Home Makala RAIS MAGUFULI NA UKUTA WA TANZANITE

RAIS MAGUFULI NA UKUTA WA TANZANITE

680
0
SHARE
Tanzania's President elect John Pombe Magufuli addresses members of the ruling Chama Cha Mapinduzi Party (CCM) at the party's sub-head office on Lumumba road in Dar es Salaam, October 30, 2015. Tanzania's ruling party candidate, John Magufuli, was declared winner on Thursday of a presidential election, after the national electoral body dismissed opposition complaints about the process and a demand for a recount. The election has been the most hotly contested race in the more than half a century of rule by the Chama Cha Mapinduzi Party, which fielded Magufuli, 56, a minister for public works. REUTERS/Sadi Said

NA PROF. HANDLEY MAFWENGA

“THE John Magufuli “JPM” tanzanite wall”. Ilizungumzwa na wahenga kuwa “ukuta bora hujenga majirani bora”, hivyo yafaa tuseme sasa kuwa “ukuta bora hujenga wafanyabiashara bora wa tanzanite” na hii inajieleza bayana, kwani Rais Dk. John Pombe Magufuli siyo wa kwanza kuamua kujenga ukuta kipindi hiki.

Hata Rais wa Marekani, Donald Trump alikerwa na uwepo wa usalama wa Wamarekani na kuweka uthubutu wa kujenga ukuta dhidi ya Mexico, ukiitwa “Donald Trump Mexico Wall”.

Tanzanite hupatikana hapa nchini tu, hakuna duniani pote, ndiyo maana kampuni iliyoitwa Tiffany & Coy Ltd iliyojishughulisha katika kusambaza zao hilo ikatoa jina la zao hilo kuitwa “tanzanite”, wakiheshimu jina la nchi inapopatikana yaani “Tanzania” “The Blessed Territory”.

Uthamani wa zao hilo hutegemea vitu vikubwa vinne, huitwa “4Cs”, ikiwemo rangi “Colour”; ambapo rangi huwa na thamani kubwa zaidi ikihusishwa pia na imani za maandiko ya dini kwenye Biblia na Quran na uwepo wa rangi za bendera mbalimbali.

Mfano hutegemei rangi nyeusi ikavutia thamani. Aidha, aina ya ukataji “cut” pia huwa na thamani tofauti, ubora yaani “clarity” na uzito wa jiwe lenyewe kwa kuzingatia kipimo chake cha “carat” yaani “carat weight” pia huwa na thamani tofauti.

Tanzanite ni zao ambalo ni rahisi kubeba na kuibwa, kwani unaweza ukaiweka mfukoni tanzanite ya thamani kubwa na ukalangua au ukavuka mpaka wa nchi na kuuza bila kujulikana.

Aidha, uuzaji wake ni wa mtandao, kwani anayeuza huwa hamjui mwenye kununua na msambazaji hamjui muuzaji wala mnunuzi, ni biashara iliyogubikwa na pepo wa kuaminiana, kuogopana ikibeba ushetani wa kutomuogopa Mungu.

Hivyo siyo rahisi kujua vituo vya uuzaji na usambazaji mithili ya biashara za dawa za kulevya,  soko hili linahusisha madalali na wachuuzi “dealers” na “brokers” ambao wengine hawana ofisi na hawatunzi hesabu za uhasibu na kodi na kusababishia Serikali kukosa kodi stahiki.

Aidha, kampuni moja inaweza kumiliki zaidi ya kampuni 20 tofauti kwa zao hilo moja, inaweza ikawa na kampuni ya uchimbaji, ikawepo ya ukataji na usafishaji, ikawepo ya masoko na ikawepo ya uuzaji, hivyo kusababisha hata usimamizi kuwa mgumu.

Hii inaweza ikaonesha kampuni ya uchimbaji iliyopo Tanzania rejesho la faida za mtaji (Return on Capital Employed) likawa dogo hata kuliko rejesho kwenye kampuni ya masoko au uuzaji zilizo nje ya Tanzania.

Rais Magufuli ameagiza ujengwe ukuta haraka kunusuru vifo vya masikini wanaokosa dawa hospitalini na huduma nyingine za jamii kulinda hadhi ya Tanzania ipatikanayo kwenye tanzanite ambayo kwa muda mrefu nchi kama India, Kenya na  Malaysia zimekuwa zikitumia hadhi yetu.

