Home Latest News Rais Biden atashinda ‘madudu’ ya Trump?

Rais Biden atashinda ‘madudu’ ya Trump?

2057
0
SHARE

NA MWANDISHI WETU

PIGO kwa Donald Trump ni kupoteza muhula wake wa pili, huku shangwe zikielekea kwa aliyekuwa mpinzani wake mkubwa katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka huu, Joe Biden.

Biden mwenye umri wa miaka 78 anakuwa rais mzee zaidi katika historia ya siasa za Marekani, rekodi ambayo ilikuwa inashikiliwa na Trump (74).

Inafahamika kuwa Biden anakiwakilisha Chama cha Democrat na anakuwa rais wa 46 wa Marekani na ataapishwa kuanza rasmi majukumu yake Januari 20, mwakani.

Tofauti na wengine wanavyoweza kufikiria, Trump aliyeingia madarakani mwaka 2016 hajaondoshwa Ikulu na mpinzani mwepesi.

Alikuwa anawania kiti cha urais na Biden ambaye anafahamika kwa utendaji kazi wake akiwa Makamu wa Rais chini ya utawala wa Barack Obama (2009 – 2017).

Ushindi wake wa kura milioni 75, idadi kubwa zaidi kuwahi kumpitisha rais katika historia ya Marekani, umemfanya Trump na washirika wake waendelee kupaza sauti ya kutotambua matokeo.

Hata hivyo, unaweza kuwa ushindi wa kuibua kila aina ya furaha kwa kambi ya Biden lakini unaokwenda sambamba na mtihani mzito alionao kiongozi huyo katika kuijenga Marekani aliyoachiwa na mtangulizi wake, Trump.

JANGA LA CORONA

Kwa Marekani, kama zilivyo nchi za Ulaya,  ugonjwa wa Corona bado ni pasua kichwa na hicho kinakwenda kuwa kibarua kizito kwa Biden katika majukumu yake mapya ndani ya Ikulu ya Marekani.

Mtangulizi wake, Trump, alikumbana na ukosolewaji mkubwa kwa kile alichotajwa kupuuzia namna ya kukabiliana na ugonjwa huo, ikiwamo kutoupa umuhimu utaratibu wa kuvaa barakoa.

Kwa miezi nane sasa, sehemu kubwa ya majimbo ya Marekani yako hoi kutokana na athari za Corona.

Kufikia Alhamisi ya wiki iliyopita, tayari idadi ya maambukizi mapya ilishafikia 121,888 na watu zaidi ya 231,000 wameshapoteza maisha.

Kwa kipindi chote cha kampeni zake, Biden aliwaahidi Wamarekani kuwa ana nguvu ya kutosha ya kukabiliana na janga hilo.

Moja kati ya mikakati aliyosema ingesaidia ni kuwasiliana na magavana wa majimbo na kuona wanavyoweza kutambulisha kanuni mpya za kulazimisha watu kuvaa barakoa.

Aidha, Biden alisema ataanzisha mpango wa taifa wa kupanua zoezi la upimaji kwa wananchi.

Katika hilo, alisema ataongeza idadi ya wataalamu ili wafikie 100,000, na pia atahakikisha kunakuwapo na vituo 10 kwenye kila jimbo.

Mbali ya hilo, alisema atapigania wananchi wawe na kinga na tiba ya Corona bila malipo endapo itapatikana.

Sasa, akiwa ameshapata ridhaa ya Wamarekani,  Biden amebeba ‘msalaba’  wa kuwaonesha wananchi namna ya kuondosha Corona katika mitaa yao.

HALI YA UCHUMI

Ukiachilia mbali hilo la Corona, Biden ana kibarua kingine mbele ya uchumi wa Marekani uliotibuliwa na janga hilo lililoanza mwanzoni mwa mwaka huu.

Wakati wa kampeni zake mwezi uliopita, alisema endapo angechagulia, angeanza kushughulika na mikakati ya kufufua uchumi wa kila jimbo.

“Nitafika kwa gavana wa kila jimbo, meya na viongozi wengine wa chini ili kujua sapoti wanayotaka na kiasi cha fedha wanachohitaji,” alisema Biden.

