Home Makala Rais wetu aanze kutoka nje sasa

Rais wetu aanze kutoka nje sasa

878
0
SHARE

Rais MagufuliNa Tobias Nsungwe

KUTOKANA na staili yake ya uongozi watu wengi duniani  wana hamu sana ya kumuona Rais John Magufuli. Namna yake ya uongozi inadaiwa kutofautiana sana na viongozi wengi wa Afrika. Wakati anaingia madarakani takribani miezi 11 iliyopita kishindo chake kilisikika, Nigeria, Afrika Kusini na hata Australia.

Mpaka sasa Magufuli amezitembelea nchi mbili tu yaani Rwanda na Uganda huku akiacha kwenda kwenye mialiko mingi nje ya nchi. Ni takribani mwaka mmoja sasa tangu Rais awe madarakani ni vyema akaanza  kutuwakilisha yeye mwenyewe nje ya nchi.

Wakati Magufuli akiahirisha safari zake kwa ‘kutingwa’ na kazi nyingi nyumbani, mtangulizi wake Jakaya Kikwete amekuwa akisafiri mara kadhaa. Amekuwa akiitwa na taasisi mbalimbali za kimataifa kumpongeza na kumshukuru kutokana na mchango wake wa maendeleo ya Tanzania na Afrika yaliyotokana na ziara za nje alizozifanya Kikwete akiwa Rais wa Tanzania kwa miaka 10.

Katikati ya mwezi huu Kikwete alikuwa mjini New York, Marekani,  ambako alialikwa na taasisi isiyo ya kiserikali ya Speak up Africa iliyompa tuzo kutambua mchango wa uongozi wake Tanzania unaodaiwa uliyalinda makundi maalumu kama wanawake na watoto.

Akizungumza katika hafla hiyo, Mkurungenzi Mtendaji wa taasisi hiyo, Mama Kate Campana, alimsifu Kikwete kwa kuendelea kuisemea Afrika hata baada ya kustaafu. Alimpongeza pia kwa juhudi zake za kupambana na ugonjwa wa Malaria na vifo vya kina mama na mtoto. Dalili zinaonyesha bado tutaendelea kuona Kikwete akiendelea kusafiri mara kwa mara kutokana na mtandano na uhusiano mzuri aliouweka na viongozi wa kimataifa tangu angali Waziri wa Mambo ya Nje.

Mkutano wa 71 wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa  uliofanyika mwezi huu ni miongoni mwa ziara za hivi karibuni kabisa ambazo Rais Magufuli aliona ni busara asiende. Kumbuka pia Rais alifuta ziara yake ya siku tatu nchini Zambia katika hatua za mwisho.

Katika mkutano wa Umoja wa Mataifa Rais Magufuli alitarajiwa kuhudhuria mkutano huo kwa mara ya kwanza na kwamba angeweza kutumia fursa hiyo kuonana na viongozi wenzake wa mataifa na mashirika makubwa duniani.

Sababu za kufuta safari hiyo ilielezwa kwamba ni tukio la tetemeko la ardhi lililotokea mkoani Kagera.

Hata hivyo Rais angeamua kuhudhuria mkutano wa UN naamini Watanzania wengi wasingemlaumu kwani shughuli za uratibu wa kushughulikia maafa ya tetemeko ungeweza kufanywa hata na wasaidizi wake.

Miongozi wa ziara za kwanza kufutwa ni pale Rais Magufuli alipoacha kuhudhuria Mkutano wa Wakuu wa Nchi za Jumuia ya Madola (CHOGM), uliofanyika nchini Malta kati ya Novemba 27-29, 2015. Katika mkutano ule angeweza kukutana na viongozi wengine kama aliyekuwa Waziri Mkuu wa Uingereza, David Cameron na viongozi wengine.

Hakuhudhuria pia mkutano wa Shirika la Biashara Duniani (WTO) mjini Nairobi Desemba 2015. Magufuli hakwenda pia kwenye mkutano wa Umoja Afrika (AU) wa Januari 2016 na badala yake aliwakilishwa na Makamu wa Rais, Samia Suluhu Hassan.

