Home Makala ‘RAIS MAGUFULI ANATAKIWA KUPAMBANA NA UFISADI WA KATIBA’

‘RAIS MAGUFULI ANATAKIWA KUPAMBANA NA UFISADI WA KATIBA’

1160
0
SHARE
Rais Dk. John Magufuli

Na FARAJA MASINDE

KUWAPO kwa amani na mshikamano ni moja ya mambo ambayo yamekuwa chachu na kusifika kwa jina la Tanzania kama nchi ya amani, huku wengine wakienda mbali na kuuita kisiwa.

Sifa hizo ni kutokana na ukarimu na mshikamano ambao wamekuwa nao Watanzania wao kwa wao au kwa wageni wanaotembelea nchini kwa ajili ya kujifunza mambo mbalimbali.

Hata hivyo, hatuwezi kupingana na ukweli kuwa msingi wa mambo yote hayo ni kutokana na kuwapo kwa misingi thabithi ambayo iliasisiwa na Baba wa Taifa, Hayati Julias Nyerere.

Ni uthabithi huo ndio umefanya Watanzania kushirikiana kwenye shida na raha na hata kuungana na kuwa kitu kimoja pale linapokuja suala la utaifa, jambo ambalo huenda lisiwe rahisi kwa mataifa mengine ambayo yametawaliwa na machafuko.

Hata hivyo, pamoja na kuwapo kwa utulivu huo, siku za hivi karibuni kumekuwa na matukio mbalimbali ambayo yamekuwa yakitishia ustawi wa Taifa letu, hatua ambayo imeanza kuwashtua hadi baadhi ya viongozi wa dini nchini.

Miongoni mwa viongozi hao ni Askofu William Mwamalanga ambaye ni Mwenyekiti wa Kamati ya Kitaifa ya maendeleo ya amani na haki za binadamu kwa jamii ya madhehebu ya dini nchini, anayeamini kuwa chanzo cha matukio yote yanayoendelea kutokea nchini ni chuki ambayo imelifunika Taifa kwa sasa.

Mwamalanga katika mahojiano aliyofanya na RAI, anakiri kuwa  chuki ndiyo chanzo cha mambo yote yanayoendelea nchini kwa sasa kuanzia kwa viongozi wa Serikali hadi wananchi wa kawaida.

Anasema iwapo chuki hiyo haitakemewa basi inaweza kabisa kukwamisha jitihada za Tanzania kupiga hatua kimaendeleo hususan kuelekea kwenye uchumi wa viwanda kama ilivyo azma ya Serikali.

“Chuki imekuwa ni mzigo mkubwa unaolikabili Taifa kwa sasa kuanzia ngazi za juu za utendaji wa serikalini hadi kwa wananchi, jambo ambalo limegeuka kuwa janga hatari kwa Tanzania linalotokana na chukizo la Mungu.

“Tumeanza kuiona chuki kuanzia juu mpaka uchochoroni na ndiyo maana kwa sasa mahubiri ya nchi nzima ya maaskofu yamekuwa ni juu ya chuki, kwani hii imekuwa ni mzigo mkubwa unaolikabili Taifa, kwani hata wenye mawazo mazuri ya kujenga wamekuwa wakipuuzwa kutokana tu na chuki.

“Mfano mzuri ukiangalia suala la Mbunge Tundu Lissu au Zitto Kabwe ambao wamekuwa wakitoa mawazo mazuri yenye kujenga uchumi, wamekuwa wakipuuzwa kutokana na kutokuwa kwenye chama dola, jambo ambalo ni chanzo cha siasa chafu zinazoongozwa na chuki,” anasema Askofu Mwamalanga.

Anafafanua kuwa, chanzo kikubwa kinachopelekea chuki hiyo ni kutokana na wanasiasa ambao wamekuwa wakitumia chuki na visasi kwa ajili ya kupata umaarufu na madaraka, jambo ambalo anasema linapaswa kupigwa marufuku.

“Mfano ukiuliza mawaziri ambao walikuwa wakitangaza kila siku kuwa wanaenda kufanya ziara za kushtukiza au kutumbua majipu, ukiuliza leo hii zimezaa matunda gani hakuna hata mmoja atakayekujibu isipokuwa ni chuki tu ndio iliyokuwa imetawala.