Katika hotuba yake hiyo ya Oktoba, mwaka huu, alisema italipa Bunge kipindi cha mwezi mmoja tu liwe limefikisha mswada wa namna ya kuirejesha Marekani katika hali yake nzuri ya kiuchumi.

Juu ya Corona ilivyoharibu uchumi, zaidi ya watu milioni 20 wamejikuta wakipoteza ajira zao katiaka maeneo mbalimbali, ikiwamo viwandani.

Maeneo mengi yameshuhudia ofisi (kampuni, viwanda, migahawa n.k) ikiwa imefungwa, hivyo kuzidi kuuweka kwenye hali tete uchumi wa taifa hilo kubwa duniani.

Lakini, Biden hakuweka wazi mipango itakayotumika kuimarisha uchumi, bali aliishia kusema:

“Tutatoa fedha zitakazopitishwa na Bunge ili ziende na kuwawezesha watu waendeele na biashara zao.”

Katika hatua nyingine ya kunusuru uchumi wa Marekani, Biden aliahidi neema kwa waliopoteza ajira zao kutokana na janga la Corona, akisema kuna mkakati wa kuwarejeshea vyanzo vyao vya mapato.

UBAGUZI WA RANGI

Takwimu zinaonesha njia ya Ikulu kwa Biden ilisafishwa na idadi kubwa ya kura za watu weusi wanaoishi nchini humo.

Ukweli wa madai hayo ni kwamba sehemu kubwa ya kura za ushindi alijikusanyia katika majimbo ya Philadelphia, Detroit, Milwaukee na Atlanta, ambayo yana idadi kuwa ya jamii hiyo yenye asili ya Afrika.

Kwa miaka ya hivi karibuni, hasa kwa sehemu kubwa ya utawala wa Trump, taswira ya Marekani ilionekana kuchafuliwa na vitendo vya ubaguzi wa rangi.

Uzuri ni kwamba Biden anakiri kuwapo kwa tatizo la ubaguzi kati ya watu weusi na wazungu na ameahidi kulifanyia kazi.

Mauaji ya watu weusi yamekuwa yakishamiri kila iitwayo leo, ikitosha kumtolea mfano kijana George Floyd, ambaye aliuawa na polisi wa kizungu na kusababisha maandamano makubwa nchini Marekani.

Katika mikutano yake ya kampeni,  mara kadhaa Biden alitumia kaulimbiu ‘Black lives matter’, ambayo ilitumiwa kulaani mateso wanayopitia watu weusi katika ardhi ya taifa hilo.

Ahadi kubwa ya Biden katika kukomesha utemi wa ngozi nyeupe ni kuwawezesha kiuchumi watu weusi kwa kuzipa fedha biashara zao.

Kutekeleza hilo, aliahidi mbele ya wapiga kura wake kwamba Serikali atakayoiongoza itatenga kiasi cha Dola za Marekani bilioni  30.

UHUSIANO WA KIMATAIFA

Chini ya utawala wa miaka minne ya Trump, Marekani ilionekana kuwa na sura isiyovutia katika mwenendo wake wa sera za mambo ya nje.

Kwa macho ya wengi, Trump aliifanya Marekani iwe inatembea yenyewe,  huku akiwa hajali kuhusu kuvunja uhusiano wake na mjajirani.

Mathalan, wiki chache kabla ya Uchaguzi Mkuu, Trump alitangaza kuiondosha Marekani katika Shirika la Afya la Umoja wa Mataifa (WHO).

Kwa Biden, walau yamekuwapo matumaini ya Marekani kurudi kundini na kushirikiana an mataifa mengine.

Wakati wa kampeni zake,  aliahidi kufufua uhusiano wa Marekani na washirika wake, hasa NATO, Umoja ambao Trump alitishia kuuondoshea msaada wa kifedha.

Pia, tofauti na Trump, Biden ameonesha msimamo wa wastani mbele ya uhusiano wa Marekani na China, ikitoa taswira kwamba huenda ‘bifu’ la muda mrefu kati ya nchi hizo likafikia ukomo ndani ya utawala wake.

Isisahaulike pia, Biden ameitupia jicho la huruma Iran, nchi ambayo Trump alijitoa katika mazungumzo ya kuiondolea vikwazo vya kiuchumi.