Lakini ukuta huo siyo wa kwanza, kwani

(1) “Kabla ya Kristo, watawala wa kale Shulgi na Shu-sin walijenga ukuta mkubwa kuwazuia Waamori ambao walikuwa wakiingia huko Mesopotania, ukuta huu uliitwa ‘Ukuta wa Waamori”, ambao ulikuwa mrefu zaidi ya maili mia moja kati ya Mji wa Tigris na Mto Euphrate ambako sasa hujulikana kama Iraq.

(2) Mnamo mwaka, 461 Kabla ya Kristo, katika mji wa Athens huko Ugiriki kulijengwa ukuta kulinda udhaifu wa kijeshi uliojitokeza kwa kuunganisha eneo la katikati ya Jiji hilo na Bandari za Piraeus na Phalerum.

Ukuta huu mrefu ulisaidia Jiji hilo kujiweka karibu na bahari na kujilinda na maadui hadi ulipovunjwa na Jenerali wa Kirumi, Sulla mwaka 486 Kabla ya Kristo.

(3) Ukuta mkubwa sana wa Gorgan uliojulikana kama “Nyoka Mwekundu” kwa jinsi ulivyojengwa na tofali nyekundu za ajabu, ulikuwa na urefu wa Maili 121 ambao ulikwenda eneo la Pwani ya Kusini mwa Bahari ya Caspian kuelekea Milima ya Elburz, ambako sasa kunaitwa Iran.

Ukuta huu ulijengwa na “Alexander the Great” na ulijulikana kama “Ukuta wa Alexander”, lakini utafiti wa hivi karibuni umebaini ukuta huo ulijengwa na Waajemi wa Kisasaniani katika Karne ya 5 Baada ya Kristo.

Ukuta huu ulitumika kuwalinda Waajemi dhidi ya Wahefuthaiti na maadui wengine wa Kaskazini.

(4) Baada ya Kristo, Mfalme Hadrian aliamuru ujengwe ukuta wa Mawe kuzuia Warumi waliokuwa Uingereza wakati huo dhidi ya makabila mengine yaliyovamia Kaskazini ya Uingereza na nchini Scotland. Ukuta huu ulijulikana kama “Ukuta wa Hadrian”, ukiwa na urefu wa maili 73 kuanzia mto Tyne Mashariki.

Ukuta ulikuwa na upana wa futi 10 na urefu wa futi 15. Ukuta huu ulitumika pia kutoza kodi-na kuwa na minara ya ulinzi, ukuta huu ulikuwa kielelezo cha pekee cha Warumi hadi walipojitoa Uingereza katika Karne ya 5.

 

Katika kipindi chake cha uhai wa miaka 1600 ukuta huo umeonekana kubomoka bomoka na kuondoka katika uhalisia wake, japo ni moja ya eneo la kihistoria ambalo linatembelewa sana nchini Uingereza.

(5) Ukuta mwingine ni ule uliojengwa nchini China, uitwao “Ukuta wa Simulizi”, uliojengwa kwa mawe na mbao wenye urefu wa maelfu ya maili kutoka Jangwa la Gobi kuelekea mpaka wa Korea ya Kaskazini.

Ujenzi ulianza karne ya tatu Kabla ya Kristo, chini ya mfalme Qin Shi Huang, ingawa eneo maarufu lilijengwa kati ya karne ya 14 na 17 baada ya Kristo, ili kulinda nasaba za ujambazi.

Eneo hili lina urefu wa kwenda juu wa futi 25 na lilijengwa na matofali na chokaa, ukigubikwa na minara ya kuchukua picha iliyotumia mawasiliano ya moshi na ishara za kivita pale ambapo walishambuliwa, lakini mnamo mwaka 1550 alitokea mtawala wa Mongolia, Altan Khan, akaivamia Beijing.

(6) Ukuta maarufu wa urefu wa maili 14 ukizunguka Jiji la Istanbul zamani ukiitwa mji wa Watheodosia ulijengwa Karne ya tano wakati wa Utawala wa Theodosia wa Pili.

Ukuta huu uliitwa “Ukuta wa Watheodosia”, uliozuia wanajeshi wasifanye uvamizi, makundi ya wanajeshi yalilinda muda wote kwa kile kilichoitwa “Vita ya Kigiriki” dhidi ya maadui wowote ambao wangejaribu kuwavamia.

(7) Katika miaka ya awali ya vita vya wenyewe kwa wenyewe, Ujerumani Magharibi ilikuwa ni eneo ambalo maelfu ya raia wa Ujerumani Mashariki walikimbilia katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Ujerumani Magharibi.

Lengo likiwa ni kukabiliana na hali hiyo, utawala wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Ujerumani Mashariki ulijenga ukuta ambao uliizunguka Ujerumani Magharibi Agosti 13, 1961.

