Home Latest News RAMAPHOSA BADO ANA KIBARUA KIGUMU

RAMAPHOSA BADO ANA KIBARUA KIGUMU

4975
0
SHARE
HASSAN DAUDI

WIKI iliyopita, Rais wa Afrika Kusini, vurugu zilizotokea Kaskazini Magharibi mwa Afrika Kusini zilimfanya Rais wake, Cyril Ramaphosa, arejee nchini mapema akitokea jijini London, Uingereza, alikokwenda kuhudhuria Mkutano wa Jumuhiya ya Madola.

Ramaphosa amelitaja sekeseke hilo lililosababisha kukamatwa kwa waandamanaji 23 waliokuwa wakipambana na jeshi la polisi kuwa ni nyeti na lisilopaswa kupuuzwa.

Vituo vya televisheni vilionesha polisi wakitumia bunduki za plastiki kukabiliana na nguvu ya waandamanaji hao waliokuwa wakivamia maduka na kuchoma matairi ya magari.

Ramaphosa alipofika Afrika Kusini, aliwataka wahusika wa vurugu hizo kutulia na kuwasilisha matakwa yao kwa njia ya amani.

Kwa muda mrefu sasa, kumekuwa na vurugu katika eneo hilo ka Kaskazini Magharibi wa taifa hilo linalotajwa kuwa na ukubwa wa kilomita za mraba milioni 1.22 na wakazi wanaozidi milioni 57.

Huku ikiwa ni miezi miwili pekee imepita tangu alipoingia Ikulu, akichukua nafasi ya Jacob Zuma aliyelazimishwa kujiuzulu na chama chake cha ANC (African National Congress), Ramaphosa amefanikiwa kurejesha imani ya Waafrika Kusini kwa Serikali yao.

Ramahosa aliyewahi kushika wadhifa wa Katibu Mkuu wa ANC, aliwakosha wengi kwa hatua yake ya kulivunja baraza la mawaziri alilolikuta, ambalo kwa kiasi kikubwa lilikuwa likinuka ruswa wakati wa utawala wa Zuma.

Pia, uamuzi wake wa kuigusa Mamlaka ya Ukusanyaji Kodi (SARS) kwa ‘kumtumbua’ aliyekuwa mwenyekiti wake, Tom Moyane, uliwakosha wengi, ikizingatiwa kuwa alikuwa akishutumiwa vikali kwa kashfa zake za rushwa.

Ikumbukwe kuwa chini ya Moyane, uzembe wa SARS katika ukusanyaji mapato ulitajwa kuinyima Serikali ya Afrika Kusini Dola za Marekani bilioni 4, ambazo ni zaidi ya Sh Tril. 9 za Tanzania.

Aidha, alionesha kuwa chaguo sahihi kwa kitendo chake cha kuitaka wizara ya madini kuhakikisha watu weusi, ambao ni zaidi ya asilimia 80 ya wananchi wote wa Afrika Kusini, wanapewa kipaumbele katika biashara ya rasilimali hiyo.

Kwa upande mwingine, huku hayo yakionekana kukipamba kipindi chake kifupi Ikulu, bado Ramaphosa anakabiliwa na changamoto lukuki ambazo kama zitaendelea, basi huenda zikautia doa utawala wake.

Kwanza, bado kiongozi huyo anakabiliwa na kibarua kizito katika kuuondosha umasikini unaotawala kwa wananchi wake wengi.

Kwa mujibu wa ripoti ya sasa ya Benki ya Dunia (WB), uchumi wa Taifa hilo utakuwa kwa asilimia 1.4 pekee mwaka huu.

Hata maandamo ya Kaskazini Magharibi ni matokeo ya maisha mabovu waliyonayo wakazi wa eneo hilo, ikiwamo ukosefu wa makazi bora na huduma za kijamii.

Hilo limekuwa likichagizwa na janga la idadi kubwa ya vijana wasio na ajira, ikielezwa kuwa ni asilimia 50 katika maeneo mengi ya Afrika Kusini.

Chanzo kikubwa kwa sasa ni mfumo wa elimu nchini humo unaotajwa kuwa mbovu na unaozalisha wahitimu wasioweza kushindana katika soko la ajira.

Pia, Ripoti ya Shirika la Utafiti kwa Masomo ya Hebabu na Sayansi (TIMSS) imedai kuwa kwa mwaka, ni asilimia 4 pekee ya wanafunzi wanaoanza shule ya msingi na hatimaye kupata Shahada ya kwanza.

Mbali ya hilo, Ramaphosa anakabiliwa na mtihani mwingine wa baadhi ya teuzi zake, ikiwamo ile ya Mkuu wa Jimbo la Kaskazini Magharibi aliyopewa Supra Mahumapelo.

Sehemu kubwa ya wakazi zaidi ya milioni tatu wa eneo hilo wamekuwa wakimpinga kiongozi wao huyo, wakimnyooshea vidole kwa tuhuma za rushwa.

Wananchi wake wamekuwa wakishinikiza ajiuzulu, juhudi ambazo sasa zinaungwa mkono na Chama cha Kikomunisti cha SACP na Chama cha Umoja wa Wafanyabiashara cha COSATU.

Ikumbukwe kuwa hata uteuzi wa Ramaphosa katika kiti cha Umakamu wa Rais, ulikosolewa vikali alipompa wadhifa huo David Mabuza.

Akiwa Mkuu wa Jimbo la Mpumalanga katika uongozi wa Zuma, Mabuza alitajwa mara kadhaa kujihusiha na vitendo vya rushwa na hata kuratibu mauaji ya viongozi wa vyama vya upinzani katika eneo lake.

Orodha hiyo ya mawaziri wasio na taswira yenye afya mbele ya Waafrika Kusini inamjumuhisha pia Malusi Gigaba (Waziri wa Mambo ya Ndani), aliyekuwa Waziri wa Fedha katika utawala wa Zuma.

Ukiacha hilo, Ramaphosa anatakiwa kuufuta mzimu wa uhalifu, yakiwamo matukio ya ubakaji na mauaji ya mara kwa mara yanayotokea katika maeneo mbalimbali, ikielezwa kuwa watu 49 hupoteza maisha kwa siku.

Ifahamike kuwa matukio ya watalii kuporwa wanapokodi vyombo vya usafiri yamekuwa yakiyatikisa maeneo yaliyo karibu na viwanja vya ndege, hivyo kutishia ustawi wa sekta hiyo ambayo imekuwa ikiiingizia kiasi kikubwa Serikali ya Afrika Kusini.

Mwisho, Rais Ramaphosa ana changamoto kubwa ndani ya ANC, kwamba huenda ‘anatembea mwenyewe’ katika vita yake ya kuisafisha Ikulu iliyokuwa inanuka rushwa chini ya Zuma.

Kuthibitisha kuwa amezungukwa na wachache wanaomuunga mkono ndani ya chama hicho, ushindi wake uliompeleka Ikulu ulikuwa wa tofauti ya kura 179 pekee dhidi ya mke wa zamani wa Zuma, Dlamini-Zuma.