Home Latest News Rais Magufuli amejikana

Rais Magufuli amejikana

1274
0
SHARE

RAIS John Magufuli, amejikana, ameikana familia kubwa ya watawala wanaopenda kuendelea kuishi Dar es Salaam, ameukana utamaduni wa ovyo wa kutotii matakwa ya muda mrefu ya mwasisi wa Taifa hili, Hayati Mwalimu Julius Nyerere.

Matakwa yanayotaka makao makuu ya nchi kuwa Dodoma, hitaji hilo linalazimisha shughuli zote za dola kuhamia huko.

Pamoja na ukweli kwamba Mwalimu Nyerere ambaye ndiye mwasisi wa takwa la makao makuu kuhamia Dodoma, yeye mwenyewe alishindwa.

Ukweli huo hauondoi sifa na uhalisia wa shughuli zote za serikali kuhamia Dodoma kwa sababu nia ya Mwalimu Nyerere ilikuwa njema.

Azimio hilo lilifikiwa mwaka 1973, na kukubaliwa na TANU, ambapo makubaliano hayo yalisukuma kuanzishwa kwa Mamlaka ya ustawishaji wa Makao Makuu (CDA), ambao kazi yake kubwa ni kupanga mji.

Pamoja na kukwama kwa uongozi wa Mwalimu, lakini waliiona haja hiyo kwa sababu kadhaa zikiwemo za kurahisha utoaji wa huduma kwa jamii na nchi kuwa na uhakika wa kiulinzi na kiusalama  kutoka pande zote.

Nafikiri pamoja na Mwalimu kukwama, lakini walifikia uamuzi huo baada ya kujiridhisha na kuiona haja hiyo.

Hali ya wakubwa kusita kuhamia Dodoma iliendelea katika awamu zote za utawala, shughuli nyingi za kiserikali ziliendelea kufanyika Dar es Salaam, huku chache hasa zile za vikao vya  Bunge zikifanyika huko.

Serikali imekuwa ikilazimika kutumia fedha nyingi kuwasafirisha watendaji wake ili kuhudhuria masuala mbalimbali vikiwemo vikao vya Bunge.

Jambo la kufurahia ni ujasiri wa Rais Magufuli kwa kuamua kujikana na kuikana familia ya kupenda na kuponda raha ndani ya jiji la Dar es Salaam.

Magufuli amefanya hivyo kwa kuendeleza dhamira njema ya kuhakikisha haki na usawa unakuwapo huku taratibu stahiki zikifuatwa.

Nia hii inaashiria mwanga wa karabai kubwa ya neema unaopaswa kumulika katika maeneo yote ya nchi bila kujali nani atafaidika na nani atapata maumivu ya muda mfupi.

Hii maana yake ni kuwa yeye ni Rais wa watanzania wote na mwenye uwezo wa kuishi popote bila kujali nafasi yake,

Hatua hii inanipeleka kwenye andiko lililopo ndani ya Biblia katika kitabu cha Marko, ambacho kinaeleza wazi namna Yesu Kristo alivyoikana familia yake kwa maslahi ya wengi.

Katika kitabu cha Marko, 3:31-35 andiko linasema:31 Mama yake Yesu na ndugu zake wakafika wakasimama nje wakamtuma mtu amwite. 32 Umati wa watu waliokuwa wameketi kumzunguka wakamwambia, “Mama yako na ndugu zako wako nje, wana kutafuta.”

33 Akawauliza, “Mama yangu na ndugu zangu ni akina nani?”

34 Akawatazama wale watu waliokuwa wameketi kumzunguka, akasema, “Hawa ndio mama zangu na ndugu zangu. 35 Mtu yeyote anayetenda mapenzi ya Mungu ndiye ndugu yangu na dada yangu na mama yangu.”

Nikiri wazi kuwa Rais Magufuli hawezi kuyafikia wala kuyakaribia matendo ya Yesu, lakini yapo baadhi ya mambo anaweza kufananishwa nayo si moja kwa moja.

Binafsi nimeguswa na uamuzi wake huu wa kutaka serikali yake yote kuhamia Dodoma, ni uamuzi mgumu ambao unaibua maswali na hoja lukuki.

Tayari wapo baadhi ya watu walioanza kumkosoa kwa sababu na hoja zao wanazoziona ni sahihi. Si jambo baya kukosoa hasa pale panapostahili, lakini kwenye eneo hili, nafikiri yuko sahihi na anapaswa kupongezwa.

Zipo changamoto zitakazosababisha uchelewaji na pengine ukwamishaji wa suala hili, lakini jambo muhimu kwa sasa ni kuanza kufanikisha dhamira hii njema.

Makando kando yote yatakayoibuka kwenye mchakato huu yatatatuliwa mbele ya safari, muhimu ni kuanza na kuonesha nia ya dhati ya kuhamia Dodoma.

Uamuzi huu mgumu, unazo faida na hasara zake, lakini hatuna sababu ya kuangalia hasara, badala yake tujielekeze kwenye faida ambazo hazitaonekana kwa haraka na huenda kizazi cha juzi na jana kisiyafaidi matunda haya.

Kwa fikra zangu naiona haja ya shughuli zote za kiserikali kuhamia Dodoma huku mji wa Dar es Salaam, ukiachwa huru ili uendelee kuwa kitovu cha biashara.

JIMMY CHARLES, +255 688 063 839