Home Maoni RAJABU JUMA: CCM WAMETURAHISISHIA USHINDI KINONDONI

RAJABU JUMA: CCM WAMETURAHISISHIA USHINDI KINONDONI

838
0
SHARE

NA JOHANES RESPICHIUS

MOJA ya majimbo yenye ushindani wa hali ya juu katika uchaguzi mdogo unaotarajiwa kufanyika Februari 17 ni Jimbo la Kinondoni ambalo imeshuhudiwa vyama vya siasa 12 vikisimamisha wagombea vikiongozwa na Chama tawala CCM, Chadema na CUF.

Wiki hii RAI limefanya mahojiano na mgombea ubunge wa jimbo hilo anayeipeperusha bendera ya CUF inayoungwa mkono na Mwenyekiti wake, Profesa Ibrahim Lipumba, Rajabu Salim Juma.

Pamoja na mambo mengine mgombea huyo alidadavua mambo mbalimbali ikiwamo historia yake na changamoto anazokumbana nazo katika kipindi hiki cha kampeni.

RAI: Jimbo la Kinondoni linaonekana kuwa na ushindani mkubwa, umejiandaa vipi kuukabili ushindani huo?

JUMA: Ushindani ni mkubwa lakini nimejipanga vizuri natambua kwamba nimezaliwa katika jimbo hili nazifahamu kero za Kinondoni naamini wananchi watanipigania.

Kuna vyama ambavyo vimekuja kusindikiza tu lakini hawana dhamira ya kushinda uchaguzi kwa sababu katika vyama vilivyoshiriki 12 kuna baadhi havina hata matawi kwenye kata. Unategemea vipi kushinda jimbo lenye kata 10 wakati huna hata mjumbe lakini ukiangalia vyama vyenye taswira kama Chadema na CCM ambayo imepoteza mwelekeo kwa kumsimamisha mgombea aliyetoka CUF jambo ambalo limewakera wananchi wengi.

Mpaka jimbo hili linapatikana watu walihangaika, wengine waligongwa, walipigwa mabomu na wengine walikamatwa kwahiyo haya ni mateso kwa wananchi lakini Mtulia hakujali akaachia jimbo kwahiyo CCM kumrudisha ni kutusaidia kazi.

Pia wanaccm waliokijenga chama hawawezi kumchagua Mtulia kwani wanaamini walikuwa na watu wenye sifa za kugombea na baada ya yeye kuachia jimbo kuna watu walishajipanga kwahiyo kuleta mtu ambaye hata mwezi kwenye chama hana kimewaumiza.

Na Chadema kwa mujibu wa Mwenyekiti wake Freean Mbowe alishatoa tamko kwamba hawatashiriki uchaguzi mdogo kwa sababu kuna mapungufu hivyo mpaka Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) iwaite kujadiliana namna ya kuondoa mapungufu.

Swali ni je, wameamua kuweka mgombea hayo mapungufu yameondoshwa? na haioni kwamba kisiasa inapoteza ninachokiona ni kwamba Chadema imekuja kupoteza nguvu ya kilipigania jimbo la Kinondoni ni kama wanaisaidia CCM.

Isitoshe ukiangalia mkakati wa Ukawa tuligawana majimbo hili la Kinondoni alipewa CUF kwa minajili hiyo hawakupaswa kusimamisha mgombea wakiachie chama ambacho ndicho chenye jimbo.

Wakati hayo yakiendelea wao walikuwa na uchaguzi jimbo la Longindo ambalo lilikuwa mikononi mwao kama lilivyo la Kinondoni wakakataa kushiriki likachukuliwa na CCM leo hii wanatuletea mgombea huku.

RAI: Unasema Chadema haikufuata utaratibu wa Ukawa, lakini Profesa Lipumba amewahi kusema kuwa hayupo kwenye umoja huo. Unazungumziaje hilo?

JUMA: Suala la kusema kwamba mwenyekiti wangu alijitenga na masuala ya Ukawa hili halina nafasi katika jimbo la Kinondoni kwa sababu Profesa Lipumba alipojiuzulu uenyekiti watu wengi walivunjika moyo lakini bado sisi kama viongozi tulisimama imara hatukuacha kufanya harakati.

Kwahiyo hakuna hoja ya kwamba Mwenyekiti alijitenga na Ukawa, alikaa pembeni kwa msimamo na mtazamo alionao lakini sisi hatukurudi nyuma hivyo bado tunaishangaa Chadema ilitumia fursa gani ya kutokuwasiliana na wanajimbo kuweza kusimamisha mgombe ambaye CUF ndiyo inatetea kiti chake.

RAI: Mpaka unateuliwa kuwa mgombea wa jimbo la Kinondoni umepata ushirikiano gani kutoka katika upande wa Katibu Mkuu, Maalim Seif?