Ukuta huo ulijulikana kama “Ukuta wa Berlin”, ambapo klabu ya Yanga mwaka 1982 ilitohoa na  kuiita ngome yake ya ulinzi kuwa ‘Ukuta wa Berlin’.

Ngome ya Yanga iliundwa na kipa Hamis Kinye, Joseph Fungo, Yussuf Ismail Bana, Rashid Idd Chama, Uncle J-Juma Shaaban, Ahmad “Amasha Mathematician”, Hussein Kondo “Mmakonde”, Phred Felix Minziro “Majeshi”, Athman Juma Chama, Isihaka Hassan Chuku, Allan Shomari na Charles Boniphace Mkwasa”, ukuta huo ulitengenezwa na kocha Rud Gutendolph, raia wa Burgaria akitokea Ujerumani aliyeanzia kufundisha timu ya Taifa “Taifa Stars”.

Ukuta huo ulibomolewa na Zamoyoni Mogella “Golden Boy-Morgan” wa Simba na kusambaratishwa kabisa na mshambuliaji Mohammed Salim wa Coastal Union mwaka, 1984 mwanzoni.

Ukiachia hasira za Ahmad Amasha kumvunja mguu ndugu yangu Yussuf Ambwene, beki wa kulia wa CDA mwaka 1983 na kupewa kadi nyekundu iliyosababisha akose mechi dhidi ya Simba ikitokea Brazil ilikokaa siku 45 ikipelekwa na Hayati Samuel Sitta wakati huo  akiwa kigogo wa CDA ambaye aliipenda sana Simba na Mzee wetu Rashid Mfaume Kawawa na Mzee Aboubakar Mwilima (Mungu awalaze mahali pema peponi), Simba ilikuwa chini ya Makocha wa Brazil, Edil Silva na Nizol.

Ukuta wa Berlin wa Ujerumani ulikuwa ni kikwazo kilichojengwa na saruji ambacho kiligawa ardhi ya mji wa Berlin kimuundo na kiitikadi hadi ukuta huo ulipofunguliwa Novemba, 1989. Ukuta huo ulijumuisha minara iliyojengwa sambamba na ukuta wa saruji, ikiwa ni pamoja na eneo kubwa ambalo lilijulikana kama: “Kipande cha Kifo” ambacho kilijumuisha vizuizi vya magari.

Upande wa Ujerumani Mashariki ulichukulia ukuta huo kuwa ni ulinzi wa idadi kubwa ya watu wake dhidi ya utawala wa Kifashisti na hivyo kulinda mapenzi na nia ya raia wake ya kujenga Dola la Kisoshalisti la Ujerumani Mashariki.

Kwa ujumla ukuta huo ulilenga kuzuia uhamaji mkubwa wa watu baada ya Vita Kuu ya Pili ya Dunia.

Jamhuri ya Kidemokrasia ya Ujerumani Mashariki ilipingana kwa kasi na nchi zilizounda Umoja wa NATO, ikiwamo Ujerumani Magharibi wakizichukulia nchi hizo kuwa ni za kifashisti.

Ujerumani Magharibi waliuita ukuta huo “Ukuta wa Aibu”, jina lililotolewa na Willy Brandt, akituhumu ukuta huo kuzuia haki ya uhuru wa kuishi na kutembea mahali popote chini ya mwavuli wa haki za binadamu.

Mnamo mwaka, 1989 kukatokea Mapinduzi karibu na Ujerumani Mashariki katika nchi za Poland na Hungary, hivyo kulazimika kufungua ukuta huo na kuubomoa rasmi mwaka 1990 hadi 1992 na kuifanya Ujerumani iweze kuungana tena.

Ni vyema ukuta huu unaojengwa kuzuia madini ya vito ya tanzanite dhidi ya ufisadi wa utoroshaji tanzanite, dhidi ya kulinda nia ya Watanzania kujenga dola la uchumi wa viwanda, Dola la Tanzania likipigana kwa kasi na mtandao wa biashara haramu ya ulanguzi wa tanzanite na ukwepaji kodi wa makusudi uwe wa kihistoria ili usije ukabomolewa baadaye na mafedhuli.

Yafaa ubaki kuwa ni urithi wa kizazi na kizazi katika Taifa  letu, aidha, pawepo pia na ukiritimba na udhibiti wa haki miliki ya vito, yaani “Intellectual Property rights” ili kupewa kipaumbele katika kuhakiki na kudhibiti ongezeko la thamani kwenye zao hilo ”.