Home Habari Rais Magufuli aivuruga dunia

Rais Magufuli aivuruga dunia

2563
0
SHARE

rainewhabari july.inddNA MWANDISHI WETU

KASI ya utendaji kazi wa Rais John Magufuli imeonekana kuvutia idadi kubwa ya wananchi wa nchi mbalimbali duniani ambao
sasa wanawashinikiza viongozi wao kuiga mwenendo wake kiutendaji.

Wiki tano za Rais Magufuli madarakani, zimesababisha baadhi ya marais na viongozi wa juu wa nchi mbalimbali duniani kunyooshewa kidole na raia wao, ambao hawaridhishwi na mwenendo wa serikali za nchi zao.

Kauli, makala na maoni ya kumsifi a Rais Magufuli na kuwaponda viongozi wa nchi nyingine za Afrika na Ulaya yamekuwa yakimiminika katika mitandao ya kijamii, magazeti maarufu duniani na hata katika mikutano mbalimbali.

Asilimia kubwa ya watoa maoni wanaitumia kasi ya Magufuli kama
mfano unaopaswa kuigwa na viongozi wao, ambao wanaonekana kufumbia macho baadhi ya mambo.

Viongozi wa mataifa
saba duniani, tayari wameshakumbana na kadhia ya wananchi wao kuwataka kujifunza uongozi kutoka kwa Magufuli, ambaye anatekeleza majukumu yake kwa kujiita mtumbua jipu.

Mataifa yaliyokunwa na kasi ya Magufuli ni Kenya, Sweden, Afrika Kusini, Nigeria, Malawi, Australia, Ghana, Uganda na Umoja wa
Ulaya.

ASIFIWA SWEDEN:

Gazeti maarufu la kila siku nchini humo, Dagens Nytheter limeandika habari ya kumsifia Rais Magufuli kutokana na mafanikio aliyoyapata ndani ya muda mfupi tangu apewe
dhamana ya kuiongoza nchi.

Dagens Nytheter ambalo ni gazeti maarufu linalotoka kila siku nchini humo, katika toleo lake la mwishoni mwa wiki iliyopita linataja aina ya utendaji kazi wa Rais Magufuli kuwa umewaweka
katika wakati mgumu marais wenzake wa nchi jirani kwa sababu wananchi wao wameonyesha wivu kwa Watanzania kwa kupata
kiongozi mchapa kazi.

Pia gazeti hilo limetanabaisha kuwa kabla ya kuingia Ikulu, tayari Rais Magufuli alikuwa ameshapata maadui mbalimbali wakiwamo
wa ndani ya chama chake CCM kutokana na msimamo wake wa kubana matumizi ya Serikali.

ZUMA ATAKIWA KUJIFUNZA

Mtandao maarufu wa The South African.com ulichapisha habari iliyobeba kichwa cha habari kuwa Mambo 10 ambayo Rais Jacob Zuma anapaswa kujifunza kutoka kwa Magufuli.

Katika chapisho la habari hiyo lilielezea mambo mbalimbali aliyoyafanya Rais Magufuli huku likimpamba kutokana na utendaji wake.
Taarifa hiyo imeelezea namna Rais Magufuli alivyoanza kupambana na wakwepa kodi, wala rushwa na wazembe serikalini.
Desemba 3, mwaka huu mtandao wa e-NCA ulichapishwa habari
iliyokwenda kwa kichwa kisemacho Rais Magufuli si kiongozi wa Afrika.

Habari hiyo imetanabaisha aina ya utendaji kazi wa Rais Magufuli kuwa haufanani na wa viongozi wengine wa bara hili, ambao wengi wao wameendekeza njaa na rushwa.
Mtandao huo umeeleza kuwa ndani ya kipindi cha mwezi mmoja sasa tangu Rais Magufuli aingie madarakani amekuwa katika mapambano dhidi ya rushwa.

KIONGOZI PAYU AFUTA SHEREHE

Naye rais wa Umoja wa Vijana ya Afrika(Pan Africa Youth Union) , Francine Muyumba alifuta sherehe ya kuadhimisha mwaka mmoja tangu ateuliwe kuwa kiongozi wa umoja huo, akidai anaunga mkono juhudi za Rais Magufuli.

Muyumba ameungana na mamilioni ya watumiaji wa mtandao wa Twitter wenye kumuunga mkono Magufuli uliobeba kauli mbiu
ya “WhatWouldMagufuliDo” ambao unatumika kupambanua utendaji wa Rais Magufuli.

