kumtegea akosee ili mseme “Tuliwaambia!’…

Itafaa nini kupoteza miaka mitano au kumi kwa kusubiri ashindwe? Hiyo ni fedheha kwa taifa na vizazi vijavyo, ni bora kuutumia muda huu kuhakikisha anafaulu. Tutoe ushauri usio na chuki wala dhamira mbaya moyoni.

Kukosoa hata kuwe kuchungu namna gani, kuna faida kubwa mradi tu dhamira moyoni isiwe na chuki na ushabiki wa kigomvi. Na kwa wale wanaompenda, watambue kuwa kufumbia macho makosa yake na kumtetea hata kwenye makosa bayana hakutatusaidia chochote.

Ni sawa na mzazi kufumbia macho makosa ya mwanaye, na kuishia kulia mwenyewe, namaanisha kwamba Rais asipewe utukufu wa kishabiki,asipewe mapenzi ya mama anaechelea mwana kulia.

Bali apewe upendo wa kweli wa mzazi mwenye busara, ikibidi tukubali aongozwe kwa “gongo na fimbo” lenye nia njema. Hapa nasisitiza, ‘Dhamira iwe safi’.

Nne: Tutambue kuwa, ulichonacho tayari unacho, kazi ni kukipata kile ambacho unakihitaji. Pia msafiri huhesabu umbali uliobaki kuikamilisha safari, na si kupoteza muda kujisifia umbali aliokwisha kuumaliza.

Tuwekeze kuangalia alikopungukiwa Rais ili kukamilisha mahitaji yetu ya kufikia dira na matamanio yetu ya kimaendeleo, tufanye hivyo kwa dhamira safi.

Kama tayari Rais ni fundi mwashi mzuri, basi tuelekeze nguvu zetu kupata mafundi bomba na umeme, n.k. Si kushinda tunasifia jinsi alivyo mjenzi mzuri na kisha nyumba nzuri ikakosa maji na umeme.

Tusherehekee kiasi mazuri yake, na kuwekeza zaidi kutambua na kufidia kule anakopwaya. Huo ndiyo uzalendo, ikumbukwe kwamba tuko vitani hivyo tutasifiana vita ikiisha si wakati tukiwa mstari wa mbele vitani..

Tano: Kwa wale wanaomtuhumu kuwa dikteta na mvuruga demokrasia, ningewaomba wasome historia ya nchi zote zilizoendelea. Ukweli ni kuwa demokrasia ni matokeo ya maendeleo:… na si chachu ya maendeleo… Hakuna nchi iliyoendelea kwa kuheshimu mambo haya matatu kwa pamoja, yaani “ikaheshimu demokrasia’, ‘ikatii mfumo wa soko huria’, na hapo hapo ‘isivunje haki za binadamu’.

Hakuna! Kuleta maendeleo ya kweli kunahusisha kipindi cha mpito cha kukubali kizazi kimoja kipite kwenye maumivu aidha ya kivita au ya kiuchumi.

Hata nchi yetu kupata uhuru, kuna kizazi kiliteseka na hata kupoteza maisha. Historia inaonyesha mchango mkubwa wa Vita Kuu ya Dunia kwenye maendeleo ya nchi za Ulaya na Marekani.

Vipindi vya udikteta vinaonyesha kuleta mageuzi makubwa na ya kudumu kwenye nchi kama Korea ya Kusini, Singapore, Japan, China na hata Rwanda.

Kuna ushahidi kuwa wakati wa kukuza uchumi, ili kutoka kwenye ngazi moja ya kimaendeleo kwenda nyingine taifa linapita kwenye vita vya kiuchumi. Na kwenye vita hakuna demokrasia… Kuna dhamira ya kushinda, uthubutu, kujituma, kusikiliza intelijensia ya vita na kutii amri.

Tusibebe falsafa zilizokuja baada ya ushindi wa vita vya kiuchumi tukadhani zote zitatufaa kila wakati bali tutambue kuwa nchi tunazoziiga zilifanya mageuzi ya viwanda na kilimo ambayo wananchi wala hawakushirikishwa! Tukubali kuna kuumia na kuharibu ili kutengeneza.

Cha msingi dhamira iwe safi! Tukubali kupita kwenye kipindi kigumu cha mpito… kiuchumi na pengine kupoteza baadhi ya raha na starehe… au kufanya kazi ngumu kupita kiasi. Wananchi wa China wamefanya kazi ngumu sana ili kuliwezesha taifa lao kupata nguvu ya kiuchumi ya sasa, haikuwa kazi rahisi kulikwamua Taifa la China toka kwenye lindi la umasikini.

Sita: Tusipepese macho, tusilale usingizi, wala tusibweteke tukisubiri Rais afanye kila kitu. Tunapokuwa safarini, dereva akisifiwa kupita kiasi-anaweza kuvimba kichwa na kusababisha ajali; pia abiria wakinyamaza kimya kupita kiasi – dereva anaweza kusinzia au kuendesha bila nidhamu kwasababu haonywi na hivyo kusababisha ajali.

Hali kadhalika dereva akipigiwa kelele sana na abiria, kelele zenye hasira na kutukanwa, anaweza kuhamaki na kukasirika, au pengine kuingia woga na hivyo kusababisha ajali. Hapa nawasihi wananchi tufuatilie kila kitu ambacho Rais wetu anakifanya kwa upendo wa dhati.

Tujishughulishe naye kwa kutumia ukweli na dhamira safi… Tutoe hoja tunazoziamini kwa malengo sahihi. Bila kufanya hivi, miaka itapita, na siku ya uchaguzi itarejea tena, huku tukiwa hakuna tuliloambulia.

Saba: Kuna hoja kuwa Rais hashauriki… ingawa sijui ukweli wa hili lakini tusilipuuze moja kwa moja, kama ni kweli, je inawezekana ni namna anavyoshauriwa?… Hebu tusikubali yeye mtu mmoja atushinde watu milioni. 42.

Lazima ipo njia nzuri itakayomgusa maana yeye ni binadamu na ana nia nzuri na taifa hili, lengo letu liwe moja tu… kufaulu kama Taifa. Sidhani kama tuna jinsi nyingine. Lazima tufaulu!

Mungu ibariki Tanzania na watu wake.