Home Uchambuzi Afrika Rais mpya Ethiopia ataimudu kasi ya Dk. Abiy?

Rais mpya Ethiopia ataimudu kasi ya Dk. Abiy?

2950
0
SHARE

Rais wa Ethiopia, Sahle-Work Zewde akiwa na Waziri Mkuu wa nchi hiyo Dk. Abiy Ahmed.

ERICK SHIGONGO NA MITANDAO

WIKI iliyopita taifa la Ethiopia limempata Rais mpya—Sahle-Work Zewde, ambaye pia ni mwanamke wa kwanza kuongoza nchi hiyo. Mwanamama huyo, anakuwa rais wa nne tangu chama tawala cha Ethiopian People’s Revolutionary Democratic Front (EPRDF) kishike madaraka.

Hatua hiyo imekuja baada ya Rais aliyekuwapo madarakani, Mulatu Teshome, kujiuzulu ikiwa ni miezi minane tu imepita, tangu Waziri Mkuu wa nchi hiyo, Hailemariam Desalegn ajiuzulu na kumpa nafasi Waziri Mkuu wa sasa, Dk. Abiy Ahmed, kushika hatamu.

Itakumbukwa kuwa kujiuzulu kwa Desalegn, Februari mwaka huu kuliacha maswali tata kama ilivyotokea kwa Rais Teshome ambaye pia amejiuzulu wadhifa huo bila kuwapo kwa sababu za msingi.

Hata hivyo, kujiuzulu kwa Desalegn kulidaiwa kuwa kulishinikizwa zaidi na mgogoro wa kisiasa uliokuwa umeikumba nchini hiyo hususani baada ya watu kadhaa kuuawa katika maandamano dhidi ya serikali yaliyofanywa na katika maeneo yenye makabila makubwa nchini humo ya Oromia na Amhara.

Adha, tangu alipochukua madarakani waziri mkuu mpya, Dk. Abiy hali imeanza kutengamaa katika nchi hiyo ambayo inadaiwa kuwa uchumi wake unakua kwa kasi.

Kwa muda mfupi ambao Dk. Abiy amekaa madarakani, ni dhahiri shahiri ameonesha nuru kwa Waethiopia na Afrika kwa ujumla, kwani amefanya mageuzi ambayo umma wa Ethiopia ulikuwa ukiyapigania kwa jasho na damu kwa siku nyingi.

Kiongozi huyo aliruhusu uhuru wa maoni na kukosoa serikali, pia amevionya vyombo vya dola kutowaonea wananchi wanaoikosoa serikali, kwani wao ndiyo chanzo cha mamlaka.

Pia Dk. Abiy ameachia wafungwa wengi wa kisiasa ndani ya Ethiopia, pia ameviachia huru vyombo vya habari zaidi 240 (Televisheni, Redio, Magezeti, Blogs, mitandao mbalimbali ya habari) ambavyo vilifungwa na mtangulizi wake, Mei mwaka huu aliamuru wafungwa 7,600 katika Mkoa wa Oromo kuachiwa huru pia, Mei 29, 2018, kiongozi wa kundi la Ginbot 7, Andargechew Tsege, aliachiwa kwa amri ya Rais wa Ethiopia pamoja na Muluta Teshome na wafungwa wengine wapatao 575.

Aidha, kwa mara ya kwanza, baada ya miaka 20, Dk. Abiy alizuru nchi jirani ya Eritrea ambayo imekuwa katika mgogoro na Ethiopia kwa muda mrefu licha ya kuwa na majadiliano na makubaliano yakumaliza tofauti zao (Ethiopia-Eritrea War, Algiers Agreements 2000), ambapo watawala wa Ethiopia wamekuwa wakiyapuza, lakini Abiy Ahmed ameyakubali baada ya kuzuru Eritrea Julai 8, 2018 na kutiliana saini na Rais wa Eritrea Isaias Afwerki.

Hadi sasa Ethiopia na Eritrea wameshaondoa majeshi yao katika mpaka unaozitenganisha nchi hizo, na Shirika la Ndege la Ethiopia (Ethiopia Airlines)  limeanza safari zake kutoka Addis Ababa hadi Asmara, Eritrea. Pia Rais Isaias tayari ameshatembelea Ethiopia na kufungua ‘upya’ ubalozi wa Eritrea jijini Addis Ababa.

Kwa mujibu wa katiba ya Ethiopia, rais hana nguvu ikilinganishwa na wadhifa wa waziri mkuu ambaye ndiye, aliye na nguvu za kisiasa nchini kama ilivyo kwa Israel na Ujerumani, kansela ndiye mwenye nguvu.

Katika Jamhuri nyingi duniani cheo cha rais kinashikilia mamlaka yote ya kisiasa na kidola. Jina la rais linawakilisha nguvu na uwezo wa kufanya maamuzi ya mwisho kwa mujibu wa katiba.

Duniani baadhi ya nchi zenye mfumo kama huo ni India, Ujerumani, Italia na Israeli.

Kiongozi mkuu anayefahamika zaidi wa Ujerumani ni Kansela Angela Markel na yeye ndiye mwenye mamlaka ya kuongoza serikali. Rais wa Ujerumani ambaye wengi nje ya nchi hiyo wanaweza kuwa hawajahi kumskia anaitwa Frank-Walter Steinmeier.

Kwa upande wa India mwenye mamlaka ya kiutendaji na maamuzi ya kiserikali ni Waziri Mkuu Narendra Modi. Rais wa India anaitwa Ram Nath Kovind.

Kwa upande wa Israeli mwenye hatamu za kuingoza serikali ni Waziri Mkuu Benjamin Netanyahu. Rais wa nchi hiyo ni Reuven Rivlin.

Aidha, kuchaguliwa  Sahle-Work Zewde na wabunge kuwa rais wa Ethiopia ni habari nzuri katika harakati za kuwainua wanawake wa Afrika, lakini wengi walioshangilia ushindi wake nje ya Ethiopia hawafahamu ukomo wa mamlaka yake hasa ikizingatiwa waziri mkuu wa nchi hiyo amekuwa moto wa kuotea.

Wengi wanamjumuisha Zewde katika fungu moja na Rais mstaafu wa Liberia, Ellen Johnson Sirleaf na Rais mstaafu wa Malawi, Joyce Banda.