Wengi walitarajia Rais angeutumia mkutano ule kwenda kujitambulisha kwa marais wenzake wa bara hili. Hata pale ulipofanyika Kigali Rwanda pia hakwenda.

Mwishoni wa mwezi uliopita viongozi wenzake wa Jumuia ya Kiuchumi ya Nchi za Kusini mwa Afrika (SADC) walikuwa wakimsubiri kwa hamu kwenye mkutano uliofanyika mjini Mbabane, Swaziland. Ingawa Rais Magufuli alitarajiwa kukabidhiwa uenyekiti wa mzunguko, hakufika kwenye mkutano huo na badala yake aliwakilishwa na Samia.

Dk. Magufuli pia hakuhudhuria mkutano kati ya viongozi wa Afrika na Rais Xi Ping uliofanyika nchini Afrika Kusini. Mwezi uliopita Rais Magufuli hakuwepo kwenye mkutano wa kimatifa kati ya Japan na Afrika (TICAD) uliofanyika nchini Kenya ambako aliwakilishwa na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa.

Kwa mujibu wa Waziri wa Mambo ya Nje, Dk Augustine Mahiga, mara rais anaposhindwa kuhudhuria mikutano hiyo huwaarifu viongozi wenzake. Waziri huyo aliwahi kusema kwamba huenda tukashuhudia Dk. Magufuli akibaki nyumbani bila kusafiri nje kwa muda mrefu.

Awali tuliambiwa na Dk. Mahiga kwamba Rais asingelisafiri nje ya nchi kwa vile alikuwa bado akiunda Serikali yake. Kwa sasa Rais Magufuli amekwishaunda karibu kikosi kizima cha Serikali yake kuanzia Waziri Mkuu, mawaziri na hadi wakurugenzi wa wilaya. Hilo linatosha kumfanya rais sasa kuwa na fursa ya kusafiri nchi za nje. Naamini ameteua wasaidizi anaowaamini hivyo akiwa nje ya nchi hatokosa usingizi sana.

Dk Mahiga alituambia pia kwamba rais asingelisafiri nje ya nchi kwa wakati ule kwa sababu ya ‘ukata’ na kwamba alihitaji muda kuweka misingi ya ukusanyaji mapato na kubana matumizi. Nasema hiyo haiwezi kumzuia rais kusafiri kwa sababu kupitia safari za rais nchi inakuwa na uhakika zaidi wa kupata fedha kupitia misaada, mikopo au mikataba mbalimbali.

Ni kweli Rais amekuwa akiwakilishwa na wasaidizi wake wakuu katika mikutano mbalimbali. Hata hivyo wakuu wa nchi na mashirika huwa na imani zaidi kuingia mikataba na mkuu wa nchi husika. Rais ndiye kioo cha Tanzania nje ya nchi kwa sasa. Si Makamu wa Rais au Waziri Mkuu.

Akiwa Chamwino, mjini Dodoma wakati wa kampeni za urais Septemba mwaka jana, Dk. Magufuli aliwabeza wale waliokuwa wakimlaumu Kikwete kwa kusafiri sana nje ya nchi. Alisikika akisema kuwa haikuwa busara kumlaumu mtangulizi wake kwa safari nyingi za nje kwani matunda ya safari zile yanaonekana.

Akiitaja miradi ya barabara, reli na juzijuzi Hospitali ya Mloganzila, Dar es Salaam kama mfano wa mafanikio yaliyoletwa na safari za rais wa awamu ya nne. Hakuna atakayemlaumu Rais Magufuli hata akisafiri mara ngapi ili mradi safari hizo zile na tija kwa Watanzania. Hata wapinzani wanapendekeza rais aanze kusafiri sasa. Nimewahi kumsikia Mbunge wa Mbeya mjini, Joseph Mbilinyi (Chadema) akimtaka Rais aanze kutoka ili aonane na wenzake.

Tanzania bado inaheshimika sana duniani kutokana na msingi imara aliouweka Mwalimu Julius Kambarage Nyerere. Ili kuendeleza heshima hiyo mikutano mingi bado itahitaji uwepo wa Rais mwenyewe. Si kutuma wawakilishi.