Home Makala RAIS WANGU MAGUFULI NINA NENO KWAKO

RAIS WANGU MAGUFULI NINA NENO KWAKO

549
0
SHARE

Na Victor Makinda,

Rais wangu Magufuli,  mimi mwananchi niliyejitoa kama mwakilishi wa kuwasemea  Watanzania wa kipato cha chini, nia yangu ni kukueleza kile kinachojiri huku mitaani kwetu na nini wananchi waliojawa na matumaini wangependa kukiona katika utawala wako.

Katika hili nilipata kueleza  juu ya kilimo na changamoto zinazoikabili sekta hiyo muhimu inayoajiri karibu asilimia 80 ya Watanzania. Nilielezea kuhusu nishati mbalimbali, umuhimu na urahisi wa upatikanani wake, sambamba na bei rafiki kwa wananchi wenye kipato cha chini.

Mwisho niligusia kuhusu kiu ya wananchi kuhusu kupatikana kwa Katiba mpya ambayo ingerahisisha na kuweka misingi imara ya mazuri uyafanyayo katika utawala wako, kuendelea kufanywa hata baada ya kipindi chako kupita.

Rais wangu, kazi ya urais sio rahisi, ni kazi ngumu iliyotawaliwa na lawama tele. Makosa yote wanayofanya watendaji wako, lawama zinakuja kwako. Hii ni kwa sababau Katiba imekupa mamlaka makubwa ya kuteua umtakaye na kuona anafaa na hata kumtumbua yoyote ambaye anaonesha kutokwenda na taratibu za utendaji wa utumishi wa umma.

Watanzania wanakuombea sana, ili uendelee kuongoza nchi hii kwa hekima, busara na utulivu wa hali ya juu. Mamilioni ya Watanzania wamejawa na imani kubwa, wanaaamini ikiwa utazifanyia kazi changamoto kadhaa zinazowakabili, basi upo uwezekanao mkubwa wa ahadi ya maisha bora kwa kila Mtanzania iliyotolewa na mtangulizi wako,  Jakaya Mrisho Kikwete, kutimia japo kuna wakati wengi walianza kukata tamaa.

Nikiendelea kuelezea niliyoyasikia kutoka kwa baadhi ya Watanzania, ni kuhusu uhuru wa vyombo vya habari, sambamba na uhuru wa kutoa maoni, katazo la kufanya mikutano ya hadhara ya siasa na suala linalohusu watumishi waliofukuzwa kazi kwa kubainika kuwa na vyeti feki.

Rais wangu, nikisema ule ukweli pasina chembe ya unafiki kama ambavyo wewe umezoea kusema kuwa msemakweli ni mpenzi wa Mungu, nami sitaki kuikosa fursa hiyo adhimu ya kuwa mpemzi wa Mungu,  nitakueleza ukweli Rais wangu kuwa kuna hofu kuu katika uhuru wa kutoa maoni miongoni mwa wanahabari na Watanzania waliowengi.

Uhuru wa habari upo shakani kwa kuwa baadhi ya viongozi wa Serikali na idara zake, wamekuwa waoga mno kutoa habari  kwa waandishi kwa hofu kuwa watatumbuliwa. Kana kwamba hilo halitoshi, hata unapotaka kupata maoni ya baadhi ya watendaji wa  Serikali kuhusu jambo fulani, wengi wao wamekuwa wakikwepa kufanya hivyo.

Rais wangu Magufuli, nikudokezee kidogo hali ilivyo ndani ya vyumba vya habari kwa sasa. Waandishi wa habari wamekuwa ni waoga mno na wanafanya kazi kwa  hofu, na shaka kuu, wakihofu kuwa ikiwa watakwenda ndivyo sivyo, vyombo vyao vya habari vitafungiwa. Ile kauli yako uliyoitoa hivi karibuni kuwaasa waandishi wa habari kuwa kama wanadhani kuwa wako huru, basi sio kwa kiwango hicho, imewaogofya maelefu ya waandishi. Kwa sasa wengi wao wamebaki wakiwa wanakabiliwa na hofu  na shaka katika utekelezaji wa majukumu yao ya kila siku.

Wachambuzi wa makala za kisiasa kwa sasa wamepungua, makala za uchambuzi wa masuala mbali mbali ya kisaiasa kwa sasa zinakumbwa na kwikwi. Kana kwamba wachambuzi wana hofu na shaka. Wanaweza kuwa wanaona mapungufu, lakini wanahofu kuyasema kwa hofu ya kukutwa na dhahama.

Rais wangu Magufuli,  baadhi ya Watanzania wanaipongeza hatua hii, kwani ni ukweli usiofichika kuwa ilifika wakati waandishi na wachambuzi  walikuwa wakiikosea Serikali badala ya kuikosoa.

