Home Makala RAIS MAGUFULI AMEIKATAA AFRIKA NA MAMBO YAKE YOTE!

RAIS MAGUFULI AMEIKATAA AFRIKA NA MAMBO YAKE YOTE!

512
0
SHARE

NA MARKUS MPANGALA


WAKATI nikiweka mawazo sawa ya kuandika safu hii, mezani kwangu nilikuwa na vitu viwili; karatasi nyeupe na kalamu ya wino. Nilizama katika tafakuri iliyokuwa mbele yangu na ikitokea nchi ya ng’ambo. Nchi hiyo ni Gabon.

Katikati ya tafakuri hiyo likaibuka jambo la sahibu wangu na Katibu wa Itikadi na Uenezi, Humphrey Polepole na Mwenyekiti wake wa Chama cha Mapinduzi (CCM) ambaye pia ni Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, John P. Magufuli.

Nikawa natupia jicho kwenye barua inayoeleza kuwa Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi Rais John Magufuli alikutana na Polepole wakajadili suala la vipindi vya urais ambavyo kimekuwa gumzo kwenye makolido mbalimbali.

Gumzo hilo lilikuwa chini ya ‘udhamini’ wa Mbunge wa Chemba, Juma Nkamia ambaye amewahi kubainisha dhamira ya kuwasilisha hoja binafsi ya kuliomba Bunge lijadili suala la ukomo wa urais. Kwamba ukomo huo utoke kwenye miaka mitano hadi 7.

Ingawa alisitisha lakini mjadala huo ambao wanachama wawili wa CCM na viongozi wa mbunge huyo, Humphrey Polepole na rais Magufuli waliliweka bayana kuwa hawataki kulisikia na hakuna mpango wowote kuongeza vipindi vya urais.

Hapo ndipo tafakuri yangu iliponirudisha kwenye zogo la Bunge la Gabon ambalo ndani ya wiki mbili limekuwa gumzo kama ilivyoada ya wanasiasa. Ndipo takafukiri ya taarifa ya CCM ilipoungana na kile nilichokuwa nasoma kuhusu taarifa za Bunge la huko Gabon.

Bunge ambalo limempa rais Ali Bongo mambo mawili muhimu; kuondoa ukomo wa rais, kwamba ataruhusiwa kugombea muhula mwingine hadi pale atakapochoko. Pili Bunge limempa uhuru kuwa Rais hatashtakiwa kwa jambo lolote ndani ya nchi hiyo.

Kwanza nilijilaumu kuwa sina marafiki huko Gabon ambao wanaweza kunipa taswira ya ziada mbali ya kusoma habari za nchi yenyewe. Nilikuwa nafikiria kama limetokea jirani zetu wa Kenya, Rwanda, Uganda au Malawi hakika ningepata nyepesi nyepesi nyingi mno kuanzia wanasiasa, wanahabari na wananchi wa kawaida.

Lakini kwa Gabon nilikwama. Kwanza sina marafiki, pili sina ujuzi wa kuzungumza lugha ya Kifaransa. Sikuwa na mtu wala chanzo chochote cha kunimwagia habari zaidi. Katikati ya tafakuri nzito nilianza kuunganisha mambo ambayo yamewahi kutokea barani Afrika na kile kilichotendeka Gabon kwa Rais Ali Bongo Ondimba.

Ali ni mtoto wa rais Omar Bongo. Ali alimuoa Sylvia Omar Bongo, dada yake ni Pascaline Bongo Odimba ambaye alikuwa mke wa mwanasiasa Jean Ping.  Aidha, tunafahamu kiongozi wa Upinzani nchini Gabon ni Jean Ping ambaye amewahi kuwa Mkuu wa Tume ya Umoja wa Afrika. Kwahiyo Ali Bongo na Jean Ping ni mtu na shemeji yake! kama Yoweri Museveni na Dk. Kizza Besigye, ni mtu na “mtwasi” wake.

Naam, licha ya kuwa na wanawake wengine lakini Mzee Omar Bongo alimuoa Edith Lucie Bongo Ondimba raia wa Congo-Brazzaville. Cha mno zaidi ni kwamba huyu bibie Edith ni mtoto wa rais wa Congo-Brazzaville, Denis Sassou Nguesso. Tulie kidogo hoja ikuingie kichwani.

Wakati Ali Bongo akiondolewa ukomo wa urais mwaka 2018 huko Gabon, hali nchini Congp-Brazzaville chini ya Denis Sassou Nguesso iliondoa hilo mwaka 2015. Yaani kwa Nguesso anamuona mtoto wa mkwewe (Omar Bongo) Ali Bongo akifuata nyayo zake kuongeza mihula ya kuwa rais wa nchi. Muungano wa familia na siasa za kifamilia.

Hapa kwetu Rais Magufuli amebainisha kama si kutangaza kuwa hataki kuzidisha muda wa kuwapo madarakani. Ataheshimu Katiba yetu. Pia katiba yetu inasema rais ataongoza kipindi cha miaka mitano kwa muhula, na akichaguliwa tena muhula wa pili basi ni miaka mitano, jumla miaka 10 tu.

Kwamba Rais Magufuli hataki kifanyike kama kile kilichofanyika Rwanda kwa Paul Kagame mwaka 2015 ambapo aliitisha ‘kura’ ya maoni ili wananchi waamue kama Katiba ibadilishwe ili kuondoa ukomo wa urais au astaafu.

Na vilevile taarifa ya CCM na serikali inatuambia kuwa Magufuli wetu hataki kifanyike kama kile kilichofanyika nchini Gabon kumpa ahueni Ali Omar Bongo Odimba.

Na kwamba Rais Magufuli hapendi kifanyike kama kile kilichofanyika Congo-Brazzaville mwaka 2015 kwa Dennis Suasso Nguesso aliyeondoa ukomo wa urais, kisha nyayo zake zikafuatwa na ‘mkwewe’ huko Gabon!

Magufuli wala hapendi kifanyike kama kile kilichofanyika kwa jirani yake Uganda ya Yoweri Museveni ambaye amevuka kikwazo cha umri wa kugombea urais baada ya Bunge kupitisha muswada wa kuondoa kipengele kinachomzuia mtu mwenye miaka 75 kuwania nafasi hiyo yenye hadhi ya juu duniani.

Na Rais Magufuli hakitaki kitendo kile kilichojaribiwa kufanywa na Bakili Muluzi kule Malawi kabla ya kukubali muda umemtupa mkono na kumkabidhi madaraka Rais Bingu wa Mutharika. Au kile kitendo cha Olusegun Obasanjo wa kule Nigeria ambaye alilazimika kukabidhi madaraka licha ya kutamani kuongeza muda.

Kwamba Magufuli ameikataa Afrika na mambo yake yote ya “ongeza ongeza muda wa urais’. Magufuli hataki kile kilichotaka kufanywa na Zanzibar enzi za uongozi wa Salmin Amour maarufu kwa jina la “Komandoo”.

Sawa! Kuna mjadala wa zama hadi zama. Kabla ya mwaka 1995 mjadala ulikuwa mkali juu ya vipindi vya Urais. Mwalimu Nyerere alitusimulia mjadala huo ndani ya kitabu cha “Uongozi wetu na Hatima ya Nchi yetu.”

Kuna wengine walikuwa kama Juma Nkamia, walitaka “nyongeza” au majadiliano ya muda wa rais kukaa madarakani. Walitamani zaidi. Haikutokea. Na sasa Magufuli amekataa. Tena ameikataa Afrika yote na mambo yake ya kubadilisha katiba na kuwapa ‘vinono’ waliopo madarakani.