Home Makala RC Gambo  amelewa madaraka au ana tatizo lingine?

RC Gambo  amelewa madaraka au ana tatizo lingine?

887
0
SHARE

NA ABRAHAM GWANDU, ARUSHA

WIKI iliyopita Daktari bingwa wa magonjwa ya afya ya akili kutoka Hospitali ya taifa ya muhimbili (MNH) Dk. Frank Massao alikuwa Arusha kwa ajili ya kutoa mada kwenye mkutano wa wadau wa NSSF.

Katika uwasilishaji wa mada yake alishtua wadau hao pale aliposema wafanyakazi wengi katika ofisi wakabiliwa na tatizo la ugonjwa wa akili ujulikanao kama sonona (Major Depression).

Pia akasema katika jamii kuna watu hasa wafanyakazi wenye tabia zisizofaa ‘ant-social’ ambao wao muda wote ni kwenda kinyume na wenzao, wabishi, wakorofi, wagomvi, wakali, hawashauriki, wasiotaka mambo yaende kama wenzake walivyopanga isipokuwa hadi wao waseme, wenye kujipendekeza kwa wakuu wao wa kazi nakadhalika.

Na bahati mbaya kwa mujibu wa Dk Massao ugonjwa huu huwezi kuonekana haraka kwa macho ya kawaida  kwa sababu muda wote watu wenye kuugua au wenye dalili hizo  watajitahidi kuwa na tabasamu la kuhadaa ‘foolish smile’ pale wanapochangamana na jamii.

Mengi  yamesemwa juu ya mwenendo na tabia za Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Mrisho Gambo. Kwa bahati mbaya hasemwi vizuri isipokuwa wapo wachache wanaofurahishwa na aina ya uongozi wake kwa sababu wanazojua.

Mjadala kumhusu RC Gambo unaanza mbali kidogo tangu akiwa Mkuu wa Wilaya ya Korogwe Mkoani Tanga pale alipoingia kwenye mgogoro na mwanasheria wa Halmashauri hadi wakafikishana Tume ya maadili ya viongozi wa umma.

Lakini hata alipokuwa DC Uvinza hakuacha kumbukumbu nzuri katika utumishi wake kwani kila alichokuwa akitenda ama kinaumiza watumishi au wananchi wa wilaya husika.

Alipohamishwa kituo cha kazi kutoka Uvinza kwenda Arusha ni kama alikuwa amepania kuja kuonyesha kiburi cha madaraka na mamlaka aliyokabidhiwa kwani alipofika tu alisikika akiwaeleza baadhi ya watu wake wa karibu wakiwemo waandishi wa habari kuwa amekuja kuisambaratisha Chadema hivyo wamsaidie katika kazi hiyo.

Sasa kama nilivyosema hapo juu kuhusu mada ya Dk Massao nadhani tuangalie kidogo kuhusu tukio la hivi karibuni la kuzindua ujenzi wa hospitali ya Mama na mtoto kwa ufadhili wa taasisi ya  Martenity Africa ambalo liliaibisha taifa letu pale Mkuu wa Mkoa na Mbunge wa Arusha Mjini walipohitlafiana mbele ya wafadhili hao.

Kwanza ieleweke kuwa mradi huo ulishakuwa kwenye hatua mbalimbali kabla RC Gambo hajateuliwa kushika wadhifa huo. Na wakati wa  mchakato wa hatua za awali ukifanyika Serikali iliyokuwa madarakani ni hii hii ya Chama cha Mapinduzi. Na ndio iliyotoa vibali vyote kuruhusu mradi kufanyika katika eneo ambalo kampuni ya Mawalla ilitoa kwa shirika la maendeleo la Arusha (ARDf).

Mbunge Lema alieleza na kuonyesha uthibitisho kuwa ni yeye aliyekuwa na maono ya kujenga Hospitali hiyo kwa manufaa ya wananchi wote, ni yeye aliyeomba eneo ,ni yeye aliyetafuta wafadhili na pia ni yeye aliyependekeza RC Gambo awe mgeni rasmi katika uwekaji wa jiwe la msingi na uzinduzi wa ujenzi.

Mgogoro ulianza pale ratiba ilipoonyesha Lema angekuwa miongoni mwa wazungumzaji, lakini RC Gambo akabadilisha ratiba kwa kuondoa baadhi ya wasemaji katika hafla hiyo akiwemo mbunge Lema kwasababu za ufinyu wa muda na ratiba ngumu ya mgeni rasmi.

