Home Makala RAIS MAGUFULI WAKEMEE VIONGOZI HAWA…

RAIS MAGUFULI WAKEMEE VIONGOZI HAWA…

1219
0
SHARE

NA LAMU KILIMBA

RAIS na Mwenyekiti wa chama changu chenye historia tukufu Afrika na duniani, nakusalimu kwa unyenyekevu Kidumu Chama Cha Mapinduzi! Pole na majukumu mazito ya kuwatumikia Watanzania. Rais kipenzi cha wanyonge naomba upokee ujumbe wa mambo 10 muhimu kwa chama na Taifa letu, nakuomba kwa unyenyekevu mkubwa tafadhali pokea mwendelezo wa ujumbe huu.

Sita, Rais Magufuli wanasiasa wanaingilia mambo ya kitaalamu ndani ya Taifa letu na wamekuwa wachumi wao, wataalamu wa afya, wa kilimo, wa elimu wao, wamekuwa wahasibu wao; yaani kila kitu wanataka wafanye hawajui nini maana ya ‘professionalism’, mwisho wa siku tunakosa ufanisi katika utendaji kazi maana maDC, maRC wanafanya mpaka maamuzi ya kisheria pasipo kuwaomba msaada wanasheria, tunafurahi kwa muda ipo siku Taifa litapata hasara kubwa kwa kulipa fidia mamilioni ya fedha kisa wanasiasa kufanya mambo yanayohitaji ujuzi wa kitaalamu. Hili la wanasiasa kuingilia masuala ya kitaalamu wakati mwingine linapelekea Serikali kukosa majibu sahihi juu ya changamoto zetu. Kwa mfano hatuwezi kupata majibu juu ya changamoto za elimu kupitia mwanasiasa, kupata majibu ya kisheria kwa wanasiasa, kupata majibu ya changamoto za afya kupitia wanasiasa wala mwanasiasa hawezi kupata majibu juu ya changamoto za kilimo, ndiyo maana mawaziri wetu wana makatibu wa wizara, lazima wataalamu wasikilizwe si vema wanasiasa kuwa juu ya wataalamu na haifai mwanasiasa kutoa maelekezo ya kitaalamu kwa mtaalamu. Rais natambua heshima kubwa unayowapa wataalamu na wasomi wa nchi hii ndiyo maana teuzi zako zinajali wasomi wabobezi wa mambo, nakuomba upokee ujumbe wangu wakanye wanasiasa waache kuparukia mambo ya kitaalamu, maDC, maRC, mawaziri, wabunge, maDAS, Wakurugenzi na wanasiasa wengine ni vema wafanye kazi kwa kuzingatia sheria na taratibu zetu tulizojiwekea kuliko kutunisha misuli kwa wataalamu, kisa tu hawana nguvu kimamlaka.

Saba, WanaCCM wanaogopa kutoa mawazo na kuwasahihisha viongozi wanapokosea hadharani, wanajifungia ndani wanalalamika huku hadharani wakishangilia na kupongeza. Kipindi hiki wanaCCM wamekuwa watu wa aina yake hawapo tayari kusema ukweli pale viongozi wanapokwenda kinyume na taratibu zaidi wanapongeza na kupiga vigelegele. Cha ajabu wakiwa mafichoni wanaanza kulalamika na kusema madhaifu ya viongozi, kwa kifupi kuwa wanaCCM wenzangu wamekuwa wanafiki, hata kwenye vikao hawapeleki changamoto za wapiga kura sana wanaenda kuwapongeza viongozi, wabunge wanashindwa kusimamia ilani wala wanaCCM hawana habari, madiwani wanakosea wala hakuna mwanaCCM mwenye kusema hadharani na kusahihisha. Mwenyekiti wangu raisi wangu, wewe ni muumini wa kweli na siku zote unasema ukweli, nakuomba upokee ujumbe huu kwa niaba ya wanaCCM wazalendo wa kweli tunaopenda kusema kweli kwa faida ya chama na Taifa letu, watake viongozi warejeshe utaratibu wetu mzuri wa kuambiana ukweli na kukemea makosa ya viongozi wetu, kila mwanaCCM akemee uovu unapojitokeza bila hofu pengine wanaCCM wana nidhamu ya woga, ndiyo maana wanakuwa wanafiki wa kupongeza hadharani na kuponda vijiweni kwenye kahawa, nakusihi uwaondoe hofu wanaCCM wenzangu wapone unafiki.