“Leo hii sifa ambazo wanamwagiwa Wakenya kupitia Katiba yao mpya kwa maamuzi yaliyotolewa na Mahakama ya juu nchini humo zilipaswa kuja kwa Tanzania, kwani tungekuwa na Katiba nzuri kushinda ile ya Kenya, lakini kwa ajili ya chuki tu katiba ile ikayeyuka na watu wakala fedha,” anasema Askofu Mwamalanga.

Akifafanua zaidi kuhusu Katiba, anasema Katiba ya Jaji Joseph Warioba ilikuwa ni bora kuliko ya Kenya lakini tu kwa sababu ya chuki imepelekea Katiba hiyo kukosekana licha ya gharama kubwa zilizotumika kuandaa mchakato huo, huku akiongeza kuwa  leo hii kwa ajili ya chuki Watanzania wanaishi maisha magumu ambayo hayana mfano.

“Rais Dk. John Magufuli anatakiwa kupambana na ufisadi wa Katiba, kwani ni fedha za Watanzania zilizotumika bila mafaniko yoyote kuanzia kwenye rasimu ya kwanza hadi ya pili na hii yote ni kwa sababu ya chuki ambayo imepelekea mchakato huo kufutika ghafla.

“Leo hii ni hatari kwa ajili tu ya chuki Watanzania wako tayari kuuana au hata kuhatarisha usalama wa Taifa letu, lakini pia watu hawako tayari kumuunga Mtanzania mwenzao mkono pale inapotokea amefanya vizuri, leo hii Rais Magufuli anafanya vizuri lakini ni ngumu kwa watu kumuunga mkono, hii yote ni kwa ajili ya chuki,” anasema na kuongeza:

“Ukitazama suala la ununuzi wa ndege Watanzania wamekuwa wakizipachika jina la ‘ndege za Magufuri’ ilihali alinunua kwa fedha za wananchi pia kauli za baadhi ya watendaji wa Serikali ambao wamekuwa wakifanya maamuzi kwa kusema kuwa ni maamuzi kutoka juu, ni jambo linalochochewa na chuki tu ili kumfanya rais aonekane mbaya kwa wananchi.”

Askofu Mwamalanga anasema kuwa kwa sasa hakuna kiongozi yeyote anayeonyesha utendaji uliotukuka kama ilivyokuwa awali wakati wa uteuzi kutokana tu na chuki, huku akitolea mfano Baraza la Mwaziri.

“Kwa sasa hakuna tena anayeendelea na kasi waliyokuwa nayo mwanzo kutokana na kufanya maamuzi ya chuki isipokuwa Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Wiliam Lukuvi ambaye amekuwa akifanya kazi kwa weledi.

“Tazama mgogoro wa Chama cha CUF ukiangalia ni chuki tu ambayo imetanda hadi kufikia bungeni, kwani hata Spika amekubali kuingizwa kwenye chuki hii, unasema hawa si wabunge, hawa ni wabunge ilihali wanatumia fedha za nchi, huu ni sawa na ufisadi tu, spika amekosa maamuzi ametawaliwa na chuki,” anasema.

Askofu Mwamalanga anasema Rais Magufuli anapaswa kukemea na kuhubiri juu ya chuki ambayo imepanda juu kuliko haki kwenye maeneo mbalimbali ya Serikali yake, ikiwamo kutazama kesi za wabunge wengi wa upinzani ambao wamekuwa wakishtakiwa mara kwa mara kwa makosa yanayofanana huku akiwakumbusha viongozi juu ya nafasi walizonazo.

“Lazima viongozi watambue kuwa vyeo walivyonavyo wamepata kwa neema tu na bado muda mfupi wengi wao wakiendelea na uongozi wa chuki vyeo vyao vitawakimbia, kwani ni jambo la ajabu na lilosikitisha kusikia watu wanafanya jambo kwa kisingizio cha maamuzi kutoka juu, juu wapi? ilihali ni utashi wao wenyewe,” anasema.

Anasema Rais Magufuli anapaswa kuzungumza na wasaidizi wake juu ya kuacha chuki ambayo kadiri siku zinavyozidi kwenda ndivyo inavyoendelea kuota mizizi.