Home Maoni RC, DC wafuate sheria na kanuni za utendaji

RC, DC wafuate sheria na kanuni za utendaji

1546
0
SHARE

Kwa mara nyingine tena kauli imetoka serikalini ya kuwakumbusha watendaji na viongozi wengine katika serikali kufuata kanuni, taratibu na miongozo ya utendaji, hasa wanapowashughukia kinidhamu maafisa Walio chini yao.

Safari hii kumbusho hilo limetoka kwa Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) Joseph Kakunda mapema wiki hii mjini Dodoma katika hotuba yake kwa wakuu wa wilaya na wakurugenzi wa halmashauri 66 walioteuliwa Agosti mwaka huu.

Waziri Kakunda alisema ingawa ni muhimu kuwachukulia hatua wafanyakazi wote wazembe na “kuwafyeka” wezi na wabadhirifu wa mali za umma, lakini alitoa msisitizo wa kufuata sheria na kanuni zilizopo.

Aliwataka wateule hao kuzingatia kikamilifu mipaka yao ya madaraka na kwamba hatua watakazochukua katika uongozi na utendaji wao zizingatie sheria, kanuni na taratibu zilizopo.

Mapema katika hafla hiyo Naibu Katibu Mkuu wa wizara hiyo Dk Zainab Chaula alionyesha kukerwa na vitendo vilivyoibukia siku za karibuni – vya viongozi wa wilaya kuwasweka ndani watumishi wanaowaongoza na kuwataka kufuata sheria na kanuni zilizopo.

Aliwataka viongozi hao wa wilaya kuheshimu taaluma za watumishi wanaowaongoza kwa sababu wapo katika nafasi zao kisheria, na hivyo utaratibu wa kisheria ndiyo utumike kuwashughulikia kinidhamu.

Dk Chaula alisema wizara yake imekuwa ikipokea malalamiko mengi kutoka maeneo mbali mbali nchini kuhusu adha hii.

Tunapenda kuunga mkono kauli ya viongozi hawa wawili dhidi ya mtindo ambao ulikuwa umeanza kushika kasi kwa baadhi ya viongozi katika wilaya kuwashughulikia walio chini yao hadharani – tena kwa njia inayokaribia unyanyasaji wa kibinadamu eti tu kwamba ofisa huyo anatuhumiwa makosa mbali mbali.

Tukumbuke kwamba msingi mkuu wa sheria za nchi na Katiba yake ni kwamba mtuhumiwa yoyote hawezi kuhukumiwa bila ya yeye kupewa kwanza haki ya kusikilizwa. Halafu siyo hadharani. Msingi huu ni mbali ya zile kanuni za utumishi wa umma zilizoorodheshwa.

Halafu kuna tuhuma zingine dhidi ya ‘watuhumiwa’ zinapelekea agizo la kiongozi husika wa wilaya kutokuwa na mantiki kabisa – ni makosa ambayo yanaweza kushughulikiwa kiofisi tu kimya kimya. ‘Makosa’ haya ni kama vile kuchelewa kufika kikaoni au mkutanoni, kushindwa kujibu swali aliloulizwa na kadhalika.

Ni vigumu kwa nchi yetu kujigamba tuna utawala bora na wa kufuata sheria iwapo vitendo kama hivi vitaachwa kuendelea.

Pamoja na msimamo huo tunapenda kusisitiza kauli nyingine ya Waziri Kakunda kwamba watumiushi wanaojihusisha na rushwa, wabadhirifu na wezi wa mali za umma lazima washughulikiwe kikamilifu ili kansa zima ya ufisadi itokomezwe kutoka n gazi zote serikalini.