Hivyo ilikuwa ni  lazima kuwapa wandishi uhuru wenye mipaka  ikizingatiwa kuwa , uhuru bila nidhamu  ni fujo. Kuna wakati ilikuwa ni fujo.

Pamoja na hayo, baadhi ya  Watanzania niliozungumza nao wanasema  wameacha hata kununua magazeti, kwani kwa sasa wanachikisoma  magazetini  sio kile walichozoea kukisoma huko nyuma. Ninahofu huenda mauzo ya magazeti yakapungua.

Wanasema haikuwa mbaya kuwadhibiti wandishi wa habari pamoja na wachambuzi wanaotoa maoni yao, bali walipaswa kupata maelekezo ya namna nzuri ya kuikosoa Serikali kwa vielelezo. Hapa wanazingatia kuwa wandishi wa habari ni kioo cha Serikali, ni kurunzi na ni dira kwa dola.  Habari na maoni ya wandishi wa habari vinatija mno katika shughuli za kila siku za Serikali. Ukosoaji wenye heshima na nidhamu kwa Serikali, una nafasi kubwa kuweka mambo sawa.

Kuna baadhi husema kuwa vyombo vya habari ni muhimili wa nne—Serikali yenyewe, Bunge na Mahakama.  Hivyo kuvipa uhuru wenye nidhamu vyombo vya hivi, kupata habari pasi na urasimu, sambamba na kuvipa uhuru wa kufanya uchambuzi na maoni katika nyanja mbali mbali, kunaipa Serikali nguvu zaidi ya kutatua kero za wananchi, ili kuyafikia maendeleo kwa kasi.

Rais wangu,  wengi wanalalamika  kuhusu   Sheria ya Vyombo vya Habari.  Sheria hii inaelezwa kuwa ni kaburi linaloizika taaluma ya habari, kwa kuwa sheria hiyo ina vipengele vingi vinavyowabana wanahabari na tansinia ya habari kwa ujumla.

Kuna hili linalohusu katazo la vyombo vya Dola kwa vyama vya siasa kutofanya mikutano ya hadhara ya kisiasa, na kuwaruhusu Wabunge tu kufanya hivyo katika majimbo yao . Niseme tu ukweli, hapa pana manung’uniko mengi mno. Watanzania  walio wengi niliowasikia wakizungumia kuhusu hili, wananung’unika sana juu ya katazo hili. Wanasema kwanza linakwenda kinyume na Katiba ya nchi yetu, pili wanahoji, je, katazo hili lina lengo la kuua vyama vya siasa kikiwemo CCM?

Wanahoji hivyo kwa kuwa wanaamini kuwa nguvu ya chama chochote cha siasa ni watu. Chama kama hakina wanachama, hicho hakina sifa ya kuitwa chama cha siasa. Namna ya pekee ya chama cha siasa kupata wanachama, ni kufanya mikutano ya hadhara na kunadi sera za chama husika. Hili katazo la kutofanya mikutano ya hadhara linaonekana kuwa linaweza kuleta  madhara makubwa sana kwa vyama vya siasa vya upinzania na hata chama tawala chenyewe.

Kwa nini?

Hoja za hapo juu zinajibu juu ya hofu hiyo ya wananchi na hata viongozi wa vyama hivyo. Wanahofu juu ya muda utakaoruhusiwa  vyama vya siasa kufanya siasa, na muda utakaokuwa umebaki kuelekea uchaguzi mkuu wa 2020 utakuwa hautoshi.

Watanzania niliozungumza nao na kuwasikia, wanahoji sababu hasa za msingi za kuvizuia vyama vya siasa kutofanya mikutano ya kisiasa.? Wanajiuliza kama ni kwa sababu ya kutoa fursa ya kufanya kazi za maendeleo, basi saa za kazi ingepigwa  marufuku kufanya mikutano ya siasa ya hadhara, na iruhusiwe nyakati za jioni ambapo wananchi wanakuwa katika mapumziko baada ya saa za kazi.

Raisa wangu, ustawi wa vyama vya siasa ni muhimu mno kwa mustakabari wa ukuaji wa demokrasia na maendeleo. Vyama vya siasa hutumika kama kipumulio cha wananchi na wanasiasa, pale mambo yanapokuwa magumu zaidi. Kuna masuala ambayo wananchi huyatilia shaka katika utekelezaji wake. Wananchi hupata faraja sana wanapoona viongozi wa vyama vya siasa wanayapigia kelele majukwaani. Huamini kuwa kwa kufanya hivyo, Serikali iliyopo madarakani itayafanyia kazi haraka kwa hofu ya kukataliwa na wananchi na kukimbilia upinzani. Vyama vya siasa hutoa matumaini kwa wananchi, hasa pale panapoonekana kuwa wananchi wamekata tamaa na jambo fulani.