MUTHARIKA AVURUGWA

Mtandao maarufu wa Malawi 24 nao haukubaki nyuma baada ya kuchapisha habari iliyobeba kichwa cha habari kuwa, Wamalawi hawavutiwi tena na Mutharika badala yake wamemgeukia Rais
Magufuli. Katika habari hiyo, imeelezea changamoto mbalimbali anazokumbana nazo Rais wa nchi hiyo, Peter Mutharika na kumshauri kuazima japo mbinu chache kwa Rais Magufuli ili aweze kuwahudumia wananchi hao wa Malawi.

AMTESA WAZIRI MKUU AUSTRALIA

Nyota ya Magufuli pia imezidi kung’aa na kuwavuruga viongozi wa mataifa mengine baada ya Mhariri wa Gazeti la The Courier Mail la Australia, Rowan Dean kumtaka Waziri Mkuu wa nchi hiyo Malcom
Turnbull kumuiga Magufuli.

Bila kumung’unya maneno Mhariri huyo aliufananisha uongozi wa waziri huyo aliyekaa madarakani kwa wiki tatu na uongozi wa Magufuli.
Aliendelea kufafanua kuwa kiongozi wao ameshindwa kuonesha utendaji bora, baada ya kuwa karibu na matajiri hadi akaumbuliwa na Bunge la nchi hiyo kutokana na deni la zaidi ya dola za Marekani bilioni 400.

BUHARI AWEKWA KIKAANGONI

Pia Rais Magufuli amewagusa baadhi ya raia wa Nigeria
na kuvutiwa na utendaji wake, ambapo mhariri wa Gazeti la Mail and Guardian la Afrika kusini, Charles Onyango-Obbo, katika safu
yake aliandika uchambuzi kwenye kichwa cha habari
kuwa, Magufuli si kiongozi wa Afrika, kwa mantiki ya kuwa amekuwa kiongozi asiyekuwa na tabia au hulka kama za
viongozi wengine wa Afrika ambao hudidimiza maendeleo
ya nchi zao kwa kuendekeza rushwa, ulafi , na utendaji hafi fu.

Pia katika jarida la Ventures Africa, nalo lilikuwa na kichwa cha habari kuwa Hivi ndivyo wanigeria wanavyoweza kuiga utekelezaji wa ahadi kutoka kwa Magufuli.

Pamoja na kuzungumzia kauli mbiu ya ‘Hapa kazi tu’, pia jarida hilo lilimwagia sifa Rais Magufuli kwa utendaji wake na kutoa wito kwa Rais Buhari wa nchi hiyo kuiga mfano wa Magufuli.

Balozi wa Tanzania nchini humo, Daniel Ole Njoolay amesema wananchi wa Nigeria wanamtaka Rais wao kuiga kasi ya Magufuli.

EU YAPAGAWISHWA NAE

Mbali na mitandao hiyo ya habari, pia mtazamo wa aina hiyo umeoneshwa kwa Mabalozi wa Umoja wa Ulaya baada ya kukunwa na aina ya utendaji kazi wake hasa kwa kitendo chake cha kuzuia safari za nje pamoja na kuwawajibisha watumishi wazembe kutokana na matumizi mabaya ya fedha za umma na madaraka.

AWA GUMZO GHANA

Magufuli ameibuka gumzo tena nchini Ghana ambapo watu mbalimbali walitoa maoni yao wakidai ni rais wa kipekee katika kizazi cha sasa cha uongozi.

Mwanzilishi na Mwenyekiti wa Taasisi ya 1Billion Africa ambayo inajihuisha na miradi mbalimbali ya kusaidia jamii, uongozi na uandishi wa vitabu, Prince Adu-Appiah alisema “Rais wa Tanzania
John Magufuli amekuwa wa pili kati ya viongozi bora Afrika baada ya Paul Kagame wa Rwanda.

Afrika haihitaji viongozi wa binafsi ili kuimarisha taasisi za urais na uongozi kwa masilahi ya wananchi wake.

KENYATA AKUMBANA NA KADHIA

Katika mitandao ya kijamii nchini Kenya nako jina lake limekuwa mada kuu ya kuzungumzia madudu yanaoendelea kutendwa na
watendaji wa serikali ya Rais Uhuru Kenyatta.

Kwamba hivi karibuni kuliibuka mjadala unaomtaka Rais Kenyatta ajifunze mambo kadha wa kadha kutoka kwa Rais Magufuli.

Rais Kenyatta ametakiwa kupunguza safari za nje, kwani katika miaka miwili ya uongozi wake ameshasafi ri zaidi ya safari 40, tofauti na ilivyokuwa kwa mtangulizi wake.

Wananchi wa nchi hiyo wamekuwa wakimtaka Kenyatta kujifunza mawili matatu kutoka kwa mwenzake wa Tanzania.

