Home Makala Kimataifa RAIS MPYA WA BRAZIL AKUMBWA NA KASHFA YA UFISADI

RAIS MPYA WA BRAZIL AKUMBWA NA KASHFA YA UFISADI

1161
0
SHARE

Kashfa mpya ya ufisadi imeikumba serikali mpya ya Brazil ya Rais Michel Temer wiki iliyopita baada ya waziri wake mmoja mwandamizi kujiuzulu .

Waziri huyo, Marcelo Calero, alimtuhumu rais wake kwa kumshinikiza, ili amsaidie swahiba wake mmoja wa kisiasa, kuhusu ujenzi wa ghorofa la kifahari katika mji wa Salvador, ulioko Kaskazini Mashariki mwa nchi hiyo.

Kiwanja kinachotakiwa kujengwa ghorofa hilo, ni eneo ambalo karne kwa karne lilikuwa limehifadhiwa kama kumbukumbu ya kihistoria ya taifa.

Gazeti la New York Times, liliripoti Ijumaa iliyopita kwamba Calero, aliyekuwa Waziri wa Utamaduni aliwaambia wapelelezi wa serikali kwamba Rais Temer alimshinikiza aruhusu ujenzi wa ghorofa katika eneo hilo, jengo ambalo mmiliki wake Geddel Vieira Lima, ambaye ni swahiba mkubwa wa rais huyo na ambaye anatajwa kuwa na wadhifa wa Katibu Mkuu wa Ikulu.

Kutokana na shinikizo hilo, Calero alitangaza kujiuzulu wadhifa wake wa uwaziri na katika barua yake ya kujiuzulu alisema amechukuwa hatua hiyo kwa manufaa ya taifa.

Wakati medani ya siasa nchini Brazil imeaanza tu kutulia baada ya kukumbwa na misukosuko mikubwa iliyohitimisha kuondolewa kwa Rais Dilma Rouseff kwa tuhuma za ufisadi, kashfa hii ya sasa nayo imeanza kumtikisa Rais Temer, miezi sita tu tangu amrithi Rouseff.

Viongozi wa upinzani nchini humo wamesema wataanzisha mchakato wa kumng’oa Temer kupitia Bunge kwa namna Bunge hilo hilo lilivyomng’oa Rouseff.

Na wiki iliyopita Ikulu ya Rais Temer ilikiri katika taarifa yake kwa vyombo vya habari, kwamba Rais Temer aliwahi kujadiliana na Calero kuhusu suala la jengo husika, lakini taarifa ilisisitiza kwamba Rais alikuwa anataka usuluhishi wa kitaalamu kuhusu sauala hilo.

Hata hivyo, ripoti zilizoibuka baadaye kwamba Calero alikuwa ameyarekodi kisirisiri mazungumzo yake na Rais Temer kuhusu suala hilo zilitikisa nchi wiki iliyopita, na hivyo kuweka milango wazi kwa Mahakama Kuu kuanza kulichunguza suala hilo.

Rais Temer alionekana katika hali ngumu ya kujitetea kuhusu madai ya Rouseff, kwamba kung’olewa kwake madarakani kulitokana na uchu wa madaraka uliongozwa na Temer na maswahiba wake.

Wachuguzi wa mambo walisema kwamba kama ni kweli kanda ya kurekodiwa ya Rais Temer itaonyesha, alikiuka misingi ya utawala bora kwa manufaa yake binafsi, basi urais wa kiongozi huyo utakuwa umekwisha.

Hata hivyo, kashfa hii imekuja wakati hasira zimekuwa zikipanda kuhusu harakati zinazofanywa na maswahiba wa Rais Temer katika Bunge za kujipa misamaha ya kutoshitakiwa katika kesi zilizohusu kupokea milungula ya fedha wakati wa kampeni za uchaguzi iliyowawezesha kuingia bungeni.

Temer mwenyewe alipatikana na hatia ya kukiuka sheria iliyoweka viwango vya kupokea michango ya kampeni kutoka kwa watu binafsi, na huenda akazuiliwa kugombea nafasi yoyote kwa kipindi cha miaka minane.

Rais Temer na chama chake cha Brazilian Democratic Movement Party, wako kikaangoni kutokana na kukamatwa kwa Eduardo Cunha, Mbunge kwa tuhuma za ufisadi.

Cunha ndiye alikuwa kinara harakati za kumng’oa Dilma Rouseff madarakani, na Sergio Cabral Gavana wa zamani wa mji wa Rio de Janeiro, alihusika katika ufisadi wakati wa maandalizi wa michezo ya Olympic ya mwaka huu.