Lakini  katazo hili huenda likakiathiri hata Chama cha Mapinduzi. Ndio, CCM ni chama kama vyama vingine vya siasa. Chama hiki kinategemea zaidi uungwaji mkono wa Watanzania, ili kiendelee kubaki madarakani. Namna iliyo rahisi kwa chama hiki kuendelea kuungwa mkono na kukubalika kwa Watanzania, ni viongozi wa Chama kuingia mitaani, kufanya mikutano ya hadhara, kuelezea sera na dira ya maendeleo inayotekelezwa na Chama.

Katika mazingira haya ya upinzani tuliyonayo, chama hakitakiwi kulala na viongozi wake kujifungia maofisini na katika vikao vya ndani tu. Chama kinatakiwa kwanza kulinda idadi ya wananchama iliyonayo, sambamba na kuongeza wanachama kila uchao kwa kuwashawishi kupitia utekelezaji wa sera na mikutano ya hadhara ya ufafanuzi. CCM isipofanya  hivyo, upo uwezekano mkubwa wa chama kupoteza au kupungua ushawishi kwa wananchi.

Maoni ya wengi ni kwamba, mikutano ya vyama vya siasa iruhusiwe, mkazo mkubwa uwe ni katika kuwadhibiti wanasiasa uchwara ambao huitumia mikutano hiyo na majukwaa ya kisiasa, kutoa lugha za kebehi na matusi kwa viongozi wa vyama vingine na Serikali.

Mkazo uwe katika kudhibiti mikusanyiko holela  isiyofuata taratibu na sheria.  Ulinzi uimarishwe katika kila mkutano sambamba na kuzuia uvunjifu wa amani. Vyama vya upinzani kuna wakati vinatoa dira ya wapi twende, na nini tufanye. Kutovipa nafasi ya sauti zao kusikika hadharani, inaweza kuwafanya baadhi ya viongozi wa chama tawala kujisahau na kutotenda kwa msukumo wenye kasi.

Ninajua kuwa una majukumu makubwa ya kuwahudumia Watanzania. Macho na masikio yao yako kwako. Wewe ndio tumanini pekee la kuwavusha bahari na jangwani kuelekea nchi ya asali na maziwa.

Leo nimalizie tu na hili la wafanyakazi  waliobainika kuwa na vyeti vya kughushi. Hatua hii imepongezwa na Watanzania wengi. Naam, hasa wazalendo ambao walikuwa wanakwazwa kuona nafasi zao ambazo walizistahili, zikikaliwa na watu wasio stahili.

Lakini  hapa kuna kitu wananchi wako wanahoji, kwa nini Serikali ililala usingizi wa pono kwa miongo kadhaa, huku ikiacha wananchi wakifoji nyaraka muhimu za Serikali? Kwa nini Serikali haikuwa na utaratibu wa kuajiri watumishi wake baada ya kujiridhisha na usahihi wa nyaraka za muajiriwa husika?

Haijalishi, hiyo na hayo hayawezi kufuta ukweli kuwa watu hawa walifoji nyaraka na adhabu waliyoipata iliwastahili. Lakini hebu tupia jicho lako la tatu hapa. Ingiwa na huruma kidogo kwa hawa waliopoteza ajira zao. Badhi yao wametumia ujana wao wote katika utumishi wa umma, wapo waliokuwa wanakaribia kustaafu. Hawa wengine wana umri unaozidi miaka 55. Lakini wapo waliofanya kazi miaka 10, 20 na hata zaidi.

Ni vema ukawafikiria hawa pasi kujali kuwa ni wakosaji. Wengi kama sio wote, wana familia na wategemezi lukiku. Walikuwa msaada mkubwa katika familia na jamii zao. Ndoto za walio wengi zimezimwa hapa mithili ya mshumaa uliozimika ghafla wakati wa usiku wa giza nene. Matumaini yamewapotea, hawajui nini wafanye na wapi waende.

Ni vema hawa ukawafikiria kwa fikra za msahama. Kama sio kuwarejesha kazini, baadhi yao wameitumikia Serikali kwa muda mrefu na kwa weledi mkubwa. Ni vema wakapewa chochote cha kuanzia maisha mapya mtaani. Kuwaacha hivi hivi ni kuwaangamiza wao, familia zao na jamii pana ya Kitanzania.

Leo mimi ninaishi hapa. Nitaendelea kukuletea mengine mengi. Ninaamini hutochoka kusoma maandiko haya yasiyo na chembe ya unafki yakiwa yamejikita katika ukweli. Naam, Msema ukweli ni mpenzi wa Mungu kama upendavyo kusema.

victormakinda@yahoo.com

                 0717809933