Home kitaifa Rais Magufuli angazia kituo cha Mwenge

Rais Magufuli angazia kituo cha Mwenge

1707
0
SHARE

RAI-13-KATUNIKAMA kuna jambo ambalo Rais wa awamu ya tano John Magufuli, anatakiwa kutolifumbia macho ni Kituo cha mabasi cha Mwenge.

Kwanini nasema hivyo kwanza kihistoria eneo hilo lipo Kitalu 43, Kijitonyama,  takribani  asilimia 90 ya eneo hilo linamilikiwa  na Chama  cha  Ushirika  cha  Ujenzi  wa Nyumba  Mwenge (Mwenge Housing Cooperatice Society LTD) kilichoanzishwa mwaka  1971.

Wanachama  wa chama  hicho ndio  wadau  wakubwa  wa matumizi  ya ardhi  katika  kitalu  hicho 43, na   ndio  walikuwa  wanalinda  na kupanga  matumizi  ya ardhi  kama  ramani  na mipango miji  inavyoonyesha, kabla  ya hati  kubwa  ya pamoja  kurudishwa  na kila mwanachama  kumilikishwa  kiwanja  chake  mwaka 1995.

Barabara ya  Kambarage  imepewa  jina hili  kumuenzi  Baba  wa Taifa kwani  ndiye alikuwa Muasisi  wa   Chama  hicho  pamoja  na hayati Mzee Rashidi mfaume  Kawawa   na Marehemu  Dereck  Bryson.

Ukiangalia  ramani ya barabara hiyo inaonyesha ni ‘Service  Road’ na iko  sambamba  na  Barabara  ya Ali  Hassan  Mwinyi  lengo  kuu  likiwa kuwahudumia  wakazi  wa Mwenge, katika  huduma  za usafiri  ili wakazi  hasa watoto wasifike  barabara   ya Ali  Hassan  Mwinyi  kwa kuwa ni barabara  kubwa .

Barabara  hii inatokea  barabara  ya Sam  Nujoma, kwenye   ‘Service  station’  ambapo  kiasili  au  kimichoro  ndipo  kituo cha mabasi Mwenge  kilitakiwa  kiwe,  lakini  kwa  sababu  zisizo  eleweka   eneo  hilo limevamiwa.

Eneo hilo limegawiwa kama viwanja ambako hapo awali lilikuwa likitumiwa na wanachama kama genge la kuuza bidhaa mbalimbali ili kuwahudumia  wakazi  wa Mwenge  na  Mlalakuwa.

Kwa sasa eneo hilo lote  limevamiwa  na hakuna  hatua  zozote  zinazochukuliwa  kulirudisha  katika  matumizi  yaliyopangwa ya kituo cha huduma.

Kuhamisha Kituo cha daladala kutoka  Mwenge  ni njia  mojawapo  ya kuficha  madhambi  hayo kwani  pale  palipokuwa kituo cha mabasi iliyohamishwa na kwenda Makumbusho  hapakuwa  mahali sahihi kwa kituo cha Mwenge.

Mahali sahihi palipokuwa panastahili kukaa kituo hicho ilikuwa ni eneo hilo la ‘Service  station’ na ndio  ilikuwa madhumuni yake makubwa ya kutumiwa  barabara ya Kambarage.

Iwapo sehemu hiyo ikitumiwa ipasavyo hakutakuwa  na msongamano wowote wa magari  katika  barabara  ya Ali  Hassan  Mwinyi.

Hivyo Rais Magufuli kama msimamizi wa sheria uwasaidie wakazi wa Mwenge kupata  huduma  za vituo  vya  mabasi kupitia njia hiyo kwani ukiangalia miundombinu  ya  barabara  katika  ramani  haitarajiwi  watu  wa  Mwenge  kupata  tabu ya kituo.

Njia pekee ya kurejesha mji wa Mwenge na kuwa kama  zamani  katika  mipango  miji  ya Dar es salaam ili Mwenge  irudi  kama ilivyokuwa imepangwa hapo mwanzo.

Iwapo Rais Magufuli atatuma wachunguzi wake atabaini kuwa kufungwa kwa barabara  hiyo  na kituo cha Mwenge imetokana na masuala anayopigania ya ufisadi kwa kituo  hicho  cha Mwenge  na  barabara  ya Kambarage  vilifungwa.

Naamini kama watafuatilia kwa undani watagundua kwamba hayo yalifanyika ya kukihamisha kituo hicho yalikuwa na nia ya kunufaisha biashara za Makumbusho  Complex.

Biashara ambayo imekuwa ikilalamikiwa kukingiwa kifua na aliyekuwa Mkurugenzi wa Manispaa ya Wilaya  ya Kinondoni, Injia Mussa Natty na  wengine waliokuwa wakitajwa kujihusisha na hilo ni mhandisi  wa Manispaa hiyo, Esmaili na  Injia Baraka  Nkuya.

Naamini hivyo kwa sababu wote waliotajwa katika sakata hilo hawapo hivi sasa Manispaa ya Kinondoni kutokana na tuhuma mbalimbali za ubadhilifu  wa mali  za  Umma  katika  Wilaya hiyo ya Kinondoni ikiwemo kujenga  barabara zenye  lami za  kiwango cha chini  wakati gharama walizoziandika katika  malipo  kuwa  juu.

Kwa sasa Magufuli anatakiwa awasaidie wakazi wa Mwenge ambao wanapata shida na mateso  mbalimbali ya usafiri kutoka  Mwenge   kwenda  Kariakoo,  Ubungo, Posta katika shughuli zao za kila siku.

Rais anatakiwa afuatilie kwa sababu kama barabara hiyo haitafanikiwa watakaoumia ni vijana wa shule, walemavu, wajawazito, wagonjwa na wazee wenye umri mkubwa wanapata shida  ya kutembea  kutoka  Mwenge kwenda Makumbusho kwa miguu au  kutumia  fedha  nyingi  kwa ajili  ya nauli ya  zaidi  ya mara  tatu.

Wengi wa wakazi hao wanaopata shida ni wale wenye   kipato kisichozidi 150,000 kwa mwezi hivyo  ni jukumu la Rais, Magufuli kuonyesha kuwajali wanyonge wanaohangaika kwa manufaa ya viongozi  wachache wa Manispaa  ya  Wilaya  ya  Kinondoni.

Hii ni zamu ya Magufuli kuhakikisha anaondoa tatizo hilo ili kuwaacha huru wananchi wa Mwenge ambao wamekuwa wakijaribu kila njia kuhakikisha malalamiko yao yanapatiwa ufumbuzi.

Nitashangaa iwapo nitaona kama serikali hii nayo itaendelea kuwa kimya kama ambavyo ilivyokuwa ikifanya ile ya awamu ya nne ambayo ilionekana kuwajali zaidi watu wenye uwezo.

Mwisho mwema wa ushughulikiaji wa suala la wananchi wanyonge wa kituo cha Mwenge utatoa taswira kwao kwamba ni namna gani watanufaika na utawala huu wa awamu ya nne.