JUMA: Ndio, mimi nilikuwa nashirikiana nao kama wanachama wenzangu na tulikuwa pamoja hata katika mchakato wa ndani ya chama tulikuwa vizuri.

RAI: Kwahiyo Katibu Mkuu ameunga mkono uteuzi wako?

JUMA: Kwa sasa hivi Katibu Mkuu hayupo lakini viongozi waliopo wamebariki kwa sababu chama chetu akiwepo kiongozi ndiyo anaweza kusimamia akiwa hayupo wa chini yake ndiye anakuwa na jukumu hilo.

Kwahiyo sio lazima viongozi washiriki kila hatua isitoshe kura za maoni zinasimamiwa kwenye jimbo Ofisi kuu inakwenda kuthibitisha na kama kusingekuwa na mgogoro huu jina langu lingerejea hata wasingekuwepo. Pia sijapata barua kutoka kwa Maalim inayoonesha kwamba hajatambua ushiriki wetu katika jimbo la Kinondoni.

RAI: Ni miaka kadhaa CUF imekuwa katika mpasuko wa kisiasa, hii kwako haiwezi kukuathiri hadi kushindwa kukomboa jimbo hili?

JUMA: Huu mpasuko hauwezi kusababisha kupoteza kwani wanachama wenyewe kwa kadiri siku zinavyokwenda wanatambua kwamba mgogoro uliopo ni wa kitaifa na upo kwa mujibu wa sheria ndiyo maana kwa sasa upo mahakamani, ukifika mwisho atakayeshinda kashinda na atakayeshindwa kashindwa awe mwenyekiti au katibu mkuu, chama kitaendelea.

Ukiachilia mbali mgogoro hawa ni binadamu ipo siku Profesa Lipumba na Maalim watakufa lakini hatuwezi kuacha siasa kwahiyo hawawezi kutuzuia kuendelea na michakato ya kisiasa kwa sababu kuna mpasuko.

RAI: Kumekuwa na maneno ya chini kwamba CUF upande wa Profesa Lipumba ni vibaraka wa CCM, hilo unalizungumziaje?

JUMA: Hilo mpaka tupate vielelezo ili kujua kama ni la kweli hama sio lakini si kwa maneno.

RAI: Kipaumbele chako ni kipi katika uchaguzi huu?

JUMA: Kipaumbele changu ni kusimamia na kutekeleza mahitaji ya wananchi wa Kinondoni kwa sababu mimi ni mzawa nafahamu kero zao.

Nitasimama kama kiongozi na sinunuliki, nina msimamo, najiamini na nina uhakika tunakwenda kushinda hilo lifahamike, CCM na njia zao zote watakazotumia haitatuzuia kukomboa jimbo hili.

RAI: Unazungumziaje hii hali ya baadhi ya viongozi wa kisiasa kuhama vyama vyao?

JUMA: Suala la kuhamahama vyama linakatisha tama Watazania wa kawaida kwa sababu mtu anajenga imani juu ya chama chake au anaweza kuwa anaamini kutokana na mtu aliyesimama kwahiyo inapotokea akahama chama na kuelekea sehemu nyingine wanaumia jambo linaloweza kusababisha wakagoma kupiga kura.

Wanaohamahama kutoka chama kimoja kwenda kingine hawa watu wamefilisika ilikuwa ni busara vyama wanavyokimbilia visiwape nafasi ya uongozi ili wapimwe dhamira yao.

RAI: Unamzungumziaje utendaji wa Rais Dk Magufuli katika serikali ya awamu ya tano?

JUMA: Kwa mtazamo wangu Rais Magufuli naweza kumkubali pale anapofanya kitu kizuri kinachoonekana na pale atakapokuwa anakwenda isivyo basi nitamshauri kwamba umekwenda sivyo kwa kutumia njia ya busara kuweza kumfikishia ujumbe wangu.

Lakini kama Mbunge nikiwa nimechaguliwa akiwa amefanya jambo lenye masilahi ya watanzania sitosita kumuunga mkono eti kwa sababu yeye ni mwanaccm mimi ni CUF.

RAI: Tueleze historia yako kwa ufupi?

JUMA: Mimi ni mzaliwa wa Mwananyamala Kinondoni jijijni Dar es Salaam na elimu yangu ya msingi na sekondari nimeipata nikiwa mkoani hapa na baadae nilikwenda kusoma Ikambala Mombasa nchini Kenya.

Ni mjumbe wa Kamati tendaji na Kaimu Mwenyekiti wa CUF wilaya pia katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015 nilikuwa meneja kampeni ya aliyekuwa Mbunge wa Kinondoni, Maulid Mtulia ambaye amejiunga na Chama cha Mapinduzi (CCM).