Home Habari RC MBEYA KIBOKO YA WATUMISHI WALAFI

RC MBEYA KIBOKO YA WATUMISHI WALAFI

3421
0
SHARE

Na PENDO FUNDISHA-MBEYA


Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Albert Chalamila amewataka watumishi walafi wa Halmashauri ya Jiji la Mbeya pamoja na Wilaya,  wanaomiliki vibanda vya biashatra kwenye  maeneo mbalimbali kuwasilisha taarifa zao kwenye ofisi ya Mkurugenzi.

Alitoa agizo hilo wakati akizungumza na watendaji wa halmashauri hizo kufuatia watumishi hao kudaiwa kuhodhi vibanda vingi vya biashara na kuwa kikwazo kwenye ulipaji wa kodi huku wakikodisha vibanda hivyo kwa gharama kubwa na kusababisha Halmashauri kukosa mapato.

Alisema, asilimia 60 ya vibanda vya biashara vilivyopo kwenye maeneo mbalimbali ya Wilaya ya Mbeya, vimefungwa na havifanyi kazi na uchunguzi umebaini kwamba wahusika wa vibanda hivyo ni watumishi wa serikali hivyo ni vema wakawasilisha taarifa zao.

“Hatupingi mtumishi kuhodhi kibanda cha biashara, kinachopingwa hapa ni kujimilikisha vibanda zaidi ya kimoja, halafu havifanyi kazi na mbaya zaidi watumishi hao wanaonekana kuwa kikwazo cha ulipaji wa kodi ,serikali imepanga kibanda kilipiwe shilingi 40,000, wewe mtumishi unahamasisha watu wasitoe hiyo fedha tena kwa maslahi binafsi, wakati wewe umekipangisha chumba hicho,”alisema.

Alisema, tayari ofisi yake inayo majina ya watumishi ambao wametajwa kumiliki vibanda vya serikali zaidi ya kimoja na kwamba wameonekana kuwa vinara wa  kuwahamasisha wafanyabiashara wasikubaliane na kiwango cha kodi kinachopendekezwa na halmashauri.

“Majina ya watumishi ninayo, wapo wengine wanne wanatajwa kwamba wao ndio wababe, kazi yao kuvujisha siri za vikao vya serikali na kuwafikishia wafanyabiashara na kuwahamasisha wagome sasa ninatoa siku tatu waende kwa Mkurugenzi na kujisalimisha kabla maamuzi ya kikanuni na kisheria hayajachukuliwa ikiwemo kufukuzwa kazi,”alisema

Akizungumzia hilo, Mkurugenzi wa Halmashauri ya Jiji la Mbeya, James Kasusura, alisema kikatiba mtumishi ana haki ya kufanya biashara, lakini kwa maelekezo ya Mkuu wa Mkoa wanatakiwa kuangalia watumishi wanaohodhi kinyume cha taratibu.

Alisema, kitakachofanyika ni kuendesha zoezi la utambuzi wa wamiliki wa vibanda vya biashara kwenye masoko ya Nane Nane, Sido na Mwanjelwa na kutoa mikataba mipya ya kodi na kwamba kwa watumishi ambao wanatajwa kuhodhi vibanda kinyume cha sheria ni vema wakajisalimisha kabla ya maamuzi hayajafanyika lengo ni kuhakikisha serikali inapata mapato yake.

Kwa upande mwingine Chalamila, amesema uchumi wa nchi umekuwa ukizitegemea halmashauri kwa asilimia 60 kupitia vyanzo vya ndani vya mapato, lakini fedha hizo zilikuwa zikitafunwa na watu wachache na kuliacha kundi kubwa la watanzania kwenye dimbwi la umasikini.

Chalamila, aliyasema hayo juzi, wakati akizungumza na waandishi wa habari baada ya kikao chake  na watumishi wa halmashauri ya Jiji na Wilaya ya Mbeya kumalizika, kilichofanyika kwenye ukumbi wa mikutano wa Mkapa, Jijini hapa.

Alisema, jambo analolifanya Rais wa Jamuhuri ya Muungano ya Tanzania, ni kuhakikisha uchumi wa nchi unakua kwa asilimia 100 na kwamba ili kufikia kiwango hicho ni lazima mianya ya ulaji wa fedha idhibitiwe.

“Kazi ya kudhibiti mianya hii ni ngumu, huwezi kuifanya kwa kuendelea kuwa na asilimia kubwa ya watendaji ambao si waadilifu na viongozi tulioteuliwa tunapaswa kumsaidia Rais, hivyo nimewaeleza watumishi humu ndani ambao wanajiona wamo kwenye kundi la upigaji wa fedha na kuikosesha serikali mapato wajisalimishe,”alisema.

Alisema, ni vema watu wakamuunga mkono rais badala ya kukosoa kwa kila jambo analolifaya huku akidai kuwa asilimia kubwa ya watu wanaompinga ni wanasiasa ambao wapo kimaslahi.

Alisema, baadhi ya watu wamekuwa wakishindana kujitafutia utajiri wa haraka haraka kutokana na madaraka wanayopewa, wakitumia nafasi hizo kuwa mitaji ya kuanzisha na kuendeshea biashara zao, na si kuzitumikia kwa juhudi, maarifa, uadilifu na kwa maendeleo ya sasa na yajayo ya nchi yetu.

Alisema, matukio mengi yanayohusu wizi na ubadhirifu  yanafanywa na watumishi hao wa umma, hivyo hatua anayoifanya rais ni nzuri na ya kupongezwa, na kwamba ni lazima watu wajifunze kutumia fedha ya umma kwa nidhamu kwani hiyo ni kodi ya wananchi.