Hapo wenye kufikiri wakaona tayari siasa imeingizwa makusudi katika hafla isiyokuwa ya kisiasa. Lakini kwa mshangao wa wengi wakati akitoa salam zake RC alikuwa akisisitiza kuwa watu wanaingiza siasa katika mambo ambayo sio ya kisiasa na badala ya kumtaja mbunge Lema kama mwanzilishi wa maono hayo, yeye alikuwa akirudia rudia kuishukuru kampuni ya Mawalla ambayo kwa hatua mradi ulipofikia haihusiki tena .

Kuona hivyo ndipo mbunge Lema akalipuka na kupinga maelezo ya RC Gambo akisema yamejaa hila, ghilba na wivu wenye mwelekeo wa  kumnufaisha kisiasa badala ya kuwakilisha msimamo wa serikali kwa faida ya wananchi wote.

Kama ni hivyo, nini chanzo cha mtafaruku wa Mbunge Lema na RC Gambo? Nani alikuwa sahihi na kwanini na nani alikwenda pale akiwa na dalili za ugonjwa wa sonona na tabia zisizofaa katika jamii  kama alivyobainisha Dk Massao wakati wa mkutano wa wadau wa NSSF?

Tukipata majibu ya maswali haya tutakuwa huru katika kuhukumu nani wa kubeba gharama ya aibu iliyotokea mbele ya wafadhili.

Mfano huu wa RC Gambo na Mbunge Lema tuutizame kwa picha kubwa ya nchi nzima, ni viongozi wangapi wanaongoza wananchi wakiwa na matatizo ya akili?

Je athari ya kuwa chini ya viongozi wenye tatizo hilo ni ipi? Hapa tunahitaji madaktari na wataalamu wa magonjwa ya akili wajitokeze na kutoa ushauri kwa mamalaka za uteuzi ili ikitokea kiongozi ana dalili hizo basi uteuzi wake utenguliwe ili asisababishe madhara kwa jamii anayoiongoza.

Wapo wakuu wa Mikoa na Wilaya katika Serikali hii ambao wanafanya mambo ambayo yamezua utata katika maeneo yao, wapo Mawaziri , wapo makatibu, wakurugenzi, wapo viongozi wa kisiasa kama Wenyeviti wa vyama vya siasa na  Makatibu wao, Wabunge na Madiwani. Wote hawa wanahitaji ‘vipimo’ maalumu ili jamii isiwe na mashaka nao pindi wanapotekeleza majukumu yao ya uongozi.

Wengi tulitaraji kwa umri na elimu yake RC Gambo angesaidia kuiunganisha Arusha iliyosambaratishwa na siasa za maji taka kwa miaka mingi. Uchumi wa Arusha umeyumba kutokana na tabia ya malumbano baina ya viongozi.

Tunakumbuka RC aliyefukuzwa kazi akiwa mkoa wa Mara  Magesa Mulongo jinsi alivyoivuruga Arusha kutokana na kiburi na ulevi wa madaraka  kabla hajahamishwa kituo cha kazi na kupelekwa Mwanza . Kama wananchi wa Arusha Mjini wamemchagua kiongozi wao kwa kura halali kwanini viongozi walioteuliwa wapinge uamuzi wa wananchi kwa njia haramu?

Nikiulizwa leo kwa nini wananchi wa Arusha wanaendelea kumchagua Lema pamoja na mapungufu yake ya kiuongozi yanayotajwa na mahasimu wake kisiasa, kwa kweli jibu langu nitasema hata mimi nawashangaa watu wa Arusha Mjini labda waulizeni!

Bahati mbaya sana RC Gambo ametumia mguu uleule aliotumia Magesa Mulongo, kiburi na majivuno ni tabia yake ya asili. Kama kiongozi wa umma tunataka ajirekebishe, ajaribu kuficha tabia yake ya asili. Tayari amegawa watu kwenye makundi wakiwemo wanahabari akiwaweka kwenye mizania ya hawa marafiki zangu na wale maadui zangu hili ni jambo la hatari sana kwa mustakabali wa Arusha tutakayo.

Ushauri wangu kwa RC Gambo akumbuke cheo ni dhamana, huenda kweli mamlaka ya uteuzi wake ndio inafurahishwa na namna anavyotenda majukumu yake lakini tahadhari ni kuwa yeye anayo safari ndefu kisiasa kuliko  Rais John Magufuli ambaye katiba imebainisha kikomo chake katika madaraka aliyonayo sasa .