Hoja kubwa wanayoinadi ni mambo makubwa yaliyofanywa na Magufuli katika kipindi kifupi cha utawala wake na kwamba
mambo hayo yanayazidi kwa kiasi kikubwa mambo yaliyofanywa na Kenyatta.

Aliyekuwa mtangazaji wa CNN, Jeff Koinange, ameshiriki kampeni ya kumsifu Rais Magufuli kwa hatua alizochukua na kusisitiza kuwa viongozi wa Afrika kuiga mfano wake. “Hii
ingefaa Magufuli atende yote akiwa Kenya,” aliandika Jeff Koinange.

WATUMISHI WATUMBULIWA MAJIPU

Katika kile kinachoonekana ni ukali wa ncha ya sindano ya Rais Magufuli, tayari watumishi zaidi ya 70 wametumbiliwa majipu
kutoka katika taasisi mbalimbali za umma.
Watumishi hao wamejikuta kwenye balaa hilo kutokana na wizi, ubadhirifu na uzembe kazini.

Tangu alipoingia madarakani amesababisha taasisi mbalimbali za umma zikiwamo halmashauri na manispaa kuwajibika ipasavyo.
Hivi karibuni yeye na Waziri Mkuu wake Kassim Majaliwa waliibua sakata la makontena zaidi ya 2500 yaliyopotea kinyemela bila kulipiwa kodi.

Sakata hilo limeshawaweka pembeni watumishi 27 wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA).
Katika kuendeleza kasi ya utendaji wiki iliyopita serikali ya Magufuli iliwashughulikia watumishi wengine 35 wa TRA kutokana na tuhuma za upotevu wa makontena.

Aidha, TRA imeanza kupitia upya taratibu za utoaji wa leseni katika bandari kavu (ICDs) ili kuondoa mianya na kuweka udhibiti katika uondoshaji wa mizigo katika bandari zote, ICDs na bohari
za forodha ikiwa ni pamoja na kupanga upya safu ya watumishi wake ili kudhibiti upotevu wa mapato ya kodi.

Moto wa Magufuli, pia uliwaka ndani ya Bandari ya Dar es Salaam, ambapo kulibainika upotevu wa takribani makontena 2780.
Hali hiyo ilisababisha vigogo 23 kung’olewa TPA pamoja na kuvunja Bodi ya Wakurugenzi ya mamlaka hiyo.

TANESCO KWAGUSWA

Katika kudhihirisha kuwa hana mzaha kwenye kudhibiti utendaji kazi, rungu lake lilianza kushuka ndani ya Shirika la Umeme Tanesco, ambapo uongozi wa shirika hilo uliwafukuza kazi watumishi waandamizi saba kwa tuhuma mbalimbali.

Uamuzi huo ulitangazwa na Mkurugenzi Mkuu wa Tanesco, Felschimi Mramba alisema kuwa shirika halitaweza kuwaacha
watendaji wala rushwa.

Aliendelea kufafanua kuwa wataendelea kuchukua hatua kwa watendaji wote na miongoni mwao ni wale waliofi kishwa mahakamani mkoani Kagera.

TAMISEMI
Kwa nyakati tofauti Ofi si ya Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) imekuwa ikichukua hatua kadhaa
ikiwamo kuwasimamisha kazi watumishi wa manispaa na halmashauri kwa tuhuma za ubadhirifu na uzembe au matumizi mabaya ya madaraka.

Mwishoni mwa Novemba mwaka huu Tamisemi iliagiza watumishi wawili waandamizi wa Halmashauri ya Manispaa ya Morogoro kusimamishwa kazi ili kupisha uchunguzi kuhusu utendaji wao wa kazi.

Wafanyakazi hao wanatuhumiwa kutoa kibali na kuidhinisha sehemu ya wazi karibu na njia kuu ya bomba la mafuta la Tazama
kujengwa jengo la hoteli.

Agizo hilo lilitolewa na Katibu Mkuu TAMISEMI, Jumanne Sagini, wakati akizungumza na watumishi wa Manispaa hiyo na Ofisi ya Mkuu wa mkoa alipofanya ziara ya kushtukiza hivi karibuni katika manispaa hiyo.

Novemba 13 mwaka huu Halmashauri ya wilaya ya Hai, mkoani Kilimanjaro, iliwasimamisha kazi watumishi wake wanne kwa
tuhuma za kughushi hati za mishahara na kughushi nyaraka zilizofanikisha kuchukua jumla ya kiasi cha sh. Mil 73.4 zikiwemo fedha za malipo ya muda wa kazi wa ziada kwa madaktari na
wauguzi wa Hospitali teule ya Machame.