Nane, Ni kweli kuna viashiria vya njaa siku za usoni kwani hali ya hewa si rafiki sana msimu huu kwa kilimo cha kutegemea mvua, ni kweli hali si mbaya sana kiasi cha kupiga propaganda za kuishambulia Serikali na kuleta hofu kwa Watanzania, lakini ukweli siku za usoni kuna tatizo la uhaba wa chakula, hata bei ya mazao si rafiki kwa Watanzania wenye kipato cha chini. Mfuko wa bei ni mkubwa pengine wafanyabiashara wanatumia mwanya wa ukame na kelele za njaa kupandisha bei za chakula. Rais Magufuli, Kanda ya Ziwa, ya Kati mpaka Kanda ya Magharibi msimu huu mazao hayana afya kutokana na uhaba wa mvua, tafadhali naomba usichukizwe sana na wanasiasa wanaotumia fursa hii kujijenga kisiasa, naomba tuanze kujihami kama Taifa kukwepa changamoto ya uhaba wa chakula inayoweza kujitokeza siku za usoni. Waondoe hofu maDC, Wakurugenzi na maRC ya kufukuzwa kwa kusema kuna njaa, wape ruhusa watafute njia za kukabiliana na ukame ili njaa ipite kando na wapiga kura wetu. Kwa unyenyekevu mkubwa naomba ujumbe huu upokelewe na uwe na sura ya nia njema.

Tisa, Rais tunasubiri neno lako la faraja juu ya changamoto ya ajira kwa vijana wahitimu wa elimu ya juu waliopoteza matumaini wanasubiri huruma yako, kuna walimu wa ngazi ya cheti mpaka shahada wapo mtaani hawajui wapi waende, wapo wahitimu wa fani mbalimbali wa vyuo vikuu mtaani hawajui hatima yao, wanatamani kujiajiri tatizo hawakopesheki kutokana na taratibu za taasisi ya kifedha hawana sifa ya kukopa, mitaji ya kujiajiri hawana tena siku hizi, baadhi ya viongozi waliopata ajira tangu wakiwa wanafunzi mpaka sasa wameajiriwa, wameanza kuleta kejeli eti vijana waache uvivu wajiajiri hawajui kujiajiri ni mtaji na kuwezeshwa tena hata taaluma nyingine hazitoi fursa ya kuajiriwa zaidi ya serikalini. Mfano mhitimu wa ualimu ngazi ya cheti anakwenda wapi. Vijana wanakupenda sana kwa niaba yao naomba upokee ujumbe huu, najua tatizo la ajira ni tatizo la dunia nzima, lakini tafadhali toa neno la rehema hata kwa kuwawezesha wajiajiri, tazama namna waweze kukopesheka, tazama namna ya kuwapatia fursa japo walimu. Rais Magufuli vijana tunasubiri kauli yako, hakuna tegemeo zaidi ya wewe, hakika tunatambua wewe ndiye jibu la changamoto hii ya ajira.

Kumi, Wakulima na wafanyakazi wanasubiri umiliki wa chama chao cha CCM kwani misingi yake ni kumkomboa mkulima na mfanyakazi na si sehemu ya wafanyabiashara wakubwa na matajiri kuneemeka na kuwanyonya wakulima na wafanyakazi wenye chama chao, wakulima na wafanyakazi wanahitaji kuweza kupaza sauti na kupata fursa za kiongozi ndani CCM maana ni mali yao. Ni wakati wa wakulima kupata uongozi na fursa ndani ya chama pasipo kujali kipato walichonacho, rejesha chaguzi za kupima uwezo wa kuongoza kuliko uwezo wa kifedha, rejesha CCM yenye kuheshimu na kuogopa nguvu ya wakulima na wafanyakazi. Nakumbuka vurugu za urais 2015 ndani ya chama chetu watu walitunishiana misuli ya pesa, lakini wewe ukapita pasipo pesa, hiyo ndiyo CCM ya Mwalimu Nyerere, nakuomba upokee ujumbe huu kuanzia uchaguzi wa chama wa mwaka 2017, wafanyabiashara na matajiri waheshimu wakulima na wafanyakazi wenye chama, pesa kutumika iwe historia kwenye uchaguzi ndani ya CCM, tupate viongozi bora waliokosa uongozi kisa hawana pesa za kuhonga kama wafanyabiashara matajiri. Kwa niaba ya wakulima na wafanyakazi pokea ujumbe wangu, tunaomba uondoe unyonge wa wakulima na wafanyakazi ndani ya chama chao rejesha umiliki wenye nguvu kwao, chama kiwe mali yao rasmi matajiri wakae mbali na unyonyaji wao.

Mwisho Rais na Mwenyekiti wa CCM hongera kwa kusherehekea miaka 40 ya chama chetu chenye wanachama na wafuasi wengi. Watanzania tunakuombea afya njema nasi tunasubiri mrejesho wa utendaji wako tukifuatilia kwa karibu utimizaji wa ahadi zako kwetu. Watanzania tunatarajia makubwa kwako bila shaka hutatuangusha tunasubiri mageuzi makubwa ya viwanda na uchumi wa kati .

Rais Magufuli kwa unyenyekevu mkubwa naomba ujumbe wangu utazamwe kwa mtazamo chanya, mtazamo wa mawazo ya kujenga taifa, mtazamo wa kizalendo, lengo kubwa ni kufika tuendako tukiwa salama. Naomba ujumbe wangu upokelewe Mheshimiwa Rais na Mwenyekiti wa CCM.